Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Yakobo 1-5

Kutoka kwa Yakobo mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo.

Kwa makabila Kumi na Mawili[a] ya watu wa Mungu yaliyotawanyika kote ulimwenguni: Salamu!

Imani na Hekima

Kaka na dada zangu, jueni kuwa mtakutana na adha za kila aina. Lakini hilo liwape ninyi sababu ya kuwa na furaha zaidi. Kwa sababu mnajua kuwa imani yenu inapojaribiwa ndipo mnapojifunza kuwa wavumilivu. Na uvumilivu unapaswa kukamilisha kazi yake, ili kwamba muwe watu waliokomaa na wakamilifu msiopungukiwa na kitu cho chote.

Hivyo kama mmoja wenu atapungukiwa na hekima, anapaswa kumwomba Mungu anayewapa watu wote kwa ukarimu, naye atampa hekima. Lakini anapaswa kuwa na imani anapoomba pasipo mashaka yo yote, kwani yule aliye na mashaka ni kama wimbi la baharini, linalosukumwa na upepo na kusukwa sukwa. Mtu wa jinsi hiyo asidhani kuwa anaweza kupokea cho chote kutoka kwa Bwana; yeye ni mwenye mashaka na hufikiria mambo mawili tofauti kwa wakati mmoja.

Utajiri wa Kweli

Ndugu aliye maskini na awe na furaha sana kwamba Mungu amemchukulia kuwa mtu wa maana sana. 10 Na waaminio walio matajiri wawe na furaha sana tu pale Mungu anapowashusha chini. Kwani utajiri wao hautawazuia kufa kama maua ya porini. 11 Jua linapochomoza na kuwa kali zaidi, joto lake hukausha mimea na maua huanguka chini na kupukutika na kupoteza urembo wake. Kwa jinsi hiyo hiyo, mtu tajiri atafifia katika shughuli zake.

Majaribu Hayatoki kwa Mungu

12 Amebarikiwa mtu yule anayestahimili majaribu, maana anapofaulu mitihani atapokea taji yenye uzima ambayo Mungu amewaahidi wale wanaompenda. 13 Yeyote anayejaribiwa hapaswi kusema, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu maovu hayamjaribu Mungu na hamjaribu mtu yeyote. 14 Bali kila mmoja anajaribiwa na tamaa zake mwenyewe, anapovutwa na kunaswa. 15 Kisha tamaa inapotunga mimba inazaa dhambi, na dhambi ikikomaa kabisa inazaa kifo.

16 Kaka zangu na dada zangu wapendwa msikubali kudanganywa, 17 Kila karama njema na kila tuzo kamilifu hutoka juu; hushuka chini kutoka kwa Baba aliyeumba nuru zote zilizoko mawinguni ambamo kwake yeye hakuna mabadiliko kama vile vivuli vinavyosababishwa na mzunguko wa sayari. 18 Kwa uamuzi wake mwenyewe Mungu alituzaa sisi na kuwa watoto wake kwa njia ya ujumbe wa kweli ili tuwe mazao ya kwanza[b] yenye heshima ya pekee miongoni mwa vyote alivyoviumba.

Kusikiliza na Kutii

19 Kumbukeni hili ndugu zangu wapendwa: Kila mtu awe mwepesi wa kusikia lakini awe mzito wa kusema, na mzito kukasirika, 20 kwa sababu hasira ya mwanadamu haitoi haki inayohitajiwa na Mungu toka kwetu. 21 Hivyo acheni matendo yote machafu na kila uovu uliokaa karibu yenu, na mpokee kwa unyenyekevu mafundisho yaliyopandwa ndani ya mioyo yenu. Neno hilo, lina uwezo wa kuleta wokovu wa roho zenu.

22 Usisikilize tu kile ambacho mafundisho ya Mungu yanakisema; bali fanya yale inayosema! Ikiwa utasikiliza tu, utajidanganya mwenyewe. 23 Kwani kama mtu atasikiliza mafundisho ya Mungu, lakini asitende yanayosemwa, yuko kama mtu anayeutazama uso wake kwenye kioo. 24 Anajiangalia mwenyewe kwa haraka na anapoondoka tu husahau anavyoonekana. 25 Lakini anayetazama kwa makini katika sheria kamilifu ya Mungu, inayowaletea watu uhuru, na akaendelea kufanya hivyo asiwe msikilizaji anayesahau, bali huyatunza mafundisho katika matendo, mtu huyo atakuwa na baraka katika kila analofanya.

