Beginning
Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu
(Mk 7:1-23)
15 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria kutoka Yerusalemu walimjia Yesu na kumwuliza, 2 “Kwa nini wafuasi wako hawatii desturi tulizorithi kutoka kwa viongozi wetu wakuu walioishi hapo zamani? Wafuasi wako hawanawi mikono kabla ya kula!”
3 Yesu akajibu, “Na kwa nini mnakataa kutii amri ya Mungu ili muweze kuzifuata desturi zenu? 4 Mungu alisema, ‘Ni lazima umtii baba na mama yako.’(A) Na Mungu alisema pia kuwa, ‘Kila anayemnenea vibaya mama au baba yake lazima auawe.’(B) 5 Lakini mnafundisha kuwa mtu anaweza kumwambia baba au mama yake, ‘Nina kitu ninachoweza kukupa kukusaidia, Lakini sitakupa, bali nitampa Mungu.’ 6 Mnawafundisha kutowatii baba zao. Hivyo mnafundisha kuwa si muhimu kufanya kile alichosema Mungu. Mnadhani ni muhimu kufuata mila na desturi zenu mlizonazo. 7 Enyi wanafiki! Isaya alikuwa sahihi alipozungumza kwa niaba ya Mungu kuhusu ninyi aliposema:
8 ‘Watu hawa wananiheshimu kwa maneno tu,
lakini mimi si wa muhimu kwao.
9 Ibada zao kwangu hazina maana.
Wanafundisha kanuni za kibinadamu tu.’”(C)
10 Yesu akawaita watu. Akasema, “Sikieni na mwelewe nitakachosema. 11 Si chakula kinachoingia mdomoni kinachomtia mtu unajisi,[a] bali kile kinachomtoka mdomoni mwake.” 12 Kisha wafuasi wakamjia na kumwuliza, “Unajua kuwa Mafarisayo wamekasirika kutokana na yale uliyosema?”
13 Yesu akajibu, “Kila mti ambao haukupandwa na Baba yangu wa mbinguni utang'olewa. 14 Kaeni mbali na Mafarisayo. Wanawaongoza watu, lakini ni sawa na wasiyeona wanaowaongoza wasiyeona wengine. Na kama asiyeona akimwongoza asiyeona mwingine, wote wawili wataangukia shimoni.”
15 Petro akasema, “Tufafanulie yale uliyosema awali kuhusu kile kinachowatia watu najisi.”
16 Yesu akasema, “Bado mna matatizo ya kuelewa? 17 Hakika mnajua kuwa vyakula vyote vinavyoingia kinywani huenda tumboni. Kutoka huko hutoka nje ya mwili. 18 Lakini mambo mabaya ambayo watu wanasema kwa vinywa vyao hutokana na mawazo yao. Na hayo ndiyo yanayoweza kumtia mtu unajisi. 19 Mambo mabaya haya yote huanzia akilini: mawazo maovu, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, uongo, na matukano. 20 Haya ndiyo mambo yanayowatia watu unajisi. Kula bila kunawa mikono hakuwezi kuwafanya watu wasikubaliwe na Mungu.”
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mk 7:24-30)
21 Kutoka pale, Yesu alikwenda maeneo ya Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke Mkanaani kutoka eneo hilo akatokea na kuanza kupaza sauti, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali nisaidie! Binti yangu ana pepo ndani yake, na anateseka sana.”
23 Lakini Yesu hakumjibu. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea Yesu na kumwambia, “Mwambie aondoke, anaendelea kupaza sauti na hatatuacha.”
24 Yesu akajibu, “Mungu alinituma niwasaidie kondoo wa Mungu waliopotea, watu wa Israeli.”[b]
25 Ndipo mwanamke alikuja mahali alipokuwa Yesu na kuinama mbele yake. Akasema, “Bwana, nisaidie!”
26 Akamjibu kwa kumwambia, “Si sahihi kuwapa mbwa mkate wa watoto.”
27 Mwanamke akasema, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula vipande vya chakula vinavyoanguka kutoka kwenye meza za mabwana zao.”
