Beginning
Kuhani Melkizedeki
7 Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu. Alikutana na Ibrahimu wakati Ibrahimu alipokuwa akirudi baada ya kuwashinda wafalme. Siku hiyo Melkizedeki alimbariki Ibrahimu. 2 Kisha Ibrahimu akampa sehemu ya kumi ya kila kitu alichokuwa nacho.
Jina Melkizedeki, mfalme wa Salemu, lilikuwa na maana mbili. Kwanza, Melkizedeki inamaanisha “mfalme wa haki.” Na “mfalme wa Salemu” inamaanisha “mfalme wa amani.” 3 Hakuna ajuaye baba na mama yake walikuwa ni kina nani au walitokea wapi.[a] Na hakuna ajuaye alizaliwa lini au alikufa lini. Melkizedeki ni kama Mwana wa Mungu kwa vile siku zote atakuwa kuhani.
4 Unaweza kuona kuwa Melkizedeki alikuwa mkuu sana. Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa yeye sehemu ya kumi ya kila alichoshinda kule vitani. 5 Sasa sheria inasema kwamba wale wa ukoo wa Lawi waliokuja kuwa makuhani wanastahili kupata sehemu ya kumi kutoka kwa watu wao, hata kama wao na watu wao ni wa familia ya Ibrahimu. 6 Melkizedeki wala hakutoka katika kabila la Lawi, lakini Ibrahimu akampa sehemu ya kumi ya alivyokuwa navyo. Na Melkizedeki akambariki Ibrahimu yule aliyekuwa na ahadi za Mungu. 7 Na kila mtu anajua kwamba mtu aliye wa muhimu zaidi humbariki mtu yule ambaye ana umuhimu mdogo.
8 Makuhani hawa hupata sehemu ya kumi, lakini wao ni binadamu tu wanaoishi kisha hufa. Lakini Melkizedeki, aliyepata sehemu ya kumi kutoka kwa Ibrahimu, anaendelea kuishi, kama Maandiko yanavyosema. 9 Sasa wale wa kutoka ukoo wa Lawi ndiyo wanaopata sehemu ya kumi kutoka kwa watu. Lakini tunaweza kusema kuwa Ibrahimu alipompa Melkizedeki sehemu ya kumi, kisha Lawi naye akatoa. 10 Lawi alikuwa bado hajazaliwa, lakini alikuwepo katika baba yake Ibrahimu wakati Melkizedeki alipokutana naye.
11 Watu walipewa sheria chini ya mfumo wa makuhani waliotoka katika ukoo wa Lawi. Lakini hayupo awezaye kufanywa mkamilifu kiroho kwa njia ya mfumo wa makuhani. Hivyo lilikuwepo hitaji la kuhani mwingine kuja. Namaanisha kama Melkizedeki, siyo Haruni. 12 Na anapokuja kuhani wa aina nyingine, basi sheria pia inabidi ibadilishwe. 13-14 Tunazungumza juu ya Bwana Yesu, aliyetoka katika kabila lingine. Hakuwepo yeyote kutoka katika kabila hilo kamwe aliyeweza kutumika kama kuhani madhabahuni. Ni dhahiri kwamba Bwana Yesu alitoka katika kabila la Yuda. Na Musa hakusema chochote kuhusu makuhani waliyetokana na kabila hilo.
Yesu Ni Kuhani Mfano wa Melkizedeki
15 Na mambo haya yalizidi kuwa wazi zaidi tunapomwona kuhani mwingine aliye kama Melkizedeki. 16 Alifanywa kuhani, lakini siyo kwa sababu alikamilisha mahitaji ya kuzaliwa katika familia sahihi. Alifanyika kuhani kwa nguvu ya uhai ambayo haitakwisha. 17 Hivi ndivyo Maandiko yanavyosema kumhusu yeye: “Wewe ni kuhani milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.”(A)
18 Hivyo mfumo wa sheria za zamani zilizowekwa sasa zinaisha kwa sababu zilikuwa dhaifu na hazikuweza kutusaidia. 19 Sheria ya Musa haikuweza kukamilisha kitu chochote. Lakini sasa tumaini bora zaidi limeletwa kwetu. Na kwa tumaini hilo tunaweza kumkaribia Mungu.
