Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Ufunuo 13-16

Mnyama kutoka Baharini

13 Kisha niliona mnyama mwenye pembe kumi na vichwa saba akipanda kutoka baharini. Kila pembe yake ilikuwa na taji. Alikuwa na kumkufuru Mungu lililoandikwa kwenye kila kichwa. Mnyama huyu alionekana kama chui, miguu yake ilikuwa kama ya dubu. Mdomo wake ulikuwa kama wa simba. Joka akampa huyo mnyama uweza wake wote, kiti chake cha enzi na mamlaka kuu.

Kichwa kimoja cha mnyama kilionekana kama kimejeruhiwa na kuuawa, lakini kidonda cha mauti kilipona. Watu wote ulimwenguni walishangaa, na wote walimfuata mnyama. Watu waliliabudu joka kwa sababu limempa nguvu mnyama, na pia walimwabudu mnyama. Waliuliza, “Nani ana nguvu kama mnyama? Nani anaweza kufanya vita dhidi yake?”

Mnyama aliruhusiwa kujigamba na kumtukana Mungu na kutumia nguvu zake kwa miezi arobaini na mbili. Mnyama alifungua kinywa chake ili amtukane Mungu, alitukane jina lake, mahali anapoishi, na wale wote wanaoishi mbinguni. Alipewa uwezo wa kufanya vita na watakatifu wa Mungu na kuwashinda. Alipewa uwezo juu ya kila kabila, asili, lugha na taifa. Kila anayeishi duniani angemwabudu mnyama. Hawa ni watu wote ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo tangu mwanzo wa ulimwengu. Mwanakondoo ndiye yule aliyeuawa.

Kila mtu anayesikia mambo haya azingatie hili:

10 Yeyote ambaye ni lazima awe mfungwa,
    atakuwa mfungwa.
Yeyote ambaye ni wa kuuawa kwa upanga,
    atauawa kwa upanga.

Hii inamaanisha kwamba watakatifu wa Mungu lazima wawe na subira na imani.

Mnyama Kutoka Nchi Kavu

11 Pia nikaona mnyama mwingine akija kutoka katika nchi. Alikuwa na pembe mbili kama kondoo, lakini anaongea kama joka. 12 Mnyama huyu alisimama mbele ya mnyama wa kwanza na kutumia nguvu ile ile ya mnyama wa kwanza. Alitumia nguvu hii kumfanya kila mtu aishiye duniani amwabudu mnyama wa kwanza. Mnyama wa kwanza ndiye mwenye jeraha la mauti lililopona. 13 Mnyama wa pili alifanya miujiza[a] mikuu. Alitengeneza hata moto ushuke kutoka mbinguni kuja duniani watu wakiangalia.

14 Mnyama huyu wa pili aliwadanganya watu wanaoishi duniani kwa kutumia miujiza ambayo amepewa uwezo wa kuifanya kwa ajili ya mnyama wa kwanza. Aliwaamuru watu kutengeneza sanamu ili kumheshimu mnyama wa kwanza, aliyejeruhiwa kwa upanga lakini hakufa bali akawa hai tena. 15 Mnyama wa pili alipewa uwezo wa kuipa uzima sanamu ya mnyama wa kwanza. Kisha kinyago kiliweza kuongea na kuamuru watu wote ambao hawakukiabudu wauawe. 16 Pia mnyama wa pili aliwaamuru watu wote, wakubwa na wadogo, matajiri na maskini, walio huru au watumwa, wawekewe alama kwenye mikono yao ya kulia au kwenye vipaji vya nyuso zao. 17 Hakuna ambaye angeweza kununua au kuuza bila ya kuwa na alama hii. (Alama hii ni jina la mnyama au namba ya jina lake.)

18 Kila mwenye uelewa anaweza kujua maana ya namba ya mnyama. Hili linahitaji hekima. Namba hii ni namba ya mtu. Nayo ni 666.

Watu wa Mungu Waimba Wimbo Mpya

14 Kisha nikatazama, na mbele yangu alikuwepo Mwanakondoo, amesimama juu ya Mlima Sayuni.[b] Watu 144,000 walikuwa pamoja naye. Jina lake na la Baba yake yalikuwa yameandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao.

Nikasikia sauti kutoka mbinguni yenye kelele kama mafuriko au ngurumo ya radi. Lakini ilisikika kama sauti ya wapiga vinubi wapigao vinubi vyao. Watu waliimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na viumbe wenye uhai wanne na wazee. Walioujua wimbo mpya ni wale 144,000 tu walionunuliwa kutoka duniani. Hakuna mwingine tena aliyekuwa anaujua.

