Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Waebrania 1-6

Mungu Amesema Kupitia Mwanaye

Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa kuwatumia manabii. Alisema nao mara nyingi na kwa njia nyingi tofauti. Lakini sasa katika siku hizi za mwisho Mungu amesema nasi tena kupitia Mwana wake. Mungu aliuumba ulimwengu wote kupitia Mwana wake. Na alimchagua Mwana kumiliki mambo yote. Huyo Mwana huuonesha utukufu wa Mungu. Yeye ni nakala halisi ya asili yake Mungu, na huviunganisha vitu vyote pamoja kwa amri yake yenye nguvu. Mwana aliwasafisha watu kutoka katika dhambi zao. Kisha akaketi upande wa kuume[a] wa Mungu, aliye Mkuu huko Mbinguni. Mwana akawa mkuu zaidi kuliko malaika, na Mungu akampa jina lililo kuu zaidi kuliko lolote katika majina yao.

Mungu kamwe hajamwambia malaika yeyote maneno haya:

“Wewe ni Mwanangu.
    Mimi leo hii nimekuwa Baba yako.”(A)

Mungu pia kamwe hajasema juu ya malaika,

“Nitakuwa Baba yake,
    naye atakuwa mwanangu.”(B)

Na kisha, pale Mungu anapomtambulisha Mwanaye mzaliwa wa kwanza ulimwenguni,[b] anasema,

“Basi malaika wote wa Mungu wamwabudu yeye.”[c]

Hivi ndivyo Mungu alivyosema kuhusu malaika:

“Yeye huwabadilisha malaika zake kuwa upepo[d]
    na watumishi wake kuwa miali ya moto.”(C)

Lakini hivi ndivyo alivyosema kuhusu Mwana wake:

“Mungu, ufalme wako utadumu milele na milele.
    Unatumia mamlaka yako kwa haki.
Unapenda kilicho sahihi na kuchukia kilicho na makosa.
    Hivyo Mungu, Mungu wako, amekuchagua wewe,
    na amekupa heshima na furaha zaidi kupita yeyote aliye kama wewe.”(D)

10 Pia Mungu alisema,

“Ee Bwana, mwanzo uliiumba dunia,
    na mikono yako ikaliumba anga.
11 Vitu hivi vitatoweka, lakini wewe utaendelea kuwepo.
    Vyote vitachakaa kama mavazi makuu kuu.
12 Utavikunja hivyo kama koti,
    navyo vitabadilishwa kama mavazi.
Lakini wewe hubadiliki,
    na uhai wako hautafikia mwisho.”(E)

13 Na Mungu hakuwahi kusema haya kwa malaika:

“Ukae mkono wangu wa kuume
    hadi nitakapowaweka adui zako chini ya uwezo wako.”[e](F)

14 Malaika wote ni roho ambao humtumikia Mungu nao hutumwa kuwasaidia wale watakaoupokea wokovu.

Wokovu Wetu ni Mkuu Kuliko Sheria

Hivyo tunapaswa kuwa makini zaidi kuzingatia yale tuliyofundishwa. Tunapaswa kuwa makini ili tusiondolewe polepole kutoka katika njia iliyo ya kweli. Fundisho kwamba Mungu alizungumza kupitia malaika limedhihirishwa kuwa ni la kweli. Na kila mara watu wake walipotenda jambo kinyume na fundisho lake, waliadhibiwa kwa yale waliyofanya. Waliadhibiwa walipoacha kutii fundisho hilo. Hivyo kwa hakika hata nasi tutaadhibiwa kama hatutauzingatia wokovu mkuu tulionao. Alikuwa ni Bwana Yesu aliyewaambia watu kwa mara ya kwanza juu ya wokovu huo. Na wale waliomsikiliza walithibitisha kwetu kuwa yale mambo yalikuwa ni kweli. Mungu alithibitisha hayo pia kwa kutumia ishara, maajabu, na aina zingine zote za miujiza. Na alithibitisha hayo kwa kuwapa watu vipawa tofauti kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa namna ile aliyotaka.