28 Kisha Yesu akamjibu, “Mwanamke, una imani kuu! Utapata ulichoomba.” Wakati huo huo binti wa yule mwanamke akaponywa.
Yesu Awaponya Watu Wengi
29 Kisha Yesu akatoka pale na kwenda pwani ya Ziwa Galilaya. Alipanda vilima na akaketi chini.
30 Kundi kubwa la watu likamwendea. Walileta watu wengine wengi waliokuwa wagonjwa na kuwaweka mbele yake. Walikuwepo watu wasioweza kutembea, wasiyeona, walemavu wa miguu, wasiyesikia na wengine wengi. 31 Watu walishangaa walipoona kuwa waliokuwa wasiyesema walianza kusema, walemavu wa miguu waliponywa, waliokuwa hawawezi kutembea waliweza kutembea, wasiyeona waliweza kuona. Kila mtu alimshukuru Mungu wa Israeli kwa hili.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000
(Mk 8:1-10)
32 Kisha Yesu akawaita wafuasi wake na kuwaambia, “Ninawaonea huruma watu hawa. Wamekuwa pamoja nami kwa siku tatu, na sasa hawana chakula. Sitaki niwaache waende wakiwa na njaa. Wanaweza kuzimia njiani wanaporudi nyumbani.”
33 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha watu wote hawa? Tuko nyikani mbali ni miji.”
34 Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”
Wakamjibu, “Tuna mikate saba na samaki wadogo wachache.”
35 Yesu akawaambia watu waketi chini. 36 Akaichukua mikate saba na samaki. Akamshukuru Mungu kwa sababu ya chakula. Akaigawa vipande vipande, akawapa wafuasi wake na wafuasi wakawapa watu chakula. 37 Watu wote walikula mpaka wakashiba. Baada ya hili, wafuasi walijaza vikapu saba kwa vipande vya chakula vilivyosalia ambavyo havikuliwa. 38 Walikuwepo wanaume 4,000 pale waliokula. Walikuwepo pia wanawake na watoto. 39 Baada ya wote kula, Yesu akawaambia watu wanaweza kwenda nyumbani. Alipanda mashua na kwenda eneo la Magadani.
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-13; Lk 12:54-56)
16 Mafarisayo na Masadukayo walimjia Yesu. Walitaka kumjaribu, kwa hiyo wakamwomba awaoneshe muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu.
2 Yesu akawajibu, “Ninyi watu mnapoona jua limezama, mnajua hali ya hewa itakavyokuwa. Anga ikiwa nyekundu, mnasema tutakuwa na hali ya hewa nzuri. 3 Na asubuhi, ikiwa anga ni nyeusi na nyekundu, mnasema mvua itanyesha. Hizi ni ishara za hali ya hewa. Mnaziona ishara hizi angani na mnajua zinamaanisha nini. Kwa namna hiyo hiyo, mnaona mambo yanayotokea sasa. Hizi ni ishara pia, lakini hamwelewi maana yake. 4 Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu na si waaminifu kwa Mungu. Ndiyo sababu kabla ya kuamini mnataka kuona muujiza. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia kitu cho chote. Yona[c] ndiyo ishara pekee mtakayopewa.” Kisha Yesu akaondoka mahali pale.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mk 8:14-21)
5 Yesu na wafuasi wake wakasafiri kwa kukatisha ziwa. Lakini wafuasi wakasahau kubeba mikate. 6 Yesu akawaambia, “Mwe waangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
7 Wafuasi wakajadiliana maana ya hili. Wakasema, “Amesema hivi kwa sababu tumesahau kubeba mikate?”
8 Yesu alipotambua kuwa wanajadiliana hili, akawauliza, “Kwa nini mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Imani yenu ni ndogo. 9 Bado hamwelewi? Mnakumbuka mikate mitano waliyokula watu 5,000 na vikapu vingi mlivyojaza mikate iliyosalia? 10 Na mnakumbuka mikate saba waliyokula watu 4,000 na vikapu vingi mlivyojaza wakati ule? 11 Hivyo inakuwaje mnadhani kuwa mimi ninajali sana kuhusu mikate? Ninawaambia muwe waangalifu na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
12 Ndipo wafuasi wakaelewa Yesu alimaanisha nini. Hakuwa akiwaambia wajilinde na chachu inayotumika katika mikate bali wajilinde na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mk 8:27-30; Lk 9:18-21)
13 Yesu alikwenda eneo la Kaisaria Filipi na akawauliza wafuasi wake, “Watu wanasema mimi ni nani[d]?”
14 Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji. Wengine wanasema wewe ni Eliya. Na wengine wanasema wewe ni Yeremia au mmoja wa manabii.”
