Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Yohana 1

Yesu ni Neno la Mungu la Milele

Mwanzoni Kabla ulimwengu haujaumbwa
    alikuwepo Neno.[a]
Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu,
    na Neno alikuwa Mungu.
Alikuwepo pamoja na Mungu
    toka mwanzo.
Kila kitu kilifanyika kupitia kwake.
    Hakuna chochote katika uumbaji wa Mungu
    kilichofanyika bila yeye.
Ndani yake Neno kulikuwemo na uzima,
    na uzima huo ulikuwa nuru
    kwa ajili ya watu wa ulimwenguni.
Nuru[b] hiyo yamulika gizani,
    na giza halikuishinda.[c]

Alikuwepo mtu aliyeitwa Yohana, aliyetumwa na Mungu. Alikuja kuwaambia watu kuhusu nuru. Ili kupitia kwake watu wote waweze kusikia kuhusu yule aliye nuru na wamwamini. Yohana mwenyewe hakuwa nuru. Lakini alikuja kuwaambia watu kuhusu nuru.

Nuru ya kweli,
    anayeleta mwangaza kwa watu wote,
    alikuwa tayari kuonekana kwa ulimwengu.
10 Huyo Neno alikuwapo tayari ulimwenguni.
    Ulimwengu uliumbwa kupitia yeye,
    lakini ulimwengu haukumkubali.
11 Alikuja kwa ulimwengu ulio wake,
    na watu wake mwenyewe hawakumkubali.
12 Lakini baadhi ya watu walimkubali wakamwamini
    na akawapa haki ya kuwa watoto wa Mungu.
13 Ndiyo, walikuwa watoto wa Mungu,
    lakini si kwa kuzaliwa kimwili.
Haikuhusisha matamanio
    ya kibinadamu.
Mungu mwenyewe aliwafanya
    kuwa watoto wake.
14 Neno akafanyika kuwa mwanadamu
    na akaishi pamoja nasi.
Tuliouna ukuu wa uungu wake;
    utukufu alionao Mwana pekee wa Baba.

15 Yohana alizungumza kuhusu yeye alipopaza sauti na kusema, “Huyu ndiye niliyemzungumzia habari zake niliposema, ‘Anayekuja baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa sababu alikuwepo mwanzoni, zamani kabla sijazaliwa.’”

16 Alikuwa amejaa neema na kweli ya Mungu,
    tulipokea kutoka baraka moja
    baada ya nyingine[d] kutoka kwake.
17 Hiyo ni kusema kuwa,
    sheria ililetwa kwetu kupitia Musa.
Lakini neema na kweli imekuja
    kupitia Yesu Kristo.
18 Hakuna aliyewahi kumwona Mungu
    isipokuwa Mwana peke yake,
ambaye yeye mwenyewe ni Mungu,
    ametuonesha jinsi Mungu alivyo.
Yuko karibu sana na Baba
    kiasi kwamba tunapomwona,
    tumemwona Mungu.

Yohana Azungumza Juu ya Kristo

(Mt 3:1-12; Mk 1:1-8; Lk 3:1-9,15-17)

19 Viongozi wa Kiyahudi kule Yerusalemu walituma baadhi ya makuhani na Walawi kwa Yohana kumwuliza, “Wewe ni nani?” Yohana akawaeleza kweli. 20 Akajibu kwa wazi bila kusitasita, “Mimi siyo Masihi.”

21 Wakamwuliza, “Sasa wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?”

Yohana akawajibu, “Hapana, mimi siye Eliya.”

Wakamwuliza tena, “Je, wewe ni Nabii?”[e]

Naye akawajibu, “Hapana, mimi siyo nabii.”

22 Kisha wakamwuliza, “Wewe ni nani basi? Tueleze habari zako. Tupe jibu la kuwaambia wale waliotutuma. Unajitambulisha mwenyewe kuwa nani?”

23 Yohana akawaambia maneno ya nabii Isaya:

“‘Mimi ni mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
    Nyoosheni njia kwa ajili ya Bwana.’”(A)

24 Wale Wayahudi walitoka kwa Mafarisayo. 25 Wakamwambia Yohana, “Unasema kuwa wewe siyo Masihi. Na unasema kuwa wewe siyo Eliya wala nabii. Sasa kwa nini unawabatiza watu?”

26 Yohana akajibu, “Nawabatiza watu kwa maji. Lakini yupo mtu hapa kati yenu ambaye ninyi hamumjui. 27 Yeye ndiye yule anayekuja baada yangu. Nami sina sifa za kuwa mtumwa anayefungua kamba za viatu vyake.”

