Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Ufunuo 9-12

Tarumbeta ya Tano Yaanzisha Kitisho cha Kwanza

Malaika wa tano alipopuliza tarumbeta yake, niliiona nyota ikianguka kutoka angani mpaka duniani. Nyota ilipewa ufunguo wa kufungulia shimo refu sana liendalo kuzimu. Kisha nyota ikafungua shimo refu sana liendalo kuzimu. Moshi ukatoka kwenye shimo kama moto utokao kwenye tanuru kubwa. Jua na anga vikawa giza kwa sababu ya moshi uliotoka kwenye shimo.

Nzige wakatoka kwenye moshi na wakateremka kwenda duniani. Walipewa nguvu ya kuuma kama nge. Waliamriwa kutoharibu nyasi au mimea ya mashambani na mti. Walitakiwa kuwadhuru watu wasio na alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao tu. Hawakupewa mamlaka ya kuwaua lakini kuwatia maumivu kwa muda wa miezi mitano, maumivu kama ambayo mtu huyasikia anapoumwa na nge. Siku hizo watu watatafuta kifo, lakini hawatakiona. Watataka kufa, lakini kifo kitajificha.

Nzige hao walionekana kama farasi walioandaliwa kwa ajili ya mapigano. Vichwani mwao walivaa kitu kilichoonekana kama taji ya dhahabu. Nyuso zao zilionekana kama nyuso za wanadamu. Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake. Meno yao yalikuwa kama meno ya simba. Vifua vyao vilionekana kama ngao za chuma. Sauti zilizotoka katika mbawa zao zilikuwa kama za farasi wengi na magari ya farasi yaendayo vitani. 10 Walikuwa na mikia kama ya nge. Nguvu ya kuwasababishia wanadamu maumivu kwa miezi mitano ilikuwa kwenye mikia yao. 11 Walikuwa na mtawala, aliyekuwa malaika wa kuzimu. Jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni.[a] Na kwa Kiyunani ni Apolioni.[b]

12 Kitisho cha kwanza kimepita sasa. Bado vinakuja vitisho vingine viwili.

Mlio wa Tarumbeta ya Sita

13 Malaika wa sita alipopuliza tarumbeta yake, nilisikia sauti ikitoka katika pembe[c] zilizo katika pembe[d] nne za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu. 14 Ikamwambia malaika wa sita aliyekuwa na tarumbeta, “Wafungue huru malaika wanne waliofungwa pembezoni mwa mto mkuu Frati.” 15 Malaika hawa wanne walikuwa wamewekwa tayari kwa ajili ya saa hii, siku hii, mwezi na mwaka huu. Malaika waliachwa huru ili waue theluthi moja ya watu duniani. 16 Nikasikia kuwa idadi ya askari waliowaendesha farasi walikuwa milioni mia mbili.

17 Katika maono yangu, niliona farasi na waendesha farasi wakiwa juu ya farasi. Walionekana hivi: Walivaa dirii za chuma vifuani mwao zilizokuwa za rangi nyekundu, rangi ya bahari iliyoiva na za rangi ya njano kama baruti. Vichwa vya farasi vilionekana kama vichwa vya simba. Farasi walikuwa wanatoa moto, moshi na baruti katika vinywa vyao. 18 Theluthi ya watu wote duniani walikufa kutokana na mapigo haya matatu yaliyokuwa yanatoka vinywani mwa farasi: moto, moshi na baruti. 19 Nguvu ya farasi ilikuwa kwenye midomo na mikia yao. Mikia yao ilikuwa kama nyoka walio na vichwa vya kuwauma na kuwadhuru watu.

20 Watu wengine duniani hawakufa kwa mapigo haya. Lakini watu hawa bado hawakubadili mioyo yao na kuacha kuabudu vitu walivyovitengeneza kwa mikono yao wenyewe. Hawakuacha kuabudu mapepo na sanamu zilizotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, au kusikia au kutembea. 21 Hawakubadili mioyo yao na kuacha kuua watu wengine au kuacha uchawi, dhambi ya uzinzi na wizi.

Malaika Na Kitabu kidogo

10 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni akiwa amevikwa wingu na upinde wa mvua ulizunguka kichwa chake. Uso wake ulikuwa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Malaika alikuwa ameshika kitabu kidogo kilichofunguliwa. Akaweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na mguu wa kushoto nchi kavu. Alipaza sauti yake kama simba anavyounguruma na sauti za radi saba zikasikika.

Radi saba ziliongea, na nikaanza kuandika. Lakini nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Usiandike ambacho radi saba zinasema. Yaache mambo hayo yawe siri.”