20 Vile vile, ni muhimu kwamba Mungu aliweka ahadi kwa kiapo alipomfanya Yesu kuwa kuhani mkuu. Watu hawa wengine walipofanyika makuhani, hapakuwepo kiapo. 21 Lakini Yesu akafanyika kuhani kwa kiapo cha Mungu. Mungu alimwambia:
“Bwana anaweka ahadi kwa kiapo
naye hatabadili mawazo yake:
‘Wewe ni kuhani milele.’”(B)
22 Hivyo hii inamaanisha kwamba Yesu ni uhakika wa agano zuri zaidi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wake.
23 Pia, mmoja wa hawa makuhani wengine alipofariki, asingeendelea kuwa kuhani. Hivyo walikuwepo makuhani wengi wa jinsi hii. 24 Lakini Yesu anaishi milele. Hatakoma kufanya kazi kama kuhani. 25 Hivyo anaweza kuwaokoa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake. Yesu anaweza kufanya hivi milele, kwa sababu anaishi siku zote na yuko tayari kuwasaidia watu wanapomjia Mungu.
26 Hivyo Yesu ni aina ya kuhani mkuu tunayemhitaji. Yeye ni mkamilifu. Hana dhambi ndani yake. Hana kasoro na havutwi na watenda dhambi. Naye amepandishwa juu ya mbingu. 27 Hayuko sawa na hawa makuhani wengine. Walitakiwa kutoa sadaka kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, na kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Lakini Yesu hahitaji kufanya hivyo. Alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya nyakati zote. Alijitoa mwenyewe. 28 Sheria huchagua makuhani wakuu ambao ni watu na wanao udhaifu ule ule ambao watu wote wanao. Lakini baada ya sheria, Mungu alisema kiapo ambacho kilimfanya Mwana awe kuhani mkuu. Na Mwana huyo, aliyekamilishwa kwa njia ya mateso, atatumika kama kuhani mkuu milele yote.
Yesu Kuhani Wetu Mkuu
8 Hii ndiyo hoja tunayosema: Tunaye kuhani mkuu wa jinsi hiyo, anayeketi upande wa kuume[b] wa kiti cha enzi cha Mungu Mkuu mbinguni. 2 Kuhani wetu mkuu anahudumia katika Patakatifu pa Patakatifu.[c] Anahudumia katika mahali pa hakika kwa ibada[d] palipotengenezwa na Bwana, siyo na mtu yeyote duniani.
3 Kila kuhani mkuu anayo kazi ya kutoa sadaka na sadaka kwa Mungu. Hivyo kuhani wetu mkuu pia anahitajika kutoa kitu kwa Mungu. 4 Kama kuhani wetu mkuu angekuwa anaishi duniani, asingekuwa kuhani. Nasema hivi kwa sababu tayari hapa wapo makuhani ambao wanafuata sheria kwa kutoa sadaka kwa Mungu. 5 Kazi ambayo makuhani hawa wanafanya hakika ni nakala tu na kivuli cha yaliyoko mbinguni. Ndiyo sababu Mungu alimwonya Musa alipokuwa amejiandaa kujenga Hema Takatifu: “Uwe na uhakika kufanya kila kitu sawasawa na kielelezo nilichokuonesha kule mlimani.”(C) 6 Lakini kazi ambayo tayari imetolewa kwa Yesu ni kuu zaidi ya kazi iliyotolewa na makuhani hao. Kwa jinsi hiyo hiyo, agano jipya ambalo Yesu alilileta kutoka kwa Mungu kuja kwa watu wake ni kuu zaidi kuliko lile la zamani. Na agano jipya limeelemea katika ahadi bora zaidi.
7 Kama kusingekuwa na makosa katika agano la kwanza, kisha kusingekuwa na haja ya agano la pili. 8 Lakini Mungu aligundua kitu kilichokuwa na kasoro kwa watu, akasema:
“Wakati unakuja, asema Bwana,
nitakapofanya agano jipya na watu wa Israeli na watu wa Yuda.