Kristo Akawa Kama Watu Ili Awaokoe

Mungu hakuwachagua malaika wawe watawala juu ya ulimwengu mpya unaokuja. Ulimwengu huo ujao ni ndiyo ambao tumekuwa tukiuzungumzia. Imeandikwa mahali fulani katika Maandiko:

“Kwa nini watu ni muhimu sana kwako?
    Kwa nini hata unafikiri juu yao?
Kwa nini unamjali mwana wa mwanadamu?[f]
    Je, yeye ni muhimu kiasi hicho?
Kwa muda mfupi ulimfanya awe chini kuliko malaika.
    Ukamvisha taji yenye utukufu na heshima.
Ukaweka kila kitu chini ya udhibiti wake.”[g](G)

Kama Mungu aliweka vitu vyote chini ya udhibiti wake, basi hakikuwepo chochote kilichoachwa ambacho hakukitawala. Lakini bado hatujamwona akitawala juu ya vyote. Kwa kipindi kifupi Yesu aliwekwa chini kuliko malaika, lakini sasa tunamwona akiwa amevaa taji ya utukufu na heshima kwa sababu aliteseka na kufa. Kwa sababu ya neema ya Mungu, Yesu alikufa kwa ajili ya kila mmoja.

10 Mungu aliyeumba vitu vyote na ambaye kwa utukufu wake vitu vyote vipo; alitaka watu wengi wawe watoto wake na kuushiriki utukufu wake. Hivyo alifanya yale aliyohitaji kuyafanya. Alimkamilisha yeye anayewaongoza watu hao kuuelekea wokovu. Kwa njia ya mateso yake Mungu alimfanya Yesu kuwa Mwokozi mkamilifu.

11 Yesu, ambaye anawafanya watu kuwa watakatifu, na wale wanaofanywa kuwa watakatifu wanatoka katika familia moja. Hivyo haoni aibu kuwaita kaka na dada zake. 12 Anasema,

“Mungu, nitawaeleza kaka na dada zangu habari zako.
    Mbele za watu wako wote nitaziimba sifa zako.”(H)

13 Pia anasema,

“Nitamwamini Mungu.”(I)

Na pia anasema,

“Nipo hapa, na pamoja ni wapo watoto
    niliopewa na Mungu.”(J)

14 Watoto hawa ni watu walio na miili ya damu na nyama. Hivyo Yesu mwenyewe akawa kama wao na akapata uzoefu ule ule waliokuwa nao. Yesu alifanya hivi ili, kwa kufa kwake, aweze kumharibu yeye aliye na nguvu ya mauti, Ibilisi. 15 Yesu akawa kama watu hawa na akafa ili aweze kuwaweka huru. Walikuwa kama watumwa maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa kwao kifo. 16 Kwa uwazi, siyo malaika ambao Yesu huwasaidia. Yeye huwasaidia watu waliotoka kwa Ibrahimu. 17 Kwa sababu hii, Yesu alifanyika kama sisi, kaka na dada zake kwa kila namna. Akawa kama sisi ili aweze kuhudumu kwa niaba yetu mbele za Mungu wa kuhani mkuu aliye mwaminifu na mwenye rehema. Ndipo angetoa sadaka ya kuziondoa dhambi za watu. 18 Na sasa anaweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa. Yuko radhi kuwasaidia kwa sababu yeye mwenyewe aliteseka na alijaribiwa.

Yesu Ni Mkuu Kuliko Musa

Hivyo, kaka na dada zangu, ninyi mliochaguliwa na Mungu muwe watu wake watakatifu, mfikirieni Yesu. Yeye ndiye tunayeamini kuwa Mungu alimtuma kuja kutuokoa na awe kuhani wetu mkuu. Mungu akamfanya kuhani wetu mkuu, naye akawa mwaminifu kwa Mungu kama Musa alivyokuwa. Naye alifanya kila kitu ambacho Mungu alimtaka akifanye katika nyumba ya Mungu. Mtu anapojenga nyumba, watu watamheshimu mjenzi zaidi kuliko ile nyumba. Ndivyo ilivyo kwa Yesu. Anastahili heshima kubwa kuliko Musa. Kila nyumba huwa imejengwa na mtu fulani, lakini Mungu alijenga kila kitu. Musa alikuwa mwaminifu kama mtumishi katika nyumba yote ya Mungu. Aliwajulisha watu yale ambayo Mungu angeyasema katika siku zijazo. Lakini Kristo ni mwaminifu katika kuitawala nyumba ya Mungu kama Mwana. Nasi tu nyumba ya Mungu, kama tukibaki wajasiri katika tumaini kuu tunalofurahia kusema kuwa tunalo.

