Beginning
Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
(Mt 19:1-12)
10 Naye aliondoka mahali pale, na kufika katika nchi ya Uyahudi ng'ambo ya Mto Yordani. Na makundi ya watu wakamjia tena na kama alivyofanya daima aliwafundisha.
2 Kisha baadhi ya Mafarisayo walimwendea na kumwuliza “Je, ni sahihi mtu kumtaliki mkewe?” Nao walimwuliza hivyo ili kumjaribu.
3 Yesu akawajibu, “Musa aliwapa amri mfanye nini?”
4 Wakasema, “Musa alimpa ruhusa mume kuandika hati ya kutangua ndoa[a] na kisha kumtaliki mke wake.”
5 Yesu akawaambia, “Musa aliwaandikia amri hii kwa sababu ninyi ni wakaidi na hamkutaka kuyapokea mafundisho ya Mungu. 6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji wake Mungu ‘aliwaumba mwanaume na mwanamke’.(A) 7 ‘Basi kwa sababu ya hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, na kujiunga na mkewe. 8 Na hao wawili wataungana pamoja na kuwa mwili mmoja.’(B) Nao si wawili tena bali ni mwili mmoja. 9 Kwa hiyo, mtu yeyote asitenganishe kile ambacho Mungu amekiunganisha pamoja.”
10 Walipokuwa ndani ya nyumba ile kwa mara nyingine, wanafunzi wake wakamwuliza Yesu juu ya jambo hili. 11 Naye akawaambia, “yeyote atakayemtaliki mke wake na kuoa mwanamke mwingine, anazini kinyume cha mkewe. 12 Na ikiwa mke atamtaliki[b] mumewe na kuolewa na mume mwingine, basi naye anafanya zinaa.”[c]
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mt 19:13-15; Lk 18:15-17)
13 Nao watu wakawaleta watoto wadogo kwa Yesu, ili aweze kuwawekea mikono na kuwabariki. Hata hivyo wanafunzi wake waliwakemea. 14 Yesu alipoona hayo, alikasirika, na akawaambia, “Waruhusuni watoto hao waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu kama hao. 15 Ninawaambia kweli, Yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyoupokea hataweza kuingia ndani yake.” 16 Naye Yesu akawakumbatia watoto kifuani mwake na akaweka mikono yake juu yao na kuwabariki.
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mt 19:16-30; Lk 18:18-30)
17 Na alipokuwa ameanza safari, mtu mmoja alimkimbilia, akafika na kupiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?
18 Yesu akamwuliza, kwa nini unaniita mimi mwema? Hakuna aliye mwema isipokuwa Mungu peke yake. 19 Je, unazijua amri: Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo, usidanganye wengine, uwaheshimu baba na mama yako.”(C)
20 Naye akamwambia Yesu, “Mwalimu, nimeyatii hayo tangu ujana wangu.”
21 Yesu akamwangalia. Naye akashikwa na upendo kwa mtu yule, na hivyo akamwambia, “umekosa kitu kimoja: Nenda ukaviuze vyote ulivyo navyo kisha ukawape walio maskini, nawe utakuwa umejitunzia hazina mbinguni. Kisha uje ukanifuate.”
22 Yule mtu alisikitishwa sana na usemi huo, na akaondoka kwa huzuni kwa kuwa alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu aligeuka kuwatazama wanafunzi wake na kuwaambia wake, “Angalieni jinsi ilivyo vigumu sana kwa walio na mali nyingi kuingia katika ufalme wa Mungu.”
24 Wanafunzi wake walistaajabishwa na maneno yale. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, ni vigumu[d] sana kuuingia ufalme wa Mungu. 25 Kwani ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuuingia ufalme wa Mungu.”
26 Nao walistajaabu zaidi, na wakaambiana wao kwa wao, “Ni nani basi atakayeweza kuokolewa?”
27 Huku akiwatazama, Yesu alisema, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, lakini kwa Mungu linawezekana, kwa sababu yote yanawezekana kwake Mungu.”
28 Petro akaanza kumwambia, “Tazama! Tumeacha kila kitu tukakufuata.”
29 Yesu akasema, “Nawaambieni kweli: Hakuna aliyeacha nyumba, kaka, dada, mama, baba, watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili 30 ambaye hatapata malipo mara mia zaidi katika nyakati hizi; nyumba, kaka, dada, mama, watoto, na mashamba, pamoja na mateso; na uzima wa milele katika kizazi kinachokuja. 31 Lakini wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho baadaye na wale walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza baadaye.”
Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake
(Mt 20:17-19; Lk 18:31-34)
32 Walikuwa wote njiani wakipanda kuelekea Yerusalemu, na Yesu alikuwa akitembea mbele yao. Nao walisumbuka sana. Na wale waliowafuata walikuwa na hofu pia. Kwa mara nyingine Yesu akawachukua wale wanafunzi kumi na mbili pembeni, na akaanza kuwaeleza yale yatakayomtokea Yerusalemu. 33 “Sikilizeni! Tunaelekea hadi Yerusalemu na Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria, nao watamtia hatiani na kumpa hukumu kifo, kisha watamtoa kwa wale wasio Wayahudi, 34 Nao watamdhihaki, na watamtemea mate, na watamchapa kwa viboko vya ngozi, nao watamwua. Ndipo atafufuka baada ya siku ya tatu.”
Yakobo na Yohana Waomba Kutawala Pamoja na Yesu
(Mt 20:20-28)
35 Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, walimwendea Yesu, wakamwambia, “Mwalimu tunataka utufanyie kile tunachokuomba.”
36 Yesu akawaambia, “Ni kitu gani mnachotaka niwafanyie?”
37 Nao wakamwambia, “Uturuhusu tuketi pamoja nawe katika utukufu wako, mmoja wetu aketi kulia kwako na mwingine kushoto kwako.”
38 Yesu akawaambia, “Hamjui mnachokiomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninachokinywea[e] mimi? Au mnaweza kubatizwa ubatizo ninaobatizwa?”
39 Wakamwambia, “Tunaweza.”
Kisha Yesu akawaambia, “Mtakinywa kikombe cha mateso ninachokunywa mimi, na mtabatizwa ubatizo[f] ninaobatizwa mimi. 40 Lakini kuhusu kuketi kulia kwangu ama kushoto kwangu siyo mamlaka yangu kusema. Mungu ameandaa nafasi hizo kwa ajili ya wale aliowateuwa.”
41 Wale wanafunzi kumi wengine walipoyasikia maombi haya, waliwakasirikia Yakobo na Yohana. 42 Na Yesu akawaita wale wanafunzi kumi na kusema, “Mnajua kuwa miongoni mwa mataifa watawala huwa na mamlaka makubwa juu ya watu, na viongozi wenye nguvu huwakandamiza watu wao. 43 Haipaswi kuwa hivyo miongoni mwenu. Kwani yeyote atakaye kuwa mkuu miongoni mwenu basi na awe mtumishi wenu. 44 Yeyote anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima akubali kuwa mtumwa wenu wote. 45 Kwani hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa bali alikuja kuwatumikia wengine na kuyatoa maisha yake ili kuwaweka huru wengi.”
Yesu Amponya Asiyeona
(Mt 20:29-34; Lk 18:35-43)
46 Kisha wakafika Yeriko. Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati wa watu, Bartimayo mwana wa Timayo, ombaomba asiyeona, alikuwa amekaa kando ya barabara. 47 Aliposikia kwamba huyo alikuwa ni Yesu wa Nazareti, alianza kupiga kelele na kusema, “Yesu Mwana wa Daudi, unihurumie!”
48 Na watu wengi walimkemea na kumwambia anyamaze kimya. Lakini yeye alipiga kelele kwa sauti kubwa zaidi na kusema, “Mwana wa Daudi, unihurumie!”
49 Kwa hiyo Yesu akasimama na kusema, “Hebu mwiteni.”
Nao wakamwita yule mtu asiyeona na kumweleza, “Jipe moyo mkuu! Inuka! Yesu anakuita.” 50 Naye akalitupa joho lake, akaruka juu, na akamwendea Yesu.
51 Naye Yesu akamwambia, “Unataka nikufanyie nini?”
Yule mtu asiyeona akamwambia, “Mwalimu, nataka kuona tena.”
52 Hivyo Yesu akamwambia, “Nenda! Imani yako imekuponya.”[g] Na mara akaweza kuona tena, na akamfuata Yesu barabarani.
Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mt 21:1-11; Lk 19:28-40; Yh 12:12-19)
11 Walipokaribia Yerusalemu walifika eneo la Bethfage na Bethania lililo karibu na Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, 2 na kuwaagiza, “Mwende katika kijiji kilichopo ngambo yenu kule, na mara tu mtakapoingia ndani yake mtakuta mwana punda amefungwa mahali na ambaye hajawahi kupandwa na mtu yeyote. Mfungueni na kisha mumlete hapa. 3 Na mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnafanya hivi?’ ninyi mseme, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha kwenu mara moja.’”
4 Hivyo wakaondoka, nao wakamkuta mwana punda huyo amefungwa katika mtaa wa wazi karibu na mlango. Wakamfungua. 5 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu na mahali pale wakawaambia, “Je, kwa nini mnamfungua mwana punda huyo?” 6 Wanafunzi wake wakawaeleza yale walioambiwa na Yesu wayaeleze, nao wakawaacha waende zao.