28 Mambo haya yote yalitokea Bethania iliyokuwa upande mwingine wa Mto Yordani. Hapa ndipo Yohana alipowabatiza watu.

Yesu, Mwanakondoo wa Mungu

29 Siku iliyofuata Yohana akamwona Yesu akija kwake na kusema, “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu mwenye kuondoa dhambi za ulimwengu.” 30 Huyu ndiye niliyezungumza habari zake niliposema, “Kuna mtu anayekuja baada yangu aliye mkuu zaidi yangu, kwa sababu yeye aliishi muda mrefu kabla ya kuzaliwa kwangu.” 31 Nami sikumjua yeye ni nani. Lakini nilikuja kuwabatiza watu kwa maji ili watu wa Israeli waelewe kuwa huyo ndiye Masihi.

32-34 Kisha Yohana akasema maneno yafuatayo ili kila mtu asikie, “Mimi pia sikujua nani hasa alikuwa Masihi. Lakini yule aliyenituma kubatiza aliniambia, ‘Utamwona Roho akishuka na kutua kwa mtu. Huyo ndiye atakayewabatiza watu kwa Roho Mtakatifu.’ Nami nimeyaona haya yakitokea. Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama njiwa na kutulia juu ya mtu huyu. Hivyo haya ndiyo ninayowaambia watu: ‘Yeye huyo ndiye Mwana wa Mungu.’”[f]

Wafuasi wa Kwanza wa Yesu

35 Siku iliyofuata Yohana alirejea tena mahali hapo pamoja na wafuasi wake wawili. 36 Naye akamwona Yesu akitembea, hivyo akasema, “Angalieni, Mwanakondoo wa Mungu!”

37 Wale wafuasi wake wawili walimsikia Yohana akisema haya, basi wakaondoka na kumfuata Yesu. 38 Yesu aligeuka na kuwaona watu wawili wakimfuata. Akawauliza, “Mnataka nini?” Nao wakajibu wakimwuliza, “Rabi, unakaa wapi?” (Rabi tafsiri yake ni Mwalimu.)

39 Yesu akajibu, “Njooni tufuatane pamoja nanyi mtapaona ninapokaa.” Hivyo wale watu wawili wakaenda pamoja naye. Wakaona mahali alipokuwa anakaa, nao wakashinda huko pamoja naye mchana wote. Hiyo ilikuwa ni saa kumi ya jioni.

40 Watu hawa wakamfuata Yesu baada ya kusikia habari zake kutoka kwa Yohana. Mmoja wao alikuwa Andrea, nduguye Simoni Petro.

41 Kitu cha kwanza alichokifanya Andrea kilikuwa ni kwenda kumtafuta ndugu yake Simoni. Andrea alipompata nduguye akamwambia, “Tumemwona Masihi.” (Masihi tafsiri yake ni Kristo.) 42 Kisha Andrea akamleta Simoni nduguye kwa Yesu. Yesu akamtazama, na kumwambia, “Wewe ndiwe Simoni, mwana wa Yohana. Basi utaitwa Kefa.” (“Kefa” tafsiri yake ni “Petro”.[g])

43 Kesho yake Yesu akaamua kwenda Galilaya. Huko alikutana na Filipo na kumwambia, “Nifuate.” 44 Filipo alikuwa mwenyeji wa mji wa Bethsaida, kama alivyokuwa Andrea na Petro. 45 Filipo akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona mtu ambaye habari zake ziliandikwa na Musa katika sheria. Pia Manabii waliandika habari juu ya mtu huyu. Yeye ni Yesu, mwana wa Yusufu. Naye anatoka mjini Nazareti!”

46 Lakini Nathanaeli akamwambia Filipo, “Nazareti! Je, inawezakana kupata kitu chochote chema kutoka Nazareti?”

Filipo akajibu, “Njoo uone.”

47 Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake na papo hapo akasema, “Mtu huyu anayekuja ni Mwisraeli halisi, ambaye unayeweza kumwamini.”[h]

48 Nathanaeli akamwuliza Yesu, “Umenifahamu kwa namna gani?”

Yesu akamjibu, “Nilikuona pale ulipokuwa chini ya mtini,[i] kabla Filipo hajakueleza habari zangu.”

49 Kisha Nathanaeli akasema, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Nawe ni mfalme wa Israeli.” 50 Yesu akamwambia, “Je, umeyaamini haya kwa sababu nimekwambia kuwa nilikuona chini ya mtini? Utaona mambo makubwa zaidi ya haya.” 51 Kisha akasema, “Mniamini ninapowaambia kwamba mtaziona mbingu zimefunguka. Na mtawaona, ‘Malaika wa Mungu wakipanda juu na kushuka chini’[j] kwa ajili Mwana wa Adamu.”