9 Halitakuwa sawa na agano lililotengenezwa na baba zao.
Hilo ni agano nililowapa nilipowachukua kwa mkono na kuwatoa Misri.
Hawakuendelea kufuata agano nililowekeana nao,
na nikageuka mbali nao, asema Bwana.
10 Hili ni agano jipya nitakalofanya
na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana:
Nitaziweka sheria zangu katika fahamu zao,
na nitaandika sheria zangu katika mioyo yao.
Nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
11 Hakuna tena atakayemfundisha jirani yake au familia yake kumjua Bwana.
Watu wote, wakuu zaidi na wasio na umuhimu kabisa, watanijua.
12 Na nitawasamehe makosa waliyotenda,
na sitazikumbuka dhambi zao.”(D)
13 Mungu aliliita hili ni agano jipya, hivyo amelifanya agano la kwanza kuwa la zamani. Na chochote kilicho cha zamani na kisichokuwa na matumizi kiko tayari kutoweka.
Ibada Chini ya Patano la Kale
9 Patano la kwanza lilikuwa na kanuni kwa ajili ya kuabudu na mahali pa kuabudia hapa duniani. 2 Mahali hapa palikuwa ni ndani ya hema. Eneo la kwanza ndani ya hema liliitwa Patakatifu. Katika Patakatifu kulikuwepo taa na meza iliyokuwa na mikate maalumu iliyotolewa kwa Mungu. 3 Nyuma ya pazia la pili kilikuwepo chumba kilichoitwa Patakatifu pa Patakatifu. 4 Katika Patakatifu pa Patakatifu kulikuwepo madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kuchoma uvumba. Pia lilikuwepo Sanduku la Agano. Sanduku lilifunikwa kwa dhahabu. Ndani ya hilo Sanduku kulikuwemo birika la mana na fimbo ya Haruni; fimbo ambayo iliwahi kuchipusha matawi. Vilevile ndani ya Sanduku yalikuwemo mawe bapa yaliyoandikwa Amri Kumi za agano la kale kwao. 5 Juu ya Sanduku walikuwepo viumbe wenye mbawa walioonesha utukufu wa Mungu. Viumbe hawa wenye mbawa walikuwa juu ya sehemu ya rehema.[e] Lakini hatuwezi kusema chochote kuhusu hili hivi sasa.
6 Kila kitu ndani ya hema kilikuwa kimewekwa tayari kwa namna nilivyoeleza. Kisha makuhani waliingia ndani ya chumba cha kwanza kila siku kutekeleza shughuli zao za ibada. 7 Lakini ni kuhani mkuu tu aliweza kuingia kwenye chumba cha pili, na aliingia mara moja tu kwa mwaka. Pia, asingeweza kuingia ndani ya chumba hicho bila kuchukua damu pamoja naye. Aliitoa damu hiyo kwa Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi walizotenda watu bila kujua kwamba walikuwa wanatenda dhambi.
8 Roho Mtakatifu hutumia vyumba hivi viwili tofauti kutufundisha kwamba njia ya kuelekea Patakatifu pa Patakatifu haikuwa wazi wakati chumba cha kwanza kilipokuwepo. 9 Huu ni mfano kwetu leo. Inaonyesha sadaka na sadaka ambazo makuhani walizitoa kwa Mungu haziwezi kufanya dhamiri za wanaoabudu ziwe safi kabisa. 10 Sadaka na sadaka hizi ni kwa ajili tu ya vyakula na vinywaji na aina maalumu ya kuoga. Ni sheria kuhusu mwili tu. Mungu alizitoa kwa watu wake wazifuate hadi wakati wa njia yake mpya.
