Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Yohana 3-4

Yesu na Nikodemu

Alikuwepo mtu aliyeitwa Nikodemu, mmoja wa Mafarisayo. Yeye alikuwa kiongozi muhimu sana wa Kiyahudi. Usiku mmoja alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Mwalimu, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa kutoka kwa Mungu. Hayupo mtu yeyote anayeweza kutenda ishara na miujiza unayotenda bila msaada wa Mungu.”

Yesu akajibu, “Hakika nakuambia, ni lazima kila mtu azaliwe upya.[a] Yeyote ambaye hajazaliwa mara ya pili hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu.”

Nikodemu akasema, “Yawezekanaje mtu ambaye tayari ni mzee akazaliwa tena? Je, anaweza kuingia tena katika tumbo la mama yake na kuzaliwa kwa mara ya pili?”

Yesu akamjibu, “Uniamini ninapokwambia kuwa kila mtu anapaswa kuzaliwa tena kwa maji na kwa Roho. Yeyote ambaye hakuzaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Maisha pekee ambayo watu huyapata kutoka kwa wazazi wao ni ya kimwili. Lakini maisha mapya anayopewa mtu na Roho ni ya kiroho. Usishangae kwa kuwa nilikuambia, ‘Ni lazima mzaliwe upya.’ Upepo huvuma kuelekea popote unakopenda. Unausikia, lakini huwezi kujua unakotoka na unakoelekea. Hivyo ndivyo ilivyo kwa kila aliyezaliwa kwa Roho.”

Nikodemu akauliza, “Je, haya yote yanawezekana namna gani?”

10 Yesu akasema, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Israeli, inakuwaje huelewi mambo haya? 11 Ukweli ni kwamba, tunaongea yale tunayoyafahamu. Tunayasema yale tuliyoyaona. Hata hivyo ninyi hamyakubali yale tunayowaambia. 12 Nimewaeleza juu ya mambo ya hapa duniani, lakini hamniamini. Vivyo hivyo nina uhakika hamtaniamini hata nikiwaeleza mambo ya mbinguni! 13 Sikiliza, hakuna mtu aliyewahi kwenda kwa Mungu mbinguni isipokuwa Mwana wa Adamu. Yeye pekee ndiye aliyekuja duniani kutoka mbinguni.”

14 Unakumbuka yule nyoka wa shaba ambaye Musa alimwinua kule jangwani?[b] Vivyo hivyo Mwana wa Adamu anapaswa kuinuliwa juu. 15 Kisha kila anayemwamini aweze kuupata uzima wa milele.[c]

16 Kweli, hivi ndivyo Mungu alivyouonyesha upendo wake mkuu kwa ulimwengu: akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu anayemwamini asiharibiwe na mauti bali aupate uzima wa milele. 17 Mungu alimtuma Mwanawe ili kuuokoa ulimwengu. Hakumtuma kuja kuuhukumu na kuuweka hatiani, bali kuuokoa kwa njia ya mwanawe. 18 Wote wanaomwamini Mwana wa Mungu hawahukumiwi hatia yoyote. Lakini wale wasiomwamini wamekwisha kuhukumiwa tayari, kwa sababu hawakumwamini Mwana pekee wa Mungu. 19 Wamehukumiwa kutokana na ukweli huu: Kwamba nuru[d] imekuja ulimwenguni, lakini watu hawakuitaka nuru. Bali walilitaka giza, kwa sababu walikuwa wanatenda mambo maovu. 20 Kila anayetenda maovu huichukia nuru. Hawezi kuja kwenye nuru, kwa sababu nuru itayaweka wazi matendo maovu yote aliyotenda.

21 Lakini yeyote anayeifuata njia ya kweli huja kwenye nuru. Nayo nuru itaonesha kuwa Mungu amekuwepo katika matendo yake yote.