Kisha nikamwona malaika aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu akinyoosha mkono wake kuelekea mbinguni. Malaika akaapa kwa nguvu ya yule aishiye milele na milele. Ndiye aliyeziumba mbingu na vyote vilivyomo ndani yake. Aliumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, na aliumba bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Malaika alisema, “Hakutakuwa kusubiri tena! Katika siku ambazo malaika wa saba atakuwa tayari kupuliza tarumbeta yake, mpango wa siri wa Mungu utakamilika, nao ni Habari Njema ambayo Mungu aliwaambia watumishi wake, manabii.”

Kisha nikasikia tena sauti ile ile kutoka mbinguni. Ikaniambia, “Nenda ukachukue kitabu kilicho wazi mkononi mwa malaika, aliyesimama juu ya bahari na nchi kavu.”

Hivyo nilimwendea malaika nikamwomba anipe kitabu kidogo. Naye aliniambia, “Chukua kitabu na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako lakini kitakuwa kitamu kama asali mdomoni mwako.” 10 Hivyo nilichukua kitabu kidogo kutoka mkononi mwa malaika na kukila. Mdomoni mwangu kilikuwa na ladha tamu kama asali, lakini baada ya kukila, kilikuwa kichungu tumboni mwangu. 11 Kisha nikaambiwa, “Ni lazima uwatabirie tena watu wa asili tofauti, mataifa, lugha na watawala.”

Mashahidi Wawili

11 Kisha nilipewa fimbo ya kupimia, ndefu kama fimbo ya kutembelea. Nikaambiwa, “Nenda ukalipime hekalu[e] la Mungu na madhabahu na uwahesabu watu wanaoabudu humo. Lakini usipime eneo lililo nje ya hekalu. Liache. Eneo hilo wamepewa watu wasio wa Mungu. Wataonesha nguvu zao juu ya mji mtakatifu kwa miezi 42. Nami nitawapa nguvu mashahidi wangu wawili, watatabiri kwa siku 1,260. Nao watakuwa wamevaa magunia.”

Mashahidi hawa wawili ni mizeituni miwili na vinara viwili vya taa vinavyosimama mbele za Bwana wa dunia. Ikiwa mtu yeyote atajaribu kuwadhuru mashahidi hawa, moto utatoka katika vinywa vyao na kuwaua adui zao. Yeyote atakaye jaribu kuwadhuru atakufa. Mashahidi hawa wana nguvu ya kuzuia mvua isinyeshe katika wakati ambao watakuwa wanatabiri. Pia wana uwezo wa kugeuza maji kuwa damu. Wana uwezo wa kutuma kila aina ya pigo duniani. Wanaweza kufanya hivi kadri wanavyotaka.

Mashahidi wawili watakapomaliza kuutangaza ujumbe wao, mnyama atokaye kuzimu atapigana nao. Atawashinda na kuwaua. Miili ya mashahidi hawa wawili italala kwenye mtaa wa mji mkuu. Mji huu unaitwa Sodoma na Misri. Majina ya mji huu yana maana maalumu. Huu ni mji ambako Bwana aliuawa. Watu kutoka kila asili, kabila, lugha na taifa wataiangalia miili ya mashahidi hawa wawili kwa siku tatu na nusu. Watu watakataa kuwazika. 10 Na Kila aishiye duniani atafurahi kwa sababu mashahidi hawa wawili wamekufa. Watu watafanya sherehe na kupeana zawadi kwa sababu manabii hawa wawili walileta mateso mengi kwa watu waishio duniani.

11 Lakini baada ya siku tatu na nusu, Mungu akawarudishia uhai mashahidi hawa wawili. Wakasimama kwa miguu yao. Na wale waliowaona wakajaa hofu. 12 Kisha mashahidi wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikisema, “Njooni huku juu!” Na wote wawili wakaenda juu mbinguni katika wingu, adui zao wakiangalia wanavyokwenda.

13 Katika wakati huo huo kulitokea tetemeko kuu la ardhi. Sehemu ya kumi ya mji ikateketea, na watu elfu saba wakafa. Wale ambao hawakufa waliogopa sana. Wakampa utukufu Mungu wa mbinguni.

14 Kitisho cha pili kimepita. Kitisho cha tatu kinakuja haraka.

Mlio wa tarumbeta ya Saba

15 Malaika wa saba alipopuliza tarumbeta yake, zikatokea sauti kuu mbinguni, zikasema:

“Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Masihi wake sasa.
    Na atatawala milele na milele.”