15 Kisha Yesu akawauliza, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akajibu, “Wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Yesu akajibu, “Umebarikiwa, Simoni mwana wa Yona. Hakuna aliyekufundisha hilo ila Baba yangu wa mbinguni ndiye amekuonesha mimi ni nani. 18 Hivyo ninakwambia, Wewe ni Petro. Na nitalijenga kanisa langu kwenye mwamba[e] huu. Nguvu ya mauti[f] haitaweza kulishinda kanisa langu. 19 Nitawapa funguo za Ufalme wa Mungu. Mnapohukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Mnapotamka msamaha hapa duniani, msamaha huo utakuwa msamaha wa Mungu.”[g]
20 Kisha Yesu akawaonya wafuasi wake wasimwambie mtu yeyote kuwa yeye ndiye Masihi.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mk 8:31-9:1; Lk 9:22-27)
21 Kuanzia wakati huo Yesu alianza kuwaambia wafuasi wake kuwa ni lazima aende Yerusalemu. Alifafanua kuwa Viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria watamfanya apate mateso kwa mambo mengi. Na aliwaambia wafuasi wake kuwa lazima auawe. Na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu.
22 Petro akamchukua Yesu na kwenda naye faragha mbali na wafuasi wengine. Akaanza kumkosoa Yesu kwa akasema, “Mungu akuepushe mbali na mateso hayo, Bwana! Hilo halitakutokea!”
23 Ndipo Yesu akamwambia Petro, “Ondoka kwangu, Shetani![h] Hunisaidii! Hujali mambo ya Mungu. Unajali mambo ambayo wanadamu wanadhani ni ya muhimu.”
24 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Ikiwa yeyote miongoni mwenu anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima aache kujiwazia yeye mwenyewe na mahitaji yake. Ni lazima awe radhi kuubeba msalaba aliopewa na kunifuata mimi. 25 Yeyote kati yenu anayetaka kuokoa uhai wake, ataupoteza. Lakini ninyi mlioyaacha maisha yenu kwa ajili yangu mtaupata uzima wa kweli. 26 Haina maana kwenu ninyi kuupata ulimwengu wote, ikiwa ninyi wenyewe mtapotea. Mtu atalipa nini ili kuyapata tena maisha yake baada ya kuyapoteza? 27 Mimi, Mwana wa Adamu, nitarudi katika utukufu wa Baba yangu pamoja na Malaika. Na nitamlipa kila mtu kutokana na matendo yake. 28 Niaminini ninaposema wapo watu waliopo hapa watakaoishi mpaka watakaponiona nikija kama Mwana wa Adamu kutawala kama mfalme.”
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mk 9:2-13; Lk 9:28-36)
17 Siku sita baadaye, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo na akapanda nao kwenye mlima mrefu. Walikuwa peke yao huko. 2 Wafuasi wake hawa walipokuwa wakimwangalia, Yesu alibadilika. Uso wake ukawa angavu kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama mwanga. 3 Ndipo wanaume wawili waliozungumza naye wakaonekana wakiwa pamoja naye. Walikuwa Musa na Eliya.
4 Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tuko hapa. Ukitaka, nitajenga vibanda vitatu,[i] kimoja kwa ajili ya heshima yako, kingine kwa ajili ya heshima ya Musa na kingine kwa ajili ya heshima ya Eliya.”
5 Petro alipokuwa akizungumza, wingu jeupe liliwafunika. Sauti ikatoka katika wingu na akasema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda, ninafurahishwa naye. Mtiini yeye!”
6 Wafuasi waliokuwa na Yesu walipoisikia sauti hii waliogopa sana na wakaanguka chini. 7 Lakini Yesu akawaendea na kuwagusa. Akasema, “simameni, msiogope.” 8 Wafuasi wakatazama juu, wakaona kuwa Yesu yuko peke yake.
