Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
1 Yohana 1-3

Tunataka tuwaambie juu ya Neno[a] linalo toa uzima. Yeye aliyekuwepo tangu mwanzo. Huyu ndiye yule tuliyemsikia na kumwona kwa macho yetu. Tuliyaona mambo aliyeyafanya, na mikono yetu ilimgusa. Ndiyo, yeye aliye uzima alidhihirishwa kwetu. Tulimwona, na hivyo tunaweza kuwaeleza wengine juu yake. Sasa tunawaeleza habari kwamba yeye ndiye uzima wa milele aliyekuwa pamoja na Mungu Baba na alidhihirishwa kwetu. Tuna wasimulia mambo tuliyoyaona na kuyasikia kwa sababu tunawataka muwe na ushirika pamoja nasi. Ushirika tulionao ni pamoja na Mungu Baba na mwanaye Yesu Kristo. Tunawaandikia mambo haya ili furaha yetu iwe kamili.

Mungu Anatusamehe Dhambi Zetu

Tulisikia mafundisho ya kweli toka kwa Mungu. Na sasa tunayasimulia kwenu. Mungu ni nuru, na ndani yake hamna giza. Kwa hiyo kama tukisema kuwa tunashirikiana na Mungu, lakini tukaendelea kuishi katika giza, tunakuwa ni waongo, tusioifuata kweli. Tunapaswa kuishi katika nuru, ambamo Mungu yupo. Kama tunaishi katika nuru, tunashirikiana sisi kwa sisi, na sadaka ya damu yake Yesu, Mwana wa Mungu, inatutakasa kila dhambi.

Kama tukisema kuwa hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na tumeikataa kweli. Lakini kama tukiungama dhambi zetu, Mungu atatusamehe. Tunaweza kumwamini Mungu kufanya hili. Kwa sababu Mungu daima hufanya lililo haki. Atatufanya tuwe safi toka kila dhambi tuliyofanya. 10 Kama tukisema kuwa hatujafanya dhambi, tunasema kuwa Mungu ni mwongo na tumeyakana mafundisho yake.

Yesu ni Msaidizi Wetu

Wapendwa wanangu, ninawaandikieni waraka huu ili kwamba msitende dhambi. Ila kama yeyote akitenda dhambi, tunaye Yesu Kristo wa kutusaidia. Yeye daima alitenda haki, kwa hiyo anaweza kututetea mbele za Mungu Baba. Yesu ndiye njia ambapo dhambi zetu zinaondolewa. Naye haziondoi dhambi zetu tu bali anaziondoa dhambi za watu wote.

Kama tukitii mambo ambayo Mungu ametuamuru kuyafanya, tunapata uhakika ya kuwa tunamjua. Kama tukisema kuwa tunamjua Mungu lakini hatuzitii amri zake, tunasema uongo. Kweli haimo ndani mwetu. Lakini tunapotii mafundisho ya Mungu, kwa hakika upendo wake unakamilika ndani yetu. Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa tunaishi ndani yake. Kama tukisema kuwa tunaishi ndani ya Mungu, ni lazima tuishi kwa namna ambvyo Yesu aliishi.

Yesu Alituagiza Kuwapenda Wengine

Wapendwa rafiki zangu, siwaandiki ninyi amri mpya. Ni amri ile ile ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ni fundisho lile lile ambalo mmekwishalisikia. Lakini kile ninachokiandika pia ni amri mpya. Ni kweli; Mnaweza kuiona kweli ndani ya Yesu na ndani yenu ninyi wenyewe. Giza linatoweka, na nuru ya kweli tayari inang'aa.

Mtu anaweza kusema, “Niko nuruni,” lakini ikiwa anamchukia ndugu yeyote katika familia ya Mungu, basi angali bado katika giza. 10 Wao wanaowapenda ndugu wanaishi katika nuru, na hakuna kitu ndani yao cha kuwafanya watende mabaya. 11 Lakini yeyote anayemchukia nduguye wa kike au wa kiume yuko gizani. Anaishi katika giza. Hajui anakoenda, kwa sababu giza limemfanya asiweze kuona.

