Beginning
1 Salamu kutoka kwa mzee.[a]
Kwa mwanamke[b] aliyechaguliwa na Mungu na kwa wanawe.
Kweli kabisa, ninawapenda ninyi nyote. Na sio mimi peke yangu. Bali wote wanaoifahamu kweli[c] wanawapenda vile vile. 2 Tunawapenda kwa sababu ya kweli, ile kweli iliyomo ndani yetu. Kweli inayoendelea kuwemo ndani yetu milele yote.
3 Neema, rehema, na amani itakuwa pamoja nasi kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa mwanaye, Yesu Kristo, kwa kadri tuishivyo katika kweli na upendo.
4 Nilikuwa na furaha sana baada ya kufahamu habari za baadhi ya watoto wako. Nina furaha kuwa wanaifuata njia ya kweli, kama vile baba alivyo tuamuru. 5 Na sasa, mwanamke mwema, nina ombi hili: na tupendane sisi kwa sisi. Hii si amri mpya. Ni amri ile ile tuliyo kuwa nayo tangu mwanzo. 6 Na hii ndiyo maana ya kupenda: kuishi kulingana na amri zake. Na amri ya Mungu ni hii: Kwamba muishi maisha ya upendo. Mliisikia amri hii toka mwanzo.
7 Walimu wengi wa uongo wamo duniani sasa. Wana kataa kusema Yesu ni Masihi aliyekuja duniani na kufanyika mwanadamu. Kila anayekataa kuikubali kweli hii ni mwalimu wa uongo na adui wa Kristo. 8 Muwe waangalifu! Msiipoteze thawabu tuliyokwisha[d] kuitendea kazi. Mhakikishe mnaipokea thawabu kamili.
9 Kila mmoja aendelee kuyashika mafundisho aliyefundishwa juu Kristo tu. Yeyote atakayeyabadili mafundisho hayo hana Mungu. Kila anayeendelea kuyafuata mafundisho ya Kristo[e] anao wote Baba na Mwanaye. 10 Msiwakubali wale wanaowaijia lakini hawawaletei mafundisho haya. Msiwakaribishe katika nyumba zenu. Msiwape salamu zenu. 11 Kama mkiwakaribisha na kuwasalimu, mnawasaidia katika kazi zao za uovu.
12 Nina mengi ya kuwaambia. Lakini sitaki kutumia karatasi na wino. Badala yake, nataraji kuja kuwatembelea. Kisha tunaweza kujumuika pamoja na kuzungumza uso kwa uso. Ndipo furaha yetu itakamilika. 13 Watoto wa dada[f] yako aliyechaguliwa na Mungu wamekutumia upendo wao.
1 Salamu toka kwa mzee.[a]
Kwa rafiki mpendwa gayo, mtu ni mpendae kwa dhati.
2 Rafiki yangu mpendwa, najua kwamba unaendelea vizuri kiroho, kwa hiyo ninaomba kuwa mengine yote yaendelee vizuri pia nawe uwe na afya njema. 3 Baadhi ya waamini walikuja na kunieleza juu ya kweli[b] iliyo katika maisha yako. Waliniambia kuwa unaendelea kuifuata njia ya kweli. Hili lilinifanya nijisikie furaha sana. 4 Daima hili hunipa furaha iliyo kuu ninaposikia kuwa wanangu wanaifuata njia ya kweli.
5 Rafiki yangu mpendwa, inapendeza kuwa unaonesha uaminifu wako katika kazi yako yote miongoni mwa waaminio. Wengine ambao huwajui. 6 Hao waliliambia kanisa juu ya upendo ulio nao. Tafadhali wasaidie kuendelea na safari yao. Wasaidie katika njia ambayo itampendeza Mungu. 7 Safari hiyo waliyoenda ni ya kumtumikia Kristo. Hawakupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini. 8 Hivyo inatupasa kuwasaidia. Tunapowasaidia, tunashiriki kazi yao katika ile kweli.
