Beginning
Nani ni Mkuu Zaidi?
(Mk 9:33-37; Lk 9:46-48)
18 Wakati huo huo wanafunzi wake wakamjia Yesu na kuuliza, “Nani ni mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu?”
2 Yesu akamwita mtoto mdogo, akamsimamisha mbele yao. 3 Kisha akasema, “Ukweli ni huu, ni lazima mbadilike katika namna mnavyofikiri na muwe kama mtoto mdogo. Msipofanya hivi hamtaingia katika ufalme wa Mungu. 4 Aliye mkuu zaidi katika ufalme wa Mungu ni yule anayejinyenyekeza kama mtoto huyu.
5 Unapomkubali mtoto mdogo kama huyu kama aliye wangu, unanikubali mimi.
Yesu Aonya Kuhusu Chanzo cha Dhambi
(Mk 9:42-48; Lk 17:1-2)
6 Ikiwa mmoja wa watoto hawa wadogo ananiamini, na mtu yeyote akasababisha mtoto huyo kutenda dhambi, ole wake mtu huyo. Ingekuwa bora mtu huyo kufungiwa jiwe la kusagia shingoni mwake na kuzamishwa katika kina kirefu baharini. 7 Nawasikitikia watu wa ulimwengu kwa sababu ya mambo yanayofanya watu watende dhambi. Mambo haya lazima yatokee, lakini ole wake mtu yeyote anayeyafanya yatokee.
8 Mkono au mguu wako ukikufanya utende dhambi, ukate na uutupe. Ni bora ukapoteza kiungo kimoja cha mwili wako na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na mikono au miguu miwili na ukatupwa katika moto wa milele. 9 Jicho lako likikufanya utende dhambi, ling'oe na ulitupe. Ni bora kwako kuwa na jicho moja tu na ukaupata uzima wa milele kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa katika moto wa Jehanamu.
Yesu Atumia Simulizi ya Kondoo Aliyepotea
(Lk 15:3-7)
10 Iweni waangalifu, msidhani kuwa watoto hawa wadogo si wa muhimu. Ninawaambia kuwa watoto hawa wana malaika mbinguni. Na hao malaika daima wako pamoja na Baba yangu mbinguni. 11 [a]
12 Mtu akiwa na kondoo 100, lakini mmoja wa kondoo akapotea, atafanya nini? Atawaacha kondoo wengine 99 kwenye kilima na kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea. Sawa? 13 Na akimpata kondoo aliyepotea, atafurahi kwa sababu ya kondoo huyo mmoja kuliko kondoo wengine 99 ambao hawakupotea. Ninaweza kuwathibitishia, 14 Kwa namna hiyo hiyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi mmoja wa watoto hawa wadogo apotee.
Mrekebishe Kila Anayekosea
(Lk 17:3)
15 Ikiwa mmoja wa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akifanya kosa kwako,[b] umwendee na umwambie kile alichokukosea. Ufanye hivi mnapokuwa ninyi wawili tu. Ikiwa mtu huyo atakusikiliza, basi umemsaidia na umfanye kuwa kaka ama dada yako tena. 16 Lakini ikiwa mtu huyo atakataa kukusikiliza, mrudie ukiwa pamoja na ndugu wengine wawili waaminio. Ndipo watakuwepo watu wawili au watatu watakaoweza kueleza kile kilichotokea.[c] 17 Ikiwa mtu aliyetenda dhambi atakataa kuwasikiliza, ndipo uliambie kanisa. Na akikataa kulisikiliza kanisa, mchukulie kama ambavyo ungemchukulia mtu asiyemfahamu Mungu au mtoza ushuru.
18 Ninawahakikishia kuwa mnapotoa hukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Na mnapotoa msamaha, nao utakuwa msamaha wa Mungu.[d] 19 Kwa namna nyingine, ikiwa watu wawili waliopo duniani watakubaliana kwa kila wanachokiombea, Baba yangu wa mbinguni atatenda kile wanachokiomba. 20 Ndiyo, ikiwa watu wawili au watatu wanaoniamini watakusanyika pamoja, mimi nitakuwa pamoja nao.”
