Beginning
1 Salamu kutoka kwa Paulo, Sila na Timotheo.
Kwa kanisa la Thesalonike lililo mali ya Mungu baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.
2 Neema na amani viwe kwenu kutoka kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo.
3 Kaka na dada zetu, tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu. Na hivyo ndivyo tunavyopaswa kufanya, kwani mnatupa sababu ya kushukuru na imani yenu inakua zaidi na zaidi. Pamoja na hilo upendo ambao kila mmoja wenu anao kwa mwenzake nao unakua. 4 Hivyo tunayaeleza makanisa mengine ya Mungu namna tunavyojivuna kuhusu ninyi. Tunawaeleza jinsi mlivyoendelea kwa subira kuwa imara na waaminifu, ingawa mnateswa na kusumbuliwa na matatizo mengi.
Mungu Atafanya Mambo Kuwa Sawa
5 Huu ni uthibitisho kwamba Mungu ni wa haki katika hukumu zake. Hutaka kuwastahilisha katika ufalme wake. Kuteswa kwenu ni kwa ajili ya ufalme huo. 6 Ni haki kwa Mungu kuwaadhibu wale wanaowaletea matatizo. 7 Atawaletea unafuu wanaoteseka. Atawaletea ninyi nasi unafuu huo atakapokuja Bwana Yesu kutoka mbinguni ili wote wamwone, pamoja na malaika wake wenye nguvu zilizotukuka. 8 Atakuja na moto unaoteketeza kuwaadhibu wasiomjua Mungu na wanaokataa kuitii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu. 9 Wataadhibiwa na maangamizi yasio na mwisho. Hawataruhusiwa kuwa na Bwana lakini watatengwa mbali na nguvu zake za utukufu. 10 Hii itatokea siku ambapo Bwana Yesu atakuja na kupokea heshima miongoni mwa watu wake watakatifu. Na wote wanaomwamini watamstaajabu. Na hii inawajumuisha ninyi kwa sababu mliamini yale tuliyowaambia.
11 Hii ndiyo sababu daima tunawaombea. Tunamwomba Mungu wetu awasaidie kuishi katika njia njema aliyoitaka alipowachagua. Wema mlionao unawafanya mtake kufanya mema. Na imani mliyonayo inafanya mfanye kazi. Tunaomba kwamba kupitia nguvu zake Mungu atayakamilisha yote mema mliyokusudia kufanya pamoja na kazi zote zinazotokana na imani yenu. 12 Kisha jina la Bwana wetu Yesu litaheshimiwa kwa sababu yenu, nanyi mtaheshimiwa kwa sababu yake, na mtaheshimiwa kwa sababu yake. Hii inaweza kutokea tu kwa neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo.
Mambo Maovu Yatatokea
2 Kaka na dada, tuna jambo la kuwaambia juu ya kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunataka kuzungumza nanyi juu ya wakati huo tutakapokusanyika pamoja naye. 2 Msikubali kufadhaishwa na kutiwa kuhofu ikiwa mtasikia kwamba siku ya Bwana tayari imekwishawadia. Wengine wanaweza kusema kwamba wazo hili limetoka kwetu katika jambo alilotuambia Roho, au tulilosema, au katika barua tuliyoiandika. 3 Msidanganywe na chochote wanachoweza kusema kuhusu kuja kwa Bwana. Siku hiyo ya Bwana haitakuja mpaka itanguliwe na kukengeuka kwa wanadamu na kumwacha Mungu. Na siku hiyo haitakuja mpaka ajitokeze kwanza Mtu wa Uovu, yule ambaye ana uhakika kuwa ataangamizwa.[a] 4 Huyo atasimama kinyume na kujiweka mwenyewe juu ya kila kitu ambacho watu wanaabudu au kudhani kuwa kinafaa kuabudiwa. Ataenda na kuingia ndani ya Hekalu[b] na kukikalia kiti cha enzi, akidai kuwa yeye ni Mungu.
5 Niliwaambia zaidi ya mara moja nilipokuwa huko kwamba mambo yote haya yangetokea. Je, mnakumbuka? 6 Na mnafahamu kinachomzuia Mtu wa Uovu. Huyo hataruhusiwa kuonekana mpaka wakati sahihi utakapofika. 7 Tayari nguvu ya uovu inatenda kazi ulimwenguni sasa. Lakini yupo mmoja anayeizuia nguvu hiyo. Na ataendelea kuizuia mpaka atakapoondolewa. 8 Kisha huyo Mtu wa Uovu atatokea. Lakini Bwana Yesu atamuua kwa pumzi inayotoka katika kinywa chake. Bwana atakuja katika namna ambayo kila mtu atamwona, na huo utakuwa mwisho wa Mtu wa Uovu.