Yesu na Yohana Mbatizaji

22 Baada ya hayo, Yesu na wafuasi wake wakaenda katika eneo la Uyahudi. Kule Yesu alikaa pamoja na wafuasi wake na kuwabatiza watu. 23 Yohana naye alikuwa akiwabatiza watu kule Ainoni, eneo karibu na Salemu mahali palipokuwa na maji mengi. Huko ndiko watu walipoenda kubatizwa. 24 Hii ilikuwa kabla ya Yohana kufungwa gerezani.

25 Baadhi ya wafuasi wa Yohana walikuwa na mabishano pamoja na Myahudi mwingine juu ya utakatifu.[e] 26 Ndipo wakaja kwa Yohana na kusema, “Mwalimu, unamkumbuka mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Mto Yordani? Yule uliyekuwa ukimwambia kila mtu juu yake.” Huyo pia anawabatiza watu na wengi wanaenda kwake.

27 Yohana akajibu, “Mtu anaweza tu kuyapokea yale ambayo Mungu anayatoa. 28 Ninyi wenyewe mlinisikia nikisema, ‘Mimi siye Masihi. Mimi ni mtu yule aliyetumwa na Mungu kutengeneza njia kwa ajili ya Masihi.’ 29 Bibi arusi siku zote yupo kwa ajili ya bwana arusi. Rafiki anayemsindikiza bwana arusi yeye hungoja na kusikiliza tu na hufurahi anapomsikia bwana arusi akiongea. Hivyo ndivyo ninavyojisikia sasa. Ninayo furaha sana kwani Masihi yuko hapa. 30 Yeye anapaswa kuwa juu zaidi yangu mimi, na mimi napaswa kuwa chini yake kabisa.”

Ajaye Kutoka Mbinguni

31 “Anayekuja kutoka juu ni mkubwa kuliko wengine wote. Anayetoka duniani ni wa dunia. Naye huzungumza mambo yaliyo ya duniani. Lakini yeye anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wengine wote. 32 Huyo huyasema aliyoyaona na kuyasikia, lakini watu hawayapokei anayoyasema. 33 Bali yeyote anayepokea anayoyasema basi amethibitisha kwamba Mungu husema kweli. 34 Na kwamba Mungu alimtuma, na yeye huwaeleza watu yale yote Mungu aliyoyasema. Huyo Mungu humpa Roho kwa ujazo kamili. 35 Baba anampenda Mwana na amempa uwezo juu ya kila kitu. 36 Yeyote anayemwamini Mwana anao uzima wa milele. Lakini wale wasiomtii Mwana hawataupata huo uzima. Na hawataweza kuiepuka hasira ya Mungu.”

Yesu Azungumza na Mwanamke Msamaria

Yesu akatambua ya kwamba Mafarisayo wamesikia habari kuwa alikuwa anapata wafuasi wengi kuliko Yohana na kuwabatiza. (Lakini kwa hakika, Yesu mwenyewe hakumbatiza mtu yeyote huko; bali wafuasi wake ndiyo waliowabatiza watu kwa niaba yake.) Hivyo akaondoka Uyahudi na kurudi Galilaya.

Barabara ya kuelekea Galilaya ilimpitisha Yesu katikati ya nchi ya Samaria. Akiwa Samaria Yesu akafika katika mji wa Sikari, ulio karibu na shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. Mahali hapo ndipo kilikuwapo kisima cha Yakobo. Kutokana na safari yake kuwa ndefu Yesu alichoka, hivyo akakaa chini kando ya kisima. Nayo ilikuwa saa sita adhuhuri. Baadaye mwanamke Msamaria akaja kisimani hapo kuchota maji, na Yesu akamwambia, “Tafadhali nipe maji ninywe.” Hili lilitokea wakati wafuasi wake walipokuwa mjini kununua chakula.