Njia Sahihi ya Kumwabudu Mungu

26 Kama kuna anayedhani kuwa ni mshika dini, lakini bado hauzuii ulimi wake anajidanganya mwenyewe. Dini yake mtu huyu haina manufaa. 27 Dini safi na isiyo na lawama mbele za Mungu Baba, inahusisha haya: kuwatunza yatima na wajane katika mazingira mgumu na kujilinda asichafuliwe na ulimwengu.

Wapende Watu Wote

Kaka zangu na dada zangu, ninyi ni wenye imani katika Bwana wetu mtukufu Yesu Kristo. Kwa hiyo msiwachukulie baadhi ya watu kuwa wa maana zaidi kuliko wengine. Tuchukulie mtu mmoja anakuja katika mkutano wenu akiwa amevaa pete ya dhahabu ama akiwa amevaa mavazi ya thamani, na mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa na machafu naye akaja ndani. Na tuchukulie kuwa mnaonyesha kumjali zaidi yule mtu aliyevaa mavazi mazuri na kusema, “Wewe keti hapa katika kiti hiki kizuri.” Lakini unamwambia yule mtu maskini, “Wewe simama pale,” au, “Keti chini karibu na miguu yetu.” Je, hiyo haioneshi kwamba mnafikiri miongoni mwenu kuwa baadhi ya watu ni bora kuliko wengine? Mmesimama kama mahakimu wenye maamuzi mabaya?

Sikilizeni kaka na dada zangu wapendwa! Mungu aliwachagua wale walio maskini machoni pa watu kuwa matajiri katika imani. Aliwachagua kuwa warithi wa Ufalme, ambao Mungu aliwaahidi wale wanaompenda? Lakini ninyi mmewadhalilisha walio maskini! Na kwa nini mnawapa heshima kubwa watu walio matajiri? Hawa ndiyo wale ambao daima wanajaribu kuyadhibiti maisha yenu. Si ndiyo hao wanaowapeleka ninyi mahakamani? Je, si ndiyo hao hao wanaolitukana Jina zuri la Bwana wenu?[c]

Kama kweli mnaitunza sheria ya ufalme inayopatikana katika Maandiko, “Mpende jirani yako[d] kama unavyojipenda mwenyewe,”(A) mtakuwa mnafanya vizuri. Lakini kama mtakuwa mnaonyesha upendeleo, mtakuwa mnafanya dhambi na mtahukumiwa kuwa na hatia kama wavunja sheria.

10 Ninasema hivi kwa sababu yeyote anayeitunza Sheria yote, lakini akaikosea hata mmoja tu atakuwa na hatia ya kuihalifu Sheria yote. 11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,”(B) pia ndiye aliyesema, “Usiue.”(C) Hivyo, kama hutazini lakini ukaua utakuwa umevunja Sheria yote ya Mungu.

12 Mseme na kutenda kama watu watakaokuja kuhukumiwa kwa sheria inayoleta uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu ya Mungu haitakuwa na huruma kwake yeye ambaye hakuwa na rehema. Lakini rehema huishinda hukumu!

Imani na Kazi Njema

14 Ndugu zangu, ikiwa mtu atasema kuwa anayo imani lakini hafanyi kitu, imani hiyo haina manufaa yoyote. Imani ya jinsi hiyo haiwezi kumwokoa mtu yeyote. 15 Kama ndugu au dada anahitaji mavazi na anapungukiwa chakula cha kila siku, 16 na ukawaambia, “Mungu awe nanyi! Mkahifadhiwe mahala pa joto na mle vizuri!” Hiyo ina manufaa gani kwao? Usipowapa vitu wanavyovihitaji, maneno yako yanakosa maana! 17 Kwa jinsi hiyo hiyo, imani isipokuwa na matendo itakuwa imekufa.