12 Ninawaandikia, ninyi watoto wapendwa,
    kwa sababu dhambi zenu zimesamehewa kwa njia ya Kristo.
13 Ninawaandikia, ninyi akina baba,
    kwa sababu mnamjua yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia, ninyi vijana,
    kwa sababu mmemshinda yule mwovu.
14 Ninawaandikia ninyi watoto,
    kwa sababu mnamjua Baba.
Ninawaandikia ninyi, akina baba,
    kwa sababu mnamfahamu yeye aliyekuwepo tangu mwanzo.
Ninawaandikia ninyi, vijana,
    kwa sababu mna nguvu.
Mafundisho ya Neno la Mungu yimo ndani yenu,
    na mmemshinda yule mwovu.

15 Msiipende dunia hii ya uovu wala mambo yaliyomo ndani yake. Kama mkiipenda dunia, upendo wa baba haumo ndani yenu. 16 Yote yaliyomo katika dunia: yaani, tamaa halisi za kibinadamu, tamaa kwa yale mabaya tunayoyaona, na kiburi cha vitu tulivyonavyo. Lakini hakuna hata mojawapo ya haya litokalo kwa Baba. Yote yanatoka katika dunia. 17 Dunia inapita, na mambo yote ambayo watu wanayataka kutoka katika dunia nayo yanapita. Lakini yeyote atendaye mambo ambayo Mungu anayataka ataishi milele.

Msiwafuate Maadui wa Kristo

18 Wapendwa wanangu, mwisho umekaribia! Mmesikia kuwa adui wa Kristo anakuja. Na sasa maadui wengi wa Kristo tayari wapo hapa. Hivyo tunajua kwamba mwisho umekaribia. 19 Maadui hawa walikuwa miongoni mwetu, lakini walituacha. Hawakuwa wenzetu hasa. Kama wangelikuwa kweli wenzetu, wangebaki pamoja nasi. Lakini walituacha. Hii inaonesha kuwa hakuna hata mmoja wao aliyekuwa kwa hakika mwenzetu.

20 Mnayo karama[b] aliyowapa Yeye Aliye Mtakatifu.[c] Hivyo nyote mnaijua kweli. 21 Mnadhani ninawaandikia waraka huu kwa sababu hamuijui kweli? Hapana! Ninawaandikia kwa sababu mnaijua kweli. Na mnajua kuwa hakuna uongo utokao katika kweli.

22 Ni nani basi aliye mwongo? Ni yeye anayesema kuwa Yesu siyo Kristo. Yeyote anayesema hivyo ni adui wa Kristo. Yeye huyo asiyemwamini Baba wala Mwana. 23 Yeyote asiyemwamini Mwana hana Baba, ila yeye anayemkubali Mwana anaye Baba pia.

24 Mnapaswa kuendelea kuyafuata mafundisho mliyoyasikia tangu mwanzo. Kama mkifanya hivyo, mtakuwa siku zote katika Mwana na katika Baba. 25 Na hili ndilo ambalo Mwana ameliahidi kwetu sisi, uzima wa milele.

26 Ninawaandikia barua hii juu ya wale ambao wanataka kuwapotosha katika njia isiyo sahihi. 27 Kristo aliwapa karama maalumu.[d] Nanyi bado mngali na karama hiyo ndani yenu. Hivyo hamumhitaji yeyote kuwafundisha. Karama aliyowapa inawafundisha juu ya kila jambo. Ni karama ya kweli, si ya uongo. Hivyo endeleeni kuishi katika Kristo, kama karama yake ilivyowafundisha.

28 Ndiyo, wanangu wapendwa, ishini ndani yake. Kama tukifanya hivyo, hatutakuwa na hofu siku kristo atakapo kuja tena. Hatutahitaji kujificha na kuwa na aibu ajapo. 29 Mnajua ya kwamba daima Kristo alifanya yaliyo ya haki. Vivyo hivyo mnajua pia ya kwamba wote watendao haki ni watoto wa Mungu.

Tu Watoto wa Mungu

Baba ametupenda sisi sana! Hili linaonesha jinsi anavyotupenda: Tunaitwa watoto wa Mungu. Ni kweli kuwa tu watoto wa Mungu. Lakini watu waliomo duniani hawaelewi ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu, kwa sababu hawamjui yeye. Wapendwa, sasa tu watoto wa Mungu. Mungu hajatuonyesha bado namna tutakavyokuwa wakati unaoukuja. Lakini tunajua ya kwamba Kristo atakapokuja tena, tutafanana naye. Tutamwona kama alivyo. Ni mtakatifu, na kila aliye na matumaini haya katika yeye huendelea kuwa mtakatifu.

