Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Matendo 11-13

Petro Arudi Yerusalemu

11 Mitume na waamini katika Uyahudi walisikia kwamba watu wasio Wayahudi wameyapokea mafundisho ya Mungu pia. Lakini Petro alipokuja Yerusalemu, baadhi ya waamini wa Kiyahudi[a] walimkosoa. Walisema, “Uliingia katika nyumba za watu wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa na ukala pamoja nao!”

Hivyo Petro akawaelezea namna ilivyotokea. Akasema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa. Nilipokuwa nikiomba, niliona maono. Niliona kitu kikishuka chini kutoka mbinguni. Kilionekana kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa pembe zake nne. Kikaja chini karibu yangu. Nilipotazama ndani yake, niliona aina zote za wanyama, pamoja na wale wa porini, wanyama wanaotambaa na ndege. Nilisikia sauti ikiniambia. Chinja chochote hapa na ule!”

“Lakini nilisema, ‘Siwezi kufanya hivyo Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kisicho safi au kisichostahili kuliwa kama chakula.’

Lakini sauti kutoka mbinguni ikajibu tena, ‘Mungu amevitakasa vitu hivi. Usiseme havistahili kuliwa!’

10 Hili lilitokea mara tatu. Ndipo kitu chote kikachukuliwa kurudi mbinguni. 11 Saa hiyo hiyo baada ya hayo wakawepo watu watatu wamesimama nje ya nyumba nilimokuwa ninakaa. Walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kunichukua. 12 Roho Mtakatifu aliniambia niende nao bila kuwa na mashaka. Ndugu hawa hapa sita walikwenda pamoja nami, na tulikwenda katika nyumba ya Kornelio. 13 Alitwambia kuhusu malaika aliyemwona amesimama katika nyumba yake. Malaika alimwambia, ‘Tuma baadhi ya watu waenda Yafa kumchukua Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 14 Atazungumza na wewe. Ujumbe atakaokwambia utakuokoa wewe na kila mtu anayeishi katika nyumba yako.’

15 Nilipoanza kuzungumza, Roho Mtakatifu alikuja juu yao kama vile alivyokuja juu yetu mwanzo.[b] 16 Ndipo nilikumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyosema: ‘Yohana alibatiza katika maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Mungu amewapa watu hawa karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo. Hivyo ningewezaje kupinga yale ambayo Mungu alitaka kufanya?”

18 Waamini wa Kiyahudi waliposikia hili, wakaacha kubisha. Wakamsifu Mungu na kusema, “Kwa hiyo Mungu anawaruhusu watu wasio Wayahudi kubadili mioyo yao na kuwa na maisha anayotoa!”

Habari Njema Zafika Antiokia

19 Waamini walitawanyika kwa sababu ya mateso[c] yaliyoanza baada ya Stefano kuuawa. Baadhi ya waamini walikwenda mbali mpaka Foeniki, Kipro na Antiokia. Walihubiri Habari Njema katika maeneo haya, lakini kwa Wayahudi tu. 20 Baadhi ya waamini hawa walikuwa watu kutoka Kipro na Kirene. Watu hawa walipofika Antiokia, walianza kuwahubiri watu wasio Wayahudi.[d] Waliwahubiri Habari Njema kuhusu Bwana Yesu. 21 Nguvu ya Bwana iliambatana na watu hawa, na idadi kubwa ya watu waliamini na kuamua kumfuata Bwana.

22 Kanisa katika mji wa Yerusalemu liliposikia kuhusu hili, lilimtuma Barnaba kwenda Antiokia. 23-24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu na imani. Alipokwenda Antiokia na kuona jinsi Mungu alivyowabariki waamini pale, alifurahi sana. Akawatia moyo wote, akasema, “Iweni waaminifu kwa Bwana daima. Mtumikieni Yeye kwa mioyo yenu yote.” Watu wengi zaidi wakawa wafuasi wa Bwana.