Arusi Katika Mji wa Kana

Siku tatu baadaye kulikuwa na arusi katika mji wa Kana huko Galilaya, mama yake Yesu naye pia alikuwapo. Yesu na wafuasi wake nao walialikwa. Hapo arusini divai ilipungua, mama yake Yesu akamwambia mwanaye, “Hawana divai ya kutosha.”

Yesu akajibu, “Mama, kwa nini unaniambia mambo hayo? Wakati sahihi kwangu kufanya kazi haujafika bado.”

Mama yake akawaambia wahudumu wa arusi, “Fanyeni lo lote lile atakalowaambia.”

Mahali hapo ilikuwepo mitungi mikubwa sita iliyotengenezwa kwa mawe iliyotumiwa na Wayahudi katika desturi yao maalumu ya kunawa.[k] Kila mtungi mmoja ulikuwa na ujazo wa lita 80 au 120.[l]

Yesu akawaambia wale wahudumu, “Ijazeni maji hiyo mitungi.” Nao wakaijaza maji mpaka juu.

Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kiasi na mumpelekee mkuu wa sherehe.” Nao wakafanya kama walivyoambiwa. Mkuu wa sherehe akayaonja yale maji, ambayo tayari yamegeuka na kuwa divai. Naye hakujua wapi ilikotoka hiyo divai, bali wahudumu walioleta yale maji wao walijua. Akamwita bwana arusi 10 na kumwambia, “Watu wanapoandaa huleta kwanza divai iliyo bora zaidi. Baadaye, wageni wanapokuwa wametosheka, huleta divai iliyo na ubora pungufu. Lakini wewe umeandaa divai bora zaidi hadi sasa.”

11 Ishara hii ilikuwa ya kwanza aliyoifanya Yesu katika mji wa Kana ya Galilaya. Kwa hili Yesu alionesha ukuu wake wa kimungu, na wafuasi wake wakamwamini.

12 Kisha Yesu akashuka kwenda katika mji wa Kapernaumu. Mama yake, ndugu zake, na wafuasi wake nao walienda pamoja naye. Wote wakakaa huko kwa siku chache.

Yesu Asafisha Eneo la Hekalu

(Mt 21:12-13; Mk 11:15-17; Lk 19:45-46)

13 Kipindi hicho wakati wa kusherehekea Pasaka ya Wayahudi ulikaribia, hivyo ikampasa Yesu kwenda Yerusalemu. 14 Katika eneo la Hekalu aliwaona watu wakiuza ng'ombe, mbuzi na njiwa. Aliwaona wengine wakikalia meza na kufanya biashara ya kubadili fedha za watu. 15 Yesu akatengeneza kiboko kwa kutumia vipande vya kamba. Kisha akawafukuza watu wote, kondoo na ng'ombe watoke katika eneo la Hekalu. Akazipindua meza za wafanya biashara wa kubadilisha fedha na kuzitawanya fedha zao. 16 Baada ya hapo akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, “Viondoeni humu vitu hivi! Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa kununua na kuuza!”

17 Haya yaliwafanya wafuasi wake kukumbuka maneno yaliyoandikwa kwenye Maandiko: “Upendo wangu mkuu kwa Hekalu lako utaniangamiza.”(B)

18 Baadhi ya Wayahudi wakamwambia Yesu, “Tuoneshe muujiza mmoja kama ishara kutoka kwa Mungu. Thibitisha kwamba unayo haki ya kufanya mambo haya.”

19 Yesu akajibu, “Bomoeni hekalu hili nami nitalijenga tena kwa muda wa siku tatu.” 20 Wakajibu, “Watu walifanya kazi kwa miaka 46 kulijenga Hekalu hili! Je, ni kweli unaamini kwamba unaweza kulijenga tena kwa siku tatu?”

21 Lakini Yesu aliposema “hekalu hili”, alikuwa anazungumzia mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka katika wafu, wafuasi wake wakakumbuka kwamba alikuwa ameyasema hayo. Hivyo wakayaamini Maandiko, na pia wakayaamini yale aliyoyasema Yesu.

23 Yesu alikuwa Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. Watu wengi wakamwamini kwa sababu waliona ishara na miujiza alioitenda. 24 Lakini Yesu hakuwaamini wao, kwa sababu alijua jinsi watu wote wanavyofikiri. 25 Hakuhitaji mtu yeyote amwambie jinsi mtu fulani alivyo. Kwa sababu alikwishamjua tayari.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International