Mwanamke yule akajibu, “Nimeshangazwa wewe kuniomba maji unywe! Wewe ni Myahudi nami ni mwanamke Msamaria!” (Wayahudi hawana uhusiano na Wasamaria.[f])

10 Yesu akajibu, “Hujui kile Mungu anachoweza kukukirimu. Na hunijui mimi ni nani, niliyekuomba maji ninywe. Kama ungejua, nawe ungekuwa umeniomba tayari, nami ningekupa maji yaletayo uzima.”

11 Mwanamke akasema, “Bwana, utayapata wapi maji yaliyo hai? Kisima hiki kina chake ni kirefu sana, nawe huna kitu cha kuchotea. 12 Je, wewe ni mkuu kumzidi baba yetu Yakobo? Yeye ndiye aliyetupa kisima hiki. Yeye alikunywa kutoka kisima hiki, na wanawe, na wanyama wake wote.”

13 Yesu akajibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. 14 Bali yeyote anayekunywa maji ninayompa mimi hatapata kiu tena. Maji ninayowapa watu yatakuwa kama chemichemi inayobubujika ndani yao. Hayo yatawaletea uzima wa milele.”

15 Mwanamke akamwambia Yesu, “Bwana, nipe maji hayo. Kisha sitapata kiu na sitapaswa kuja tena hapa kuchota maji.”

16 Yesu akamwambia, “Nenda kamwite mumeo kisha urudi naye hapa.”

17 Mwanamke akajibu, “Lakini mimi sina mume.”

Yesu akamwambia, “Uko sahihi kusema kuwa huna mume. 18 Hiyo ni kwa sababu, hata kama umekuwa na waume watano, mwanaume unayeishi naye sasa sio mume wako. Huo ndiyo ukweli wenyewe.”

19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona ya kuwa wewe ni nabii. 20 Baba zetu waliabudu katika mlima huu. Lakini ninyi Wayahudi mnasema kuwa Yerusalemu ndipo mahali ambapo watu wanapaswa kuabudia.”

21 Yesu akasema, “Mwanamke! Niamini mimi, wakati unakuja ambapo hamtakwenda Yerusalemu wala kuja kwenye mlima huu kumwabudu Baba. 22 Ninyi Wasamaria hamwelewi mambo mengi kuhusu yule mnayemwabudu. Sisi Wayahudi tunamfahamu vizuri tunayemwabudu, kwa maana njia yake ya kuuokoa ulimwengu imepatikana kupitia Wayahudi. 23 Lakini wakati unakuja wenye nia halisi ya kuabudu watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa hakika, wakati huo sasa umekwishafika. Na hao ndiyo watu ambao Baba anataka wamwabudu. 24 Mungu ni roho. Hivyo wote wanaomwabudu wanapaswa kumwabudu katika roho na kweli.”

25 Mwanamke akasema, “Naelewa kwamba Masihi anakuja.” (Ndiye anayeitwa Kristo.)

“Atakapokuja, atatufafanulia kila kitu.”

26 Kisha Yesu akasema, “Mimi ninayezungumza nawe sasa, ndiye Masihi.”

27 Wakati huo huo wafuasi wa Yesu wakarudi toka mjini. Nao walishangaa kwa sababu walimwona Yesu akiongea na mwanamke. Lakini hakuna aliyemwuliza yule mwanamke, “Unataka nini?” Wala Yesu, “Kwa nini unaongea naye?”

28 Yule mwanamke akauacha mtungi wake wa maji na kurudi mjini. Akawaambia watu kule, 29 “Mwanaume mmoja amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya. Njooni mkamwone. Inawezekana yeye ndiye Masihi.” 30 Hivyo wale watu wakatoka mjini wakaenda kumwona Yesu!