Kila atendaye dhambi huivunja sheria ya Mungu. Ndiyo, kutenda dhambi ni sawa na kuishi kinyume na sheria ya Mungu. Mwajua ya kuwa Kristo alikuja kuziondoa dhambi za watu. Haimo dhambi ndani ya Kristo. Hivyo kila anayeishi katika Kristo haendelei kutenda dhambi. Kama wakiendelea kutenda dhambi, kwa hakika hawajamwelewa Kristo na hawajamjua kamwe.

Watoto wapendwa, msimruhusu mtu yeyote kuwadanganya. Kristo daima alitenda yaliyo haki. Hivyo kuwa mwema kama Kristo, ni lazima utende yaliyo haki. Mwovu amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kila anayeendelea kutenda dhambi ni mali ya Mwovu. Mwana wa Mungu alikuja kwa ajili ya hili: Kuziharibu kazi za Mwovu.

Wale ambao ni watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi, kwa sababu wanayo maisha mapya waliyopewa na Mungu.[e] Hawaendelei kutenda dhambi, kwa sababu wamefanyika watoto wa Mungu. 10 Hivyo tunaweza kuwatambua walio watoto wa Mungu na walio watoto wa Mwovu. Hawa ndiyo wasio watoto wa Mungu: Wale wanaotenda mambo yasiyo haki na wale wasiowapenda ndugu zao wa kike na wa kiume katika familia ya Mungu.

Ni lazima Tupendane Sisi kwa Sisi

11 Haya ni mafundisho mliyoyasikia toka mwanzo: Ni lazima tupendane sisi kwa sisi. 12 Msiwe kama Kaini. Aliyekuwa upande wa Mwovu. Kaini alimwua ndugu yake. Lakini kwa nini alimwua? Ni kwa sababu alichokifanya Kaini kilikuwa cha kiovu, na alichokifanya nduguye kilikuwa cha haki.

13 Kaka zangu na dada zangu, msishangae watu wa dunia hii wakiwachukia. 14 Tunafahamu ya kuwa tumevuka kutoka mautini na kuingia uzimani. Tunafahamu hili kwa sababu tunapendana sisi kwa sisi kama ndugu wa kike na wa kiume. Yeyote asiyewapenda kaka zake na dada zake angali amekufa. 15 Kila anayemchukia nduguye anayeamini ni muuaji. Nanyi mnajua kuwa hakuna muuaji aliye na uzima wa milele.

16 Hivi ndivyo tunavyojua jinsi upendo wa kweli ulivyo: Yesu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Hivyo nasi tunapaswa kuyatoa maisha yetu, kwa ajili ya ndugu wa kike na wa kiume katika familia ya Kristo. 17 Itakuwaje pale muumini tajiri mwenye fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote akamwona dada ama kaka yake aliye maskini na asiye na fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote. Endapo muumini huyu tajiri hatamsaidia muumini yule maskini, basi ni wazi kwamba upendo wa Mungu haumo ndani ya muumini yule tajiri. 18 Watoto wangu, upendo wetu usiwe wa maneno na kuongea tu. Hapana, upendo wetu unapaswa kuwa halisi. Hatuna budi kuuonyesha upendo wetu kwa mambo yale tunayofanya.

19-20 Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa sisi tu wa ile njia ya kweli. Pale mioyo yetu inapotufanya tujisikie kuwa na hatia, bado tunaweza kuwa na amani mbele za Mungu, kwa sababu Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu. Yeye anajua kila kitu.

21 Rafiki zangu wapendwa, ikiwa hatujisikii kuwa tunatenda yasiyo haki, basi hatupaswi kuwa na hofu tunapoenda kwa Mungu. 22 Na Mungu anatupa kile tunachomwomba. Nasi tunapokea kwa sababu tunazitii amri za Mungu na kufanya yanayompendeza. 23 Hili ndilo Mungu analoliamuru: Kwamba tumwamini Mwanaye Yesu Kristo, na kwamba tupendane sisi kwa sisi kama alivyoamuru. 24 Wote wanaozitii amri za Mungu wanaishi ndani ya Mungu. Na Mungu anaishi ndani yao. Tunajuaje kuwa Mungu anaishi ndani yetu? Tunajua kwa sababu ya Roho aliyetupa sisi.

