Beginning
1 Salamu kutoka kwa Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu.[a]
Kwenu ninyi nyote, watakatifu wa Mungu mlioko Filipi, mlio wa Kristo Yesu, wakiwemo wazee[b] na mashemasi wenu.
2 Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu, Bwana wetu, iwe pamoja nanyi.
Maombi ya Paulo
3 Ninamshukuru Mungu kila wakati ninapowakumbuka. 4 Kila wakati ninapowaombea ninyi nyote, daima ninawaombea kwa furaha. 5 Ninamshukuru Mungu kwa namna mlivyonisaidia nilipokuwa ninawahubiri watu Habari Njema. Mlinisaidia tangu siku ya kwanza mlipoamini mpaka sasa. 6 Nina uhakika kwamba Mungu, aliyeianzisha kazi njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka itakapomalizika siku ile ambayo Kristo Yesu atakuja tena.
7 Ninajua niko sahihi kwa namna ile ninayowawazia ninyi nyote kwa sababu mko karibu sana na moyo wangu. Mmechangia sehemu muhimu sana katika neema ya Mungu kwa ajili yangu wakati huu nikiwa gerezani, na wakati wowote ninapoutetea na kuuthibitisha ukweli wa Habari njema. 8 Mungu anajua kwamba ninataka sana kuwaona. Ninawapenda nyote kwa upendo wa Kristo Yesu.
9 Hili ndiyo ombi langu kwa ajili yenu:
Ya kwamba mkue zaidi na zaidi katika hekima na ufahamu kamili pamoja na upendo; 10 ya kwamba mjue tofauti kati ya kitu kilicho muhimu na kisicho muhimu ili muwe safi msio na lawama, mkiwa tayari kwa siku atakayokuja Kristo; 11 Maisha yenu yajaye matendo mengi mema yanayozalishwa na Kristo Yesu ili kumletea Mungu utukufu na sifa.
Matatizo Ya Paulo Yesaidia Kazi ya Bwana
12 Ndugu zangu, ninataka mjue kwamba yote yaliyonipata yamesaidia katika kusambaza Habari Njema, ingawa ninyi mnaweza kuwa mlitarajia kinyume chake. 13 Walinzi wote wa Kirumi na wengine wote hapa wanafahamu kuwa nimefungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo. 14 Kufungwa kwangu gerezani kumesababisha waamini walio wengi hapa kuweka tumaini lao kwa Bwana, na kuhubiri ujumbe wa Mungu kwa ujasiri mwingi pasipo woga.
15 Baadhi ya watu wanahubiri ujumbe wa Kristo kwa sababu wananionea wivu na wanataka watu wawafuate wao badala yangu. Wengine wanahubiri kwa sababu wanataka kusaidia. 16 Wanahubiri kwa sababu ya upendo. Wanafahamu kuwa Mungu ameniweka humu gerezani ili kuitetea Habari Njema. 17 Lakini wengine wanahubiri kuhusu Kristo kwa sababu wanataka kujikweza wenyewe. Chachu yao si safi. Wanafanya hivi kwa kudhani kuwa itanisababishia uchungu mwingi niwapo gerezani. 18 Lakini hiyo haijalishi. Kitu cha muhimu ni kuwa wanawahubiri watu kuhusu Kristo, wakiwa na chachu safi au isiyo safi. Ninafurahi wanafanya hivyo.
