Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
1 Timotheo 1-6

Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu atupaye tumaini.

Ninakuandikia wewe, Timotheo. Wewe ni kama mwanangu halisi kwa sababu ya imani yetu.

Neema, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu ziwe pamoja nawe.

Maonyo kuhusu Mafundisho ya Uongo

Nilipokwenda Makedonia, nilikuomba ubaki Efeso. Baadhi ya watu huko wanafundisha mambo yasiyo ya kweli, nami ninataka uwaonye waache. Uwaambie wasitumie muda wao kusimulia simulizi zisizo na maana za mambo ya kale na kutengeneza orodha ndefu ya mababu. Mambo hayo husababisha mabishano tu na hayaisaidii katika kuikamilisha kazi ya Mungu tuliyopewa, ambayo ni lazima tuikamilishe kwa imani. Kusudi langu la kukueleza ufanye jambo hili ni kutaka kukuza upendo; aina ya upendo unaooneshwa na wale ambao mawazo yao ni safi; watu ambao hufanya yale wanayojua kuwa ni sahihi na ambao imani yao kwa Mungu ni ya kweli. Lakini wengine wamekosa jambo hili la msingi katika mafundisho yao na wamepoteza mwelekeo. Sasa wanazungumza juu ya mambo yasiyo na msaada kwa mtu yeyote. Wanataka kuwa walimu wa sheria,[b] lakini hawafahamu mambo wanayosema, wanasema kwa ujasiri wote juu ya mambo wasiyoyaelewa wenyewe.

Tunajua kwamba sheria ni nzuri ikiwa mtu anaitumia kwa usahihi. Pia tunajua kwamba sheria haikutengenezwa kwa ajili ya wale wanaotenda haki. Imetengenezwa kwa ajili ya wale wanayoipinga na kukataa kuifuata. Sheria ipo kwa ajili ya wenye dhambi wanaompinga Mungu na mambo yote yanayompendeza. Ipo kwa ajili ya wale wasio na hamu ya mambo ya kiroho na kwa ajili ya wale wanaowaua baba au mama zao au mtu yeyote yule. 10 Ipo kwa ajili ya watu wanaotenda dhambi ya uasherati, kwa wanaume wanaolala na wanaume wenzao au wavulana, kwa wote wanaoteka watu na kuwauza kama watumwa, kwa wote wanaodanganya au wale wasiosema ukweli wakiwa katika kiapo, na kwa ajili ya wale walio kinyume na mafundisho ya kweli ya Mungu. 11 Mafundisho hayo ni sehemu ya Habari Njema ambayo Mungu wetu wa utukufu alinipa kuhubiri na ndani yake tunauona utukufu wake.

Shukrani kwa Rehema za Mungu

12 Ninamshukuru Kristo Yesu Bwana wetu kwa sababu aliniamini na kunipa kazi hii ya kumtumikia. Yeye hunitia nguvu ya kufanya kazi hii. 13 Hapo zamani nilimtukana Kristo. Nikiwa mtu mwenye majivuno na mkorofi, niliwatesa watu wake. Lakini Mungu alinihurumia kwa sababu sikujua nilichokuwa nafanya. Nilifanya hayo kabla sijaamini. 14 Lakini Bwana wetu alinipa kiwango kikubwa cha neema yake. Na pamoja na neema hiyo imani na upendo ulio katika Kristo Yesu vilifuata.

15 Huu ndiyo usemi wa kweli unaopaswa kukubaliwa pasipo kuuliza maswali; kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, nami ni mbaya zaidi ya wote. 16 Lakini nilipata rehema kwa sababu ili Kristo Yesu aweze kunitumia, mimi mtenda dhambi kuliko wote, ili kuonesha uvumilivu wake usio na kikomo. Alitaka niwe mfano kwa wale ambao wangemwamini na kupata uzima wa milele. 17 Heshima na utukufu kwa mfalme anayetawala milele. Hawezi kuharibiwa wala kuonekana. Heshima na utukufu apewe Mungu wa pekee milele na milele, Amina.