Ibada Chini ya Patano Jipya
11 Lakini Kristo tayari amekuja awe kuhani mkuu. Yeye ni kuhani mkuu wa mambo mema tuliyonayo sasa. Lakini Kristo hatumiki ndani ya eneo kama hema ambalo makuhani wale walitumika ndani yake. Anatumika katika eneo bora zaidi. Tofauti na hema lile, hili ni kamilifu. Halikutengenezwa hapa duniani. Siyo la ulimwengu huu. 12 Kristo aliingia Patakatifu Zaidi mara moja tu; hii ilitosha kwa nyakati zote. Aliingia Patakatifu Zaidi kwa kutumia damu yake mwenyewe, siyo damu ya mbuzi au ya ng'ombe wadogo. Aliingia hapo na kutuweka huru milele kutoka katika dhambi.
13 Damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ng'ombe zilinyunyizwa juu ya wale ambao hawakuwa safi vya kutosha tena kuweza kuingia katika eneo la kuabudia. Damu na majivu viliwafanya wawe safi tena, lakini katika miili yao tu. 14 Hivyo hakika sadaka ya damu ya Kristo inaweza kufanya mambo bora zaidi. Kristo alijitoa mwenyewe kupitia Roho wa milele kama sadaka kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa kabisa sisi kutoka katika maovu tuliyotenda. Itatupa sisi dhamiri safi ili tuweze kumwabudu Mungu aliye hai.
15 Hivyo Kristo huwaletea watu wake agano jipya kutoka kwa Mungu. Huleta agano hili ili wale walioteuliwa na Mungu waweze kuzipata baraka ambazo Mungu aliwaahidi, baraka zinazodumu milele. Hili laweza kutokea tu kwa sababu Kristo alikufa ili awaweke huru watu kutokana na dhambi zilizotendwa dhidi ya amri za agano la kwanza.
16 Mtu anapofariki na akaacha usia, ni lazima uwepo uthibitisho kwamba yule aliyeandika usia amefariki. 17 Usia haumaanishi chochote wakati aliyeuandika bado yuko hai. Unaweza kutumika mara tu baada ya kifo cha mtu huyo. 18 Ndiyo sababu ili kuthibitisha kifo damu ilihitajika ili kuanza agano la kwanza baina ya Mungu na watu wake. 19 Kwanza, Musa aliwaeleza watu kila agizo katika sheria. Kisha akachukua damu ya ndama dume[f] na kuichanganya na maji. Alitumia sufu nyekundu na tawi la hisopo kunyunyiza damu na maji katika kitabu cha sheria na kwa watu. 20 Kisha akasema, “Hii ni damu inayoweka agano liwe zuri agano ambalo Mungu aliwaagiza mlifuate.”(E) 21 Kwa jinsi hiyo hiyo, Musa alinyunyiza damu katika Hema Takatifu. Aliinyunyiza damu juu ya kila kitu kilichotumika katika ibada. 22 Sheria inasema kwamba karibu kila kitu kinapaswa kutakaswa kwa damu. Dhambi haziwezi kusamehewa bila sadaka ya damu.
Yesu Kristo ni Dhabihu yetu kwa Ajili ya Dhambi
23 Mambo haya ni nakala ya mambo halisi yaliyoko mbinguni. Nakala hizi zinapaswa kutakaswa kwa sadaka ya wanyama. Lakini mambo halisi yaliyoko mbinguni yanapaswa kuwa na sadaka zilizo bora zaidi. 24 Kristo alienda katika Patakatifu pa Patakatifu. Lakini hapakuwa mahali palipotengenezwa na mwanadamu, ambapo ni nakala tu ya ile iliyo halisi. Alienda katika mbingu, na yuko huko sasa mbele za Mungu ili atusaidie sisi.
25 Kuhani mkuu huingia katika Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kila mwaka. Huchukua pamoja naye damu ya sadaka. Lakini hatoi damu yake kama alivyofanya Kristo. Kristo alienda mbinguni, lakini siyo kujitoa mwenyewe mara nyingi kama ambavyo kuhani mkuu hutoa damu tena na tena. 26 Kama Kristo alijitoa mwenyewe mara nyingi, basi angehitaji kuteseka mara nyingi tangu wakati dunia ilipoumbwa. Lakini alikuja kujitoa mwenyewe mara moja tu. Na mara hiyo moja inatosha kwa nyakati zote. Alikuja katika wakati ambao ulimwengu unakaribia mwisho. Alikuja kuchukua dhambi zote kwa kujitoa mwenyewe kama sadaka.
