Beginning
Sauli Awa Mfuasi wa Yesu
9 Huko Yerusalemu Sauli aliendelea kuwatisha wafuasi wa Bwana, na hata kuwaambia kuwa angewaua. Alikwenda kwa kuhani mkuu, 2 na kumwomba aandike barua kwenda kwenye masinagogi yaliyokuwa katika mji wa Dameski. Sauli alitaka kuhani mkuu ampe mamlaka ya kuwatafuta watu katika mji wa Dameski waliokuwa wafuasi wa Njia ya Bwana.[a] Ikiwa angewapata waamini huko, wanaume au wanawake, angewakamata na kuwaleta Yerusalemu.
3 Hivyo Sauli alikwenda Dameski. Alipoukaribia mji, ghafla mwanga mkali kutoka mbinguni ukaangaza kumzunguka. 4 Akadondoka chini na akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli! Kwa nini unanitesa?”
5 Sauli akasema, “Wewe ni nani, Bwana?”
Sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu, unayemtesa. 6 Simama sasa na uingie mjini. Mtu mmoja huko atakueleza unachopaswa kufanya.”
7 Wanaume waliokuwa wanasafiri pamoja na Sauli walisimama pale kimya. Waliisikia sauti, lakini hawakumwona yeyote. 8 Sauli alisimama kutoka chini na kufumbua macho yake, lakini hakuweza kuona. Hivyo wale aliokuwa nao wakamshika mkono na kumwongoza kuingia Dameski. 9 Kwa siku tatu Sauli hakuweza kuona; hakula wala kunywa.
10 Alikuwepo mfuasi wa Yesu katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania. Katika maono Bwana alimwita, “Anania!”
Anania alijibu, “Niko hapa, Bwana.”
11 Bwana akamwambia, “Amka na uende katika mtaa unaoitwa Mtaa Ulionyooka. Tafuta nyumba ya Yuda[b] na uliza kuhusu mtu anayeitwa Sauli anayetoka katika mji wa Tarso. Yuko katika nyumba hiyo sasa, anaomba. 12 Ameoneshwa katika maono kuwa mtu anayeitwa Anania anamwendea na kuweka mikono juu yake ili aweze kuona tena.”
13 Lakini Anania akajibu, “Bwana, watu wengi wameniambia kuhusu mtu huyu. Wameniambia kuhusu mambo mengi mabaya aliyowatendea watu wako watakatifu katika mji wa Yerusalemu. 14 Na sasa amekuja hapa Dameski. Viongozi wa makuhani wamempa mamlaka ya kuwakamata watu wote wanaokuamini wewe.”[c]
15 Lakini Bwana Yesu akamwambia Anania, “Nenda, nimemchagua Sauli kwa kazi maalumu. Ninataka ayahubiri mataifa mengine, watawala na watu wa Israeli kuhusu mimi. 16 Nitamwonyesha yote ambayo lazima atateseka kwa ajili yangu.”
17 Hivyo Anania aliondoka na kwenda nyumbani kwa Yuda. Akaweka mikono yake juu ya Sauli na kusema, “Sauli, ndugu yangu, Bwana Yesu amenituma. Ndiye uliyemwona barabarani wakati ukija hapa. Amenituma ili uweze kuona tena, pia ujazwe Roho Mtakatifu.” 18 Ghafla, vitu kama magamba ya samaki vikaanguka kutoka kwenye macho ya Sauli. Akaanza kuona tena! Kisha akasimama na kwenda kubatizwa. 19 Baada ya kula chakula, akaanza kujisikia kuwa na nguvu tena.
Sauli Aanza Kuhubiri Juu ya Yesu Kristo
Sauli alikaa pamoja na wafuasi wa Yesu katika mji wa Dameski kwa siku chache. 20 Baadaye alianza kwenda katika masinagogi na kuwahubiri watu kuhusu Yesu. Aliwaambia watu, “Yesu ni Mwana wa Mungu!”
21 Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa. Wakaulizana, “Je, huyu si yule aliyekuwa anajaribu kuwaangamiza watu wanaomwamini Yesu[d] katika mji wa Yerusalemu? Na hakuja hapa ili awakamate wafuasi wa Yesu na kuwarudisha kwa viongozi wa makuhani?”