Tunapaswa Kuendelea Kumfuata Mungu

Ni kama vile anavyosema Roho Mtakatifu:

“Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu,
    msiifanye migumu mioyo yenu kama hapo zamani,
mlipomgeuka Mungu.
    Hiyo ndiyo siku ulipomjaribu Mungu mle jangwani.
Kwa miaka 40 jangwani, watu wako wakaona niliyoyatenda.
    Lakini walinijaribu na ustahimilivu wangu.
10 Hivyo nikawakasirikia.
    Nikasema, ‘Mawazo yao siku zote hayako sahihi.
    Hawajawahi kamwe kuzielewa njia zangu.’
11 Hivyo nilikasirika na kuweka ahadi:
    ‘Kamwe hawataingia katika sehemu yangu ya pumziko.’”(K)

12 Hivyo ndugu na dada, muwe makini ili asiwepo miongoni mwenu atakayekuwa na mawazo maovu yanayosababisha mashaka mengi ya kuwafanya muache kumfuata Mungu aliye hai. 13 Bali mhimizane ninyi kwa ninyi kila siku, maadamu mna kitu kinachoitwa “leo.”[h] Msaidiane ninyi kwa ninyi ili asiwepo miongoni mwenu atakayedanganywa na dhambi akawa mgumu sana kubadilika. 14 Tunayo heshima ya kushirikishana katika yote aliyo nayo Kristo endapo tutaendelea hadi mwisho kuwa na imani ya uhakika tuliyokuwa nayo mwanzoni. 15 Ndiyo sababu Roho anasema:

“Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu,
    msiifanye migumu mioyo yenu kama hapo zamani,
    wakati mlipogeuka mbali na Mungu.”(L)

16 Ni nani hawa walioisikia sauti ya Mungu na kugeuka kinyume naye? Walikuwa watu wote ambao Musa aliwaongoza kutoka Misri. 17 Na ni kina nani waliokasirikiwa na Mungu kwa miaka 40? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi. Na maiti zao zikaachwa jangwani. 18 Na ni watu gani ambao Mungu alikuwa akisema nao alipotoa ahadi kuwa kamwe wasingeingia mahali penye mapumziko? Alikuwa anazungumza nao ambao hawakumtii. 19 Hivyo tunaona kuwa hawakuruhusiwa kuingia na kupata pumziko la Mungu, kwa sababu hawakuamini.

Na bado tunayo ahadi ambayo Mungu aliwapa watu wake. Ahadi hiyo ni kwamba tuweze kuingia katika sehemu ya pumziko. Hivyo tunapaswa kuwa waangalifu ili asiwepo atakayeikosa ahadi hiyo. Ndiyo, habari njema kuhusu hilo zilielezwa kwetu kama ilivyokuwa kwao. Lakini ujumbe waliousikia haukuwasaidia. Waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani. Ni sisi tu tunaoamini tunaoweza kuingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu. Kama Mungu alivyosema:

“Nilikasirika na nikaweka ahadi:
    ‘Hawataingia kamwe kwenye sehemu yangu ya pumziko.’”(M)

Lakini kazi ya Mungu ilikamilika tangu wakati ule alipoumba ulimwengu. Ndiyo, mahali fulani katika Maandiko alizungumza juu ya siku ya saba ya juma. Alisema, “Hivyo katika siku ya saba, Mungu alipumzika kazi zake zote.”(N) Lakini katika Maandiko ya hapo juu Mungu alisema, “Hawataingia kamwe katika sehemu yangu ya pumziko.”

Hivyo fursa bado ipo kwa baadhi kuingia na kufurahia pumziko la Mungu. Lakini waliosikia kwanza habari njema juu yake hawakuweza kuingia, kwa sababu hawakutii. Hivyo Mungu akapanga siku nyingine maalumu. Inaitwa “leo.” Alizungumza juu ya siku hiyo kupitia kwa Daudi siku nyingi zilizopita kutumia maneno tuliyonukuu mwanzoni:

“Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu,
    msiifanye migumu mioyo yenu.”(O)

Tunajua kuwa Yoshua hakuwaongoza watu hadi sehemu ya pumziko ambayo Mungu aliwaahidi. Tunalijua hili kwa sababu Mungu alisema baadaye kuhusu siku ya pumziko. Hii inaonesha kuwa pumziko la siku ya saba[i] kwa watu wa Mungu bado linakuja. 10 Mungu alipumzika alipokamilisha kazi yake. Hivyo kila mmoja anayeingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu vilevile atapata pumziko kutoka katika kazi yake kama Mungu alivyofanya. 11 Hivyo hebu na tujitahidi tuwezavyo kuingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu. Tunapaswa kujitahidi ili asiwepo miongoni mwetu atakayepotea kwa kufuata mfano wa wale waliokataa kumtii Mungu.