7 Kisha wakamleta mwana punda yule kwa Yesu na wakaweka mavazi yao ya ziada juu ya mwana punda, naye akampanda na kukaa juu yake. 8 Watu wengi wakatandika makoti yao barabarani, na wengine wakatandika matawi waliyoyakata kwenye mashamba yaliyo jirani. 9 Wote wale waliotangulia mbele na wale waliofuata walipiga kelele kwa shangwe,
“‘Msifuni[h] Mungu!
Mungu ambariki yeye
anayekuja katika Jina la Bwana!’(D)
10 Mungu aubariki ufalme unaokuja,
ufalme wa Daudi baba yetu!
Msifuni Mungu juu mbinguni!”
11 Ndipo Yesu aliingia Yerusalemu na kwenda hadi kwenye eneo la Hekalu akizunguka na kutazama kila kitu kilichokuwepo mahali hapo. Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana, aliondoka kwenda Bethania akiwa na wanafunzi wake kumi na wawili.
Yesu Aulaani Mtini
(Mt 21:18-19)
12 Siku iliyofuata, walipokuwa wakiondoka Bethania, Yesu akawa na njaa. 13 Na kutokea mbali akauona mti wa mtini umefunikwa kwa matawi yake mengi, hivyo akausogelea karibu ili kuona kama atakuta tunda lolote juu yake. Lakini alipoufikia hakukuta tunda lolote isipokuwa matawi tu kwani hayakuwa majira ya mitini kuwepo katika mti. 14 Akauambia mtini ule, “Mtu yeyote asile matunda kutoka kwako kamwe milele!” Na wanafunzi wake waliyasikia hayo maneno.
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mt 21:12-17; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)
15 Walipofika Yerusalemu waliingia katika viwanja vya Hekalu. Yesu akaanza kuwafukuza nje wale waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza na kununua katika eneo la Hekalu. Akapindua meza za wabadilishaji wa fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 16 Pia hakumruhusu mtu yeyote abebe kitu chochote kukatiza eneo la Hekalu. 17 Yesu akaanza kuwafundisha na kuwaeleza, “Je, haikuandikwa katika Maandiko kwamba: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ambapo watu wa mataifa yote wataleta maombi yao kwangu’?(E) Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘mahali pa wezi kujificha.’(F)”
18 Na viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria waliyasikia haya, na hivyo wakaanza kutafuta njia ya kumuua. Kwani walimwogopa, kwa sababu watu wote walikuwa wamestaajabishwa na mafundisho yake. 19 Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka Yerusalemu.
Mtini na Imani, Maombi na Msamaha
(Mt 21:20-22)
20 Ilipofika asubuhi Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakitembea pamoja na wakauona ule mti wa mtini umekauka kuanzia kwenye mizizi yake. 21 Petro akakumbuka yale Yesu aliyosema kwa mti huo na kumwambia, “Mwalimu, tazama! Mti ule wa mtini ulioulaani umenyauka kabisa.”
22 Yesu akawajibu, “Mnapaswa kuweka imani yenu kwa Mungu. 23 Nawaambia kweli: Yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ukajitupe katika bahari’; kama asipokuwa na mashaka moyoni mwake, Lakini akaamini kuwa kile anachokisema kitatokea, huyo atatendewa hayo. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia chochote mtakachoomba katika sala, muamini kwamba mmekipokea na haja mliyoiomba nayo itakuwa yenu, 25 Na wakati wowote mnaposimama kuomba, mkiwa na neno lolote kinyume na mtu mwingine, mmsamehe mtu huyo. Na Baba yenu aliye mbinguni naye atawasamehe ninyi dhambi zenu.” 26 [i]
Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mt 21:23-27; Lk 20:1-8)
27 Yesu na wanafunzi wake walirudi Yerusalemu. Na walipokuwa wakitembea ndani ya viwanja vya Hekalu, viongozi wa makuhani, walimu wa Sheria na wazee walimjia Yesu 28 na kumwuliza, “Kwa mamlaka gani unafanya vitu hivi? Nani alikupa mamlaka ya kuvifanya?”
29 Yesu akawaambia, “Nitawauliza swali, na mkinijibu, ndipo nitawaeleza kwa mamlaka gani ninafanya vitu hivi. 30 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni ama ulitoka kwa watu? Sasa mnijibu basi.”
31 Walijadiliana wao kwa wao wakisema, “Tukisema ‘ulitoka mbinguni’, atasema, ‘Kwa nini basi hamumuamini?’ 32 Lakini kama tukisema kuwa ubatizo wa Yohana ulitoka kwa wanadamu, watu watatukasirikia.” Viongozi waliwaogopa watu, kwani watu wote waliamini kuwa Yohana kweli alikuwa nabii.
33 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatufahamu.”
Hivyo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”
© 2017 Bible League International