9 Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, akawaamuru akisema: “Msimwambie mtu yeyote yale mliyoyaona mlimani. Subirini mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu. Ndipo mtaweza kuwaambia watu juu ya kile mlichokiona.”
10 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Kwa nini walimu wa sheria wanasema ni lazima Eliya aje[j] kabla ya Masihi kuja?”
11 Yesu akajibu, “Wako sahihi kusema ni lazima Eliya aje, na ni kweli kuwa Eliya ataweka mambo yote kama yanavyopaswa kuwa. 12 Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja. Watu hawakumjua yeye ni nani, na walimtendea vibaya, wakafanya kama walivyotaka. Ndivyo itakavyokuwa hata kwa Mwana wa Adamu. Watu hao punde tu watamletea mateso Mwana wa Adamu.” 13 Ndipo wafuasi wakaelewa kuwa Yesu aliposema kuhusu Eliya, alikuwa anazungumza juu ya Yohana Mbatizaji.
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mk 9:14-29; Lk 9:37-43a)
14 Yesu na wafuasi walirudi kwa watu. Mtu mmoja akamjia Yesu na kuinama mbele zake. 15 Akasema, “Bwana, umwonee huruma mwanangu. Anateswa sana na kifafa alichonacho. Anaangukia kwenye moto au maji mara kwa mara. 16 Nilimleta kwa wafuasi wako, lakini wameshindwa kumponya.”
17 Yesu akajibu, “Ninyi watu mnaoishi katika nyakati hizi cha kizazi kisicho na imani. Maisha yenu ni mabaya sana! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kijana hapa.” 18 Yesu akamwamuru pepo aliye ndani ya kijana, na pepo akamtoka na yule kijana akapona.
19 Kisha wafuasi wakamjia Yesu wakiwa peke yao. Wakasema, “Tulijaribu kumtoa pepo kwa kijana, lakini tulishindwa. Kwa nini tulishindwa kumtoa pepo?”
20 Yesu akajibu, “Mlishindwa kumtoa pepo kwa sababu imani yenu ni ndogo sana. Niaminini ninapowaambia, imani yenu ikiwa na ukubwa wa mbegu ya haradali mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ondoka hapa na uende kule,’ nao utaondoka. Nanyi mtaweza kufanya jambo lolote.” 21 [k]
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mk 9:30-32; Lk 9:43b-45)
22 Baadaye, wafuasi walipokusanyika pamoja Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwenye mamlaka ya watu wengine, 23 watakaomwua. Lakini atafufuliwa kutoka kwa wafu siku ya tatu.” Wafuasi waliposikia kuwa Yesu angeuawa walihuzunika sana.
Yesu Afundisha Kuhusu Kulipa Kodi
24 Yesu na wafuasi wake walikwenda Kapernaumu. Walipofika huko watu waliokuwa wakikusanya ushuru wa Hekalu[l] wakamwendea Petro na kumwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa kodi ya Hekalu?”
25 Petro akajibu, “Ndiyo, hulipa.”
Petro akaingia katika nyumba alimokuwa Yesu. Kabla Petro hajazungumza jambo lolote, Yesu akamwambia, “Wafalme wa dunia huchukua kila aina ya kodi kutoka kwa watu. Lakini ni akina nani ambao hutoa kodi? Je, ni jamaa wa familia ya mfalme? Au watu wengine ndiyo hulipa kodi? Unadhani ni akina nani?”
26 Petro akajibu, “Watu wengine ndiyo hulipa kodi.”
Yesu akasema, “Basi wana wa mfalme hawapaswi kulipa kodi. 27 Lakini kwa kuwa hatutaki kuwaudhi watoza ushuru hawa, basi fanya hivi: Nenda ziwani na uvue samaki. Utakapomkamata samaki wa kwanza, mfungue kinywa chake. Ndani ya kinywa chake utaona sarafu nne za drakma mdomoni mwake. Ichukue sarafu hiyo mpe mtoza ushuru. Hiyo itakuwa kodi kwa ajili yangu mimi na wewe.”
© 2017 Bible League International