Hawa ni wale ambao hawakuzini na wanawake.[c] Walijiweka safi. Na Sasa wanamfuata Mwanakondoo kila aendako. Walinunuliwa kutoka miongoni mwa watu wa dunia ili kuwa wa kwanza, kuwa sadaka kwa Mungu na Mwanakondoo. Hawana hatia ya kusema uongo; hawana kosa.

Malaika Watatu

Kisha nikaona malaika mwingine akipaa juu angani, akitangaza Habari Njema ya milele kwa watu waishio duniani, watu wa kila taifa, kabila, lugha na rangi. Malaika akasema kwa sauti kuu, “Mcheni Mungu na msifuni yeye. Wakati wa Mungu kuwahukumu watu wote umefika. Mwabuduni Mungu. Aliumba mbingu, dunia, bahari na chemichemi za maji.”

Kisha malaika wa pili akamfuata malaika wa kwanza na kusema, “Ameteketezwa! Mji mkuu Babeli umeteketezwa! Aliwafanya mataifa yote kunywa mvinyo wa uzinzi wake na ghadhabu ya Mungu.”

Malaika wa tatu aliwafuata malaika wawili wa kwanza. Malaika huyu wa tatu alisema kwa sauti kuu, “Mungu atawaadhibu wote wanaomwabudu mnyama na sanamu ya mnyama na kukubali kuwa na alama ya mnyama katika vipaji vya nyuso zao au kwenye mkono wao. 10 Watakunywa mvinyo wa ghadhabu ya Mungu.[d] Mvinyo huu umeandaliwa kwa nguvu zake zote katika kikombe cha ghadhabu ya Mungu. Watateseka kwa maumivu ya moto uwakao kwa kiberiti mbele ya malaika watakatifu na Mwanakondoo. 11 Na moshi kutokana na kuungua kwao utasimama milele na milele. Hakutakuwa mapumziko, usiku na mchana kwa wale wamwabuduo mnyama au sanamu yake au wale wavaao alama ya jina lake.” 12 Hii inamaanisha kuwa ni lazima watakatifu wa Mungu wawe na subira. Ni lazima wazitii amri za Mungu nakuendelea kumwamini Yesu.

13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Liandike hili: Kuanzia sasa heri wale wanaokufa wakiwa wa Bwana.”

Roho Mtakatifu anasema, “Ndiyo, hilo ni kweli. Watapumzika kutokana na kazi yao ngumu. Yale waliyotenda yatakaa pamoja nao.”

Dunia Yavunwa

14 Nikatazama, na mbele yangu, katika wingu jeupe, alikuwepo mmoja aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa na taji ya dhahabu kwenye kichwa chake na mundu mkali mkononi mwake. 15 Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, akamwambia aliyekaa kwenye wingu, “Chukua mundu wako na ukusanye kutoka duniani. Wakati wa kuvuna umefika, na tunda limeiva duniani.” 16 Hivyo aliyekaa kwenye wingu akaupitisha mundu wake juu ya dunia. Na dunia ikavunwa.

17 Ndipo malaika mwingine akatoka hekaluni mbinguni. Malaika huyu naye alikuwa na mundu mkali. 18 Na malaika mwingine, aliyekuwa msimamizi wa moto wa madhabahu akatoka madhabahuni. Akamwita malaika mwenye mundu mkali na kusema, “Chukua mundu wako wenye makali na ukusanye mafungu ya zabibu kutoka shamba la mizabibu duniani. Zabibu zimeiva duniani.” 19 Malaika akaupitisha mundu juu ya dunia. Akakusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20 Zabibu zikaminywa kwenye shinikizo nje ya mji. Damu ikatiririka kutoka kwenye shinikizo, ikanyanyuka juu kama vichwa vya farasi kwa urefu wa kilomita mia tatu.[e]

Malaika Wenye Mapigo ya Mwisho

15 Ndipo nikaona ajabu nyingine mbinguni, ilikuwa kubwa na ya kushangaza. Walikuwepo malaika saba wenye mapigo saba. Haya ni mapigo ya mwisho kwa sababu baada ya haya, ghadhabu ya Mungu itakuwa imekwisha.

Niliona kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Wale wote waliomshinda mnyama na sanamu yake na namba ya jina lake walikuwa wamesimama kando ya bahari. Watu hawa walikuwa na vinubi walivyopewa na Mungu. Waliuimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu na wimbo wa Mwanakondoo:

“Mambo unayotenda ni makuu na ya kushangaza,
    Bwana Mungu Mwenye Nguvu.
Njia zako ni sahihi na za kweli,
    mtawala wa mataifa.
Watu wote watakucha wewe, Ee Bwana.
    Watu wote watalisifu jina lako.
    Mtakatifu ni wewe peke yako.
Watu wote watakuja na kusujudu mbele yako,
    kwa sababu ni dhahiri kuwa wewe hutenda yaliyo haki.”