Nitaendelea kufurahi, 19 kwa sababu ninajua kwamba kupitia maombi yenu na kipawa cha Roho wa Yesu Kristo mazingira haya magumu hatimaye yataniletea uhuru wangu. 20 Nimejaa tumaini na uhakika, sina sababu yeyote ya kuona haya. Nina uhakika nitaendelea kuwa na ujasiri wa kuhubiri kwa uhuru kama ambavyo nimekuwa. Na Kristo atatukuzwa kwa ninayoyafanya katika mwili wangu, ikiwa nitaishi au nitakufa. 21 Sababu yangu pekee ya kuishi ni kumtumikia Kristo. Kifo kingekuwa bora zaidi. 22 Nikiendelea kuishi hapa ulimwenguni, nitaweza kumfanyia kazi Bwana. Lakini kati ya kufa na kuishi, sijui ningechagua kipi. 23 Ungekuwa uchaguzi mgumu. Ninataka kuyaacha maisha haya ili niwe na Kristo. Hiyo ingekuwa bora zaidi kwangu; 24 hata hivyo, mnanihitaji hapa nikiwa hai. 25 Nina uhakika juu ya hili, hivyo ninajua nitakaa hapa ili niwe nanyi na niwasaidie kukua na kuwa na furaha katika imani yenu. 26 Mtafurahi sana nitakapokuwa hapo pamoja nanyi tena kutokana na kile ambacho Kristo Yesu amefanya ili kunisaidia.
27 Zaidi ya yote, hakikisheni kuwa mnaishi pamoja kama jamii ya watu wa Mungu katika namna inayoiletea heshima Habari Njema kuhusu Kristo. Kisha, ikiwa nitakuja kuwatembelea au ikiwa nitakuwa mbali nanyi na kuyasikia tu mambo kuhusu ninyi, nitajua ya kuwa mmesimama pamoja katika roho moja na kwamba mnafanya kazi pamoja kwa moyo mmoja kama timu moja, katika kuwasaidia wengine kuiamini Habari Njema. 28 Na hamtawaogopa wale walio kinyume nanyi. Imani yenu thabiti itakuwa kama ishara kwao ya kuangamia kwenu. Lakini kwa hakika ni ishara ya wokovu wenu. Na hiki ni kipawa kutoka kwa Mungu. 29 Mungu amewabariki ninyi kwa heshima si ya kumwamini Kristo tu, lakini pia ya kupata mateso kwa ajili yake. 30 Mliyaona magumu mengi niliyokabiliana nayo, na mnasikia kwamba bado nakabiliwa na masumbufu mengi. Ninyi nanyi imewapasa kuyakabili masumbufu hayo pia.
Iweni katika Umoja na Msaidiane
2 Fikirini kuhusu kile ambacho tulichonacho kwa sababu tunamilikiwa na Kristo: hamasa aliyotuletea, faraja ya upendo wake, ushirika katika Roho wake, huruma na wema aliotuonyesha. Ikiwa mnazifurahia baraka hizi, 2 basi fanyeni yale yatakayoikamilisha furaha yangu: iweni na nia moja na mpendane ninyi kwa ninyi. Iweni na umoja katika malengo yenu na katika kufikiri kwenu. 3 Msiruhusu ubinafsi au kiburi viwe dira yenu. Badala yake muwe wanyenyekevu mkiwathamini wengine kuliko ninyi wenyewe. 4 Kila mmoja wenu asijishugulishe kwa mema yake yeye mwenyewe bali kwa mema ya wengine.
5 Hivi ndivyo mnapaswa kufikiri, kuhisi na kutenda katika maisha yenu kwa pamoja, kama vile Kristo Yesu alivyofikiri:
6 Alikuwa sawa na Mungu katika namna zote,
lakini hakufikiri kwamba kuwa sawa na Mungu
kilikuwa kitu cha manufaa kwake.
7 Badala yake, aliacha kila kitu,
hata sehemu yake pamoja na Mungu.
Akakubali kuwa kama mtumwa,
akiwa katika umbo la binadamu.
Wakati wa maisha yake kama mtu,
8 Alijinyenyekeza na akawa mtiifu kabisa kwa Mungu,
hata jambo hilo liliposababisha kifo chake msalabani.
9 Hivyo ndiyo sababu Mungu alimpa mahali pa heshima sana,
na akampa jina lililo kuu kuliko majina yote.
10 Hivyo kila mtu atasujudu kumheshimu Yesu.
Kila mmoja aliye mbinguni, duniani na wale walio chini ya dunia.
11 Wote watakiri kwamba, “Yesu Kristo ni Bwana,”
na hili litamtukuza Mungu Baba.
