Beginning
Miaka Elfu Moja
20 Nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni. Malaika alikuwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake. 2 Malaika alimkamata joka, nyoka wa zamani ambaye pia anajulikana kama Ibilisi au Shetani. Malaika akamfunga joka kwa minyororo kwa muda wa miaka elfu moja. 3 Kisha akamtupia kuzimu na akaifunga. Malaika akamfungia joka kuzimu ili asiweze kuwadanganya watu wa dunia mpaka miaka elfu moja iishe. Baada ya miaka elfu moja joka lazima aachiwe huru kwa muda mfupi.
4 Kisha nikaona viti vya enzi na watu wamevikalia. Hawa ni wale waliopewa mamlaka ya kuhukumu. Na nikaona roho za wale waliouawa kwa sababu walikuwa waaminifu kwa kweli ya Yesu na ujumbe kutoka kwa Mungu. Hawakumwabudu mnyama wala sanamu yake. Hawakuipokea alama ya mnyama kwenye vipaji vya nyuso zao au mkononi mwao. Walifufuka na kutawala na Kristo kwa miaka elfu moja. 5 (Wengine waliokufa hawakufufuka mpaka miaka elfu moja ilipokwisha.)
Huu ni ufufuo wa kwanza. 6 Heri walifufuliwa mara ya kwanza. Ni watakatifu wa Mungu. Mauti ya pili haina nguvu juu yao. Watakuwa makuhani wa Mungu na Kristo. Watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja.
Kushindwa kwa Shetani
7 Miaka elfu moja itakapokwisha, Shetani ataachiwa huru kutoka kwenye gereza lake. 8 Atatoka na kwenda kuwadanganya mataifa katika dunia yote, mataifa yajulikanayo kama Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya watu kwa ajili ya vita. Kutakuwa watu wengi wasiohesabika kama mchanga katika ufukwe wa bahari.
9 Nililiona jeshi la Shetani likitembea na kujikusanya ili kuizingira kambi ya watu wa Mungu na mji anaoupenda Mungu. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuliteketeza jeshi la Shetani. 10 Na Shetani, yule aliyewadanganya watu hawa, alitupwa kwenye ziwa la moto pamoja na mnyama na nabii wa uongo. Watateseka kwa maumivu usiku na mchana milele na milele.
Watu wa Dunia Wahukumiwa
11 Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe. Nikamwona aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha enzi. Dunia na anga vikamkimbia na kutoweka. 12 Na nikaona wale waliokufa, wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi na vitabu vilifunguliwa. Na kitabu cha uzima kilifunguliwa pia. Watu walihukumiwa kwa yale waliyotenda, kama yalivyoandikwa katika vitabu.
13 Bahari ikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Mauti na kuzimu zikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Watu wote hawa walihukumiwa kutokana na matendo yao. 14 Mauti na kuzimu vilitupwa kwenye ziwa la moto. Ziwa hili la moto ni mauti ya pili. 15 Na yeyote ambaye jina lake halikuonekana limeandikwa kwenye kitabu cha uzima alitupwa kwenye ziwa la moto.
Yerusalemu Mpya
21 Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu na dunia ya kwanza vilikwisha kutoweka. Na sasa bahari haikuwepo. 2 Nikauona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya,[a] ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu. Ulikuwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyevalishwa kwa ajili ya mumewe.
3 Nikasikia sauti kuu kutoka kwenye kiti cha enzi. Ikisema, “Makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu. Yeye ataishi pamoja nao. Na wao watakuwa watu wake. Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao naye atakuwa Mungu wao. 4 Atafuta kila chozi kutoka machoni mwaona. Hakutakuwa na kifo tena, huzuni, kilio wala maumivu. Namna zote za zamani zimepita.”
5 Aliyekaa kwenye kiti cha enzi akasema, “Tazama, sasa ninakiumba kila kitu upya!” Kisha akasema, “Andika hili, kwa sababu maneno haya ni kweli na ya kuaminiwa.”
6 Akaniambia, “Imekwisha! Mimi ni Alfa na Omega,[b] Mwanzo na Mwisho. Kila mwenye kiu nitampa bure maji kutoka kwenye chemichemi ya maji ya uzima. 7 Wale wote watakaoshinda watapokea yote haya. Na nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watoto wangu. 8 Lakini waoga, wanaokataa kuniamini, wafanyao mambo ya kuchukiza, wauaji, wazinzi, wachawi, waabuduo sanamu na waongo, nitawatupa katika ziwa linalowaka moto. Hii ni mauti ya pili.”
9 Mmoja wa malaika saba akaja kwangu. Huyu alikuwa mmoja wa malaika saba waliokuwa na bakuli saba zilizojaa mapigo saba ya mwisho. Malaika akasema, “Njoo huku. Nitakuonesha bibi arusi, mke wa Mwanakondoo.” 10 Malaika akanichukua kwa Roho Mtakatifu mpaka kwenye mlima mkubwa na mrefu. Akanionyesha mji mtakatifu wa Yerusalemu. Mji ulikuwa ukiteremka kutoka mbinguni kwa Mungu.
11 Mji ulikuwa unang'aa kwa utukufu wa Mungu. Ulikuwa unang'aa kwa uangavu kama yaspi, kito cha thamani sana. Ulionekana kwa uwazi kama kioo. 12 Mji ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mbili. Kulikuwa malaika kumi na mbili kwenye milango. Kwenye kila mlango kuliandikwa jina la kabila moja la Israeli. 13 Yalikuwepo malango matatu upande wa mashariki, malango matatu kaskazini, malango matatu kusini, na malango matatu magharibi. 14 Kuta za mji zilijengwa kwenye mawe kumi na mbili ya msingi. Kwenye mawe kulikuwa kumeandikwa majina ya mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo.
