Beginning
Yohana Aiona Mbingu
4 Kisha nikatazama, na mbele yangu ulikuwepo mlango uliokuwa wazi mbinguni. Na nikasikia sauti iliyosema nami mwanzoni. Ilikuwa sauti iliyosikika kama tarumbeta. Ilisema, “Njoo huku juu, nitakuonesha yale ambayo ni lazima yatokee baada ya hili.” 2 Ghafla Roho akanichukua, na huko mbinguni kilikuwepo kiti cha enzi na mmoja amekaa juu yake. 3 Aliyekikalia alikuwa mzuri kama mawe ya thamani, kama yaspi na karneli. Pande zote kuzunguka kiti cha enzi kulikuwa upinde wa mvua wenye rangi kama zumaridi.
4 Vilikuwepo viti vingine vya enzi ishirini na nne kuzunguka kiti cha enzi vilivyokaliwa na wazee ishirini na nne. Wazee walikuwa wamevaa nguo nyeupe na taji za dhahabu vichwani mwao. 5 Mianga na ngurumo za radi vilitoka katika kiti cha enzi. Mbele ya kiti cha enzi zilikuwepo taa saba zikiwaka, ambazo ndizo Roho saba za Mungu. 6 Pia mbele ya kiti cha enzi kilikuwepo kitu kilichoonekana kama bahari ya kioo, iiliyo angavu sana.
Mbele ya kiti cha enzi na kukizunguka pande zake zote walikuwepo viumbe wenye uhai wanne. Walikuwa na macho kila mahali. 7 Kiumbe wa kwanza alikuwa kama simba. Wa pili alikuwa kama fahali. Wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu. Wa nne alikuwa kama tai anayeruka. 8 Kila mmoja wa hawa wenye uhai wanne alikuwa na mabawa sita. Walikuwa na macho kila mahali, ndani na nje. Usiku na mchana hawaachi kusema:
“Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana Mungu Mwenye nguvu zote.
Daima amekuwepo, yupo na anakuja.”
9 Wenye uhai hawa wanne walikuwa wanampa utukufu, heshima na shukrani yule anayekaa kwenye kiti cha enzi, anayeishi milele na milele. Na kila wakati walifanya hivyo, 10 wazee ishirini na nne waliinama mbele ya[a] yule anayekaa kwenye kiti cha enzi. Wanamwabudu anayeishi milele na milele. Wanaweka taji zao mbele ya kiti cha enzi na kusema:
11 “Bwana wetu na Mungu!
Unastahili kupokea utukufu, heshima na nguvu.
Uliumba vitu vyote.
Kila kinachoishi kiliumbwa kwa sababu ulitaka.”
Nani anaweza kukifungua kitabu?
5 Kisha niliona kitabu[b] katika mkono wa kulia wa aliyekaa kwenye kiti cha enzi. Kitabu hiki kilikuwa na maandishi pande zote na kilikuwa kimefungwa kwa mihuri saba. 2 Na nikamwona malaika mwenye nguvu, aliyeita kwa sauti kubwa, “Ni nani anayestahili kuivunja mihuri na kukifungua kitabu?” 3 Lakini hakukuwa yeyote mbinguni au duniani au chini ya dunia ambaye angeweza kukifungua kitabu na kutazama ndani yake. 4 Nililia sana kwa sababu hakuwepo aliyestahili kukifungua kitabu na kuangalia ndani yake. 5 Lakini mmoja wa wazee akaniambia, “Usilie! Simba[c] kutoka kabila la Yuda ameshinda. Ni mzaliwa wa Daudi. Anaweza kukifungua kitabu na mihuri yake saba.”