Iweni Kama Mungu Anavyotaka
12 Rafiki zangu wapendwa, daima mnatii yale mliyofundishwa. Kama mlivyotii nilipokuwa pamoja nanyi, ni muhimu zaidi na zaidi kwamba mtii wakati huu ambapo sipo pamoja nanyi. Hivyo ni lazima mwendelee kuishi katika namna inayoleta maana kwa wokovu wenu. Fanyeni hivi kwa wingi wa heshima na utii kwa Mungu. 13 Ndiyo, Mungu ndiye anayetenda kazi ndani na miongoni mwenu. Anawasaidia ninyi kutaka kutenda yanayomfurahisha, naye anawapa nguvu ya kuyatenda.
14 Fanyeni mambo yote pasipo kulalamika wala kubishana. 15 Nanyi mtakuwa watoto wa Mungu wasiolaumiwa na wasio na hatia. Ijapokuwa mnaishi mkiwa mmezungukwa na watu wasio waaminifu wasiojali thamani haki. Katikati ya watu hao mnang'ara kama mianga katika ulimwengu wenye giza, 16 nanyi mnawapa mafundisho yanayotoa uhai. Hivyo nitaona fahari juu yenu wakati Kristo atakapokuja tena. Ninyi ndiyo mtakaothibitisha kuwa kazi niliyoifanya haikukosa matokeo, ya kwamba nilishindana mbio na nikashinda.
17 Imani yenu inayatoa maisha yenu kama sadaka katika kumtumikia Mungu. Hata kama ni kweli kwamba sasa ninajimimina mimi mwenyewe kama sadaka ya kinywaji pamoja na sadaka yenu, ninayo furaha, na nitawashirikisha ninyi nyote furaha yangu. 18 Ninyi pia mnapaswa kufurahi na kunishirikisha furaha yenu.
Habari Kuhusu Timotheo na Epafrodito
19 Kwa baraka za Bwana Yesu, ninategemea kuwa nitamtuma Timotheo kwenu hivi karibuni. Naye atarejesha kwangu taarifa kuhusu ninyi ili nifurahi. 20 Sina mtu mwingine yeyote kama Timotheo, ambaye kwa dhati kabisa anayajali mambo yanayowahusu. 21 Wengine wote wanajishughulisha na maisha yao wenyewe. Hawajali kazi ya Yesu Kristo. 22 Mnafahamu Timotheo amejithibitisha kuwa ni mtu wa aina gani. Ametumika pamoja nami katika kuhubiri Habari Njema kwa njia ambavyo mwana angemtumikia baba yake. 23 Ninategemea kumtuma aje kwenu haraka baada ya kujua yatakayonipata. 24 Bwana hunifanya niwe jasiri ili niweze pia kuja kwenu haraka.
25 Kwa sasa, nadhani ni lazima nimrudishe Epafrodito kwenu. Ni mtumishi na mtenda kazi pamoja nami na askari mwenzangu katika jeshi la Bwana. Nilipotaka msaada, mlimtuma kwangu. Kama mjumbe wenu, alinihudumia mahitaji yangu. 26 Lakini sasa anataka kuwaona ninyi nyote tena. Ana wasiwasi sana kwa sababu mlisikia kuwa alikuwa mgonjwa. 27 Alikuwa mgonjwa karibu ya kufa. Lakini Mungu alimsaidia yeye na mimi ili nisiwe na huzuni zaidi. 28 Hivyo ninataka sana kumtuma kwenu. Ili mtakapomwona, mfurahi. Nami nitaacha kuwa na wasiwasi juu yenu. 29 Mkaribisheni kwa furaha nyingi katika Bwana. Waheshimuni watu kama Epafrodito. 30 Anapaswa kuheshimiwa kwa sababu alikaribia kufa akifanya kazi kwa ajili ya Kristo. Aliyaweka maisha yake katika hatari ili aweze kunisaidia. Ni msaada ambao msingeweza kunisaidia.