Simulizi Kuhusu Msamaha
21 Kisha Petro akamwendea Yesu na kumwuliza, “Bwana, ndugu yangu akiendelea kunikosea, ninapaswa kumsamehe anaponikosea mara ngapi? Mara saba?”
22 Yesu akamjibu, “Ninakwambia, ni lazima umsamehe zaidi ya mara saba. Ni lazima uendelee kumsamehe hata kama atakukosea saba mara sabini.[e]
23 Ninawaambia kwa sababu ufalme wa Mungu unafanana na mfalme aliyetaka kupata taarifa kutoka kwa watumishi wake. 24 Mtumishi aliyekuwa anadaiwa na mfalme tani 300[f] za fedha aliletwa kwake. 25 Hakuwa na fedha za kutosha kulipa deni lake. Hivyo mfalme aliamuru kila kitu anachomiliki mtumishi yule kiuzwe ikiwa ni pamoja na mke na watoto wake.
26 Lakini mtumishi alipiga magoti na kumsihi mfalme akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’ 27 Mfalme alimhurumia. Hivyo akamsamehe yule mtumishi deni lote na akamwacha aende akiwa huru.
28 Lakini mtumishi huyo alipoondoka, alimwona mtumishi mwingine aliyekuwa anamdai sarafu mia za fedha. Akamkaba shingo yake na akasema, ‘Nilipe pesa ninayokudai!’
29 Mtumishi anayedaiwa akapiga magoti na kumsihi akisema, ‘Nivumilie. Nitakulipa kila kitu unachonidai.’
30 Lakini mtumishi wa kwanza alikataa kumvumilia. Alimwambia hakimu kuwa alikuwa anamdai pesa, na mtumishi yule alitupwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa deni lake. 31 Watumishi wengine walipoona hili, walimhurumia mtumishi aliyefungwa gerezani. Hivyo walienda na kumwambia mfalme kila kitu kilichotokea.
32 Ndipo mfalme alimwita msimamizi wa kwanza na kumwambia, ‘Wewe ni mbaya sana! Ulinisihi nikusamehe deni lako, na nilikuacha ukaondoka bila kulipa kitu chochote! 33 Hivyo ulipaswa kumpa mtu yule mwingine anayetumika pamoja nawe rehema ile ile niliyokupa mimi.’ 34 Mfalme alikasirika sana. Hivyo alifungwa gerezani mpaka atakapoweza kulipa kila kitu anachodaiwa.
35 Mfalme huyu alifanya kama ambavyo Baba yangu wa mbinguni atawafanyia ninyi. Ni lazima umsamehe ndugu au dada yako kwa moyo wako wote, usipofanya hivyo, Baba yangu wa mbinguni hatakusamehe wewe.”
Yesu Afundisha Kuhusu Talaka
(Mk 10:1-12)
19 Yesu alipomaliza kuzungumza haya yote, aliondoka Galilaya. Alikwenda maeneo ya Yuda ng'ambo ya Mto Yordani. 2 Watu wengi walimfuata na akaponya wagonjwa wengi huko.
3 Baadhi ya Mafarisayo wakamjia Yesu. Walitaka aseme jambo fulani lisilo sahihi. Wakamwuliza, “Je, ni sahihi kwa mume kumtaliki mke wake kutokana na sababu yoyote ile kama anavyotaka?”
4 Yesu akajibu, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko: Mungu alipoumba ulimwengu, ‘aliumba watu wa jinsi ya kiume na wa jinsi ya kike.’(A) 5 Na Mungu alisema, ‘Hii ndiyo sababu mwanaume atawaacha baba na mama yake na kuungana na mke wake. Na hao watu wawili watakuwa mmoja.’(B) 6 Hivyo wao si wawili tena, bali mmoja. Ni Mungu aliowaunganisha pamoja, hivyo mtu yeyote asiwatenganishe.”