31 Wakati huyo mwanamke akiwa mjini, wafuasi wa Yesu wakamsihi Bwana wao wakamwambia, “Mwalimu, ule chakula chochote.”

32 Lakini Yesu akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkijui.”

33 Hapo wafuasi wake wakaulizana, “Kwani kuna mtu yeyote hapa aliyemletea chakula mapema?”

34 Yesu akasema, “Chakula changu ni kuimaliza kazi ile ambayo aliyenituma amenipa niifanye. 35 Mnapopanda mimea, huwa mnasema, ‘Bado miezi minne ya kusubiri kabla ya kuvuna mazao.’ Lakini mimi ninawaambia, yafumbueni macho yenu na kuyaangalia mashamba. Sasa yako tayari kuvunwa. 36 Hata sasa, watu wanaovuna mazao wanalipwa. Wanawaleta ndani wale watakaoupata uzima wa milele. Ili kwamba watu wanaopanda waweze kufurahi wakati huu pamoja na wale wanaovuna. 37 Ni kweli tunaposema, ‘Mtu mmoja hupanda, lakini mwingine huvuna mazao.’ 38 Mimi niliwatuma kukusanya mazao ambayo ninyi hamkuyahangaikia. Wengine waliyahangaikia, nanyi mnapata faida kutokana na juhudi na kazi yao.”

39 Wasamaria wengi katika mji huo wakamwamini Yesu. Wakaamini kutokana na yale ambayo walisikia yule mwanamke akiwaambia juu ya Yesu. Aliwaambia, “Yeye amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya.” 40 Wasamaria wakaenda kwa Yesu. Wakamsihi akae pamoja nao. Naye akakaa nao kwa siku mbili. 41 Watu wengi zaidi wakamwamini Yesu kutokana na mambo aliyoyasema.

42 Watu hao wakamwambia mwanamke, “Mwanzoni tulimwamini Yesu kutokana na jinsi ulivyotueleza. Lakini sasa tunaamini kwa sababu tumemsikia sisi wenyewe. Sasa tunajua kwamba hakika Yeye ndiye atakayeuokoa ulimwengu.”

Yesu Amponya Mwana wa Afisa

(Mt 8:5-13; Lk 7:1-10)

43 Siku mbili baadaye Yesu akaondoka na kwenda Galilaya. 44 (Yesu alikwishasema mwanzoni kwamba nabii huwa haheshimiwi katika nchi yake.) 45 Alipofika Galilaya, watu wa pale walimkaribisha. Hao walikuwepo kwenye sikukuu ya Pasaka kule Yerusalemu na waliona kila kitu alichofanya huko.

46 Naye Yesu akaenda tena kutembelea Kana huko Galilaya. Kana ni mahali alikoyabadili maji kuwa divai. Mmoja wa maafisa muhimu wa mfalme alikuwa anaishi katika mji wa Kapernaumu. Mwanawe afisa huyu alikuwa mgonjwa. 47 Afisa huyo akasikia kwamba Yesu alikuwa amekuja kutoka Uyahudi na sasa yuko Galilaya. Hivyo akamwendea Yesu na kumsihi aende Kapernaumu kumponya mwanawe, aliyekuwa mahututi sana. 48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu ni lazima muone ishara zenye miujiza na maajabu kabla ya kuniamini.”

49 Afisa wa mfalme akasema, “Bwana, uje kabla mwanangu mdogo hajafa.”

50 Yesu akajibu, “Nenda, mwanao ataishi.”

Mtu huyo akayaamini maneno Yesu aliyomwambia na akaenda nyumbani. 51 Akiwa njiani kwenda nyumbani watumishi wake wakaja na kukutana naye. Wakasema, “Mwanao ni mzima.”

52 Mtu huyo akauliza, “Ni wakati gani mwanangu alipoanza kupata nafuu?”

Wakajibu, “Ilikuwa jana saa saba mchana homa ilipomwacha.”

53 Baba yake akatambua kuwa saa saba kamili ulikuwa ndiyo ule wakati aliposema, “Mwanao ataishi.” Hivyo afisa huyo na kila mmoja katika nyumba yake wakamwamini Yesu.

54 Huo ulikuwa muujiza wa pili ambao Yesu aliufanya baada ya kufika kutoka Uyahudi na Galilaya.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International