6 Kisha nikamwona Mwanakondoo amesimama katikati karibu na kiti cha enzi kilichozungukwa na viumbe wanne wenye uhai. Wazee pia walikuwa wamemzunguka Mwanakondoo aliyeonekana kama aliyeuawa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambayo ni roho saba za Mungu zilizotumwa ulimwenguni kote. 7 Mwanakondoo alikuja na akakichukua kile kitabu kutoka katika mkono wa kulia wa yule aliyeketi kwenye kiti enzi. 8 Baada ya Mwanakondoo kukichukua kile kitabu, viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na wanne wakainama mbele za Mwanakondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi. Pia walikuwa wameshikilia bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni maombi ya watu watakatifu wa Mungu. 9 Na wote walimwimbia wimbo mpya Mwanakondoo:
“Unastahili kukichukua kitabu
na kuifungua mihuri yake,
kwa sababu uliuawa,
na kwa sadaka ya damu yako uliwanunua watu kwa ajili ya Mungu,
kutoka kila kabila, lugha, rangi na taifa.
10 Uliwafanya kuwa ufalme na makuhani kwa ajili ya Mungu wetu.
Nao watatawala duniani.”
11 Kisha, nilipotazama, nikasikia sauti ya malaika wengi waliozunguka kiti cha enzi pamoja na viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne. Walikuwa maelfu kwa maelfu ya malaika, elfu kumi mara elfu kumi. 12 Kwa sauti kuu malaika walisema:
“Mamlaka yote, utajiri, hekima na nguvu ni kwa Mwanakondoo aliyeuawa.
Anastahili kupokea heshima, utukufu na sifa!”
13 Ndipo nikasikia kila kiumbe kilichoumbwa kilichoko mbinguni na duniani na chini ya dunia na baharini, viumbe vyote sehemu hizo vikisema:
“Sifa zote na heshima
na utukufu na nguvu kuu ni kwa ajili yake Yeye aketiye
kwenye kiti cha enzi na kwa Mwanakondoo milele na milele!”
14 Viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amina!” Na wazee wakainama chini wakasujudu.
Mwanakondoo Afungua Kitabu
6 Kisha nilitazama Mwanakondoo alipokuwa anaufungua muhuri[d] wa kwanza kati ya mihuri saba. Kisha nikasikia sauti ya mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akisema kwa sauti kama ngurumo ya radi ikisema, “Njoo!” 2 Nilipotazama nilimwona farasi mweupe mbele yangu. Mwendesha farasi aliyekuwa amempanda farasi huyo alikuwa na upinde na alipewa taji. Alimwendesha farasi akatoka kwenda kumshinda adui na ili kupata ushindi.
3 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa pili, nilimsikia kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” 4 Nilipotazama nilimwona farasi mwekundu akitokea. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alipewa mamlaka ya kuondoa amani duniani ili watu wauane. Alipewa upanga mkubwa.
5 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tatu. Nilisikia kiumbe mwenye uhai wa tatu akisema, “Njoo!” Nilipotazama nilimwona farasi mweusi mbele yangu. Aliyekuwa anamwendesha farasi huyu alikuwa na mizani mkononi mwake. 6 Kisha nilisikia kitu kilichosikika kama sauti ikitokea pale walipokuwa viumbe wenye uhai wanne. Kikisema, “Kilo moja[e] ya ngano au kilo tatu ya shayiri itagharimu mshahara wote wa siku moja. Lakini usiharibu upatikanaji wa mafuta ya mzeituni na divai!”
7 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa nne nilisikia sauti ya kiumbe wa nne mwenye uhai akisema, “Njoo!” 8 Nilipotazama nilimwona farasi mwenye rangi ya kijivu. Aliyempanda alikuwa mauti na kuzimu ilikuwa inamfuata nyuma yake kwa karibu. Alipewa mamlaka juu ya robo ya dunia kuwaua watu kwa upanga, njaa, magonjwa na kwa wanyama wa porini waliomo duniani.