18 Timotheo wewe ni mwanangu mwenyewe kwa sababu ya ushirika wetu wa imani ya kweli. Ninayokuambia kuyatenda yanakubaliana na unabii[c] ambao ulisemwa juu yako hapo zamani. Nataka uukumbuke unabii huo na kupigana vita vizuri vya imani. 19 Endelea kumwamini Mungu na kutenda yale unayojua kuwa ni sahihi. Watu wengine hawajatenda haya, na imani yao sasa imeharibiwa. 20 Himenayo na Iskanda ni mfano wa watu hao. Nimewakabidhi kwa Shetani ili wafundishwe kutosema kinyume cha Mungu.

Mungu Anataka Tumwombee Kila Mtu

Kwanza kabisa, ninakuagiza uwaombee watu wote. Uwaombee kwa Mungu ili awabariki na kuwapa mahitaji yao. Kisha umshukuru Yeye. Unapaswa kuwaombea watawala na wote wenye mamlaka. Uwaombee viongozi hawa ili tuweze kuishi maisha yenye utulivu na amani, maisha yaliyojaa utukufu kwa Mungu na yanayostahili heshima. Hili ni jambo jema na linampendeza Mungu Mwokozi wetu.

Mungu anataka kila mtu aokolewe na aielewe kweli kikamilifu. Kuna Mungu mmoja tu, na kuna mwanadamu mmoja tu anayeweza kuwaleta pamoja wanadamu wote na Mungu wao. Huyo mtu ni Kristo Yesu kama mwanadamu. Alijitoa mwenyewe kulipa deni ili kila mtu awe huru. Huu ni ujumbe ambao Mungu alitupa wakati unofaa. Nami nilichaguliwa kama mtume kuwaambia watu ujumbe huo. Ninasema kweli. Sidanganyi. Nilichaguliwa kuwafundisha wasio Wayahudi na nimefanya kazi hii kwa imani na ukweli.

Maagizo Maalumu kwa Wanawake na Wanaume

Nataka wanaume walio kila mahali waombe. Ni lazima wawe watu wanaoishi kwa kumpendeza Mungu na wanaonyoosha mikono yao wanapoomba na wawe watu wasio na hasira na wanaopenda mabishano.

Na ninawataka wanawake wajipambe kwa namna inayofaa. Mavazi yao yawe yanayofaa na yanayostahili. Hawapaswi kuvutia watu kwa kutengeneza nywele zao kwa mitindo ya ajabu ama kwa kuvaa dhahabu, vito au lulu au nguo za gharama. 10 Lakini wajipambe na kuvutia kwa matendo mema wanayofanya. Hayo ndiyo yanayofaa zaidi kwa wanawake wanaosema kuwa wamejitoa kwa ajili ya Mungu.

11 Mwanamke anapaswa kujifunza akisikiliza kwa utulivu huku akiwa radhi kutii kwa moyo wake wote. 12 Simruhusu mwanamke kumfundisha mwanaume au kumwelekeza jambo la kufanya. Bali lazima asikilize kwa utulivu, 13 kwa sababu Adamu aliumbwa kwanza na Hawa akaumbwa baadaye. 14 Na Adamu hakudanganywa.[d] Bali mwanamke ndiye aliyedanganywa naye akatenda dhambi. 15 Lakini wanawake wataokolewa kwa jukumu lao la kuzaa watoto.[e] Wakiendelea kuishi katika imani, upendo, utakatifu na tabia njema.

Viongozi katika Kanisa

Usemi huu ni wa kweli kwamba yeyote mwenye nia ya kuhudumu kama mzee,[f] anatamani kazi njema. Mzee[g] lazima awe mtu mwema asiyelaumiwa na mtu yeyote. Anapaswa kuwa mwaminifu kwa mke wake.[h] Anapaswa kuwa na kiasi, mwenye busara na mwenye mwenendo mzuri katika maisha, anayeheshimiwa na watu wengine, aliye tayari kuwasaidia watu kwa kuwakaribisha katika nyumba yake. Ni lazima awe mwalimu mzuri. Askofu asizoee kunywa mvinyo wala kuwa mgomvi. Bali awe mpole na mtu wa amani, na asiyependa fedha. Ni lazima awe kiongozi mzuri kwa familia yake mwenyewe. Hii ina maana kwamba watoto wake wanamtii kwa heshima zote. Ikiwa mtu hawezi kuiongoza familia yake mwenyewe, hawezi kulitunza Kanisa la Mungu.

