Beginning
Yohana Aeleza Kuhusu Kitabu Hiki
1 Huu ni ufunuo[a] kutoka kwa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa ili awaoneshe watumishi wake yale ambayo ni lazima yatokee muda mfupi ujao. Yesu Kristo alimtuma malaika wake ili amwonyeshe Yohana, mtumishi wake, 2 ambaye amesema kila kitu alichokiona. Ni ukweli alioambiwa na Yesu Kristo; ni ujumbe kutoka kwa Mungu. 3 Ana heri anayesoma maneno ya ujumbe huu kutoka kwa Mungu kwa kupaza sauti na wale wanaousikia ujumbe huu na kuyatendea kazi yaliyoandikwa ndani yake. Wakati uliosalia ni mfupi.
Yohana Ayaandikia Makanisa
4 Kutoka kwa Yohana,
Kwenda kwa makanisa saba yaliyo katika Asia:
Neema na amani ziwe kwenu kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo daima na anayekuja; na kutoka katika roho saba zilizoko mbele ya kiti chake cha enzi; 5 na kutoka kwa Yesu Kristo aliye shahidi mwaminifu. Aliye wa kwanza miongoni mwa watakaofufuliwa kutoka kwa wafu na ndiye mtawala wa wafalme wote wa dunia.
Yesu ndiye anayetupenda na ametuweka huru na dhambi zetu kwa sadaka ya damu yake. 6 Ametufanya sisi kuwa ufalme wake na makuhani wanaomtumikia Mungu, Baba yake. Utukufu na nguvu viwe kwa Yesu milele na milele! Amina.
7 Tazama, Yesu anakuja pamoja na mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma.[b] Watu wote wa dunia watamwombolezea.[c] Ndiyo, hili litatokea! Amina.
8 Bwana Mungu asema, “Mimi ni Alfa na Omega.[d] Mimi ndiye niliyepo, aliyekuwepo na anayekuja. Mimi ni Mwenye Uwezo Wote.” 9 Mimi ni Yohana, mwamini mwenzenu. Tuko pamoja katika Yesu na tunashirikiana mambo haya: mateso, ufalme na uvumilivu wenye subira. Nilikuwa katika kisiwa cha Patmo[e] kwa sababu nimekuwa mwaminifu kwa ujumbe wa Mungu na kwa ajili ya kweli ya Yesu. 10 Siku ya Bwana, Roho Mtakatifu alinitawala. Nilisikia sauti kuu nyuma yangu iliyosikika kama tarumbeta. 11 Ilisema, “Yaandike kwenye kitabu yale unayoyaona na uyatume kwa makanisa saba ya Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”
12 Niligeuka nyuma nimwone aliyekuwa anazungumza nami. Nilipogeuka, niliona vinara saba vya taa vya dhahabu. 13 Nikamwona mmoja katikati ya vinara aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa vazi refu, na mshipi wa dhahabu uliofungwa kuzunguka kifua chake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji. Macho yake yalikuwa kama miali ya moto. 15 Miguu yake ilikuwa kama shaba ing'aayo inapochomwa katika tanuru. Sauti yake ilikuwa kama kelele za mafuriko ya maji. 16 Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia. Upanga wenye makali kuwili ulitoka kinywani mwake. Uso wake ulikuwa jua linalong'aa sana mchana.
17 Nilipomwona nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Aliweka mkono wake wa kulia juu yangu na kusema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ndiye ninayeishi. Nilikufa, lakini tazama, niko hai milele na milele! Na ninashikilia funguo za mauti na Kuzimu. 19 Hivyo andika unachokiona. Yaandike mambo yanayotokea sasa na mambo yatakayotokea baadaye. 20 Hii ni maana iliyofichwa ya nyota na vinara saba vya taa vya dhahabu ulivyoviona: Vinara saba ni makanisa saba. Nyota saba ni malaika wa makanisa saba.”
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Efeso
2 “Andika hivi kwa malaika[f] wa kanisa lililoko Efeso:
Huu ni ujumbe kutoka kwake yeye anayeshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia na kutembea katikati ya vinara vya taa saba vya dhahabu.
2 Ninayajua matendo yako, unavyofanya kazi kwa bidii na usivyokata tamaa. Ninajua kwamba huwakubali watu waovu. Umewajaribu wote wanaojiita mitume lakini si mitume. Umegundua kuwa ni waongo. 3 Huachi kujaribu. Umestahimili taabu kwa ajili ya jina langu na hujakata tamaa.