7 Mafarisayo wakauliza, “Sasa kwa nini Musa alitoa amri ya kumruhusu mwanaume kumtaliki mke wake kwa kuandika hati ya talaka?”[g]
8 Yesu akajibu, “Musa aliwaruhusu kuwataliki wake zenu kwa sababu mlikataa kupokea mafundisho ya Mungu. Lakini talaka haikuruhusiwa hapo mwanzo. 9 Ninawaambia kuwa, kila anayemtaliki mke wake, isipokuwa kutokana na uzinzi, na akamwoa mwanamke mwingine, anazini.”
10 Wafuasi wakamwambia Yesu, “Ikiwa hiyo ndiyo sababu pekee ambayo mtu anaruhusiwa kumtaliki mke wake, ni bora kutooa.”
11 Akajibu, “Tamko hili ni la kweli kwa baadhi ya watu, lakini si kwa kila mtu. Bali ni kwa wale tu waliopewa karama hii. 12 Kuna sababu tofauti kwa nini baadhi ya wanaume hawaoi.[h] Wengine wamezaliwa wakiwa hawana uwezo wa kuzaa watoto, wengine walifanywa hivyo katika maisha yao ya baadaye. Na wengine walichagua kutokuoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Hili liko hivyo kwa kila anayeweza kulikubali.”
Yesu Awakaribisha Watoto
(Mk 10:13-16; Lk 18:15-17)
13 Ndipo watu wakawaleta watoto wao wadogo kwa Yesu ili awabariki na kuwaombea. Wafuasi wake walipoliona hili, waliwakataza watu wasiwalete watoto kwa Yesu. 14 Lakini Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto hawa wadogo.” 15 Baada ya Yesu kuwabariki watoto, aliondoka huko.
Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu
(Mk 10:17-31; Lk 18:18-30)
16 Mtu mmoja alimwendea Yesu na kumwuliza, “Mwalimu, nifanye jambo gani lililo jema ili niweze kuupata uzima wa milele?”
17 Yesu akajibu, “Kwa nini unaniuliza kuhusu jambo gani lililo jema? Mungu pekee yake ndiye mwema. Lakini ikiwa unataka kuupata uzima wa milele, zitii amri.”
18 Yule mtu akauliza, “Amri zipi?”
Yesu akajibu, “‘Usiue, usizini, usiibe, usiseme uongo, 19 mheshimu baba na mama yako,’(C) na ‘mpende jirani yako[i] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(D)
20 Yule kijana akasema, “Ninazitii amri hizi zote. Nifanye nini zaidi?”
21 Yesu akajibu, “Ikiwa unataka kuwa mkamilifu, nenda ukauze kila kitu unachomiliki. Uwape pesa maskini na utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha njoo unifuate!”
22 Lakini kijana aliposikia Yesu anamwambia kuhusu kugawa pesa yake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Hivyo aliondoka.
23 Ndipo Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Ukweli ni huu, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 24 Ndiyo, ninawaambia, ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
25 Wafuasi waliposikia hili walishangaa. Wakauliza, “Sasa ni nani ataweza kuokolewa?”
26 Yesu akawatazama na kuwaambia, “Hili haliwezekani kwa wanadamu, Lakini yote yanawezekana kwa Mungu.”
27 Petro akamwambia, “Tuliacha kila kitu tulichonacho na kukufuata wewe. Tutapata nini?”
28 Yesu akawaambia, “Wakati wa ulimwengu mpya utakapofika, Mwana wa Adamu ataketi kwenye kiti chake cha enzi, kikuu na chenye utukufu mwingi. Na ninaweza kuwaahidi kuwa ninyi mnaonifuata mtaketi kwenye viti kumi na viwili vya enzi, na mtayahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 Kila aliyeacha nyumba, ndugu, dada, baba, mama, watoto au shamba na akanifuata atapata zaidi ya yale aliyoacha. Na atapata uzima wa milele. 30 Watu wengi walio wa kwanza sasa watakuwa wa mwisho siku zijazo. Na walio wa mwisho sasa watakuwa wa kwanza siku zijazo.
© 2017 Bible League International