Ni lazima askofu asiwe yule aliyeamini hivi karibuni. Hii inaweza kumfanya awe na kiburi. Kisha anaweza akahukumiwa kwa kiburi chake kama vile Shetani alivyopanga. Pia, ni lazima askofu aheshimiwe na watu walio nje ya Kanisa. Kwa namna hiyo hataweza kukosolewa na kuabishwa na wengine na kunasa kwenye mtego wa Shetani.

Mashemasi

Kwa njia hiyo hiyo, watu wanaoteuliwa kuwa mashemasi inawapasa kuwa wale wanaostahili kuheshimiwa. Wasiwe watu wanaosema mambo wasiokuwa nayo moyoni au wanaotumia muda wao mwingi katika ulevi. Wasiwe watu wanaowaibia fedha watu wengine kwa udanganyifu. Ni lazima waifuate imani ya kweli ambayo Mungu ameiweka wazi kwetu na sikuzote wawe watu wanaotenda mambo yaliyo sahihi. 10 Hao unapaswa kuwapima kwanza. Kisha, ukigundua kuwa hawawezi kushitakiwa jambo lolote baya walilotenda, basi wanaweza kuwa mashemasi.

11 Kwa njia hiyo hiyo wanawake wanaoteuliwa kuwa mashemasi wanapaswa kuwa wale wanaoastahili kuheshimiwa. Wasiwe wanawake wanaosema mambo mabaya juu ya watu wengine. Ni lazima wawe na kiasi. Ni lazima wawe wanawake wanaoweza kuaminiwa kwa kila jambo.

12 Wanaume walio mashemasi lazima wawe waaminifu katika ndoa. Ni lazima wawe viongozi wema wa watoto na familia zao binafsi. 13 Mashemasi wanaofanya kazi yao vyema wanajitengenezea nafasi nzuri ya kuheshimiwa. Nao kwa kiasi kikubwa sana wanajihakikishia imani yao katika Kristo Yesu.

Siri ya Maisha Yetu

14 Ninatarajia kuja kwenu hivi karibuni. Lakini ninakuandikia maneno haya sasa, 15 ili kwamba, hata kama sitakuja mapema, utafahamu jinsi ambavyo watu wanapaswa kuishi katika familia[i] ya Mungu. Familia hiyo ni kanisa la Mungu aliye hai. Na Kanisa la Mungu ni msaada na msingi wa ukweli. 16 Ndiyo, Mungu ametuonesha siri ya maisha yanayompa heshima na kumpendeza Yeye. Siri hii ya ajabu ni ukweli ambao wote tunakubaliana nao:

Kristo[j] alijulikana kwetu katika umbile la kibinadamu;
    alioneshwa na Roho[k] kuwa kama alivyojitambulisha;
alionwa na malaika.
    Ujumbe kuhusu Yeye ulitangazwa kwa mataifa;
watu ulimwenguni walimwamini;
    alichukuliwa juu mbinguni katika utukufu.

Maonyo juu ya Walimu wa uongo

Roho anasema wazi wazi kwamba katika siku za mwisho wengine watajitenga na imani. Watazitii roho zinazodanganya, na kufuata mafundisho ya mashetani. Mafundisho hayo yanafundishwa na watu wanaodanganya na kuwafanyia hila wengine. Watu hawa waovu hawapambanui kati ya mema na maovu. Ni kana kwamba dhamiri zao zimeharibiwa kwa chuma cha moto. Wanasema ni vibaya kuoa. Na wanasema kwamba kuna baadhi ya vyakula ambavyo watu lazima wasile. Lakini Mungu aliumba vyakula hivi, na wale wanaoamini na kuelewa ukweli wanaweza kuvila kwa shukrani. Kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, hakuna chakula kitakachokataliwa kama kikikubaliwa kwa shukrani. Kila kitu alichokiumba kiliumbwa kitakatifu kwa namna alivyosema na kwa maombi.

