Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Marko 8-9

Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000

(Mt 15:32-39)

Wakati mwingine katika siku zile kundi kubwa la watu lilikusanyika na halikuwa na chakula. Yesu akawaita wanafunzi wake na kuwaambia, “Nawahurumia watu hawa, kwa sababu hata sasa wamekuwa nami kwa siku tatu, na hawana kitu cha kula.”

Nikiwaacha waende majumbani mwao wakiwa na njaa, wataanguka njiani; na baadhi yao wametoka mbali.

Wanafunzi wake wakamjibu, “Wapi mtu yeyote atapata chakula cha kutosha mahali hapa jangwani cha kuwalisha watu hawa?”

Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakajibu, “Saba.”

Kisha Yesu akaliagiza kundi la watu kuketi chini ardhini Akachukua mikate ile saba, akashukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake waigawe. Nao wakaigawa kwenye kundi. Kulikuwapo pia samaki wadogo wachache. Yesu akawabariki wale samaki na kuwaambia waigawe nayo pia.

Watu walikula na kushiba. Wakakusanya vikapu saba vilivyojaa mabaki. Ilikuwa kama watu 4,000. Kisha Yesu akawaacha waende. 10 Mara Yesu akapanda katika mashua na wanafunzi wake, na akafika katika wilaya ya Dalmanutha.

Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu

(Mt 16:1-4; Lk 11:16,29)

11 Mafarisayo wakamwendea Yesu na kuanza kubishana naye. Ili kumjaribu wakamwomba ishara kutoka mbinguni. 12 Yesu alihema kwa nguvu na kusema, “Kwa nini kizazi kinataka ishara? Ninawaambia ukweli: hakuna ishara itakayooneshwa kwa kizazi hiki.” 13 Kisha Yesu akawaacha, akapanda tena katika mashua, na akaondoka kwenda upande wa pili wa ziwa.

Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu

(Mt 16:5-12)

14 Wakati huo huo wanafunzi walikuwa wamesahau kuleta mikate yo yote, na hawakuwa na kitu kingine isipokuwa mkate mmoja. 15 Yesu akawaonya, akasema, “Mwe mwangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ile ya Herode.”

16 Nao wakaanza kujadiliana haya miongoni mwao: “Labda alisema hivi kwa sababu hatukuwa na mkate wowote.”

17 Akijua walichokuwa wakikisema, akawaambia, “Kwa nini mnajadiliana juu ya kutopata mkate? Je! Bado hamwoni na kuelewa? Je! Mmezifunga akili zenu. 18 Mnayo macho; Je! Hamwoni? Mnayo masikio; Je! Hamwezi kusikia? Mnakumbuka? 19 Nilipomega na kugawa mikate mitano kwa watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”

Wakasema “Kumi na viwili”.

20 “Nilipomega na kugawa mikate saba kwa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa masalia ya mikate?”

Wakasema “Saba”.

21 Kisha akawaambia, “Bado hamwelewi?”

Yesu Amponya Kipofu katika Kijiji cha Bethsaida

22 Walipofika katika kijiji cha Bethsaida, baadhi ya watu walimleta asiyeona kwa Yesu, na kumsihi Yesu amguse. 23 Yesu alimshika mkono yule asiyeona na kumtoa nje ya kijiji. Kisha Yesu alimtemea mate yule asiyeona kwenye macho yake, akaweka mkono wake juu ya asiyeona, na kumwuliza, “Je! Unaona kitu chochote?”

24 Kipofu akatazama juu na kusema, “Ninaona watu; wanaonekana kama miti inayotembea.”

25 Kisha Yesu akaweka mikono yake tena kwenye macho ya yule asiyeona. Naye akafumbua wazi macho yake yote. Kwani alipona kutokuona kwake na kuona kila kitu kwa uwazi. 26 Kisha Yesu akamwambia arudi nyumbani, na pia akamwambia, “Usiingie kijijini.”

Petro Atambua Yesu ni Nani

(Mt 16:13-20; Lk 9:18-21)

27 Yesu na wanafunzi wake walikwenda kwenye vijiji vinavyozunguka Kaisaria Filipi. Wakiwa njiani aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?”

28 Nao wakamjibu, “Yohana Mbatizaji. Wengine husema wewe ni Eliya. Na wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”

29 Kisha akawauliza wao, “Na ninyi; Je! Mnasema mimi ni nani?”

Petro akamjibu, “Wewe ni masihi.”

30 Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote kuhusu yeye.

Yesu Asema ni Lazima Afe

(Mt 16:21-28; Lk 9:22-27)

31 Ndipo alianza kuwafundisha akisema: “Mwana wa Adamu lazima apate mateso mengi, na kukatataliwa na wazee, wakuu wa makuhani na walimu wa Sheria, na ni lazima atauawa na Kufufufuka baada ya siku ya tatu.” 32 Yesu aliwaambia haya kwa uwazi bila kuwaficha.