22 Lakini Sauli aliendelea kuwa nguvu katika kuthibitisha kwamba Yesu ndiye Masihi. Uthibitisho wake ulikuwa na nguvu kiasi kwamba Wayahudi walioishi Dameski hawakuweza kubishana naye.
Sauli Awatoroka Wayahudi
23 Baada ya siku nyingi kupita, baadhi ya Wayahudi waliweka mpango wa kumwua Sauli. 24 Waliyalinda malango ya mji usiku na mchana. Walitaka kumwua Sauli, lakini aliambiwa kuhusu mpango wao. 25 Usiku mmoja baadhi ya wafuasi ambao Sauli aliwafundisha walimsaidia kuondoka mjini. Walimweka katika kikapu, wakamtoa kwa kumshusha kupitia kwenye tundu lililokuwa kwenye ukuta wa mji.
Sauli Katika Mji wa Yerusalemu
26 Kisha Sauli alikwenda Yerusalemu. Akajaribu kujiunga na kundi la wafuasi, lakini wote walimwogopa. Hawakuamini kuwa naye amekuwa mfuasi wa Yesu. 27 Lakini Barnaba alimkubali Sauli, akamchukua na kumpeleka kwa mitume. Akawaeleza namna ambavyo Sauli alimwona Bwana akiwa njiani na namna ambavyo Bwana aliongea naye. Kisha akawaambia namna ambavyo Sauli amehubiri kwa ujasiri kuhusu Yesu katika mji wa Dameski.
28 Sauli alikaa na wafuasi na kwenda kila mahali katika mji wa Yerusalemu akihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. 29 Kila mara alibishana na Wayahudi waliokuwa waliozungumza Kiyunani,[e] ambao walianza kutengeneza mpango wa kumwua. 30 Waamini walipoujua mpango huu, walimchukua Sauli mpaka Kaisaria, na kutoka huko walimsafirisha mpaka katika mji wa Tarso.
31 Kanisa katika Uyahudi yote, Galilaya na Samaria likawa na wakati wa amani. Na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, vikundi hivi vya waamini vikawa na nguvu katika imani na kuonesha utii kwa ajili ya Bwana kwa namna walivyoishi. Hivyo kanisa kila mahali liliongezeka kwa idadi.
Petro akiwa Lida na Yafa
32 Petro alikuwa akisafiri katika sehemu zote za Uyahudi, Galilaya na Samaria, na akasimama kuwatembelea waamini[f] walioishi Lida. 33 Huko alikutana na mtu aliyeitwa Ainea, ambaye alikuwa amepooza na hakuweza kutoka kitandani kwa miaka nane. 34 Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo amekuponya. Simama na kiweke kitanda chako vizuri!” Ainea alisimama saa ile ile. 35 Watu wote walioishi Lida na tambarare ya Sharoni walimwona, na wakaamua kumfuata Bwana.
36 Katika mji wa Yafa kulikuwa na mfuasi wa Yesu aliyeitwa Tabitha, Jina lake kwa Kiyunani lilikuwa Dorkasi.[g] Daima aliwatendea watu mambo mema na kuwapa pesa wale wenye mahitaji. 37 Petro alipokuwa Lida, Tabitha aliugua na kufa. Waliusafisha mwili wake na kuuweka chumbani ghorofani. 38 Wafuasi waliokuwa Yafa wakasikia kuwa Petro yuko Lida, mji ambao haukuwa mbali na Yafa. Hivyo waliwatuma watu wawili, waliomsihi Petro wakisema, “Tafadhali njoo kwetu haraka!”
39 Petro alijiandaa na kwenda pamoja nao. Alipofika, walimchukua na kumpeleka kwenye chumba ghorofani. Wajane wote walisimama wakamzunguka huku wakilia na wakamwonesha mavazi ambayo Tabitha alitengeneza alipokuwa hai. 40 Petro akawatoa watu wote chumbani. Akapiga magoti na kuomba. Kisha akaugeukia mwili wa Tabitha na kusema, “Tabitha! Simama.” Akafumbua macho yake. Alipomwona Petro akaketi. 41 Petro akamshika mkono na akamsaidia kusimama. Ndipo akawaita waamini na wajane chumbani. Akawaonyesha Tabitha; akiwa hai!
42 Watu kila mahali katika mji wa Yafa wakatambua kuhusu hili, na wengi wakamwamini Bwana. 43 Petro alikaa Yafa siku nyingi nyumbani kwa mtu mmoja aitwaye Simoni, aliyekuwa mtengenezaji wa ngozi.
