Beginning
1 Salamu kutoka kwa Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo.
Kwenu ninyi nyote mliopokea imani inayowapa baraka sawa nasi. Mlipewa imani kwa sababu Mungu wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo hufanya yaliyo mema na haki.
2 Mpewe neema na amani zaidi na zaidi, kwa sababu sasa mnamjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
Mungu Ametupa Kila Kitu Tunachohitaji
3 Yesu ana nguvu ya Mungu. Na nguvu yake imetupa heshima ili tuishi maisha yanayomtukuza na kumpendeza Mungu. Tuna vitu hivi kwa sababu tunamjua. Yesu alitualika kwa utukufu na nguvu ya uungu wake. 4 Na kupitia haya, alitupa ahadi kuu mno. Ili kwamba kwa hizo mnaweza kushiriki katika kuwa kama Mungu na ukaepuka maangamizo ya kiroho yanayokuja kwa watu ulimwenguni kwa sababu ya mambo maovu wanayotaka.
5 Kwa sababu mna baraka hizi, jitahidini kadri mnavyoweza kuongeza mambo haya: katika imani yenu ongezeni wema, katika wema wenu ongezeni maarifa; 6 katika maarifa yenu ongezeni kiasi; katika kiasi chenu ongezeni uvumilivu; katika uvumilivu wenu ongezeni kumwabudu Mungu; 7 katika kumwabudu Mungu kwenu ongezeni huruma kwa ndugu katika Kristo na kwa wema huu ongezeni upendo. 8 Ikiwa mambo haya yote yatakaa ndani yenu na kukua, mtazaa matunda mazuri yakiwa ni matokeo ya ninyi kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. 9 Lakini wale wasiokua na sifa hizi ndani yao ni wasiyeona. Hawataweza kuona kwa uwazi yale waliyonayo. Wamesahau kuwa dhambi zao ziliondolewa kutoka kwao na wakawa safi.
10 Ndugu zangu, Mungu aliwaita na akawachagua ili muwe wake. Jitahidini mhakikishe kuwa mnapata yale aliyonayo Mungu kwa ajili yenu. Mkifanya hivi hamtajikwa na kuanguka. 11 Na mtakaribishwa kwa baraka kuu katika ufalme usio na mwisho, ufalme wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
12 Mnayajua mambo haya tayari. Mko imara katika kweli mliyo nayo. Lakini daima nitajitahidi kuwakumbusha. 13 Nikiwa bado naishi hapa duniani, nadhani ni sahihi kwangu kuwakumbusha. 14 Ninajua kuwa ni lazima nitauacha mwili huu kitambo kijacho kwani Bwana wetu Yesu Kristo amenionyesha. 15 Nitafanya kwa kadri ninavyoweza kuhakikisha kuwa daima mtayakumbuka mambo haya hata baada ya kifo changu.
Tuliuona Utukufu wa Kristo
16 Tuliwaambia kuhusu nguvu ya Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake katika nguvu kuu. Mambo tuliyowaambia hayakuwa simulizi za kuvutia zilizotungwa watu. Hapana, tuliuona ukuu wa Yesu kwa macho yetu wenyewe. 17 Yesu aliisikia sauti ya Mungu Mkuu na Mwenye Mtukufu alipopokea heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba. Sauti ilisema, “Huyu ni Mwanangu, ninayempenda. Ninafurahishwa naye.” 18 Nasi tuliisikia sauti hiyo. Sauti hiyo ilitoka mbinguni tulipokuwa na Yesu juu ya mlima mtakatifu.[a]
19 Hili linatufanya tuwe na ujasiri kwa yale waliyosema manabii. Na ni vizuri ninyi mkifuata yale waliyosema, ambayo ni kama mwanga unaoangaza mahali penye giza. Mna mwanga unaoangaza mpaka siku inapoanza na nyota ya asubuhi huleta mwanga mpya katika fahamu zenu. 20 Jambo la muhimu kuliko yote ambalo ni lazima mlielewe ni hili ya kwamba hakuna unabii katika Maandiko unaotokana na mawazo ya nabii. 21 Nabii hakusema kile alichotaka kusema. Lakini wanadamu waliongozwa na Roho Mtakatifu kusema ujumbe uliotoka kwa Mungu.
Walimu wa Uongo
2 Hapo zamani walikuwepo manabii wa uongo miongoni mwa watu wa Mungu. Ndivyo itakavyokuwa miongoni mwenu hata sasa. Watakuwepo walimu wa uongo katika kundi lenu, watakaoingiza mawazo yao wenyewe yatakayowaangamiza watu. Na watafundisha kwa werevu ambao mtashindwa kujua kuwa ni waongo. Watakataa hata kumtii Bwana aliwanunua. Na hivyo watajiangamiza haraka wao wenyewe. 2 Watu wengi watawafuata katika mambo madaya ya kimaadili wanayotenda. Na kwa sababu yao, wengi wataikashifu njia ya kweli tunayoifuata. 3 Manabii hawa wa uongo wanachotaka ni pesa zenu tu. Hivyo watawatumia ninyi kwa kuwaambia mambo yasiyo ya kweli. Lakini hukumu ya walimu hawa wa uongo imekwisha andaliwa kwa muda mrefu wala hawatakwepa. Mungu atawaangamiza, hajalala usingizi.