Yohana Aonya juu ya Walimu wa Uongo

Rafiki zangu wapenzi, manabii wengi wa uongo wapo duniani sasa. Hivyo msiiamini kila roho, lakini zijaribuni hizo roho ili muone kama zinatoka kwa Mungu. Hivi ndivyo mwezavyo kuitambua Roho ya Mungu. Roho inayosema, “Naamini kuwa Yesu ni Masihi aliye kuja duniani na akafanyika mwanadamu.” Roho hiyo inatoka kwa Mungu. Roho inayokataa kutamka hayo juu ya Yesu, hii ni roho iliyo adui kwa Kristo. Mmesikia kuwa adui wa kristo anakuja, na sasa amekwishakuja naye yupo tayari ulimwenguni.

Wanangu wapenzi, ninyi ni wa Mungu, hivyo mmeshawashinda tayari hawa manabii wa uongo. Hii ni kwa sababu yule aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliyeko duniani. Wao ni wa ulimwengu. Hivyo kile wanachokisema ni cha ulimwengu pia. Na ulimwengu husikia kile wanachokisema. Lakini sisi tunatokana na Mungu. Kwa hiyo watu wanaomjua Mungu hutusikia sisi. Lakini watu wasiotokana na Mungu hawatusikii sisi. Hivi ndivyo tunavyiojua Roho iliyo ya kweli na ile iliyo ya uongo.

Upendo Hutoka kwa Mungu

Wapenzi rafiki, tunatakiwa tupendane sisi kwa sisi, kwa sababu upendo watoka kwa Mungu. Yeyote apendae amefanyika mwana wa Mungu. Na kila apendae anamfahamu Mungu. Kila asiyependa hamfahamu Mungu, kwa sababu Mungu ni Pendo. Hivi ndivyo Mungu alivyo tuonyesha pendo lake sisi: Alimtuma mwanawe wa pekee ulimwenguni kutupatia sisi uzima katika yeye. 10 Upendo wa kweli ni upendo wa Mungu kwa ajili yetu, si upendo wetu kwa Mungu. Alimtuma mwanawe kama njia ya kuziondoa dhambi zetu.

11 Hivyo ndivyo Mungu atupendavyo, rafiki wapenzi! Kwa hiyo tupendane sisi kwa sisi. 12 Hakuna aliyemwona Mungu. Ila tukipendana sisi kwa sisi, Mungu anaishi ndani yetu. Kama tukipendana sisi kwa sisi, Upendo wa Mungu unafikia shabaha yake na unafanywa kamili ndani yetu.

13 Twatambua kuwa tunaishi katika Mungu na mungu ndani yetu. Twalitambua hilo kwa sababu ametupa Roho wake. 14 Tumeona kuwa Baba alimtuma mwanaye aje kuwa Mwokozi wa ulimwengu, na hili ndilo tunalowaambia watu sasa. 15 Yeyote anayesema, “Naamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu,” huyo ni mtu anayeishi ndani ya Mungu, na Mungu anaishi ndani ya mtu huyo. 16 Hivyo twalifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu, na tunalitumainia pendo hilo.

Mungu ni pendo. Kila anae ishi katika pendo anaishi ndani ya Mungu, na Mungu ndani yao. 17 Kama pendo la Mungu limekamilishwa ndani yetu, tunaweza kuwa bila hofu siku ambayo Mungu atahukumu ulimwengu. Hatutakuwa na hofu, kwa sababu katika ulimwengu huu tunaishi kama Yesu.[f] 18 Palipo na upendo wa Mungu, hakuna hofu, kwa sababu upendo wa Mungu ulio kamili unaondoa hofu. Ni hukumu yake ndiyo inayomfanya mtu kuwa na hofu. Hivyo pendo lake halikamilishwi kwa mtu ambaye ndani yake kuna hofu.

