Beginning
1 Salamu kutoka kwa Paulo, mtumwa wa Mungu na mtume aliyetumwa na Yesu Kristo. Kazi yangu ni kuwasaidia wateule wa Mungu kumwamini Yeye zaidi na kuyaelewa kwa kina mafundisho ya Kristo. Mafundisho haya yatawaongoza kuishi katika njia inayomtukuza na kumpendeza Mungu. 2 Na kisha wakatarajie kuishi pamoja na Mungu milele. Kabla ya mwanzo wa ulimwengu, Mungu aliahidi uzima wa milele kwa watu wake. 3 Na wakati sahihi ulipotimia aliidhihirisha ile habari njema. Ujumbe huo ulikabidhiwa kwangu kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu kumwambia kila mtu.
4 Nakuandikia wewe Tito, mwanangu halisi katika imani tunayoshiriki:
Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu[a] Mwokozi wetu iwe nanyi.
Kazi ya Tito Krete
5 Nilikuacha kule Krete ili uweze kuyakamilisha yale yaliyokuwa yamebaki kufanyiwa kazi. Kisha nakuagiza uteue wazee na kuwaweka kuwa viongozi katika kila mji. 6 Anayeweza kuteuliwa ni yule ambaye halaumiwi kwa matendo yoyote mabaya, na aliye mwaminifu kwa mkewe,[b] na anao watoto wanaoamini Mungu[c] na ambao sio wakaidi. 7 Kwa sababu kila askofu,[d] anao wajibu wa kuitunza kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiyelaumiwa kwa kutenda mabaya yoyote. Asiwe mtu mkorofi. Asiwe mtu aliye mwepesi wa hasira. Asiwe mgomvi. Asiwe mtu mwenye kujipatia fedha toka kwa watu kwa njia ya udanganyifu. 8 Mzee anapaswa kuwa mtu anayewakaribisha watu nyumbani mwake. Anapaswa kuyapenda yaliyo mema. Azingatie kuishi maisha yaliyo matakatifu. Na awe na uwezo wa kudhibiti nafsi yake. 9 Anapaswa kuwa mwaminifu kwa ujumbe ule ule wa kweli tunaofundisha. Kwa namna hiyo ataweza kuwatia moyo wengine kwa mafundisho ya kweli na yenye manufaa.[e] Na ataweza kuwathibitishia wale wanaopinga mafundisho yake ya kuwa hawako sahihi.
10 Aina hii ya mafundisho ni muhimu kwa sababu wako watu wengi wasiopenda kumsikiliza mtu yeyote. Hao wanazungumzia mambo yao wenyewe yasiyo ya maana na kuwapotosha wengine waiache kweli. Ninaongelea hasa baadhi ya Wayahudi waaminio.[f] 11 Ni lazima wanyamazishwe kwani wanaivuruga jamii nzima kwa kufundisha mambo ambayo wasingepaswa kuyafundisha, lakini wanafanya hivyo ili kujipatia mapato yasiyo ya uaminifu! 12 Mmoja miongoni mwa watu wa kwao, Nabii kutoka Krete, alisema:
“Wakrete ni waongo daima.
Si bora kuliko wanyama wa porini.
Daima wapo tayari kula,
lakini hawapendi kufanya kazi.”
13 Usemi huu ni kweli, kwa hivyo wakaripie vikali ili wawe imara katika imani yao 14 na wasiendelee kuzisikilliza simulizi zinazopotosha za Kiyahudi na amri za wanadamu walioiacha kweli.
15 Kwa wale watu wenye mawazo yaliyo safi, kila kitu ni safi. Lakini hakuna kinachoweza kuwa safi kwa wasioamini ambao dhambi zao zimewafanya kuwa wachafu. Mawazo yao daima huwa yasiyo haki, na dhamiri zao pia zimekuwa chafu. 16 Hao hudai kuwa wanamjua Mungu, lakini matendo yao maovu yanaonesha kwa hakika kuwa hawamjui. Ni watu wenye kuchukiza mno na wasiotii, na hawafai kwa lo lote lililo jema.
Kufuata Mafundisho ya Kweli
2 Lakini wewe Tito daima uwaambie waaminio mambo yanayokubaliana na mafundisho ya kweli na yenye uzima. 2 Wanaume wazee wanapaswa kuwa na kiasi na kufanya mambo yenye kuleta heshima. Wanapaswa kuwa na busara katika maisha yao. Kuwa na nguvu katika imani kwa Mungu, upendo kwa wengine, na uvumilivu.