15 Malaika aliyezungumza na mimi alikuwa na fimbo ya kupimia iliyotengenezwa kwa dhahabu. Alikuwa na fimbo hii ili kuupima mji, malango na ukuta wake. 16 Mji ulijengwa kimraba. Urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Malaika aliupima mji kwa fimbo. Mji ulikuwa na urefu wa kilomita 2,400,[c] upana wake ulikuwa kilomita 2,400, na kimo chake kwenda juu kilikuwa kilomita 2,400. 17 Malaika akaupima ukuta pia. Kimo cha ukuta kilikuwa ni mita 60[d] kwenda juu. (Malaika alikuwa anatumia vipimo ambavyo watu hutumia.) 18 Ukuta ulijengwa kwa yaspi. Mji ulijengwa kwa dhahabu safi, iliyo safi kama kioo.
19 Mawe ya msingi wa ukuta wa mji yalikuwa na kila aina ya vito vya thamani ndani yake. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa yaspi, la pili lilikuwa yakuti samawi, la tatu lilikuwa kalkedoni, la nne lilikuwa zumaridi, 20 la tano lilikuwa sardoniki, la sita lilikuwa akiki, la saba lilikuwa krisolitho, la nane lilikuwa zabarajadi, la tisa lilikuwa yakuti ya manjano, la kumi lilikuwa krisopraso, la kumi na moja lilikuwa hiakintho na la kumi na mbili lilikuwa amethisto. 21 Malango kumi na mbili yalikuwa lulu kumi na mbili. Kila lango lilitengenezwa kwa lulu moja. Mitaa ya mji ilitengenezwa kwa dhahabu safi, inayong'aa kama kioo.
22 Sikuona hekalu ndani ya mji. Bwana Mungu Mwenye Nguvu na Mwanakondoo ndiyo waliokuwa hekalu la mji. 23 Mji haukuhitaji jua wala mwezi kuung'arizia. Utukufu wa Mungu uliupa mji mwanga. Mwanakondoo ndiye alikuwa taa ya mji.
24 Mataifa watatembea katika mwanga unaotoka katika mji ule.[e] Watawala wa dunia wataleta utukufu wao katika mji. 25 Milango ya mji haitafungwa hata siku moja, kwa sababu hakutakuwa usiku huko. 26 Ukuu na heshima ya mataifa vitaletwa katika mji. 27 Kilicho najisi hakitaingia katika mji. Atendaye mambo ya kuchukiza na mwongo hawataingia katika mji huo. Walioandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tu, ndiyo watakaoingia katika mji huo.
22 Malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, ulikuwa anga'avu kama kioo. Mto hutiririka kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. 2 Hutiririka kupitia katika mtaa mkuu wa mji. Mti wa uzima[f] uko kila upande wa mto, na huzaa tunda kila mwezi, mara kumi na mbili kwa mwaka. Majani ya mti ni kwa ajili ya kutibu mataifa.
3 Katika mji ule hakuna mtu au kitu kitakachokuwa chini ya laana ya Mungu tena. Kiti cha ufalme cha Mungu na Mwanakondoo vitakuwa ndani ya mji. Watumishi wa Mungu watamwabudu yeye. 4 Watauona uso wake. Jina la Mungu litaandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Hakutakuwa usiku tena. Watu hawatahitaji mwanga wa taa au mwanga wa jua. Bwana Mungu atawapa mwanga. Watatawala kama wafalme milele na milele.
6 Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminiwa. Bwana, Mungu awavuviaye manabii, amemtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake mambo ambayo lazima yatokee hivi karibuni: 7 ‘Sikiliza, Naja upesi! Heri anayetii maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.’”
8 Mimi ni Yohana. Mimi ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Baada ya kuyasikia na kuyaona, niliinama chini kusujudu miguuni pa malaika aliyeyaonesha kwangu. 9 Lakini malaika aliniambia, “Usinisujudie mimi! Mimi ni mtumishi kama wewe na ndugu zako manabii, ni mtumishi kama wale wote wanaoyatii maneno yaliyo katika kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
10 Kisha malaika akaniambia, “Usiyafanye siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, wakati umekaribia kwa mambo haya kutokea. 11 Kila atendaye mabaya aendelee kutenda mabaya. Yeyote aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Atendaye mema aendelee kutenda mema. Aliye mtakatifu aendelee kuwa mtakatifu.”
12 “Sikiliza, nakuja upesi! Nakuja na ujira ili kumlipa kila mtu sawa sawa na matendo yake. 13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14 Heri walioosha kanzu zao.[g] Watakuwa na haki ya kula chakula kutoka kwenye mti wa uzima. Wanaweza kuingia katika mji kwa kupitia katika malango yake. 15 Nje ya mji ni kwa ajili wale waishio kama mbwa; wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wapendao kudanganya na kujifanya wema.
16 Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kukuambia mambo hayo kwa ajili ya makanisa. Mimi ni mzao wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi.”
17 Roho Mtakatifu na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Kila asikiaye hili aseme pia, “Njoo!” Wote wenye kiu waje wanywe maji ya uzima bure ikiwa wanataka.
18 Ninamwonya kila mtu anayesikia maneno ya unabii wa kitabu hiki: Ikiwa mtu yeyote ataongeza chochote kwa haya, Mungu atampa mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19 Na ikiwa mtu yeyote akitoa sehemu yoyote ya maneno ya kitabu hiki cha unabii, Mungu ataondoa sehemu ya urithi wa mtu huyo katika mti wa uzima na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yesu ndiye anayesema kwamba haya yote ni kweli. Sasa anasema, “Ndiyo, naja upesi.”
Amina! Njoo, Bwana Yesu!
21 Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja na watu wote.
© 2017 Bible League International