Uwe Mtumishi Mwema wa Kristo Yesu

Waambie haya kaka na dada huko. Hii itakuonesha wewe kuwa ni mtumishi mwema wa Kristo Yesu. Utaonyesha kwamba umefundishwa maneno ya imani na mafundisho mazuri uliyoyafuata. Usitumie muda wowote katika masimulizi ya kipuuzi ambayo hayakubaliani na ukweli wa Mungu. Badala yake jizoeshe mwenyewe kuishi maisha ya kumheshimu na kumpendeza Mungu. Kufanya mazoezi ya mwili wako kuna manufaa kidogo kwako. Lakini kujaribu kumpendeza Mungu kwa njia zote kunakufaa zaidi. Kunakuletea baraka katika maisha haya na maisha ya baadaye pia. Huu ni usemi wa kweli ambao unaweza kukukubaliwa bila kuuliza swali: 10 Tunayo matumaini kwa Mungu aliye hai, Mwokozi wa watu wote. Ambaye hasa, ni Mwokozi wa wale wote wanaomuamini. Na hii ndiyo sababu tunafanya kazi na kupambana.

11 Amuru na kufundisha mambo haya. 12 Wewe ni kijana, lakini usiruhusu yeyote kukufanya wewe kama si mtu muhimu. Uwe mfano kuonesha waamini namna wanavyoweza kuishi. Waoneshe kwa namna unavyosema, unavyoishi, unavyopenda, unavyo amini, na namna ya maisha yako safi.

13 Endelea kusoma Maandiko kwa watu, watie moyo, na uwafundishe. Fanya hivyo mpaka nitakapo kuja. 14 Kumbuka kutumia kipawa ulichonacho, ambacho ulipewa kupitia unabii wakati kundi la wazee lilipo kuweka mikono juu yako. 15 Endelea kufanya haya, na jitoe maisha yako kutenda hayo. Kisha kila mtu anaweza kuona namna ilivyo vema unavyotenda. 16 Uwe mwangalifu katika maisha na mafundisho yako. Endelea kuishi na kufundisha kwa usahihi. Kisha, utajiokoa mwenyewe na wale wanaosikiliza mafundisho yako.

Usiseme kwa hasira kwa mtu mzima. Lakini sema naye kama baba yako. Watunze vijana kama kaka zako. Watendee wanawake wazee kama mama zako. Na watendee wanawake vijana kwa heshima zote kama vile ni dada zako.

Kuwatunza Wajane

Watunze wajane ambao hasa wanahitaji msaada. Lakini mjane akiwa na watoto au wajukuu, jambo la kwanza ambalo wanahitaji kujifunza ni hili: kutimiza wajibu waliyonao kwa wanafamilia wao. Kwa kuwapa heshima na kuwahudumia, watakuwa wanawalipa fadhila wazazi wao na pia mababu na nyanya zao. Na haya ndiyo mambo yanaompendeza Mungu. Mjane ambaye hakika anahitaji msaada ni yule ambaye ameachwa pekee yake. Anamuamini Mungu kumtunza katika mahitaji yake. Anayemuomba msaada Mungu wakati wote. Lakini mjane anayetumia maisha yake kujipenda ni hakika amekufa angali hai. Wambie waumini huko kutunza familia zao wenyewe ili kwamba asiwepo yeyote atakayesema wanafanya vibaya. Kila mtu atunze watu wa kwao, muhimu sana watunze familia zao. Kama hawatendi hayo watakuwa hawakubaliani na tunayoamini. Watakuwa wabaya kuliko hata asiyeamini.

Ili kuongezwa kwenye orodha ya wajane, mwanamke ni lazima awe na umri wa miaka 60 au zaidi, awe aliyekuwa mwaminifu kwa mume[l] wake. 10 Ni lazima ajulikane kwa mema aliyoyafanya: kulea watoto, kukaribisha wageni kwenye nyumba yake, kuwasaidia watu wa Mungu wenye uhitaji,[m] wenye shida, na kutumia maisha yake kufanya wema wa aina zote.