Yesu Kristo ni wa Muhimu Zaidi
3 Kwa hiyo sasa, kaka na dada zangu, furahini kwa kuwa ninyi ni wa Bwana. Sisiti kuwaandikia mambo haya haya, kwa sababu yatawasaidia ninyi kuwa imara na salama.
2 Mjihadhari na mbwa, mjihadhari na wafanyakazi waovu, mjihadhari na watu wanaotaka kumkata kila mtu ambaye hajatahiriwa.[c] 3 Lakini sisi ndiyo wenye tohara[d] ya kweli, tunaomwabudu Mungu kupitia Roho wake. Hatutumaini katika namna tulivyo kwa kuzaliwa au kwa yale tuliyoyakamilisha. Tunajivuna kuwa sisi ni milki ya Kristo Yesu. 4 Hata kama ninaweza kujitumainisha mimi mwenyewe, bado sifanyi hivyo. Ikiwa kuna watu wanadhani wana sababu za kutumaini sifa za kibinadamu, wanapaswa kujua kuwa nina sababu zaidi za kufanya hivyo. 5 Nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa. Mimi ni Myahudi wa kabila la Benjamini. Mimi ni Mwebrania halisi, hata wazazi wangu pia. Nikawa Farisayo na nilitii torati kwa uangalifu sana. 6 Nilikuwa na hamu sana ya kumridhisha Mungu[e] hata nikalitesa kanisa. Kwa usahihi niliitii sheria ya Musa.
7 Wakati fulani mambo haya yote yalikuwa muhimu kwangu. Lakini kwa sababu ya Kristo, sasa ninayachukulia mambo haya yote kuwa yasiyo na thamani. 8 Na si haya tu, lakini sasa ninaelewa kuwa kila kitu ni hasara tu ukilinganisha na thamani kuu zaidi ya kumjua Kristo Yesu, ambaye sasa ni Bwana wangu. Kwa ajili yake nilipoteza kila kitu. Na ninayachukulia yote kama kinyesi, ili nimpate Kristo. 9 Ninataka niwe wake. Katika Kristo ninayo haki mbele za Mungu, lakini kuwa na haki mbele za Mungu hakuji kwa kuitii sheria, Bali inakuja toka kwa Mungu kupitia imani kwa[f] Kristo. Mungu anatumia imani yangu kwa Kristo kunihesabia haki. 10 Ninachotaka ni kumjua Kristo na nguvu iliyomfufua kutoka kwa wafu. Ninataka kushiriki katika mateso yake na kuwa kama yeye hata katika kifo chake. 11 Kisha mimi mwenyewe naweza kuwa na matumaini kwamba nitafufuliwa kutoka kwa wafu.
Kuyafikia Malengo
12 Sisemi kuwa nimekwisha kupata ujuzi huo au kuifikia shabaha ya mwisho. Lakini bado ninajitahidi kuifikia shabaha kwa kuwa ndivyo ambavyo Kristo Yesu anataka nifanye. Ndiyo sababu alinifanya kuwa wake. 13 Kaka na dada zangu, ninajua ya kuwa bado nina safari ndefu. Lakini kuna kitu kimoja ninachofanya, nacho ni kusahau yaliyopita na kujitahidi kwa kadri ninavyoweza kuyafikia malengo yaliyo mbele yangu. 14 Ninaendelea kupiga mbio kuelekea mwisho wa mashindano ili niweze kushinda tuzo ambayo Mungu ameniitia kutoka mbinguni kwa njia ya Kristo Yesu.
15 Sisi sote tuliokua kiroho tunapaswa kufikiri namna hii. Na ikiwa kuna jambo lolote ambalo hamkubaliani nalo, Mungu atalifunua kwenu. 16 Lakini tunapaswa kuendelea kuifuata kweli tuliyonayo tayari.