3 Vivyo hivyo wafundishe wanawake wazee wawe na mwenendo mzuri. Wafundishe wasiwe wachochezi na wasiwe watumwa wa mvinyo. Wanapaswa kufundisha yale yaliyo mema. 4 Kwa jinsi hiyo wataweza kuwakumbusha wanawake vijana jinsi wanavyopaswa kuishi. Wanawake vijana wanapaswa kuwaonesha upendo waume zao na kuwapenda watoto wao. 5 Wanapaswa kuwa na busara na wasafi kiroho, wakizitunza nyumba zao, kuwa wakarimu, na kuwa tayari kuwatumikia waume zao wenyewe, ili asiwepo atakayeudharau ujumbe wa Neno la Mungu.
6 Kadhalika endelea kuwahimiza wanaume vijana kuwa na busara. 7 Katika kila kitu ujioneshe kuwa wewe ni mfano wa matendo mema. Katika mafundisho yako onesha kuwa una moyo safi na uko makini. 8 Ufundishe kile ambacho ni sahihi kwa wazi, ili asiwepo yeyote atakayepinga mafundisho yako. Tumia mazuri ambayo hayatasemwa vibaya ili wale wanaokupinga waaibishwe kwa ajili ya kukosa lo lote baya la kusema dhidi yetu.
9 Wafundishe watumwa kuwatii bwana zao katika kila jambo, wajitahidi kuwapendeza na sio kubishana nao 10 wala kwa siri wasiwaibie bali waudhihirishe uaminifu kamili, ili katika mambo yote wayapatie sifa njema mafundisho kutoka kwa Mungu, Mwokozi wetu.
11 Maana Mungu ameidhihirisha neema yake inayookoa kwa watu wote. 12 Hiyo inatufundisha kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia ili tuishi katika ulimwengu wa sasa kwa njia ya werevu, haki na kuionesha heshima yetu kwa Mungu, 13 kadri tunavyosubiri ile Siku iliyobarikiwa tunayoitumaini ambapo utukufu wa Mungu wetu mkuu na Mwokozi Yesu Kristo itakapofunuliwa. 14 Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili aweze kutuweka huru sisi kutoka katika uovu wote na kuweza kutusafisha kwa ajili yake watu walio wake mwenyewe, wale walio na shauku ya kufanya matendo mema.
15 Endelea kufundisha ukihimiza na kukemea kuhusu mambo haya, na fanya hivyo kwa mamlaka yote, na mtu yeyote asikudharau.
Njia Sahihi ya Maisha
3 Uwakumbushe watu wako ya kuwa wanapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya watawala wao na uongozi wa dola. Wanapaswa kuwatii viongozi hao na kuwa tayari kufanya kila jema wanaloweza. 2 Waambie hawapaswi kumtukana mtu yeyote, bali wawe wema na wapole kwa watu wote.
3 Hapo zamani hata sisi tulikuwa wajinga, wakaidi na tulidanganyika. Tulikuwa watumwa kwa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu. Tulichukiwa na watu nasi tukachukiana wenyewe kwa wenyewe.
4 Lakini Mungu Mwokozi wetu alitudhihirishia
wema na upendo alionao kwa wanadamu.
5 Alituokoa kwa sababu yeye ni mwenye rehema,
siyo kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda na kupata kibali chake,
bali ni kwa rehema yake.
Yeye aliziosha dhambi zetu,
akatupa maisha mapya kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Ikawa kama kuzaliwa kwa mara ya pili.
6 Mungu ametumiminia Roho Mtakatifu kwa wingi kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu.
7 Kwa neema yake Mungu alituweka huru mbali na dhambi.
Akatufanya kuwa warithi wake tulio na tumaini la uzima wa milele.
8 Huu ni usemi wa kuaminiwa. Nawataka ninyi kuyasisitiza mambo haya, ili wale waliokwisha kumwamini Mungu waweze kujitoa katika matendo mema. Mambo haya ni mazuri na ya kuwanufaisha watu.
9 Lakini yaepuke mabishano ya kipumbavu, majadiliano kuhusu koo, mabishano na ugomvi kuhusu Sheria, maana hayana faida na hayafai. 10 Mwepuke mtu anayesababisha matengano baada ya onyo la kwanza na la pili, 11 kwa sababu unajua kuwa mtu wa jinsi hiyo amepotoka na anatenda dhambi. Amejihukumu mwenyewe.