9 Niliandika barua kwa kanisa, ila Diotrefe hasikilizi yale tunayosema. Yeye daima anataka kuwa kiongozi. 10 Nitakapokuja, nitaongea naye mbele ya kanisa juu ya hiki anachokifanya. Anadanganya na kusema mambo mabaya juu yetu, lakini hayo siyo yote. Anakataa kuwapokea na kuwasaidia wanaoamini wanaosafiri kwenda huko. Na hawaruhusu watu wengine kuwasaidia. Kama wakifanya hivyo, anawazuia wasikusanyike na kanisa tena.
11 Rafiki yangu mpendwa, usiige lililo baya; bali iga lililo jema. Yeyote anayetenda yaliyo mema hutoka kwa Mungu. Ila yeyote anayetenda maovu bado hajamjua Mungu.
12 Kila mtu azungumza yaliyo mema juu ya Demetrio, na kweli inakubaliana na yale wasemayo. Pia, twasema mema juu yake. Na unafahamu kuwa tusemayo ni kweli.
13 Nina mambo mengi nataka kukueleza. Lakini sipendi kutumia kalamu na wino. 14 Natumaini kukutembelea hivi karibuni. Hapo tunaweza kukaa pamoja na kuongea uso kwa uso. 15 Amani kwako. Rafiki walio pamoja nami hapa wakutumia upendo wao. Tafadhali wapatie upendo wetu kila rafiki waliopo huko.
1 Salamu kutoka kwa Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo. Kwa wale waliochaguliwa na kupendwa na Mungu Baba na kulindwa ndani ya Yesu Kristo.
2 Rehema, amani na upendo viwe pamoja nanyi zaidi na zaidi.
Mungu Atawaadhibu Watendao Mabaya
3 Rafiki wapendwa, nilitaka sana kuwaandikia kuhusu wokovu tunaoshiriki pamoja. Lakini nimejisikia kuwa ni muhimu niwaandikie kuhusu kitu kingine: Ninataka kuwatia moyo kuipigania kwa nguvu imani ambayo Mungu aliwapa watakatifu wake. Mungu alitoa imani hii mara moja na ni nzuri wakati wote. 4 Baadhi ya watu wamejiingiza kwa siri kwenye kundi lenu. Watu hawa wamekwisha kuhukumiwa kuwa wakosaji kwa sababu ya matendo yao. Zamani zilizopita manabii waliandika kuhusu watu hao. Wako kinyume na Mungu. Wameigeuza neema ya Mungu kujihalalishia kutenda chochote wanachotaka. Wanakataa kumtii Mkuu aliye peke yake, Bwana wetu Yesu Kristo.
5 Ninataka kuwasaidia mkumbuke baadhi ya vitu mnavyovifahamu tayari: Kumbukeni kwamba Bwana[a] aliwaokoa watu wake kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini. 6 Na kumbukeni malaika waliopoteza mamlaka yao ya kutawala. Waliacha mahali pao pa kuishi. Hivyo Bwana amewaweka gizani, wamefungwa kwa minyororo ya milele, mpaka watakapohukumiwa siku iliyo kuu. 7 Pia kumbukeni miji ya Sodoma na Gomora na miji mingine iliyoizunguka. Kama wale malaika, watu wa miji ile walikuwa na hatia ya dhambi ya uzinzi, hata wakataka kuzini na malaika. Na waliadhibiwa kwa moto wa milele. Miji hii ni mfano kwa waovu watakaoteseka kwa adhabu ya moto wa milele.
8 Ni sawasawa na watu hawa waliojiingiza kwenye kundi lenu. Wanaongozwa na ndoto, wanajichafua wenyewe kwa dhambi. Wanapuuza mamlaka ya Bwana na kusema mambo mabaya kinyume na walio watukufu.[b] 9 Hata malaika mkuu Mikaeli hakufanya hivi. Mikaeli alibishana na Ibilisi kuhusu nani angeuchukua mwili wa Musa. Lakini Mikaeli hakutamka hukumu kwa Ibilisi kwa mashitaka yake ya uongo. Badala yake, Mikaeli alisema, “Bwana mwenyewe akuadhibu!”