4 Lakini nina neno hili nawe umeuacha upendo uliokuwa nao hapo mwanzo. 5 Hivyo kumbuka ulipokuwa kabla ya kuanguka. Ugeuze moyo wako na utende yale uliyoyatenda mwanzoni. Usipobadilika, nitakuja kwako na kutoa kinara chako cha taa mahali pake. 6 Lakini unafanya vizuri kuyachukia matendo ya Wanikolai.[g] Mimi pia nayachukia mambo wanayotenda.
7 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda, nitawapa haki ya kula matunda kutoka kwenye mti wa uzima, ulio katika Bustani ya Mungu.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Smirna
8 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna:
“Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa na akawa hai tena.
9 Ninayajua matatizo yako, na ninajua kwamba wewe ni maskini, lakini hakika wewe ni tajiri! Ninayajua matusi unayoteseka kutoka kwa watu wanaojiita Wateule wa Mungu.[h] Lakini si Wayahudi halisi. Watu hao ni wa kundi[i] la Shetani. 10 Usiogope mambo yatakayokupata hivi karibuni. Ninakwambia, Ibilisi atawafunga gerezani baadhi yenu ili kuipima imani yenu. Mtateseka kwa siku kumi, lakini iweni waaminifu, hata ikiwa mtatakiwa kufa. Mkiendelea kuwa waaminifu, nitawapa thawabu[j] ya uzima wa milele.
11 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa. Wale watakaoshinda hawatadhuriwa na mauti ya pili.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Pergamo
12 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo:
Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye na upanga wenye makali kuwili unaotoka katika kinywa chake.
13 Ninapafahamu mahali unapoishi. Unaishi mahali kilipo kiti cha enzi cha Shetani, lakini wewe ni mwaminifu kwangu. Hukukataa kueleza kuhusu imani yako kwangu hata wakati wa Antipa. Antipa alikuwa shahidi wangu mwaminifu[k] aliyeuawa katika mji wako, mji ambao shetani anaishi.
14 Lakini nina vitu vichache kinyume nawe. Una watu huko wanaofuata mafundisho ya Balaamu. Balaamu alimfundisha Balaki namna ya kuwafanya watu wa Israeli kutenda dhambi. Walitenda dhambi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa ajili ya sanamu na kwa kufanya uzinzi. 15 Ndivyo ilivyo hata kwa kundi lako. Una watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai. 16 Hivyo igeuzeni mioyo yenu! Msipobadilika, nitakuja kwenu haraka na kupigana kinyume na watu hawa kwa kutumia upanga unaotoka katika kinywa changu.
17 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa!
Kila atakayeshinda nitampa mana iliyofichwa. Pia nitampa kila mshindi jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya juu yake. Na hakuna atakayejua jina hili isipokuwa yule atakayepata jiwe hili.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Thiatira
18 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira:
Huu ni ujumbe kutoka kwa Mwana wa Mungu, aliye na macho yanayong'aa kama moto na miguu kama shaba inayong'aa.
19 Ninayajua matendo yako. Ninajua kuhusu upendo wako, imani yako, huduma yako na uvumilivu wako. Ninajua kwamba unafanya zaidi sasa kuliko ulivyofanya kwanza. 20 Lakini ninalo hili kinyume nawe: Umemruhusu yule mwanamke Yezebeli afanye anachotaka. Anasema kwamba yeye ni nabii,[l] lakini anawapotosha watu wangu kwa mafundisho yake. Yezebeli huwaongoza watu wangu kutenda dhambi ya uzinzi na kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu. 21 Nimempa muda ili aubadili moyo wake na kuiacha dhambi yake, lakini hataki kubadilika.
22 Hivyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso. Na wale wote wanaozini naye watateseka sana. Nitafanya hivi sasa ikiwa hawataacha mambo anayofanya. 23 Pia, nitawaua wafuasi wake. Ndipo makanisa yote wataona kuwa mimi ndiye ninayefahamu kile ambacho watu wanadhani na kufikiri. Na nitamlipa kila mmoja wenu kutokana na kile alichotenda.
24 Lakini ninyi wengine mlioko Thiatira ambao hamjafuata mafundisho yake. Hamjajifunza mambo yanayoitwa ‘Siri za ndani za Shetani.’ Hivi ndivyo ninawaambia: Sitawatwika mzigo wowote. 25 Shikeni katika kweli mliyo nayo tu mpaka nitakapo kuja.