9 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa tano, niliziona baadhi ya roho za wale waliokuwa waaminifu kwa neno la Mungu na kweli waliyopokea zikiwa chini ya madhabahu. 10 Roho hizi zilipiga kelele kwa sauti kuu zikisema, “Mtakatifu na Bwana wa kweli, ni lini utakapowahukumu watu wa dunia na kuwaadhibu kwa kutuua sisi?” 11 Kisha kila mmoja wao alipewa kanzu ndefu nyeupe. Wakaambiwa wasubiri kwa muda mfupi kwani bado walikuwepo ndugu zao katika utumishi wa Kristo ambao ni lazima wauawe kama wao. Roho hizi ziliambiwa zisubiri mpaka mauaji yote yatakapokwisha.
12 Kisha nilitazama wakati Mwanakondoo anaufungua muhuri wa sita. Kulitokea tetemeko kubwa la ardhi na jua likawa jeusi kama gunia jeusi[f] na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 Nyota zikaanguka chini duniani kama mtini uangushavyo tini zake upepo unapovuma. 14 Anga iligawanyika katikati na pande zote zikajiviringa kama kitabu.[g] Na kila mlima na kisiwa kiliondolewa mahali pake.
15 Kisha watu wote wa ulimwengu, wafalme, watawala, makamanda wa majeshi, matajiri, wenye mamlaka na nguvu, kila mtumwa na asiye mtumwa, walijificha katika mapango na nyuma ya miamba milimani. 16 Waliiambia milima na miamba, “Tuangukieni. Tuficheni mbali na uso wa yule aketiye kwenye kiti cha enzi. Tuficheni dhidi ya hasira ya Mwanakondoo! 17 Siku kubwa ya hasira yao imefika. Hakuna anayeweza kupingana nayo.”
Watu 144,000 wa Israeli
7 Baada ya hili kutokea, niliwaona malaika wanne wamesimama kwenye pembe nne za dunia wakiwa wamezishikilia pepo nne za dunia. Walikuwa wanazuia upepo kupuliza katika nchi au katika bahari au kwenye mti wowote. 2 Kisha nikaona malaika mwingine akija akitokea upande wa mashariki. Malaika huyu alikuwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Malaika akawaita kwa sauti kuu malaika wale wanne. Malaika hawa wanne walikuwa malaika ambao Mungu amewapa mamlaka ya kuidhuru dunia na bahari. Malaika akawaambia, 3 “Msiidhuru nchi au bahari au miti kabla hatujawawekea alama kwenye vipaji vya nyuso zao wale wanaomtumikia Mungu wetu.”
4 Kisha nikasikia idadi ya watu wenye alama ya Mungu kwenye vipaji vya nyuso zao. Walikuwa watu 144,000. Walitoka katika kila kabila la Israeli:
5 Kutoka katika kabila la Yuda walikuwa elfu kumi na mbili
Kutoka katika kabila la Rubeni walikuwa elfu kumi na mbili
Kutoka katika kabila la Gadi walikuwa elfu kumi na mbili
6 Kutoka katika kabila la Asheri walikuwa elfu kumi na mbili
Kutoka katika kabila la Naftali walikuwa elfu kumi na mbili
Kutoka katika kabila la Manasse walikuwa elfu kumi na mbili
7 Kutoka katika kabila la Simeoni walikuwa elfu kumi na mbili
Kutoka katika kabila la Lawi walikuwa elfu kumi na mbili
Kutoka katika kabila la Isakari walikuwa elfu kumi na mbili
8 Kutoka katika kabila la Zabuloni walikuwa elfu kumi na mbili
Kutoka katika kabila la Yusufu walikuwa elfu kumi na mbili
Kutoka katika kabila la Benjamini walikuwa elfu kumi na mbili.
Umati Mkubwa
9 Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu. Walikuwa wengi hakuna mtu angeweza kuwahesabu wote. Walikuwa wametoka katika kila taifa, kabila, rangi za watu na lugha za dunia. Walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo. Wote walikuwa wamevaa majoho meupe na wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Walipaza sauti kwa nguvu, wakasema “Ushindi ni wa Mungu wetu, anayeketi kwenye kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo.”