11 Lakini usiwaweke wajane wachanga katika orodha. Nguvu zao za mahitaji ya mwili zinawavuta wajiondea kwa Kristo, wanataka kuolewa tena. 12 Kisha watahukumiwa kustahili adhabu kwa kutofanya walichoahidi kutenda hapo kwanza. 13 Pia, wajane hawa vijana wanaanza kupoteza muda wao kwa kujihusisha na mambo ya watu wengine yasiyowahusu. Wanazungumzia mambo ambayo wasingepaswa kuzungumza. 14 Hivyo nataka wajane vijana kuolewa, kuzaa watoto, na kutunza nyumba zao. Kama wakifanya hivi, adui yetu hatakuwa na sababu ya kutupinga kwa sababu yao. 15 Lakini wajane wengine vijana wamegeuka na kumfuata Shetani.

16 Kama yupo mwanamke aliyeamini aliye na wajane katika familia yake, ni lazima awatunze yeye mwenyewe. Ndipo Kanisa halitakuwa na mzigo wa kuwatunza hao bali kuwatunza ambao hawana mtu yeyote wa kuwasaidia.

Mambo mengine zaidi juu ya Wazee na mengineyo

17 Wazee wanaoliongoza Kanisa katika njia nzuri wanapaswa kupokea heshima mara mbili;[n] hasa wale wanaofanya kazi ya kuhubiri na kufundisha. 18 Kama Maandiko yanavyosema, “Mnyama wa kazi akitumika kutenganisha ngano, usimzuie kula nafaka.”(A) Na Maandiko pia yanasema, “Mfanyakazi anatakiwa kupewa ujira wake.”(B)

19 Usimsikilize yeyote anayemshitaki mzee. Unatakiwa kuwasikiliza tu kama wapo wawili au watatu ambao wanaweza kusema alichokosea mzee. 20 Waambie wazee wanaotenda dhambi kwamba wana hatia, ufanye hivi mbele ya kanisa lote ili wengine wapate kuonywa.

21 Mbele ya Mungu na Kristo Yesu na malaika walioteuliwa, nakuambia fanya hukumu hizo bila upendeleo. Mtendee kila mtu sawa sawa.

22 Fikiri kwa makini kabla ya kuweka mikono yako juu ya yeyote kumfanya mzee. Usishiriki dhambi za wengine, na ujitunze uwe safi.

23 Timotheo, acha kunywa maji tu, kunywa na kiasi kidogo cha mvinyo. Hii itakusaidia tumbo lako, na hutaugua mara kwa mara.

24 Dhambi za watu wengine ni rahisi kuziona, hizo zinaonesha kwamba watahukumiwa. Lakini dhambi za wengine zitajulikana tu hapo baadaye. 25 Inafanana na mambo mazuri wanayofanya watu. Zingine ni rahisi kuonekana. Lakini hata kama si dhahiri sasa, hakuna hata moja itakayojificha milele.

Maagizo maalumu kwa Watumwa

Wote ambao ni watumwa waoneshe heshima kubwa kwa mabwana zao. Ndipo jina la Mungu na mafundisho yetu hayatakosolewa. Baadhi ya watumwa wanao mabwana ambao ni waamini, hivyo hao ni ndugu. Je, inamaanisha wasiwaheshimu mabwana zao? Hapana, watawatumikia hata kwa uzuri zaidi, kwa sababu wanawasaidia waaminio, watu wawapende.

Haya ni mambo ambayo lazima uyafundishe na kumwambia kila mtu kufanya.