Petro na Kornelio
10 Kulikuwa mtu aliyeitwa Kornelio katika mji wa Kaisaria. Mtu huyu alikuwa ofisa wa kikosi kilichoitwa “Kikosi cha Kiitalia” katika jeshi la Rumi. 2 Alikuwa mcha Mungu. Yeye na watu wengine wote walioishi katika nyumba yake walikuwa wanamwabudu Mungu wa kweli. Alitoa pesa zake nyingi kuwasaidia maskini miongoni mwa Wayahudi na daima alimwomba Mungu kwa kufuata utaratibu kama ilivyokuwa. 3 Mchana mmoja yapata saa tisa, kwa uwazi na dhahiri Kornelio aliona maono. Alimwona malaika kutoka kwa Mungu akimwendea na akamwambia, “Kornelio!”
4 Akiwa anashangaa na kuogopa, Kornelio akasema, “Unataka nini, bwana?”
Malaika akamwambia, “Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako unazowapa maskini. Anakukumbuka kwa yote uliyotenda. 5 Tuma baadhi ya watu sasa waende katika mji wa Yafa wakamlete mtu anayeitwa Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 6 Anakaa kwa mtu ambaye naye pia anaitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko kwenye ufukwe wa bahari.” 7 Malaika aliyeongea na Kornelio akaondoka. Ndipo Kornelio aliita watumishi wake wawili na askari mmoja. Askari alikuwa mcha Mungu, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. 8 Kornelio akawaelekeza kila kitu watu hawa watatu kisha akawatuma kwenda Yafa.
9 Siku iliyofuata wakati wa adhuhuri walipokuwa wanaukaribia mji wa Yafa, Petro alipanda juu ya paa[h] kuomba. 10 Alihisi njaa na akataka chakula. Lakini walipokuwa wanamwandalia chakula ili ale, aliona maono. 11 Aliona mbingu zikifunguka na kitu kama shuka kubwa kikishushwa chini kutoka mbinguni kwa pembe nne. 12 Ndani yake mlikuwa aina zote za wanyama, watambaao na ndege. 13 Kisha sauti ikamwambia, “Petro simama uchinje chochote hapa kisha ule.”
14 Lakini Petro akasema, “Siwezi kufanya hivyo, Bwana! Sijawahi kula kitu chochote kisicho safi au kisicho stahili kutumiwa kwa chakula.”
15 Lakini sauti ikamwambia tena, “Mungu amekwisha vitakasa vitu vyote hivi. Usiseme havistahili kuliwa.” 16 Hili lilimtokea mara tatu. Kisha likachukuliwa mbinguni. 17 Petro alijiuliza maono haya yalikuwa na maana gani.
Watu ambao Kornelio aliwatuma walishaiona nyumba ya Simoni na walikuwa wamesimama mlangoni. 18 Waliuliza, “Je, Simoni Petro yuko hapa?”
19 Petro akiwa bado anafikiri kuhusu maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Sikiliza, kuna watu watatu wanakutafuta. 20 Inuka na ushuke chini. Nenda nao, usisite, kwa sababu nimewatuma.” 21 Hivyo Petro akashuka chini na kuwaambia, “Nafikiri mimi ndiye mnayemtafuta. Kwa nini mmekuja hapa?”
22 Wale watu wakasema, “Malaika mtakatifu amemwambia Kornelio akualike nyumbani mwake. Ni mtu mwema na hutenda kwa haki, na anamwabudu Mungu na Wayahudi wote wanamheshimu. Malaika alimwambia akualike nyumbani kwake ili asikilize yale utakayosema.” 23 Petro akawakaribisha ndani watu wale ili walale usiku huo.
Siku iliyofuata Petro alijiandaa na kuondoka na wale watu watatu. Baadhi ya waamini katika mji wa Yafa walikwenda pamoja naye. 24 Siku iliyofuata walifika katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa anawasubiri na alikuwa amewakusanya jamaa na rafiki zake wa karibu nyumbani mwake.
25 Petro alipoingia ndani ya nyumba, Kornelio alimlaki kisha akaanguka miguuni kwa Petro na akamwabudu. 26 Lakini Petro akamwambia asimame. Petro akasema, “Simama! Mimi ni mtu tu kama wewe.” 27 Petro aliendelea kuzungumza na Kornelio. Ndipo Petro akaingia ndani na kuona kundi kubwa la watu wamekusanyika pale.