10 Lakini watu hawa hukashifu mambo wasiyoyaelewa. Wanaelewa baadhi ya mambo, isipokuwa wanayaelewa mambo haya si kwa kufikiri bali kwa kuhisi, kama wanyama wasiofikiri. Na haya ni mambo yanayowaangamiza. 11 Itakuwa vibaya kwao kwa kuwa wameifuata njia ambayo Kaini[c] aliitumia. Kwa kutafuta fedha, wamejiingiza katika kosa lile lile la Balaamu.[d] Wamepigana kinyume na Mungu kama alivyofanya Kora.[e] Na wataangamizwa vile vile kama Kora.
12 Watu hawa ni kama madoa machafu miongoni mwenu, wanawatia aibu mnapokutanika pamoja kuonesha upendo miongoni mwenu na kula chakula kwa pamoja kama kanisa. Pasipo kuwa na aibu wanakula pamoja nanyi. Wanajijali wao wenyewe tu. Wao ni kama mawingu yasiyo na mvua yanayosukumwa na upepo kila upande. Wako kama miti isiyo na matunda wakati wa mavuno ambayo hung'olewa kutoka ardhini. Hivyo wamekufa mara mbili. 13 Kama mapovu machafu juu ya mawimbi ya bahari, kila mtu anaweza kuona mambo ya aibu wanayoyafanya. Ni kama nyota zinazotangatanga angani. Nao wameandaliwa mahali penye giza kuu milele.
14 Henoko, mtu wa kizazi cha saba kutoka Adamu, alisema hivi kuhusu watu hawa: “Tazama! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika watakatifu. 15 Kumhukumu kila mmoja. Atawaadhibu wale wote walio kinyume naye kutokana na maovu waliyotenda kwa sababu ya kutokumheshimu. Ndiyo, Bwana atawaadhibu watenda dhambi wote hawa wasiomheshimu. Atawaadhibu kwa sababu ya mambo maovu waliyosema kinyume naye.”
16 Watu hawa daima hulalamika na kutafuta ubaya kwa wengine. Daima hutenda mambo maovu wanayotaka kufanya. Hujisifu wenyewe. Huwatendea vyema baadhi ya watu kuliko wengine ili wapate vitu wanavyovitaka.
Tahadhari na Mambo ya Kufanya
17 Rafiki wapendwa, kumbukeni mambo ambayo mitume wa Bwana Yesu Kristo walisema kuwa yatatokea. 18 Walisema, “Katika nyakati za mwisho kutakuwa watu wanaomcheka Mungu na kufanya yale wanayotaka kufanya tu, mambo ambayo ni kinyume na Mungu.” 19 Hawa ni watu wanaowagawa katika makundi. Si wa rohoni kwa sababu hawana Roho Mtakatifu.
20 Lakini ninyi, rafiki wapendwa, itumieni imani yenu takatifu zaidi kusaidiana ninyi kwa ninyi ili muwe imara zaidi katika imani. Ombeni kwa msaada wa Roho Mtakatifu. 21 Jiwekeni salama katika upendo wa Mungu, kadri mnavyomsubiri Bwana Yesu Kristo kuionesha rehema yake kwenu kwa kuwapa uzima wa milele.
22 Waonesheni rehema walio na mashaka. 23 Waokoeni wale wanaoishi katika hatari ya moto wa jehanamu. Muwatendee wengine kwa rehema, lakini muwe waangalifu kuwa maisha yao maovu yasichafue mwenendo wenu mwema.[f]
Msifuni Mungu
24 Mungu ana nguvu na anaweza kuwafanya msianguke. Anaweza kuwaingiza katika uwepo wa utukufu wake bila makosa yoyote ndani yenu na akawapa furaha kuu. 25 Ni Mungu peke yake, aliye Mwokozi wetu. Kwake uwepo utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kupitia Yesu Kristo kwa wakati uliopita, uliopo na milele. Amina.
© 2017 Bible League International