25 Kisha Barnaba alikwenda katika mji wa Tarso kumtafuta Sauli. 26 Alipompata, alimpeleka Antiokia. Walikaa pale mwaka mzima. Kila wakati kanisa lilipokusanyika, Barnaba na Sauli walikutana nao na kuwafundisha watu wengi. Ni katika mji wa Antiokia ambako wafuasi wa Bwana Yesu walianza kuitwa “Wafuasi wa Kristo”.[e]

27 Katika wakati huo huo baadhi ya manabii walitoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. 28 Mmoja wao, aliyeitwa Agabo, huku akisaidiwa na Roho Mtakatifu, alisimama na kuzungumza. Alisema, “Wakati mbaya sana unakuja katika dunia yote. Hakutakuwa chakula kwa ajili ya watu kula.” (Kipindi hiki cha njaa kilitokea Klaudio alipokuwa mtawala wa Kirumi) 29 Wafuasi wa Bwana wakaamua kwamba kila mmoja wao atatuma kiasi anachoweza kuwasaidia ndugu wote[f] wanaoishi Uyahudi. 30 Walikusanya pesa na kuwapa Barnaba na Sauli, waliozipeleka kwa wazee, katika Uyahudi.

Matatizo Mengi kwa waamini

12 Katika wakati huu huu, Mfalme Herode akaanza kuwatesa baadhi ya waamini waliokuwa sehemu ya kanisa. Aliamuru Yakobo aliyekuwa kaka yake Yohana, auawe kwa upanga. Herode alipoona kuwa Wayahudi wamelifurahia jambo hili, aliamua kumkamata Petro pia. Hii lilitokea katika kipindi cha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Alimkamata Petro na kumfunga gerezani, ambako alilindwa na kundi la askari kumi na sita.[g] Herode alipanga kumleta Petro mbele ya watu ili ahukumiwe, lakini alisubiri mpaka baada ya sikukuu ya Pasaka. Hivyo Petro aliwekwa gerezani lakini kanisa lilikuwa likiomba kwa Mungu bila kuacha kwa ajili yake.

Petro Atolewa Nje ya Gereza

Wakati wa usiku kabla ya siku ambayo Herode alipanga kumhukumu mbele ya watu, Petro, akiwa amefungwa minyororo miwili, alikuwa amelala katikati ya askari wawili. Na askari waliokuwa nje ya mlango walikuwa wanalinda gereza. Ghafla malaika wa Bwana alikuwa amesimama pale, na chumba kilijaa mwanga. Malaika akamwamsha Petro kwa kumpiga upande, akasema, “Amka haraka!” Minyororo ikaanguka kutoka mikono mwa Petro. Malaika akasema, “Vaa nguo na viatu vyako.” Petro alifanya kama alivyoambiwa. Kisha malaika akasema, “Vaa koti lako na unifuate.”

Hivyo malaika akatoka nje na Petro alimfuata. Hakujua kama kweli malaika alikuwa anafanya hili. Alidhani alikuwa anaona maono. 10 Petro na malaika wakavuka lindo la kwanza na lindo la pili. Kisha walifika kwenye lango la chuma lililowatenganisha na mji. Lango likafunguka. Baada ya kuvuka lango na kutembea umbali wa kama mtaa mmoja, malaika akatoweka ghafla.

11 Ndipo Petro akatambua kuwa haikuwa ndoto. Akawaza moyoni akisema, “Sasa ninajua kwamba Bwana hakika alimtuma malaika wake kwangu. Ameniokoa kutoka kwa Herode na kutoka kwenye mabaya yote ambayo Wayahudi walidhani yatanipata.”

12 Petro alipotambua hili, alikwenda nyumbani kwa Mariamu, mama yake Yohana, aliyeitwa Marko. Watu wengi walikuwa wamekusanyika pale wakiomba. 13 Petro alibisha kwenye mlango wa nje. Mtumishi wa kike aliyeitwa Rhoda alikuja ili afungue mlango. 14 Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi sana hata akasahau kufungua mlango. Akakimbilia ndani na kuliambia kundi, “Petro yuko mlangoni!” 15 Waamini wakamwambia, “Wewe una kichaa!” Lakini alipoendelea kusema kwamba ni kweli Petro yuko mlangoni. Waamini walisema, “Lazima atakuwa malaika wa Petro.”