28 Petro akawaambia watu wale kuwa, “Mnaelewa kuwa ni kinyume na sheria yetu kwa Myahudi kushirikiana au kumtembelea mtu ambaye si Myahudi. Lakini Mungu amenionyesha kuwa nisimchukulie mtu yeyote kuwa yu kinyume na desturi za Kiyahudi. 29 Ndiyo sababu sikubisha watu wenu waliponiambia kuja hapa. Sasa, tafadhali niambieni kwa nini mmeniita hapa.”
30 Kornelio akasema, “Siku nne zilizopita, kama saa tisa mchana nilikuwa ninaomba ndani ya nyumba yangu. Ghafla akawepo mtu mmoja amesimama mbele yangu amevaa mavazi meupe yanayong'aa. 31 Akasema, ‘Kornelio, Mungu amesikia maombi yako na ameona sadaka zako kwa maskini. Anakukumbuka wewe na yote uliyofanya. 32 Hivyo tuma baadhi ya watu kwenye mji wa Yafa na wamwambie Simoni Petro kuja. Anakaa na mtu mwingine anayeitwa Simoni, mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko pembeni mwa bahari.’ 33 Hivyo nikawatuma kwako haraka. Imekuwa vizuri sana umekuja hapa. Sasa sote tupo hapa mbele za Mungu na tuko tayari kusikia kila kitu ambacho Bwana amekwamuru utuambie.”
Petro Ahubiri Katika nyumba ya Kornelio
34 Petro akaanza kwa kusema: “Hakika sasa ninaelewa ni kwa nini Mungu hawachukulii kundi fulani la watu kuwa bora kuliko wengine. 35 Anamkubali yeyote anayemwabudu na anayetenda haki. Haijalishi wanatoka katika taifa lipi. 36 Mungu amezungumza na watu wa Israeli. Aliwaletea Habari Njema kwamba amani imekuja kupitia Yesu Kristo ambaye ndiye Bwana wa watu wote.
37 Mnafahanu kilichotokea katika Uyahudi yote. Kilianzia Galilaya baada ya Yohana kuwaambia watu kuwa inawapasa kubatizwa. 38 Mnajua kuhusu Yesu kutoka Nazareti. Mungu alimfanya Masihi kwa kumpa Roho Mtakatifu na nguvu. Yesu alikwenda kila mahali akiwatendea mema watu. Akawaponya wale waliokuwa wakitawaliwa na yule Mwovu, akionyesha kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.
39 Tuliona yote ambayo Yesu alitenda katika Uyahudi na katika mji wa Yerusalemu. Lakini aliuawa. Walimpigilia kwenye msalaba uliotengenezwa kwa mti. 40 Lakini siku ya tatu baada ya kifo chake, Mungu alimfufua na kumfanya aonekane wazi wazi. 41 Hakuonekana kwa Wayahudi wote, lakini alionekana kwetu sisi tu, ambao Mungu tayari alikwisha kutuchagua tuwe mashahidi. Tulikula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu.
42 Yesu alitwambia twende na kuwaeleza watu. Alituagiza tuwaeleza kwamba yeye ndiye ambaye Mungu amemchagua kuwa mwamuzi wa wote walio hai na wote walio kufa. 43 Na ya kwamba kila atakayemwamini Yesu, atasamehewa dhambi zake kupitia nguvu jina Lake. Manabii wote wanakubali kuwa jambo hili ni la kweli.”
Roho Mtakatifu Awashukia Watu Wasio Wayahudi
44 Petro alipokuwa bado anazungumza, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanamsikiliza. 45 Waamini wa Kiyahudi waliofuatana na Petro walishangaa kwamba Roho Mtakatifu amemiminwa kama zawadi hata kwa watu wasio Wayahudi. 46 Waliwasikia wakiongea lugha mbalimbali na kumsifu Mungu. Ndipo Petro akasema, 47 “Je, mtu yeyote anawezaje kuzuia watu hawa wasibatizwe katika maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea!” 48 Hivyo Petro akawaambia wambatize Kornelio pamoja na jamaa zake na rafiki zake katika jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba Petro akae nao kwa siku chache.
© 2017 Bible League International