Baada ya mafundisho haya Petro alimchukua Yesu pembeni na kuanza kumkemea. 33 Lakini Yesu aligeuka nyuma na kuwaangalia wanafunzi wake, na kumkemea Petro kwa kumwambia, “Shetani,[a] toka mbele yangu! Huyajali yale anayoyajali Mungu bali yale wanayoyaona wanadamu kuwa ni muhimu.”

34 Kisha Yesu akaliita kundi lote pamoja na wanafunzi wake kwake, akawaambia, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, lazima ajikane yeye mwenyewe, na ni lazima auchukue msalaba wake mwenyewe kisha anifuate. 35 Kwa kuwa kila anayetaka kuusalimisha uhai wake, ataupoteza, na yeyote atakayeupoteza uhai wake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili atausalimisha. 36 Itampa mtu manufaa gani akiupata ulimwengu wote kisha akaupoteza uhai wake? 37 Mtu anaweza kuubadilisha uhai wake na kitu gani? 38 Hiki ni kizazi chenye dhambi na kisichokuwa na uaminifu. Hivyo, mtu yeyote atakayenionea haya mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea haya mtu huyo siku ile atakaporudi katika utukufu wa Baba yake akiwa na malaika wake watakatifu.”

Naye Yesu aliwaambia, “Ninawaambia Ukweli: baadhi yenu mnaosimama hapa mtauona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu kabla ya kufa kwenu.”

Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya

(Mt 17:1-13; Lk 9:28-36)

Baada ya siku sita, Yesu akamchukua Petro, Yakobo na Yohana na kuwaongoza hadi mlima mrefu wakiwa peke yao tu. Na mwonekano wa Yesu ulibadilika mbele yao. Huko Yesu akabadilika sura nyingine akiwa mbele yao. Mavazi yake yakiwa na mng'ao, na meupe kabisa kuliko mtu anavyoweza kufua nguo kwa sabuni na kuitakatisha. Huko Eliya na Musa pia wakawatokea, na Yesu alizungumza na manabii hao wawili.

Petro akafungua kinywa chake na kumwambia Yesu, “Mwalimu, ni vyema tupo hapa. Tufanye basi vibanda vitatu; moja kwa ajili yako, moja kwa ajili ya Musa na moja kwa ajili ya Eliya.” Petro aliyasema haya kwa sababu hakujua aseme nini, kwa sababu yeye na wenzake walikuwa wamepata hofu.

Ndipo wingu likaja na kuwafunika wote kwa kivuli chake. Na sauti ikatoka mawinguni, ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikilizeni yeye.”

Ndipo ghafula walipokuwa wakiangalia huku na huko, hawakuona mtu yeyote akiwa pamoja nao isipokuwa Yesu peke yake.

Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote kile walichokiona mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka katika wafu.

10 Hivyo hawakuwaeleza wengine juu ya jambo lile bali walijadiliana miongoni mwao wenyewe juu ya maana ya “kufufuka kutoka kwa wafu.” 11 Wakamwuliza Yesu, “kwa nini walimu wa sheria wanasema Eliya lazima aje kwanza?”

12 Yesu akawaambia, “Ndiyo, Eliya atakuja kwanza[b] kuja kuyaweka mambo yote sawa kama jinsi yalivyokuwa hapo mwanzo. Lakini kwa nini imeandikwa juu ya Mwana wa Adamu[c] ya kwamba itampasa kuteswa na kudhalilishwa? 13 Lakini ninawaambia, Eliya amekuja,[d] na walimtendea kila kitu walichotaka, kama vile ilivyoandikwa[e] kuhusu yeye.”

Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu

(Mt 17:14-20; Lk 9:37-43a)

14 Wakati Yesu, Petro, Yakobo, na Yohana walipowafikia wanafunzi wengine, waliliona kundi kubwa la watu lililowazunguka na wakawaona walimu wa Sheria wakibishana nao. 15 Mara tu watu wote walipomwona Yesu, walishangazwa, na wakakimbia kwenda kumsalimia.

16 Akawauliza, “Mnabishana nao kitu gani?”

17 Na mtu mmoja kundini alimjibu, “Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako ili umponye. Yeye amefungwa na pepo mbaya anayemfanya asiweze kuzungumza. 18 Na kila mara anapomshambulia humtupa chini ardhini. Naye hutokwa mapovu mdomoni na kusaga meno yake, huku akiwa mkakamavu. Nami niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze kutoka ndani yake, lakini hawakuweza.”

19 Kisha Yesu akajibu na kuwaambia, “ninyi kizazi kisichoamini, kwa muda gani niwe pamoja nanyi? Kwa muda gani nitapaswa kuchukuliana nanyi? Mleteni huyo mvulana kwangu.”

20 Wakamleta yule mvulana kwake. Na yule pepo alipomwona Yesu, kwa ghafula akamtingisha yule mvulana ambaye alianguka chini kwenye udongo, akivingirika na kutokwa povu mdomoni.