Baada ya hili nikaona hekalu, mahali patakatifu pa Mungu[f] mbinguni. Likiwa wazi; kisha malaika saba wenye mapigo saba wakatoka nje ya hekalu. Walikuwa wamevaa kitani safi inayong'aa. Wamevaa mikanda mipana ya dhahabu vifuani mwao. Kisha mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akawapa malaika bakuli saba za dhahabu. Bakuli zilikuwa zimejaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. Hekalu lilikuwa limejaa moshi uliotoka katika utukufu na nguvu ya Mungu. Hakuna ambaye angeweza kuingia hekaluni mpaka mapigo saba ya malaika saba yamemalizika.

Bakuli Zilizojazwa Ghadhabu ya Mungu

16 Kisha nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni. Ikiwaambia malaika saba, “Nendeni mkazimimine bakuli saba zenye ghadhabu ya Mungu juu ya dunia.”

Malaika wa kwanza akaondoka. Akaimimina bakuli yake duniani. Ndipo wale wote waliokuwa na alama ya mnyama na walioiabudu sanamu yake wakapata majipu mabaya yenye maumivu makali.

Malaika wa pili akaimimina bakuli yake baharini. Bahari ikawa kama damu ya mtu aliyekufa. Kila kitu kinachoishi baharini kikafa.

Malaika wa tatu akaimimina bakuli yake juu ya mito na chemichemi za maji. Mito na chemichemi za maji zikawa damu. Ndipo nikasikia malaika wa maji akimwambia Mungu:

“Wewe ni yule uliyepo na uliyekuwepo daima.
    Wewe ni Mtakatifu.
    Uko sahihi kwa hukumu hizi ulizofanya.
Watu walimwaga damu za
    watakatifu na manabii wako.
Sasa umewapa watu hao damu ili wanywe.
    Hiki ndicho wanachostahili.”

Pia nikasikia madhabahu ikisema:

“Ndiyo, Bwana Mungu Mwenye Nguvu,
    hukumu zako ni za kweli na za haki.”

Malaika wa nne akaimimina bakuli yake juu ya jua. Jua lilipewa nguvu kuwachoma watu kwa moto. Watu wakaungua kwa joto kali. Wakalilaani jina la Mungu, mwenye mamlaka juu ya mapigo haya. Lakini walikataa kubadili mioyo na maisha yao, na kumpa Mungu utukufu.

10 Malaika wa tano akaimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha mnyama. Giza likaufunika ufalme wa mnyama. Watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu. 11 Wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majipu waliyokuwa nayo. Lakini walikataa kubadili mioyo yao na kuyaacha maovu wanayotenda.

12 Malaika wa sita akaimimina bakuli yake juu ya mto mkuu Frati. Maji yaliyokuwa mtoni yakakauka. Hili likaandaa njia kwa ajili ya watawala kutoka mashariki kuweza kupita. 13 Kisha nikaona roho chafu tatu zilizoonekana kama vyura. Walitoka katika kinywa cha joka, kinywa cha mnyama, na kinywa cha nabii wa uongo. 14 Roho hizi chafu ni roho za mapepo. Zina nguvu za kutenda miujiza.[g] Nazo huenda kwa watawala wa ulimwengu wote na kuwakusanya kwa ajili ya mapigano siku ile Mungu Mkuu Mwenye Nguvu.

15 “Sikilizeni! Nitakuja kama mwizi wakati msioutarajia. Heri watakaokuwa macho na waliovaa nguo zao. Hawatakwenda wakiwa uchi na kuona aibu watakapoonwa na watu.”

16 Ndipo roho chafu zikawakusanya pamoja watawala pamoja mahali ambapo kwa Kiebrania panaitwa “Armagedoni”.

17 Malaika wa saba akaimimina bakuli yake angani. Sauti kuu ikatoka hekaluni katika kiti cha enzi. Ikasema, “Imekwisha!” 18 Kisha kukawa na mwako wa radi, kelele, ngurumo za radi na tetemeko kuu la nchi. Hili lilikuwa tetemeko kuu kuwahi kutokea tangu watu walipokuwepo duniani. 19 Mji mkuu ukagawanyika vipande vitatu. Miji ya mataifa ikaharibiwa. Na Mungu hakusahau kuuadhibu Babeli Mkuu. Aliupa mji ule kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu yake kuu. 20 Kila kisiwa kikatoweka na milima ikasawazika, hakukuwa milima yoyote tena. 21 Mvua yenye mawe makubwa kutoka mbinguni ikawanyeshea watu. Mawe haya yalikuwa na uzito wa kilo 40[h] kila jiwe. Watu wakamlaani Mungu kwa sababu ya mvua hii ya mawe. Hali hiyo Ilitisha sana.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International