18 Lakini mtu anaweza kuleta hoja kusema, “Watu wengine wanayo imani, na wengine wanayo matendo mema.” Jibu langu litakuwa, huwezi kunionyesha imani yako pasipo kufanya tendo lolote. Lakini mimi nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. 19 Je, mnaamini kwamba kuna Mungu mmoja tu? Vema! Hata mapepo yanaamini na kutetemeka kwa hofu.

20 Wewe mjinga! Je, unahitaji uthibitisho kwamba imani bila matendo haina manufaa? 21 Je, si baba yetu Ibrahimu alihesabiwa haki na Mungu kwa matendo yake alipomtoa sadaka mwanae Isaka juu ya madhabahu? 22 Kwa hakika unaweza kuiona imani hiyo ilifanya kazi pamoja na matendo yake. Kwa hiyo imani yake ilikamilishwa na matendo yake. 23 Ndipo yakatimizwa yale yaliyo kwenye Maandiko kuwa, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa imani hiyo akafanywa kuwa mwenye haki[e] kwa Mungu,”(D) na kwa sababu hiyo akaitwa “Rafiki wa Mungu”.(E) 24 Mnamwona mtu huyo amefanywa kuwa mwenye haki kwa Mungu kwa matendo yake wala siyo kwa imani peke yake.

25 Je, Rahabu[f] yule kahaba si alifanywa kuwa mwenye haki na Mungu kwa matendo aliyofanya, alipowasaidia wale waliokuwa wakipeleleza nchi kwa niaba ya watu wa Mungu. Aliwakaribisha nyumbani mwake na kuwawezesha kutoroka kwa njia nyingine.

26 Hivyo, kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo, imani imekufa ikiwa haina matendo.

Kuyamudu Mambo Tunayosema

Kaka na dada zangu, msiwe walimu wengi miongoni mwenu. Mnajua kuwa sisi tulio walimu tutahukumiwa zaidi tena kwa umakini kweli.

Ninawatahadharisha kwa sababu sote tunakosa mara kwa mara. Na kama kuna mtu asiyekosa kwa maneno yake, huyo ni mkamilifu, huyo anaweza kuumudu mwili wake wote. Tunawaweka lijamu katika midomo ya farasi, ili waweze kututii sisi. Kwa lijamu hizo tunaweza kuidhibiti miili yao. Au tuchukue meli kama mfano: Hata kama ni kubwa mno na husukumwa na upepo mkali, zinaongozwa kwa usukani mdogo sana na kwenda po pote alikokusudia nahodha kuipeleka. Kwa jinsi hiyo hiyo, ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini unaweza kujivuna kuwa umetenda mambo makubwa sana.

Fikiri jinsi ambavyo msitu mkubwa unaweza kuwashwa moto kwa mwali mdogo tu! Ndiyo, ulimi ni mwali wa moto. Ulimi unawakilisha ulimwengu wa uovu miongoni mwa viungo vya mwili wetu. Ulimi huo huo huuchafua mwili wote, na unaweza kuwasha moto maisha yote ya mtu. Nao unapata moto wake kutoka Jehanamu.

Aina zote za wanyama na ndege, mijusi na viumbe vya baharini wanaweza kufugwa na wanadamu wamekuwa wanawafuga. Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia na umejaa sumu ya kuua. Kwa ulimi huo tunambariki Bwana na Baba, na kwa huo huo tunawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu! 10 Kutoka katika kinywa hicho hicho hutoka baraka na laana. Kaka na dada zangu, haipaswi kuwa hivyo. 11 Chemichemi ya maji haiwezi kutoa maji matamu na maji machungu kutoka katika tundu moja, je inawezekana? 12 Ndugu zangu, je mtini unaweza kuzaa zeituni? Au mzabibu waweza kuzaa tini? Kwa hakika haiwezekani! Wala chemichemi ya maji chumvi haiwezi kutoa maji matamu.