4 Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwaacha bila kuwaadhibu. Aliwatupia kuzimu. Aliwaweka malaika wale katika mapango yenye giza, wanakofungiwa mpaka wakati watakapohukumiwa na Mungu.
5 Na Mungu aliwaadhibu watu waovu walioishi zamani. Alileta gharika katika ulimwengu uliojaa watu waliokuwa kinyume na Mungu. Lakini alimwokoa Nuhu na watu wengine saba waliokuwa pamoja naye. Nuhu ndiye aliyewaambia watu kuhusu kuishi kwa haki.
6 Pia, Mungu aliiadhibu miji miovu ya Sodoma na Gomora. Aliichoma kwa moto mpaka kila kitu kikawa majivu. Alitumia miji hiyo kama mfano wa kile kitakachowapata watu walio kinyume na Mungu. 7 Lakini alimwokoa Lutu, mtu mwema aliyeishi huko. Lutu aliugua sana moyoni kutokana na mwenendo wa kimaisha usiofaa na matendo ya uasi ya wale watu. 8 Kila siku mtu huyu mwema aliishi miongoni mwa watu walioharibika, na moyo wake mwema uliumia kutokana na uhalifu na uvunjaji wa sheria aliyouona na kusikia.
9 Unaona namna ambavyo Mungu anajua kuwaokoa wale wanaomheshimu kutokana na matatizo yao. Na Bwana anajua jinsi ya kuwaweka watu waovu kifungoni hadi atakapowaadhibu siku ya hukumu. 10 Hukumu hiyo ni kwa wale ambao daima wanaofuata tamaa za udhaifu wao wa kibinadamu. Hiyo ni kwa ajili ya wale ambao wanadharau mamlaka ya Bwana.
Walimu hawa wa uongo hufanya chochote wanachotaka, na hujivuna sana. Wala hawaogopi kuwanenea mabaya viumbe wenye nguvu walioko angani. 11 Malaika wa Mungu ni hodari zaidi na wana nguvu kuliko viumbe hawa. Lakini hata hivyo malaika hao wa Mungu hawawatukani na kuwanenea mabaya viumbe hawa mbele za Bwana.
12 Lakini walimu hawa wa uongo wanasema uovu dhidi ya mambo wasiyoyaelewa. Wako kama wanyama ambao hufanya mambo bila ya kufikiri, ni kama wanyama wa porini waliozaliwa ili wakamatwe na kuuawa. Nao kama wanyama wataangamizwa. 13 Wamesababisha watu wengi kuteseka. Hivyo hata wao watateseka. Hayo ndiyo malipo yao kwa yale waliyofanya.
Wanadhani ni jambo la kufurahisha kutenda dhambi ambapo kila mtu anaweza kuwaona. Wanazifikiria sherehe zenye matendo yasiyofaa hata wakati wa mchana kweupe. Hivyo wao ni kama madoa ya uchafu na ni fedheha mnapokula pamoja nao. 14 Kila wakati wanapomwona mwanamke, wanamtamani na kumtaka. Wanatenda dhambi kwa njia hii daima. Na wanawasababisha wanyonge kutenda dhambi. Wamejifunza vyema wao wenyewe kuwa walafi. Wako chini ya laana.[b]
15 Walimu hawa wa uongo waliiacha njia sahihi na wakaiendea njia mbaya. Waliifuata njia ile ile aliyoifuata Balaamu. Alikuwa mwana wa Beori, aliyependa kulipwa kwa kufanya mabaya. 16 Alikemewa na punda kwa sababu alikuwa anatenda jamba baya. Punda alizungumza kwa sauti ya kibinadamu na akamzuia nabii yule kutenda kwa wazimu.
17 Walimu hawa wa uongo ni kama chemichemi zisizo na maji. Ni kama mawingu yanayosukumwa na dhoruba. Mahali penye giza nene pameandaliwa kwa ajili yao. 18 Wanajisifu kwa maneno yasiyo na maana. Wanawaongoza watu katika mitego ya dhambi. Wanawatafuta watu ambao wamechana na maisha ya kutenda dhambi na wanawarudisha tena katika kutenda dhambi. Wanafanya hivi kwa kutumia mambo ya aibu ambayo watu wanataka kuyatenda katika mapungufu yao ya kibinadamu. 19 Walimu hawa wa uongo wanawaahidi watu hao uhuru, lakini wao wenyewe hawako huru. Ni watumwa wa akili iliyoharibiwa na dhambi. Ndiyo, watu ni watumwa wa kitu chochote kinachowashinda.