Mafundisho ya Uongo na Utajiri wa Kweli

Watu wengine wanafundisha uongo na hawakubaliani na mafundisho ya kweli ambayo yanatoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Hawakubali mafundisho ambayo yanatuongoza kumheshimu na kumpendeza Mungu. Wanajivunia wanayoyafahamu, lakini hawaelewi chochote. Wamepagawa na wana ugonjwa wa kupenda mabishano na mapigano ya maneno. Na hayo yanaleta wivu, ugomvi, matusi, na uovu wa kutoaminiana. Daima wanaleta shida, kwa sababu ni watu ambao kufikiri kwao kumeharibiwa. Wamepoteza ufahamu wao wa ukweli. Wanafikiri kwamba kujifanya wanamheshimu Mungu ni njia ya kupata utajiri.

Kuishi kwa kumheshimu Mungu, hakika, ni njia ambayo watu hutajirika sana, kwa sababu inamaanisha wanaridhika na walivyo navyo. Tulipokuja ulimwenguni, tulikuja bila kitu, na tutakapokufa hatutachukua chochote. Hivyo, kama tukiwa na chakula na nguo, tutaridhika navyo. Watu ambao wanatamani kuwa matajiri wanajiletea majaribu wenyewe. Wananasa katika mtego. Wanaanza kutaka vitu vingi vya kijinga ambavyo vitawaumiza na kuwaharibu. 10 Kupenda fedha kunasababisha aina zote za uovu. Watu wengine wamegeuka kutoka kwenye imani yetu kwa sababu wanataka kupata fedha nyingi zaidi. Lakini wamejisababishia wenyewe maumivu mengi na huzuni.

Baadhi ya mambo ya Kukumbuka

11 Lakini wewe ni mali ya Mungu. Hivyo kaa mbali na mambo hayo yote, daima jaribu kutenda mema ili umheshimu Mungu na uwe na imani, upendo, uvumilivu, na upole. 12 Tunatakiwa tupigane kutunza imani yetu. Jaribu kwa bidii kadri unavyoweza kushinda vita vya thawabu. Tunza uzima wa milele. Ni uzima mliyouchagua kuupata mlipoikiri imani yenu katika Yesu; huo ukweli wa ajabu mliousema waziwazi kwa wote kuusikia. 13 Mbele ya Mungu na Kristo Yesu nakupa amri. Yesu ni yule aliyeshuhudia ukweli aliposimama mbele ya Pontio Pilato. Mungu ndiye anayetoa uhai kwa kila kitu. Nakuambia haya sasa: 14 Tenda niliyokuamuru kufanya bila dosari au kulaumu mpaka muda atakapo rudi. 15 Mungu atafanya hayo yatokee wakati utakapotimia. Yeye ni mwenye utukufu zaidi na mtawala pekee, mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana. 16 Mungu pekee hafi, anaishi katika nuru angavu sana ambayo watu hawawezi kusogea karibu. Hakuna mtu aliyemwona Mungu; wala anayeweza kumuona. Heshima na nguvu ni zake milele. Amina.

17 Wape amri hii wale ambao ni matajiri wa vitu vya ulimwengu huu. Waambie wasiwe na majivuno, bali wamtumaini Mungu wala si katika fedha zao. Fedha haziwezi kuaminiwa, lakini Mungu anatuhudumia kwa ukarimu mkubwa na anatupa vitu vyote ili tufurahi. 18 Waambie wale ambao ni matajiri watende mema. Wawe matajiri katika kuzifanya kazi njema. Na uwambie wawe tayari kutoa na kuwapa wengine vitu. 19 Kwa kufanya hivi, watajiwekea hazina kwa ajili yao wenyewe. Na hazina hiyo itakuwa ni msingi imara huo utakuwa msingi imara ambao maisha yao ya siku zijazo yatajengwa. Wataweza kuwa na maisha yaliyo ya kweli kabisa.

20 Timotheo, Mungu ameweka vitu vingi kwako uvitunze. Uvitunze vyema. Jitenge na watu wanaosema mambo yasiyofaa ambayo hayatoki kwa Mungu na wale wanaokupinga na “elimu” ambayo siyo “elimu” kabisa. 21 Watu wengine wanaodai kuwa na “elimu” wamepotea mbali kabisa kutokana na wanachoamini.

Ninaomba neema ya Mungu iwe kwenu nyote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International