Maelekezo ya Mwisho na Salamu
12 Nilipomtuma kwako Artema au Tikiko, jitahidi kuja Nikopoli ili kuonana nami, kwa sababu nimeamua kukaa huko wakati wa msimu wa baridi. 13 Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena pamoja na Apolo kwa lo lote watakalohitaji kwa ajili ya safari yao, ili wasipungukiwe na kitu cho chote. 14 Watu wetu wanapaswa kujifunza kujihusisha katika kutenda mema ili kusaidia kukitokea mahitaji, ili wasiwe watu wasiokuwa na manufaa.
15 Wote nilio pamoja nami wanakusalimu. Uwasalimu wote wanaotupenda katika imani.
Neema ya Mungu iwe nanyi nyote.
1 Kutoka kwa Paulo mfungwa kwa kusudi la Kristo Yesu,[a] na kutoka kwa Timotheo ndugu yetu. Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtenda kazi pamoja nasi; 2 kwa Afia dada yetu, Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa linalokutania nyumbani mwako.
3 Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo ziwe pamoja nawe.
Upendo na Imani ya Filemoni
4 Namshukuru Mungu wangu siku zote kila ninapokukumbuka katika maombi yangu, 5 kwa sababu nasikia juu ya upendo na uaminifu ulionao katika Bwana Yesu na unaouonesha kwa watu wa Mungu. 6 Ninaomba kwamba ile imani unayoishiriki pamoja nasi ikusaidie wewe kuelewa kila fursa tulio nayo ya kutenda mema kama wale tunaomwamini Kristo. 7 Nimepokea furaha kubwa na faraja kutokana na upendo wako, kwa sababu mioyo ya watu wa Mungu imepata nguvu mpya kwa juhudi zako ndugu yangu.
Mpokee Onesimo Kama Kaka
8 Hivyo hiyo ndiyo sababu nakuagiza wewe kufanya jambo unalopaswa kulifanya. Kwa mamlaka niliyo nayo katika Kristo naweza kukuamuru kufanya hilo. 9 Lakini sikuamuru; bali kwa sababu ya upendo nakusihi ufanye hivyo. Mimi Paulo, niliye mzee wa umri sasa, na sasa mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu. 10 Ninakusihi kuhusu mwanangu Onesimo niliyemleta[b] katika maisha mapya tulio nayo katika Bwana nilipokuwa gerezani. 11 Huyo ambaye siku za nyuma hakuwa wa manufaa kwako, lakini sasa anafaa[c] sio kwako tu bali hata kwangu mimi.
12 Ninamrudisha kwako, kitu ambacho kimekuwa kigumu sawa na kuupoteza moyo wangu.[d] 13 Ningetamani kuendelea kuwa naye hapa, ili aendelee kunihudumia kwa niaba yako nitakapokuwa bado gerezani kwa ajili ya Habari Njema. 14 Lakini sikuwa tayari kufanya jambo lo lote bila ruhusa yako, ili kila jambo lako zuri litendeke bila lazima bali kwa hiari yako mwenyewe.
15 Labda sababu ya Onesimo kutenganishwa nawe kwa kipindi kifupi ni kuwezesha muwe pamoja siku zote, 16 si mtumwa tena, bali ni zaidi ya mtumwa; kama ndugu mpendwa. Nampenda sana lakini wewe utampenda zaidi, sio tu kama kaka katika familia yenu, bali pia kama mmoja wa walio katika familia ya Bwana.
17 Ikiwa unanitambua mimi kama niliye mwenye imani moja nawe, basi mpokee Onesimo na umkubali kama vile ambavyo ungenikubali. 18 Endapo amekukosea jambo lo lote au unamdai kitu cho chote, unidai mimi badala yake. 19 Mimi Paulo naandika kwa mkono wangu mwenyewe ya kwamba nitakulipa. Tena sina sababu ya kukumbusha kuwa una deni kwangu juu ya maisha yako. 20 Kwa hiyo kaka yangu, kama mfuasi wa Bwana, tafadhali nipe upendeleo[e] katika hili. Ndipo itakuwa faraja kuu kwangu kama kaka yako katika Kristo. 21 Ninapokuandikia barua hii nina ujasiri mkubwa kwamba utakubaliana nami na najua kwamba utafanya zaidi ya haya ninayokuomba.
22 Pamoja na hayo naomba uniandalie chumba cha kufikia, kwa sababu nina matumaini kwamba kwa maombi yenu nitaachiliwa na kuletwa kwenu.
Salamu za Mwisho
23 Epafra mfungwa pamoja nami katika Kristo Yesu anakusalimu. 24 Marko, Aristarko, Dema, na Luka watendakazi pamoja nami nao wanakusalimu.
25 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.
© 2017 Bible League International