Hekima ya Kweli

13 Nani miongoni mwenu aliye na hekima na ufahamu? Na aoneshe hekima yake kwa mwenendo mzuri, kwa matendo yake yanayofanywa kwa unyenyekevu unaoletwa na hekima. 14 Lakini kama mtakuwa na wivu wenye uchungu na ubinafsi ndani ya mioyo yenu, hamwezi kujivunia hekima yenu; kwamba kujivuna kwenu kungekuwa ni uongo unaoficha ukweli. 15 Hii sio aina ya hekima inayotoka juu mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyotoka kwa Roho wa Mungu bali ni ya kishetani. 16 Kwa sababu pale penye wivu na ubinafsi, basi panakuwepo vurugu na kila aina ya matendo maovu. 17 Lakini hekima inayotoka mbinguni juu kwanza juu ya yote ni safi, kisha ni ya amani ina upole na ina busara. Imejaa rehema na huzaa mavuno ya matendo mema. Haina upendeleo wala unafiki. 18 Wale wenye bidii ya kuleta amani na wanaopanda mbegu zao kwa matendo ya amani, watavuna haki kama mavuno yao.

Jitoe Mwenyewe kwa Mungu

Mapigano na magombano yanatokea wapi miongoni mwenu? Je, hayatoki kutoka ndani yenu wenyewe, kutoka katika tamaa zenu za starehe ambazo zinafanya vita siku zote ndani ya miili yenu? Mnataka mambo lakini hamyapati, hivyo mnaua na mnakuwa na wivu juu ya watu wengine. Lakini bado hamwezi kuyafikia mnayoyataka, hivyo mnagombana na kupigana. Nanyi ndugu zangu hampokei mambo mnayoyataka kwa sababu hamumwombi Mungu. Na mnapoomba, lakini hampokei cho chote kwa sababu mnaomba kwa dhamiri mbaya, ili muweze kuvitumia mlivyopatiwa kwa anasa zenu.

Watu msio waaminifu, hamjui kwamba kuupenda ulimwengu ni sawa na kumchukia Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hujifanya mwenyewe kuwa adui wa Mungu. Je, kile Maandiko yanachokisema hakina maana yoyote kwenu? Ile roho ambayo Mungu aliifanya ikae ndani yetu wanadamu imejaa tamaa yenye wivu? Lakini Mungu ametuonesha sisi, rehema kuu zaidi. Ndiyo maana Maandiko yanasema:

Mungu huwapinga wenye kiburi,
    lakini huwapa neema wale walio wanyenyekevu.(F)

Kwa hiyo jiwekeni chini ya Mungu. Mpingeni Shetani naye atawakimbia ninyi. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Iosheni mikono yenu ninyi wenye dhambi na kuitakasa mioyo yenu enyi wanafiki! Ombolezeni na kulia! Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa maombolezo, na furaha yenu igeuzwe kuwa huzuni kubwa. 10 Jinyenyekezeni chini ya Bwana, naye atawainua juu.

Wewe Siyo Hakimu

11 Ndugu, msiendelee kukosoana ninyi kwa ninyi. Yeye anayemnenea mabaya ndugu yake au anayemhukumu ndugu yake atakuwa anailaumu Sheria na atakuwa anaihukumu Sheria. Na kama utaihukumu Sheria, hautakuwa unafanya yale yanayosemwa na Sheria, bali utakuwa ni hakimu. 12 Kuna Mtoa Sheria mmoja tu na hakimu, ndiye Mungu aliye na uwezo wa kuokoa na kuangamiza. Hivyo wewe unafikiri ni nani, wewe unayemhukumu jirani yako?

Mwache Mungu Apange Maisha Yako

13 Sikilizeni mnaosema, “Leo au kesho tutasafiri kwenda kwenye mji huu au ule, na tutakaa mwaka mzima pale, tutafanya biashara hapo na kujipatia fedha nyingi.” 14 Hamjui hata yatakayotokea katika maisha yenu kesho yake tu. Kwani ninyi ni mvuke tu ambao huonekana kwa kipindi kifupi tu kisha hutoweka. 15 Badala yake, nyakati zote mngesema, “Kama Bwana anapenda, tutaishi na tutafanya hivi au vile.” 16 Kama ilivyo, ninyi mna kiburi na kujivuna. Majivuno yote ya jinsi hiyo ni uovu! 17 Hivyo sasa, mnaposhindwa kufanya mliyoyajua ni haki, mtakuwa na hatia ya dhambi.