21 Yesu akamwuliza babaye, “Kwa muda gani amekuwa katika hali hii?”

Yule babaye akajibu akisema, “amekuwa katika hali hii tangu utoto. 22 Mara nyingi anamtupa katika moto ama katika maji ili kumwua. Lakini ikiwa unaweza kufanya kitu chochote, uwe na huruma na utusaidie.”

23 Yesu akamwambia, “Una maana gani kusema ‘ikiwa unaweza’? Kila kitu kinawezekana kwake yeye anayeamini.”

24 Mara, babaye yule mvulana alilia kwa sauti kubwa na kusema, “Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu.”

25 Yesu alipoona lile kundi likizidi kuwa kubwa, alimkemea yule pepo mchafu na kumwambia, “Wewe pepo uliyemfanya mvulana huyu asiweze kusikia na asiweze kusema, nakuamuru, utoke ndani yake, na usimwingie tena!”

26 Na pepo yule alilia kwa sauti, akamtupa yule mvulana chini katika mishituko ya kutisha, kisha akatoka, naye akawa kama mtu aliyekufa, kiasi kwamba watu wengi wakadhani ya kuwa amekufa. 27 Lakini Yesu akamshika yule mvulana mikononi, na kumwinua naye akasimama.

28 Baada ya Yesu kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuuliza wakiwa peke yao, “Kwa nini sisi hatukuweza kumfukuza pepo yule?”

29 Naye akawaambia, “Aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa maombi.”[f]

Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake

(Mt 17:22-23; Lk 9:43-45)

30 Wakaondoka mahali pale na kusafiri kupitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote kujua walikuwa huko, 31 alitaka kuwafundisha wanafunzi wake peke yake. Na Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kuwekwa mikononi mwa watu wengine, nao watamwua. Kisha siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32 Lakini hawakuuelewa usemi huu, na walikuwa wanaogopa kumuuliza zaidi.

Nani ni Mkuu Zaidi?

(Mt 18:1-5; Lk 9:46-48)

33 Kisha wakaja Kapernaumu. Na Yesu alipokuwa ndani ya nyumba aliwauliza, “Je, mlikuwa mnajidiliana nini njiani?” 34 Lakini wao walinyamaza kimya, kwa sababu njiani walikuwa wamebishana juu ya nani kati yao alikuwa ni mkuu zaidi.

35 Hivyo Yesu aliketi chini, akawaita wale kumi na mbili, na akawaambia, “Ikiwa yupo mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, inapasa basi awe wa mwisho kuliko wote na mtumishi wa wote.”

36 Akamchukua mtoto mdogo mikononi mwake na kumsimamisha mbele yao. Akimkumbatia mtoto huyo, Yesu alisema, 37 “Yeyote atakayemkaribisha mtoto mdogo kama huyu hapa kwa sababu ya jina langu basi ananikaribisha na mimi pia. Yeyote anayenikubali mimi hanikubali mimi tu bali anamkubali pia yeye aliyenituma.”

Yeyote Ambaye Hayuko Kinyume Chetu Yuko Pamoja Nasi

(Lk 9:49-50)

38 Yohana akamwambia Yesu, “Mwalimu tulimwona mtu akifukuza pepo kwa jina lako. Nasi tulijaribu kumzuia, kwa sababu hakuwa mmoja wetu.”

39 Lakini Yesu akawaambia, “Msimzuie, kwa sababu hakuna atendaye miujiza kwa jina langu kisha mara baada ya hilo aseme maneno mabaya juu yangu. 40 Yeye ambaye hapingani na sisi basi yuko pamoja na sisi. 41 Yeyote anayewapa ninyi kikombe cha maji kwa sababu ninyi ni wake Kristo.[g] Hakika ninawaambia ukweli kwamba, hatapoteza thawabu yake.

Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi

(Mt 18:6-9; Lk 17:1-2)

42 Yeyote anayemsababisha mmoja wa hawa walio wadogo ambao wananiamini mimi kujikwaa na kuanguka, itakuwa bora kwake ikiwa atatupwa baharini huku amefungwa jiwe la kusagia shingoni mwake. 43 Ikiwa mkono wako unakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili na kuenda Jehanamu, ambako kuna moto usiozimika. 44 [h] 45 Na ikiwa mguu wako utakusababisha ufanye dhambi, ukate. Ni bora kwako kuingia katika uzima wa milele ukiwa mlemavu kuliko kuwa na miguu miwili na kutupwa Jehanamu. 46 [i] 47 Na kama jicho lako litakusababisha ufanye dhambi, liondoe. Ni bora uingie katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja kuliko kuwa nayo macho mawili na kutupwa Jehanamu, 48 ambapo waliomo watatafunwa na funza wasiokufa na kuchomwa na moto usiozimika kamwe.(A)

49 Kwa kuwa kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.[j]

50 Chumvi ni njema. Lakini ikiwa chumvi itaharibika, utawezaje kuifanya chumvi tena? Muwe na chumvi miongoni mwenu na muishi kwa amani ninyi kwa ninyi.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International