12 Neno la Mungu[j] liko hai na linatenda kazi. Lina ukali kupita upanga ulio na makali sana na hukata hadi ndani yetu. Hukata ndani hadi sehemu ambayo nafsi na roho huwa zimeunganishwa pamoja. Neno la Mungu hukata hadi katikati ya maungio na mifupa yetu. Linahukumu mawazo na hisia ndani ya mioyo yetu. 13 Hakuna chochote ulimwenguni mwote kinachoweza kufichika mbele za Mungu. Anaweza kuviona vitu vyote kwa uwazi kabisa. Kila kitu kiko wazi mbele zake. Na kwake tutapaswa kujieleza jinsi tulivyoishi.

Yesu Kristo Ndiye Kuhani Wetu Mkuu

14 Tunaye kuhani mkuu sana ambaye ameenda kuishi na Mungu kule mbinguni. Yeye ni Yesu Mwana wa Mungu. Hivyo tuendelee kuitamka imani yetu katika yeye. 15 Yesu, kuhani wetu mkuu, anaweza kuuelewa udhaifu wetu. Yesu alipoishi duniani, alijaribiwa katika kila njia. Alijaribiwa kwa njia hizo hizo tunazojaribiwa, lakini hakutenda dhambi. 16 Tukiwa na Yesu kama kuhani wetu mkuu, tunaweza kujisikia huru kuja mbele za kiti cha enzi cha Mungu ambako kuna neema. Hapo tunapata rehema na neema ya kutusaidia tunapokuwa tunahitaji.

Kila kuhani Mkuu wa Kiyahudi alichaguliwa kutoka miongoni mwa watu. Kuhani huyo anapewa kazi ya kuwasaidia watu katika mambo wanayopaswa kumfanyia Mungu. Anapaswa kumtolea Mungu sadaka na sadaka za dhambi. Kuhani mkuu anao udhaifu wake binafsi. Hivyo anapaswa kuwa mpole kwa wale wanaokosea kwa sababu ya kutokujua. Hutoa sadaka kwa ajili ya dhambi zao, lakini kutokana na udhaifu wake anapaswa pia kutoa sadaka kwa ajili dhambi zake mwenyewe.

Kuwa kuhani mkuu ni heshima. Lakini hayupo anayejichagua mwenyewe kwa ajili ya kazi hii. Mtu huyo anapaswa kuwa amechaguliwa na Mungu kama alivyokuwa Haruni. Ndivyo ilivyo hata kwa Kristo. Hakujichagua mwenyewe kuwa na heshima na kuwa kuhani mkuu. Lakini Mungu alimchagua. Mungu akamwambia:

“Wewe ni mwanangu.
    Leo nimekuwa baba yako.”(P)

Na katika sehemu nyingine ya Maandiko Mungu anasema:

“Wewe ni kuhani mkuu milele;
    kama Melkizedeki alivyokuwa kuhani.”(Q)

Yesu alipoishi duniani alimwomba Mungu, akiusihi msaada kutoka kwa yule anayeweza kumwokoa kutoka mauti. Alimwomba Mungu kwa sauti kuu na kwa machozi. Na Mungu alizisikia sala zake kwa sababu ya heshima yake kuu kwa Mungu. Yesu alikuwa mwana wa Mungu, lakini aliteseka, na kwa njia ya mateso yake alijifunza kutii chochote alichosema Mungu. Hili lilimfanya yeye awe kuhani mkuu mkamilifu, anayetoa njia kwa ajili ya kila mmoja anayemtii ili kuokolewa milele. 10 Mungu alimfanya yeye kuhani mkuu, kama alivyokuwa Melkizedeki.

Tahadhari Kuhusu Kuanguka

11 Tunayo mambo mengi ya kuwaeleza kuhusu hili. Lakini ni vigumu kufafanua kwa sababu mmeoteza shauku ya kusikiliza. 12 Mmekuwa na muda wa kutosha ambapo sasa mngepaswa kuwa walimu. Lakini mnahitaji mtu awafundishe tena mafundisho ya Mungu ya mwanzo. Bado mnahitaji mafundisho ambayo yako kama maziwa. Hamjafikia kiwango cha chakula kigumu. 13 Yeyote anayeishi kwa kutegemea maziwa tu bado ni mtoto mchanga, hayupo tayari kuelewa zaidi kuhusu kuishi kwa haki. 14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu ambao wamekua. Kutokana na uzoefu wao wamejifunza kuona tofauti baina ya jema na ovu.