Onyo kwa Matajiri na Wachoyo

Sikilizeni, ninyi matajiri! Ombolezeni na kulia kwa sauti kwa ajili ya dhiki inayowajia. Utajiri wenu umeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu zenu na fedha vimeliwa na kutu! Hiyo kutu itakuwa ni ushuhuda dhidi yenu, na itaila miili yenu kama kwa moto. Mmejilimbikizia mali kwa ajili yenu katika kizazi hiki cha siku za mwisho! Angalieni! Mmeyazuia malipo ya wafanyakazi waliopalilia mashamba yenu. Sasa wananililia! Na kilio cha hao wanaovuna pia kimeyafikia masikio ya Bwana Aliye na Nguvu.

Mmeishi maisha ya anasa duniani na kujifurahisha na kila kitu mlichotaka. Mmeinenepesha miili yenu, kama wanyama walio tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmehukumu na kuua wale watu wasio na hatia, na ambao hawakupingana nanyi.

Uwe Mstahimilivu

Hivyo kina kaka na kina dada, muwe na subira; hadi kuja kwa mara ya pili kwa Bwana. Kumbukeni kuwa mkulima huyasubiria mazao yake yenye thamani yakue ardhini. Huyangoja kwa subira mpaka yapate mvua za masika na za vuli.[g] Hata ninyi pia mnapaswa kungoja kwa subira. Muwe imara mioyoni mwenu, kwa sababu kuja kwa Bwana mara ya pili kumekaribia. Kaka na dada zangu, msiendelee kunung'unikiana ninyi kwa ninyi, ili msije kuhukumiwa kuwa na hatia. Tazameni! Hakimu anasimama mlangoni akiwa tayari kuingia ndani.

10 Kina kaka na kina dada, fuateni mfano wa manabii waliosema kwa jina la Bwana. Wao walipata mateso mengi mabaya lakini walivumilia. 11 Na tunatoa heshima kubwa sana kwa wale wote waliostahimili mateso. Mmesikia juu ya uvumilivu wa Ayubu,[h] na mnayajua ya kuwa baada ya yote hayo Bwana alimsaidia. Hii basi inaonesha ya kuwa Bwana ni mwenye wingi wa rehema na huruma.

Uwe Makini na Unayosema

12 Juu ya mambo yote kaka zangu na dada zangu, usitumie kiapo unapotoa ahadi, Usiape kwa mbingu wala kwa dunia, ama kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe “Ndiyo halisi”, na “Hapana” yenu na iwe “Hapana halisi”, ili msije mkaingia katika hukumu ya Mungu.

Nguvu ya Maombi

13 Je, miongoni mwenu kuna aliye na shida? Anapaswa kuomba. Je, yupo yeyote mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. 14 Je, kuna yeyote kwenu aliye mgonjwa? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa kumwombea na kumpaka mafuta katika jina la Bwana. 15 Maombi yanayofanywa kwa imani yatamfanya mgonjwa apone, na Bwana atampa uzima. Kama atakuwa ametenda dhambi, Bwana atamsamehe.

16 Hivyo muungame dhambi ninyi kwa ninyi, na kuombeana ninyi kwa ninyi ili muweze kuponywa. Maombi yanayofanywa na mtu mwenye haki yana nguvu sana na yana matokeo makubwa sana. 17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi tulivyo. Aliomba kwamba mvua isinyeshe, na haikunyesha katika ardhi kwa miaka mitatu na nusu. 18 Kisha akaomba tena inyeshe, na anga ikatoa mvua, na ardhi ikatoa mazao.

Kuwasaidia Watu Wanapotenda Dhambi

19 Kaka na dada zangu Ndugu zangu, kama mmoja wenu atapotoka katika kweli, na mwingine akamrejeza, 20 yule aliyemrejeza atambue kuwa yule anayemrejeza mtenda dhambi kutoka katika njia yake mbaya ataiokoa roho ya huyo mtu kutoka katika kifo cha milele na atasababisha dhambi nyingi zisamehewe.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International