9 Kuja kwa Mtu wa Uovu itakuwa kazi ya Shetani. Atakuja na nguvu kuu, na atafanya aina zote za miujiza ya uongo, ishara, na maajabu. 10 Mtu wa Uovu atatumia kila aina ya uovu kuwatia ujinga wote walio njiani kuelekea kuangamia. Wamepotea kwa sababu walikataa kuupenda ujumbe wenye ukweli kuhusu Yesu na kuokolewa. 11 Hivyo Mungu atawaacha wadanganyike hata kuamini uongo.[c] 12 Wote watahukumiwa kwa sababu hawakuamini ujumbe wa kweli na kwa kuwa walifurahia kufanya maovu.
Mmechaguliwa kwa ajili ya Wokovu
13 Ndugu zangu, ninyi ni watu mnaopendwa na Bwana. Na imetupasa tumshukuru Mungu daima kwa sababu yenu. Hayo ndiyo tunayotakiwa kuyatenda, kwa sababu Mungu aliwaita kuwa miongoni mwa watu[d] wa kwanza kuokolewa. Mmeokolewa na Roho aliyewafanya muwe watu wa Mungu walio watakatifu kupitia kuiamini kweli. 14 Mungu aliwaita ninyi mpate wokovu. Aliwaita kwa kutumia Habari Njema tuliwahubiri. Mliitwa ili mshiriki katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. 15 Hivyo simameni imara na kuendelea kuamini mafundisho tuliyowapa tulipokuwa huko na kupitia barua yetu.
16-17 Tunaomba kwamba Bwana Yesu Kristo na Mungu Baba yetu awafariji na kuwaimairisha katika kila jambo jema mnalotenda na kusema. Mungu alitupenda na kutupa kupitia neema matumaini ya ajabu na faraja isiyo na mwisho.
Tuombee nasi
3 Na sasa, ndugu zangu, mtuombee. Ombeni kwamba mafundisho ya Bwana yaendelee kuenea haraka na kwamba watu watayaheshimu, kama ilivyotokea kwenu. 2 Mtuombee tupate ulinzi kutokana na watu wabaya na waovu. Mnafahamu, siyo wote wanamwamini Bwana.
3 Lakini Bwana ni mwaminifu. Atawapa nguvu na ulinzi dhidi ya Mwovu. 4 Tuna uhakika kwa sababu ya Bwana mnayemtumikia na mtaendelea kuyafanya yale tunayowaamuru. 5 Tunaomba kwamba Bwana atasababisha mjisikie upendo wa Mungu na kukumbuka subira ya ustahimilivu wa Kristo.
Wajibu wa Kufanya kazi
6 Kwa mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo tunawaambia kukaa mbali na mwamini yeyote anayekataa kufanya kazi. Watu kama hao wanaokataa kufanya kazi hawafuati mafundisho tuliyowapa. 7 Ninyi wenyewe mnafahamu kwamba mnatakiwa kuishi kwa kuiga mfano wetu. Hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi wala hatukuishi pasipo utaratibu unaofaa. 8 Hatukupokea chakula kutoka kwa yeyote bila ya kukilipia. Tulifanya kazi ili tusiwe mzigo kwa yeyote. Tulifanya kazi usiku na mchana. 9 Tulikuwa na haki ya kuomba mtusaidie. Lakini tulifanya kazi ili tuwe mfano wa kuigwa nanyi. 10 Tulipokuwa nanyi, tuliwapa kanuni hii: “Yeyote asiyefanya kazi asile.”
11 Tunasikia kwamba watu wengine katika kundi lenu wanakataa kufanya kazi. Hawashughuliki kufanya kazi badala yake wanashughulika kwa kuyafuatilia maisha ya wengine. 12 Maagizo yetu kwao ni kuwakataza kuwasumbua wengine, waanze kufanya kazi na kupata chakula chao wenyewe. Ni kwa mamlaka ya Bwana Yesu Kristo tuwaagize kufanya hivi. 13 Msichoke kabisa kutenda wema.
14 Wakiwapo wengine huko wanaokataa kufanya tunayowaambia katika barua hii, basi mkumbuke wao ni kina nani. Msichangamane nao. Ndipo pengine wanaweza kujisikia aibu. 15 Lakini msiwafanye kama adui. Washaurini waachane na tabia hiyo kama watu wa nyumbani mwake Mungu.
Maneno ya Mwisho
16 Tunaomba kwamba Bwana wa amani awape amani wakati wote na kwa njia yo yote. Bwana atakuwa pamoja nanyi nyote.
17 Hizi ni salamu zangu kwa mwandiko wangu: Paulo. Ninafanya hivi katika barua zangu zote kuonesha zinatoka kwangu. Hivi ndivyo ninavyoandika.
18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote.
© 2017 Bible League International