16 Kisha wazee 24 wakaanguka chini nyuso zao zikiwa chini wakamwabudu Mungu. Hawa ni wazee ambao wanakaa kwenye viti vyao vya heshima mbele za Mungu. 17 Wazee wakasema:

“Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi.
    Wewe ndiye uliyepo na ambaye daima umekuwepo.
Tunakushukuru kwa sababu umetumia uweza wako mkuu
    na umeanza kutawala.
18 Mataifa walikasirika,
    lakini sasa ni wakati kwa ajili ya hasira yako.
    Sasa ni wakati wa waliokufa kuhukumiwa.
Ni wakati wa kuwapa thawabu watumishi wako, manabii,
    na kuwapa thawabu watu wako watakatifu,
    wakubwa na wadogo, wanaokuheshimu wewe.
Ni wakati wa kuwaangamiza watu wanaoiangamiza dunia!”

19 Kisha hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa. Sanduku la Agano likaonekana ndani ya hekalu lake. Kisha kukatokea miali ya radi na miungurumo ya radi, kelele, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

Joka na Mwanamke Anayezaa

12 Jambo la ajabu lilionekana mbinguni: Mwanamke aliyevalishwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake alionekana. Alikuwa na taji yenye nyota kumi na mbili kichwani pake. Alikuwa na mimba na alilia kwa uchungu kwa sababu alikuwa karibu ya kuzaa.

Kisha ajabu nyingine ikaonekana mbinguni: Alikuweko huko joka mkubwa mwekundu. Joka huyo alikuwa na vichwa saba na alikuwa na taji juu ya kila kichwa. Na alikuwa na pembe kumi. Mkia wake ulizoa theluthi ya nyota na kuziangusha duniani. Joka hili lilisimama mbele ya mwanamke aliyekuwa karibu ya kuzaa mtoto. Lilitaka kumla mtoto mara atakapozaliwa.

Mwanamke alimzaa mtoto wa kiume, atakayewatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya chuma. Na mwana wa mwanamke huyu alichukuliwa juu mbinguni kwa Mungu, kwenye kiti chake cha enzii. Mwanamke alikimbilia jangwani mpaka mahali ambako Mungu amemwandalia. Huko angetunzwa kwa siku 1,260.

Kisha kulikuwa vita mbinguni. Mikaeli[f] na malaika zake walipigana na joka. Nalo joka na malaika zake wakapigana na Mikaeli pamoja na malaika zake, lakini joka na malaika zake hawakuwa na nguvu za kutosha kushinda, na hivyo wakapoteza nafasi zao mbinguni. Likatupwa chini kutoka mbinguni. (Joka hili kubwa ni nyoka yule wa zamani, aitwaye Ibilisi au Shetani, anayeudanganya ulimwengu wote.) Joka na malaika zake walitupwa duniani.

10 Kisha nilisikia sauti kubwa mbinguni ikisema:

“Ushindi na uweza na ufalme wa Mungu wetu
    na mamlaka ya Masihi wake umekuja sasa,
kwa sababu mshitaki wa kaka na dada zetu
    ametupwa chini.
Ndiye aliyewashitaki kwa Mungu,
    mchana na usiku.
11 Walimshinda kwa sadaka ya damu ya Mwanakondoo
    na kwa ujumbe wa Mungu waliowaambia watu.
Hawakuyapenda maisha yao sana.
    Hawakuogopa kifo.
12 Hivyo furahi, ewe mbingu
    na wote waishio humo!
Lakini ole kwa nchi na bahari,
    kwa sababu Ibilisi ameshuka kwako.
Amejaa ghadhabu.
    Anajua ana muda mchache.”

13 Joka alipoona amekwisha tupwa chini duniani, alimkimbiza mwanamke aliyemzaa mtoto wa kiume. 14 Lakini mwanamke alipewa mabawa mawili ya tai mkuu. Aliweza kuruka mpaka mahali palipoandaliwa kwa ajili yake jangwani. Huko atatunzwa kwa muda wa miaka mitatu na nusu akiwa mbali na joka. 15 Kisha joka lilitoa maji kama mto kutoka katika kinywa chake kuelekea kwa mwanamke ili mafuriko yamchukue. 16 Lakini nchi ilimsaidia mwanamke. Nchi ilifungua kichwa chake na kumeza mto uliotoka kwenye kinywa cha joka. 17 Kisha joka lilimkasirikia sana mwanamke. Likaenda kufanya vita na watoto wake wengine. Watoto wa mwanamke ni wale wanaozitii amri za Mungu na wanayo kweli ambayo Yesu aliifundisha.

18 Joka lilisimama ufukweni mwa bahari.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International