16 Lakini Petro aliendelea kubisha mlangoni. Waamini walipoufungua mlango na kumwona, wakashangaa. 17 Petro akawafanyia ishara kwa mkono wake kuwaambia wanyamaze. Akawaeleza namna Bwana alivyomtoa nje ya gereza. Akasema, “Mwambieni Yakobo na ndugu wengine kilichotokea.” Kisha akawaacha na kwenda sehemu nyingine.

18 Siku iliyofuata askari walichanganyikiwa. Walijiuliza nini kimempata Petro. 19 Herode alimtafuta kila mahali lakini hakumpata. Hivyo aliwahoji walinzi na kuamuru wauawe.

Kifo cha Herode Agripa

Baadaye, Herode alihama kutoka Uyahudi na kwenda katika mji wa Kaisaria na kukaa huko kwa muda. 20 Herode aliwakasirikia sana watu katika miji ya Tiro na Sidoni. Lakini miji hii ilihitaji chakula kutoka katika nchi yake, hivyo baadhi yao walimjia wakitaka amani naye. Waliweza kumshawishi Blasto mtumishi binafsi wa Mfalme ili awasaidie.

21 Herode alichagua siku maalumu ya kukutana nao. Siku hiyo alivaa vazi zuri la kifalme. Aliketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu. 22 Watu wakapaza sauti zao na kusema, “Hii ni sauti ya mungu, siyo mwanadamu!” 23 Herode hakumpa Mungu utukufu. Hivyo malaika wa bwana akampiga kwa ugonjwa. Akaliwa na minyoo ndani na kufa.

24 Ujumbe wa Mungu ulikuwa unasambaa, ukiwafikia watu wengi zaidi.

25 Baada ya Barnaba na Sauli kumaliza kazi yao Yerusalemu, walirudi Antiokia, walimchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.

Barnaba na Sauli Wapewa Kazi Maalum

13 Walikuwepo baadhi ya manabii na walimu katika kanisa la Antiokia. Walikuwa Barnaba, Simeoni (ambaye pia aliitwa Nigeri[h]), Lukio (kutoka mji wa Kirene), Manaeni (aliyekua pamoja na Mfalme Herode[i]), na Sauli. Watu hawa wote kwa pamoja walikuwa wanamwabudu Bwana na wamefunga Roho Mtakatifu alipowaambia, “Nitengeeni Barnaba na Sauli ili wanifanyie kazi maalumu. Wao ndio niliowachagua kuifanya kazi hiyo.”

Hivyo kanisa lilifunga na kuomba. Wakaweka mikono yao juu ya Barnaba na Sauli, wakaagana nao na kuwaacha waende.

Barnaba na Sauli Wakiwa Kipro

Barnaba na Sauli walitumwa na Roho Mtakatifu. Walikwenda katika mji wa Seleukia. Kutoka hapo walitweka tanga na kusafiri mpaka kwenye kisiwa cha Kipro. Barnaba na Sauli walipofika kwenye mji wa Salami, walihubiri ujumbe wa Mungu katika masinagogi ya Kiyahudi. Yohana ambaye pia anaitwa Marko alikuwa pamoja nao ili kuwasaidia.

Walisafiri wakitisha kisiwa chote mpaka kwenye mji wa Pafo. Huko walimkuta mwanaume wa Kiyahudi aliyeitwa Bar-Yesu aliyekuwa akifanya uchawi. Alikuwa nabii wa uongo. Alikaa daima karibu na Sergio Paulo, aliyekuwa gavana na mtu makini sana. Sergio Paulo aliwaalika Barnaba na Sauli waende kumtembelea kwa sababu alitaka kusikia ujumbe wa Mungu. Lakini mchawi Elima (Bar-Yesu kama alivyoitwa kwa Kiyunani) alizungumza kinyume nao ili kuwapinga, akijaribu kumzuia gavana asimwamini Yesu. Kisha Sauli (ambaye pia anajulikana kama Paulo), akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkazia macho Elima 10 na kusema, “Ewe mwana wa Ibilisi, uliyejaa uongo na aina zote za hila za uovu! Wewe ni adui wa kila kilicho cha kweli. Hautaacha kuzibadili kweli za Bwana kuwa uongo? 11 Sasa Bwana atakugusa na utakuwa asiyeona. Hautaweza kuona kitu chochote kwa muda, hata mwanga wa jua.”