20 Watu wanaweza kuwekwa huru ulimwenguni kutoka katika matendo ya aibu. Wanaweza kuyakwenda haya kwa kumwamini Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Lakini wakiyarudia maovu hayo na yakawatawala, hali yao inakuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzoni. 21 Ndiyo, ingekuwa bora kwao kutoijua kamwe njia sahihi. Ingekuwa bora kuliko kuijua njia sahihi kisha kugeuka kutoka katika mafundisho matakatifu waliyopewa. 22 Walichofanya ni kama “Mbwa anayekula matapishi yake.”(A) Na “Kama nguruwe aliyeoshwa, kisha anarudi kugaagaa matopeni.”
Yesu Atarudi
3 Rafiki zangu, hii ni barua yangu ya pili kuwaandikia. Barua zote mbili nimewaandikia ili kusaidia fikra zenu njema zikumbuke kitu. 2 Ninataka mkumbuke maneno ambayo manabii watakatifu walisema huko nyuma. Na mkumbuke amri ambayo Bwana na Mwokozi wetu aliwapa. Aliwapa amri hiyo kupitia mitume wake waliowafundisha.
3 Ni muhimu kwenu kuelewa kitakachotokea siku za mwisho. Watu watawacheka kwa yale mliyofundishwa. Wataishi kwa kufuata maovu wanayotaka kufanya. 4 Watasema, “Yesu aliahidi kuwa atarudi. Yuko wapi? Baba zetu wamekufa, lakini ulimwengu unaendelea kama ambavyo umekuwa tangu ulipoumbwa.”
5 Lakini watu hawa hawataki kukumbuka kilichotokea zamani. Anga ilikuwepo, na Mungu aliiumba dunia kwa kutumia maji. Hili lilitokea kwa neno la Mungu. 6 Kisha ulimwengu uliangamizwa kwa maji wakati wa gharika. 7 Na neno hilo hilo la Mungu linaiweka anga na dunia tuliyonayo sasa. Vimewekwa ili vichomwe moto. Vimewekwa kwa ajili ya siku ya hukumu na kuangamia kwa watu wote walio kinyume na Mungu.
8 Lakini rafiki zangu wapendwa msisahau jambo hili moja ya kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu moja, na miaka elfu moja ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kufanya alichoahidi kama ambavyo watu wengine wanaelewa maana ya kukawia. Lakini Bwana amewavumilia. Hataki mtu yeyote aangamie. Anataka kila mtu abadili njia zake na aache kutenda dhambi.
10 Lakini siku atakayorudi Bwana itakuwa siku isiyotarajiwa na kila mtu kama ambavyo mwizi huja. Anga itatoweka kwa muungurumo wa sauti kuu. Kila kitu kilicho angani kitateketezwa kwa moto. Na dunia na kila kitu kilichofanyika ndani yake kitafunuliwa na kuhukumiwa[c] na Mungu. 11 Kila kitu kitateketezwa kwa namna hii. Sasa mnapaswa kuishi kwa namna gani? Maisha yenu yanapaswa kuwa matakatifu na yanayompa heshima Mungu. 12 Mnapaswa kuangalia mbele, kuiangalia siku ile ya Bwana, mkifanya kile mnachoweza ili ije mapema. Itakapofika, anga itateketezwa kwa moto na kila kitu kilicho angani kitayeyuka kwa joto. 13 Lakini Mungu alituahidi. Na tunasubiri alichoahidi, yaani anga mpya na dunia mpya. Mahali ambapo hakia unaishi.
14 Rafiki wapendwa, tunasubiri hili litokee. Hivyo jitahidini kadri mnavyoweza msiwe na dhambi wala kosa. Jitahidini kuwa na amani na Mungu. 15 Kumbukeni kuwa tumeokolewa kwa sababu Bwana wetu ni mvumilivu. Ndugu yetu mpendwa Paulo aliwaambia jambo hili hili alipowaandikia kwa hekima aliyopewa na Mungu. 16 Ndivyo anavyosema katika barua zake zote anapoandika kuhusu mambo haya. Sehemu zingine katika barua zake ni ngumu kuzielewa, na kuna baadhi ya watu huzifafanua vibaya. Watu hawa ni wajinga na wasioaminika. Watu hawa hutoa pia maana potofu kwa Maandiko mengine. Lakini kwa kufanya hivi wanajiangamiza wao wenyewe.
17 Rafiki wapendwa, tayari mnajua kuhusu hili. Hivyo iweni waangalifu. Msiwaruhusu watu hawa waovu wakawaongoza kwenye upotevu kwa mabaya wanayofanya. Jichungeni msipoteze imani yenu iliyo imara. 18 Lakini mkue katika neema na kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu ni wake, sasa na hata milele! Amina.
© 2017 Bible League International