11 Wazee na wenye uhai wanne walikuwa pale. Malaika wote walikuwa wamesimama kuwazunguka na kukizunguka kiti cha enzi. Malaika wakainamisha nyuso zao, wakasujudu mpaka chini mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu. 12 Walisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, nguvu na uweza ni vyake Mungu wetu milele na milele. Amina!”
13 Kisha mmoja wa wazee akaniuliza, “Watu hawa waliovaa kanzu nyeupe ni akina nani? Wametoka wapi?”
14 Nikajibu, “Wewe unajua ni akina nani, bwana.”
Mzee akasema, “Hawa ni wale waliokuja kutokana na mateso makuu. Wamefua kanzu zao[h] kwa kutumia damu ya Mwanakondoo, wako safi na ni weupe. 15 Hivyo sasa watu hawa wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Wanamwabudu Mungu mchana na usiku hekaluni mwake. Naye aketiye kwenye kiti cha enzi atawalinda. 16 Hawatasikia njaa tena. Hawatasikia kiu tena. Jua halitawadhuru. Hakuna joto litakalowachoma. 17 Mwanakondoo mbele ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao. Atawaongoza kwenda kwenye chemichemi za maji ya uzima. Na Mungu atafuta kila chozi kutoka kwenye macho yao.”
Muhuri wa Saba
8 Mwanakondoo alipoufungua muhuri wa saba, kulikuwa ukimya mbinguni kama nusu saa hivi. 2 Niliwaona malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu. Walipewa tarumbeta saba.
3 Malaika mwingine akaja na kusimama kwenye madhabahu. Malaika huyu alikuwa na chetezo ya dhahabu. Malaika alipewa ubani mwingi ili autoe pamoja na maombi ya watakatifu wote wa Mungu. Malaika akaweka sadaka hii juu ya madhabahu ya dhahabu mbele ya kiti cha enzi. 4 Moshi kutoka kwenye ubani ukatoka kwenye mikono ya malaika kwenda kwa Mungu. Moshi ukaenda kwa Mungu ukiwa na Maombi ya watakatifu. 5 Kisha malaika akaijaza chetezo moto kutoka madhabahuni na kuitupa chini duniani, kukatokea miali, radi na ngurumo zingine na tetemeko la ardhi.
Sauti ya Tarumbeta ya Kwanza
6 Kisha malaika saba wenye tarumbeta walijiandaa kupuliza tarumbeta zao.
7 Malaika wa kwanza alipuliza tarumbeta yake. Mvua ya mawe na moto uliochanyanyikana na damu vilimwagwa chini duniani. Theluthi moja ya dunia na nyasi zote za kijani na theluthi ya miti vikaungua.
8 Malaika wa pili alipopuliza tarumbeta yake. Kitu fulani kilichoonekana kama mlima mkubwa unaowaka moto kilitupwa baharini. Na theluthi moja ya bahari ikawa damu. 9 Na theluthi moja ya viumbe walioumbwa wanaokaa baharini wakafa na ya meli theluthi moja zikaharibika.
10 Malaika wa tatu alipopuliza tarumbeta yake. Nyota kubwa, inayowaka kama tochi ikaanguka kutoka mbinguni. Ilianguka kwenye theluthi moja ya mito na chemichemi za maji. 11 Jina la nyota hiyo lilikuwa Uchungu.[i] Na theluthi moja ya maji yote yakawa machungu. Watu wengi wakafa kutokana na kunywa maji haya machungu.
12 Malaika wa nne alipopuliza tarumbeta yake. Theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota vikapigwa. Hivyo theluthi moja yao vikawa giza. Theluthi moja ya mchana na usiku ikakosa mwanga.
13 Nilipokuwa ninatazama, nilimsikia tai aliyekuwa anaruka juu sana angani akisema kwa sauti kuu, “Ole! Ole! Ole kwa wale wanaoishi duniani! Shida kuu zitaanza baada ya sauti za tarumbeta ambazo malaika wengine watatu watapuliza.”
© 2017 Bible League International