1-2 Hivyo tusiendelee tena na masomo ya msingi juu ya Kristo. Tusiendelee kurudia kule tulikoanzia. Tuliyaanza maisha yetu mapya kwa kugeuka kutoka katika uovu tuliotenda zamani na kwa kumwamini Mungu. Hapo ndipo tulipofundishwa kuhusu mabatizo,[k] kuwawekea watu mikono,[l] ufufuo wa wale waliokwisha kufa, na hukumu ya mwisho. Sasa tunahitajika kuendelea mbele hadi kwenye mafundisho ya ukomavu zaidi. Na hayo ndiyo tutayafanya Mungu akitupa kibali.

4-6 Baada ya watu kuiacha njia ya Kristo, je unaweza kuwafanya wabadilike tena katika maisha yao? Ninazungumzia wale watu ambao mwanzo walijifunza kweli, wakapokea karama za Mungu, na kushiriki katika Roho Mtakatifu. Walibarikiwa kusikia ujumbe mzuri wa Mungu na kuziona nguvu kuu za ulimwengu wake mpya. Lakini baadaye waliziacha zote, na siyo rahisi kuwafanya wabadilike tena. Ndiyo sababu wale watu wanaomwacha Kristo wanamsulibisha msalabani kwa mara nyingine, wakimwaibisha yeye mbele ya kila mtu.

Watu wengine wako kama ardhi inayopata mvua nyingi na kuzaa mazao mazuri kwa wale wanaoilima. Aina hiyo ya ardhi inazo baraka za Mungu. Lakini watu wengine wako kama ardhi ambayo huzalisha miiba na magugu tu. Haifai na iko katika hatari ya kulaaniwa na Mungu. Itateketezwa kwa moto.

Rafiki zangu, sisemi haya kwa sababu nafikiri kuwa yanawatokea ninyi. Kwa hakika tunatarajia kuwa mtafanya vizuri zaidi; kwamba mtayafanya mambo mema yatakayotokea katika wokovu wenu. 10 Mungu ni wa haki, na ataikumbuka kila kazi mliyoifanya. Atakumbuka kuwa mliuonesha upendo wenu kwake kwa kuwasaidia watu wake na kwamba mnaendelea kuwasaidia. 11 Tunamtaka kila mmoja wenu awe radhi na mwenye shauku ya kuuonyesha upendo kama huo katika maisha yenu yote. Ndipo mtakapokuwa na uhakika wa kupata kile mnachokitumaini. 12 Hatupendi muwe wavivu. Tunapenda muwe kama wale, kwa sababu ya imani yao na uvumilivu, watapokea kile Mungu alichoahidi.

13 Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu. Na hayuko yeyote aliye mkuu kuliko Mungu, hivyo akaweka ahadi yenye kiapo kwa jina lake mwenyewe; kiapo ambacho atatimiza alichoahidi. 14 Alisema, “Hakika nitakubariki. Nitakupa wewe wazaliwa wengi.”(R) 15 Ibrahimu akangoja kwa uvumilivu hili litimie, na baadaye akapokea kile Mungu alichoahidi.

16 Mara nyingi watu hutumia jina la mtu aliye mkuu zaidi yao ili kuweka ahadi yenye kiapo. Kiapo huthibitisha kwamba walichokisema ni kweli, na hakuna haja ya kubishana juu ya hilo. 17 Mungu alitaka kuthibitisha kuwa ahadi yake ilikuwa kweli. Alitaka kuthibitisha hili kwa wale ambao wataipokea ahadi. Aliwataka waelewe kwa uwazi kwamba makusudi yake kamwe hayabadiliki. Hivyo Mungu akisema kitu fulani kingetokea, na akathibitisha aliyosema kwa kuongezea kiapo. 18 Mambo haya mawili hayawezi kubadilika: Mungu hawezi kusema uongo anaposema kitu, na hawezi kudanganya anapoweka kiapo.

Hivyo mambo yote hayo ni ya msaada mkubwa kutusaidia sisi tuliomjia Mungu kwa ajili ya usalama. Yanatuhimiza kuling'ang'ania tumaini lililo letu. 19 Tumaini hili tulilonalo ni kama nanga kwetu. Ni imara na la uhakika na hutulinda salama. Huenda hadi nyuma ya pazia[m] katika mahali patakatifu zaidi kwenye hekalu la kimbingu la Mungu. 20 Tayari Yesu amekwisha kuingia hapo na kuifungua njia kwa ajili yetu. Amefanyika kuhani mkuu milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International