Ndipo kila kitu kikawa giza kwa Elima. Akazunguka kila mahali na akapotea. Alikwenda kila mahali akijaribu kumpata mtu wa kumshika mkono ili amwongoze. 12 Gavana alipoyaona haya, akaamini. Akayashangaa mafundisho kuhusu Bwana.

Paulo na Barnaba Waenda Antiokia ya Pisidia

13 Paulo na watu waliokuwa pamoja naye walitweka tanga na kusafiri kwa merikebu kutoka Pafo mpaka Perge, mji uliokuwa Pamfilia. Hapo Yohana Marko aliwaacha na akarudi Yerusalemu. 14 Waliendelea na safari yao kutoka Perge na kwenda Antiokia, mji karibu na Pisidia.

Siku ya Sabato walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi na kuketi chini. 15 Sheria ya Musa na maandishi ya manabii vilisomwa. Kisha viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe Paulo na Barnaba, wakisema, “Ndugu zetu, ikiwa mna kitu chochote cha kusema kitakachowasaidia watu hapa, tafadhali semeni.”

16 Paulo akasimama, akanyoosha mkono wake ili wamsikilize, akasema, “Watu wa Israeli nanyi nyote msio Wayahudi mnaomwabudu Mungu wa kweli, tafadhali nisikilizeni! 17 Mungu wa Israeli aliwachagua baba zetu. Na watu wetu walipoishi Misri kama wageni, aliwafanya wakuu. Kisha akawatoa katika nchi ile kwa nguvu kuu. 18 Aliwavumilia kwa miaka arobaini walipokuwa jangwani. 19 Mungu aliangamiza mataifa saba katika nchi ya Kanaani na kuwapa nchi yao watu wake. 20 Yote haya yalitokea katika kipindi cha kadiri ya miaka mia nne na hamsini.[j]

Baada ya hili, Mungu akawapa watu wetu waamuzi kuwaongoza mpaka wakati wa nabii Samweli. 21 Ndipo watu wakaomba kuwa na mfalme. Mungu akawapa Sauli, mwana wa Kishi. Sauli alitoka katika kabila la Benjamini. Alikuwa mfalme kwa miaka arobaini. 22 Baada ya Mungu kumwondoa Sauli katika ufalme, Mungu alimfanya Daudi kuwa Mfalme wao. Hiki ndicho Mungu alisema kuhusu Daudi: ‘Daudi, mwana wa Yese, ni mtu ambaye Mimi mwenyewe nimemchagua. Atafanya kila kitu nitakachotaka afanye.’

23 Kama alivyoahidi, Mungu amemleta mmoja wa wazao wa Daudi katika Israeli ili awe Mwokozi wao, mzao huyo wa Daudi ni Yesu. 24 Kabla Yesu hajaja, Yohana aliwaambia watu wote wa Israeli wanachopaswa kufanya. Waliwaambia wabatizwe kuonesha kuwa walitaka kubadili maisha yao. 25 Yohana alipokuwa anamaliza kazi yake, alisema, ‘Mnadhani mimi ni nani? Mimi siyo Masihi.[k] Masihi atakuja baadaye, nami sistahili kuwa mtumwa wake wa kufungua kamba za viatu vyake.’

26 Ndugu zangu, wana katika familia ya Ibrahimu na ninyi watu wengine ambao pia mnamwabudu Mungu wa kweli, sikilizeni! Habari kuhusu wokovu huu imeletwa kwetu. 27 Wayahudi waishio Yerusalemu na viongozi wao hawakutambua kuwa Yesu ni Mwokozi. Maneno ambayo manabii waliandika kuhusu yeye yalikuwa yakisomwa kila siku ya Sabato, lakini hawakuyaelewa. Walimhukumu Yesu. Walipofanya hivi, waliyatimiliza maneno ya manabii. 28 Hawakupata sababu ya msingi kwa nini Yesu afe, lakini walimwomba Pilato amwue.