27 Kila mtu atakufa mara moja tu. Baada ya hapo ni kuhukumiwa. 28 Hivyo Kristo alitolewa kama sadaka mara moja kuchukua dhambi za watu wengi. Na atakuja mara ya pili, lakini siyo kujitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi. Atakuja mara ya pili kuleta wokovu kwa wale wanaomngojea.
Yesu Kristo, Dhabihu Pekee Tunayoihitaji
10 Sheria ya Musa ilitupa sisi picha tu isiyo wazi sana ya mambo yaliyokuwa yanakuja baadaye. Sheria siyo picha kamili ya mambo halisi. Sheria huwaambia watu kutoa sadaka zile zile kila mwaka. Wale wanaokuja kumwabudu Mungu wanaendelea kutoa sadaka. Lakini sheria haiwezi kamwe kuwakamilisha wao. 2 Kama sheria ingeweza kuwakamilisha watu, sadaka hizi zingekuwa zimekoma. Tayari wao wangekuwa safi kutoka katika dhambi, na bado wasingehukumiwa moyoni mwao. 3 Lakini hayo siyo yanayotokea. Dhabihu zao zinawafanya wazikumbuke dhambi zao kila mwaka, 4 kwa sababu haiwezekani kwa damu ya fahali na mbuzi kuondoa dhambi.
5 Hivyo baada ya Kristo kuja ulimwenguni alisema:
“Huhitaji sadaka na sadaka,
lakini umeandaa mwili kwa ajili yangu.
6 Hukuridhishwa na sadaka za kuteketezwa
na sadaka kuondoa dhambi.
7 Kisha nikasema, ‘Nipo hapa, Mungu.
Imeandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria.
Nimekuja kufanya yale unayopenda.’”(F)
8 Kwanza Kristo alisema, “Wewe hufurahishwi na sadaka na sadaka. Hukuridhishwa na sadaka za kuteketezwa na sadaka ili kuondoa dhambi.” (Hizi ndizo sadaka zote ambavyo sheria inaagiza.) 9 Kisha akasema, “Niko hapa, Mungu. Nimekuja kufanya yale unayopenda.” Hivyo Mungu akafikisha mwisho wa mfumo wa zamani wa utoaji sadaka na akaanzisha njia mpya. 10 Yesu Kristo alifanya mambo ambayo Mungu alimtaka ayafanye. Na kwa sababu ya hilo, tunatakaswa kwa njia ya sadaka ya mwili wa Kristo. Kristo aliitoa sadaka hiyo mara moja, inayotosha kwa nyakati zote.
11 Kila siku makuhani husimama na kutekeleza shughuli zao za kidini. Tena na tena hutoa sadaka zilezile, ambazo kamwe haziwezi kuondoa dhambi. 12 Lakini Kristo alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya dhambi, na sadaka hiyo ni nzuri kwa nyakati zote. Kisha akakaa mkono wa kuume wa Mungu. 13 Na sasa Kristo anawasubiria hapo adui zake wawekwe chini ya mamlaka yake.[g] 14 Kwa sadaka moja Kristo akawakamilisha watu wake milele. Ndio wale wanaotakaswa.
15 Roho Mtakatifu pia anatuambia juu ya hili. Kwanza anasema:
16 “Hili ndilo agano[h] nitakaloweka
na watu wangu baadaye, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu ndani ya mioyo yao.
Nitaziandika sheria zangu katika fahamu zao.”(G)
17 Kisha anasema,
“Nitazisahau dhambi zao
na nisikumbuke kamwe uovu walioutenda.”(H)