19 Tunapenda kwa sababu Mungu alitupenda sisi kwanza. 20 Kama tukisema kuwa tunampenda Mungu na tunamchukia mmojawapo wa kaka na dada zetu katika familia ya Mungu, basi sisi tu waongo. Kama hatuwezi kumpenda mtu tunayemwona, tutawezaje kumpenda Mungu, ambaye hata hatujamwona. 21 Mungu ametupa amri hii: Kama tunampenda Mungu, Ni lazima pia tupendane sisi kwa sisi kama kina kaka na kina dada.

Watoto wa Mungu Ushindeni Ulimwengu

Watu wanao amini kuwa Yesu ni Masihi ni wana wa Mungu. Na kila ampendae Baba pia anawapenda watoto wa Baba. Twatambuaje kuwa tunawapenda watoto wa Mungu? Twatambua kwa sababu tunampenda Mungu na tunazitii amri zake. Kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na amri za Mungu si ngumu kwetu, kwa sababu kila ambae ni mwana wa Mungu ana uwezo wa kushinda dhidi ya ulimwengu. Ni imani yetu iliyoshinda vita dhidi ya ulimwengu. Hivyo ni nani anayeushinda ulimwengu? Ni wale tu wanaoamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu.

Mungu alituambia kwa Habari ya Mwanae

Yesu Kristo ndiye aliyekuja. Alikuja kwa maji na damu.[g] Hakuja kwa maji peke yake. Lahasha, Yesu alikuja kwa vyote maji na damu. Na Roho atuambia kuwa hili ni kweli. Roho ndiye Kweli. Kwa hiyo kuna mashahidi watatu wanao tuambia habari za Yesu: Roho, Maji, na Damu. Mashuhuda hawa watatu wanakubaliana.

Tunawaamini watu wanaposema jambo llililo kweli. Lakini kile anachosema Mungu ni muhimu zaidi. Na Hivi ndivyo Mungu alivyotuambia: Alituambia ukweli kuhusu Mwanaye. 10 Kila amwaminiye Mwana wa Mungu anayo kweli ambayo Mungu alituambia. Lakini watu wasiomwamini Mungu wanamfanya Mungu kuwa mwongo, kwa sababu hawaamini kile ambacho Mungu ametueleza kuhusu mwanaye. 11 Hiki ndicho ambacho Mungu alitueleza: Mungu ametupatia uzima wa milele, na uzima huu umo katika wanawake. 12 Yeyote aliye na mwana anao uzima wa milele, lakini asiye na mwana wa mungu hana huo uzima wa milele.

Tunao uzima wa Milele Sasa

13 Ninawaandikia barua hii ninyi mnaomwamini Mwana wa Mungu ili mjue ya kwamba sasa mnao uzima wa milele. 14 Tunaweza kwenda kwa Mungu tukiwa na ujasiri huo. Hii ina maana kuwa tunapomwomba Mungu mambo (na mambo hayo yakakubaliana na matakwa yake kwetu), Mungu huyajali yale tunayosema. 15 Hutusikiliza kila wakati tunapomwomba. Hivyo tunatambua kuwa yeye hutupa kila tunachomwomba.

16 Utakapomwona muumini mwenzio akitenda dhambi (Dhambi isiyomwongoza kwenye mauti), unapaswa kumwombea. Kisha Mungu atampa uzima. Ipo aina ya dhambi inayomwongoza mtu hadi mauti ya milele. Sina maana ya kusema unapaswa kuombea aina hiyo ya dhambi. 17 Daima kutenda yasiyo haki ni dhambi. Lakini ipo dhambi isiyomwongoza mtu katika mauti ya milele.

18 Tunajua kwamba wale waliofanyika watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi. Mwana wa Mungu anawahifadhi salama.[h] Yule Mwovu hawezi kuwagusa. 19 Tunajua kwamba sisi ni wa Mungu, Lakini yule Mwovu anautawala ulimwengu wote. 20 Nasi tunajua kwamba Mwana wa Mungu amekuja na ametupa uelewa. Hivyo sasa tunaweza kumjua yeye aliye kweli, na tunaishi katika Mungu huyo wa kweli. Nasi tumo ndani ya mwanaye, Yesu Kristo. Yeye ndiye Mungu wa kweli, naye ndiye uzima wa milele. 21 Kwa hiyo, watoto wapendwa, mjiepushe na miungu wa uongo.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International