29 Wayahudi hawa walimtendea Yesu mambo yote mabaya ambayo Maandiko yalisema yangempata Yesu. Kisha walimteremsha Yesu kutoka msalabani na kumweka kaburini. 30 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu! 31 Baada ya hili, kwa siku nyingi, wale waliofuatana na Yesu kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu walimwona. Wao sasa ni mashahidi wake kwa watu wetu.

32 Tunawahubiri Habari Njema kuhusu ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu. 33 Sisi ni wazao wao, na Mungu ameitimiza ahadi hii kwa ajili yetu. Mungu aliitimiza ahadi hii kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Tunasoma pia kuhusu hili katika Zaburi 2:

‘Wewe ni Mwanangu.
    Leo nimekuwa baba yako.’(A)

34 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Yesu hatarudi kaburini na kuwa mavumbi. Hivyo Mungu alisema,

‘Nitawapa ahadi ya kuaminiwa na
    takatifu niliyoiahidi kwa Daudi.’(B)

35 Lakini Zaburi nyingine inasema,

‘Hautaruhusu Mtakatifu wako aoze kaburini.’(C)

36 Daudi aliyatenda mapenzi ya Mungu alipokuwa hai. Kisha alikufa na kuzikwa kama baba zake wote. Na mwili wake ulioza kaburini! 37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuoza kaburini. 38-39 Ndugu zangu, eleweni yale tunayowaambia. Mnaweza kupata msamaha wa dhambi kupitia huyu Yesu. Sheria ya Musa haikuwatoa kutoka katika dhambi zenu. Lakini mnaweza kuwa huru mbali na hukumu. 40 Hivyo iweni waangalifu! Msiruhusu walichosema manabii kikawatokea ninyi:

41 ‘Sikilizeni enyi watu wenye mashaka!
    Mnaweza kushangaa,
    lakini sasa nendeni na mfe.
Kwa sababu kipindi cha wakati wenu,
    nitafanya kitu ambacho hamtaamini.
Hata kama kitafafanuliwa kwenu!’”(D)

42 Paulo na Barnaba walipokuwa wanaondoka kwenye sinagogi, watu waliwaomba warudi tena Sabato inayofuata ili wawaeleze zaidi kuhusu mambo haya. 43 Baada ya mkutano, watu wengi, Wayahudi na wale waliobadili dini zao na kufuata dini ya Kiyahudi, waliwafuata Paulo na Barnaba; nao waliwatia moyo watu hawa waendelee kuitumaini neema ya Mungu.

44 Siku ya Sabato iliyofuata, karibu watu wote katika mji walikusanyika ili wasikie neno la Bwana. 45 Wayahudi waliokuwepo pale walipowaona watu wote hawa, wakaingiwa na wivu sana. Wakakashifu na kubishia kila kitu alichosema Paulo. 46 Lakini Paulo na Barnaba walihubiri kwa ujasiri. Walisema, “Tulikuwa tuuhubiri ujumbe wa Mungu kwenu ninyi Wayahudi kwanza, lakini mmekataa kusikiliza. Mmeweka wazi kuwa hamstahili kuupata uzima wa milele. Hivyo tutakwenda sasa kwa wale wasio Wayahudi. 47 Hivi ndivyo Bwana alivyotuambia kufanya:

‘Nimewafanya ninyi mwanga kwa ajili ya mataifa mengine,
    kuwaonesha watu ulimwenguni kote njia ya wokovu.’”(E)

48 Wasio Wayahudi waliposikia Paulo akisema hivi, walifurahi sana. Waliuheshimu ujumbe wa Bwana, na wengi wao wakauamini. Hawa ni wale waliochaguliwa kuupata uzima wa milele.

49 Na hivyo ujumbe wa Bwana ulihubiriwa katika nchi yote. 50 Lakini Wayahudi pale walisababisha baadhi ya wanawake muhimu waifuatayo dini na viongozi wa mji kuwakasirikia na kuwachukia Paulo na Barnaba na wakawafukuza mjini. 51 Hivyo Paulo na Barnaba wakakung'uta mavumbi ya miguu yao.[l] Kisha wakaenda katika mji wa Ikonia. 52 Lakini wafuasi wa Bwana katika Antiokia walijaa furaha na walijazwa Roho Mtakatifu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International