18 Na baada ya kila kitu kusamehewa, hakuna tena haja ya sadaka ili kuziondoa dhambi.
Mkaribieni Mungu
19 Hivyo ndugu na dada, tuko huru kabisa kupaingia Patakatifu pa Patakatifu. Tunaweza kufanya hivi bila hofu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Yesu. 20 Tunaingia kwa njia mpya ambayo Yesu alitufungulia. Ni njia iliyo hai inayotuelekeza kupitia pazia; yaani mwili wa Yesu. 21 Na tunaye kuhani mkuu zaidi anayeisimamia nyumba ya Mungu. 22 Ikiwa imenyunyiziwa kwa damu ya Kristo, mioyo yetu imewekwa huru kutokana na dhamiri yenye hukumu, na miili yetu imeoshwa kwa maji safi. Hivyo mkaribieni Mungu kwa moyo safi, mkijaa ujasiri kwa sababu ya imani katika Kristo. 23 Tunapaswa kuling'ang'ania tumaini tulilonalo, bila kusitasita kuwaeleza watu juu yake. Tunaweza kumwamini Mungu kuwa atatimiza aliyoahidi.
Saidianeni Ninyi kwa Ninyi Kuwa Imara
24 Tunahitaji kumfikiria kila mtu kuona jinsi tunavyoweza kuhamasishana kuonesha upendo na kazi njema. 25 Tusiache kukutana pamoja, kama wanavyofanya wengine. Hapana, tunahitaji kuendelea kuhimizana wenyewe. Hili linazidi kuwa muhimu zaidi na zaidi kadri mnavyoona ile Siku inakaribia.
Msigeuke Mbali ya Mwana wa Mungu
26 Kama tutaamua kuendelea kutenda dhambi baada ya kujifunza ukweli, ndipo hakutakuwa sadaka nyingine itakayoondoa dhambi. 27 Tukiendelea kutenda dhambi, kitakachokuwa kimebaki kwetu ni wakati wa kutisha wa kuingoja hukumu na moto wa hasira utakaowaangamiza wale wanaoishi kinyume na Mungu. 28 Yeyote aliyekataa kuitii Sheria ya Musa alipatikana ana hatia kutokana na ushuhuda uliotolewa na mashahidi wawili au watatu. Watu wa jinsi hiyo hawakusamehewa. Waliuawa. 29 Hivyo fikiri jinsi watu watakavyostahili kuhukumiwa zaidi ambao wanaonesha kumchukia mwana wa Mungu; watu wanaoonesha kuwa hawana heshima kwa sadaka ya damu iliyoanzisha agano jipya na mara moja ikawatakasa au wale wanaomkashifu Roho wa neema ya Mungu. 30 Tunajua kuwa Mungu alisema, “Nitawaadhibu watu kwa ajili ya makosa wanayofanya”;(I) nitawalipa tu Pia alisema, “BWANA atawahukumu watu wake.”(J) 31 Ni jambo la kutiisha kukutana na hukumu kutoka kwa Mungu aliye hai.
Endeleeni na Ujasiri na Uvumilivu Mlionao
32 Zikumbukeni siku za kwanza mlipojifunza kweli. Mlikuwa na mashindano magumu pamoja na mateso mengi, lakini mkaendelea kuwa imara. 33 Mara zingine watu waliwasemea mambo ya chuki na kuwatesa hadharani. Na nyakati zingine mliwasaidia wengine waliokuwa wakitendewa vivyo hivyo. 34 Ndiyo, mliwasaidia magerezani na kushiriki katika mateso yao. Na bado mlikuwa na furaha wakati kila kitu mlichokimiliki kilipochukuliwa kutoka kwenu. Mkaendelea kufurahi, kwa sababu mlijua kwamba mnacho kitu kilicho bora zaidi; kitu kitakachoendelea milele.
35 Hivyo msipoteze ujasiri mliokuwa nao zamani. Ujasiri wenu utalipwa sana. 36 Mnahitajika kuwa na subira. Baada ya kufanya yale anayotaka Mungu, mtapata aliyowaahidi.
37 “Karibu sana sasa, yeye ajaye
atakuja wala hatachelewa.
38 Mtu aliye sahihi mbele zangu
ataishi akiniamini mimi.
Lakini sitafurahishwa na yule
anayegeuka nyuma kwa ajili ya woga.”(K)
39 Lakini sisi siyo wale wanaogeuka nyuma na kuangamia. Hapana, sisi ni watu walio na imani na tunaokolewa.
© 2017 Bible League International