26 Nitawapa nguvu juu ya mataifa wale wote watakaoshinda na wakaendelea kutenda yale ninayotaka mpaka mwisho. 27 Watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma. Watayavunja vipande vipande kama vyombo vya udongo wa mfinyanzi.[m] 28 Watakuwa na nguvu ile ile niliyoipokea kutoka kwa Baba yangu, na nitawapa nyota ya asubuhi. 29 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Sardi
3 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi:
Huu ni ujumbe kutoka kwake Yeye mwenye roho saba na nyota saba.
Ninayajua matendo yako. Watu husema kuwa u hai, lakini hakika umekufa. 2 Amka! Jitie nguvu kabla ya nguvu kidogo uliyonayo haijakuishia kabisa. Unachofanya hakistahili kwa Mungu wangu. 3 Hivyo usisahau kile ulichopokea na kusikia. Ukitii. Geuza moyo na maisha yako! Amka, la sivyo nitakuja kwako na kukushtukiza kama mwizi. Hautajua wakati nitakapokuja.
4 Lakini una watu wachache katika kundi lako hapo Sardi waliojiweka safi. Watatembea pamoja nami. Watavaa nguo nyeupe, kwa kuwa wanastahili. 5 Kila atakayeshinda atavikwa nguo nyeupe kama wao. Sitayafuta majina yao katika kitabu cha uzima. Nitawakiri mbele za Baba yangu na malaika zake ya kuwa wao ni wangu. 6 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.
Barua ya Yesu kwa kanisa la Filadelfia
7 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia:
Huu ni ujumbe kutoka kwake aliye mtakatifu na wa kweli, anayeshikilia ufunguo wa Daudi. Anapofungua kitu, hakiwezi kufungwa. Na anapofunga kitu hakiwezi kufunguliwa.
8 Ninayajua matendo yako. Nimeweka mbele yako mlango ulio wazi ambao hakuna anayeweza kuufunga. Ninajua wewe ni dhaifu, lakini umeyafuata mafundisho yangu. Hukuogopa kulisema jina langu. 9 Sikiliza! Kuna kundi[n] la Shetani. Wanasema kuwa wao ni Wayahudi, lakini ni waongo. Si Wayahudi halisi. Nitawafanya waje mbele yako na kusujudu kwenye miguu yako. Watajua ya kuwa ninakupenda. 10 Umeifuata amri yangu kwa uvumilivu. Hivyo nitakulinda wakati wa shida itakayokuja ulimwenguni, wakati ambapo kila aishiye duniani atajaribiwa.
11 Naja upesi. Ishikilie imani uliyonayo, ili mtu yeyote asiichukue taji yako. 12 Wale watakaoshinda watakuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu. Hawataliacha hekalu la Mungu tena. Nitaandika juu yao jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu. Mji huo ni Yerusalemu mpya.[o] Unateremka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Pia nitaandika jina langu jipya juu yao. 13 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.
Barua ya Yesu kwa Kanisa la Laodikia
14 Andika hivi kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia:
Huu ni ujumbe kutoka kwa yeye aliye Amina,[p] shahidi mwaminifu na wa kweli, aliye chanzo cha uumbaji wa Mungu.
15 Ninayajua matendo yako. Wewe si moto wala baridi. Ninatamani kama ungekuwa moto au baridi! 16 Lakini wewe ni vuguvugu tu, si moto, wala baridi. Hivyo niko tayari kukutema utoke mdomoni mwangu. 17 Unasema wewe ni tajiri. Unadhani ya kuwa umekuwa tajiri na huhitaji kitu chochote. Lakini hujui kuwa wewe ni mnyonge, mwenye masikitiko, maskini, asiyeona na uko uchi. 18 Ninakushauri ununue dhahabu kutoka kwangu, dhahabu iliyosafishwa katika moto. Kisha utakuwa tajiri. Nakuambia hili: Nunua kwangu mavazi meupe. Ndipo utaweza kuifunika aibu ya uchi wako. Ninakuagiza pia ununue kwangu dawa ya kuweka kwenye macho yako, nawe utaweza kuona.
19 Mimi huwasahihisha na kuwaadhibu wale niwapendao. Hivyo onesha kuwa kuishi kwa haki ni muhimu kwako kuliko kitu kingine. Geuzeni mioyo na maisha yenu. 20 Niko hapa! Nimesimama mlangoni nabisha hodi. Ikiwa utaisikia sauti yangu na ukaufungua mlango, nitaingia kwako na kula pamoja nawe. Nawe utakula pamoja nami.
21 Nitamruhusu kila atakayeshinda kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi. Ilikuwa vivyo hivyo hata kwangu. Nilishinda na kuketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. 22 Kila anayesikia hili azingatie kile ambacho Roho anayaambia makanisa.”
© 2017 Bible League International