17 Kaka na dada zangu, unganeni pamoja na mfuate mfano wangu. Mtazame na mjifunze pia kutoka kwa wale wanaoishi katika namna tuliyoionesha kwenu. 18 Wapo wengi ambao mwenendo wao unaonesha kuwa ni adui za msalaba wa Kristo. Nimekwishawaambia kuhusu hao mara nyingi. Na inanifanya nitokwe machozi ninapowaambia kuhusu watu hao sasa. 19 Wanauendea uharibifu kwa namna wanavyoishi. Wanaabudu tamaa za mili yao kana kwamba hizo ndizo Mungu. Wanatenda mambo ya aibu na wanajivuna kwa kutenda mambo hayo. Wanayawazia mambo ya kidunia tu. 20 Lakini sisi tunatawaliwa na serikali iliyoko mbinguni. Tunamsubiri Mwokozi wetu, Bwana wetu Yesu Kristo atakayekuja kutoka mbinguni. 21 Ataibadilisha miili yetu minyenyekevu na kuifanya iwe kama mwili wake yeye mwenyewe, mwili wenye utukufu. Kristo atafanya hivi kwa nguvu yake inayomwezesha kutawala juu ya vyote.
Maagizo ya Mwisho
4 Kaka na dada zangu wapenzi, ninawapenda na ninataka kuwaona. Mnanifurahisha na ninajivuna kwa sababu yenu. Endeleeni kuwa imara kumfuata Bwana kama nilivyowaambia.
2 Ninawasihi Euodia na Sintike, ninyi nyote wawili ni wa Bwana, hivyo muwe na mtazamo mmoja. 3 Kwa ajili ya hili ninamwomba rafiki yangu aliyetumika pamoja nami kwa uaminifu: Wasaidieni wanawake hawa. Waliwahubiri watu Habari Njema kwa bidii kama watendaji wenzangu tukiwa pamoja na Klementi na wengine waliofanya kazi pamoja nami. Majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.[g]
4 Furahini katika Bwana daima. Ninasema tena, furahini.
5 Kila mtu auone wema na uvumilivu wenu. Bwana yu karibu kuja. 6 Msisumbuke kitu chochote, lakini salini na kumwomba Mungu kwa mahitaji yenu. Mshukuruni Mungu wakati mnapomwomba yale mnayohitaji. 7 Na kwa kuwa ninyi ni milki ya Kristo Yesu, amani ya Mungu itailinda mioyo na mawazo yenu isipate wasiwasi. Amani yake inaweza kutenda haya zaidi ya akili za kibinadamu.[h]
8 Na sasa, mwisho kabisa, kaka na dada zangu, fikirini kuhusu yale yaliyo ya kweli, ya kuheshimiwa, ya haki, yaliyo safi, yenye kupendeza, na yanayosemwa vema. 9 Yatendeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu, niliyowaambia na yale mliyoyaona nikitenda. Na Mungu atoaye amani atakuwa pamoja nanyi.
Paulo Apokea Zawadi Kwa Furaha
10 Nimefurahi sana katika Bwana kwa sababu mmeonesha tena kuwa mnanijali. Mmeendelea kujali juu yangu, lakini haikuwepo njia ya kuonesha hili. 11 Ninawaambia hili, si kwa sababu ninahitaji msaada kutoka kwa yeyote. Nimejifunza kuridhika na kile nilichonacho na chochote kinachotokea. 12 Ninajua namna ya kuishi ninapokuwa na vichache na ninapokuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuishi katika hali zote, ninapokuwa na vyakula vingi au ninapokuwa na njaa, ninapokuwa na vingi zaidi ya ninavyohitaji au ninapokuwa sina kitu. 13 Kristo ndiye anayenitia nguvu kuyakabili mazingira yote katika maisha.
14 Lakini mlifanya vyema mliposhiriki nami katika kipindi changu kigumu. 15 Enyi watu wa Filipi kumbukeni nilipokuja mara ya kwanza kuwahubiri Habari Njema watu wa Makedonia. Nilipoondoka huko, ninyi ndiyo kanisa pekee ambalo lilishirikiana nami katika uhusiano ulioendelea wa kutoa na kupokea. 16 Ukweli ni kuwa hata nilipokuwa Thesalonike, zaidi ya mara moja mlinitumia kila kitu nilichohitaji. 17 Si kwamba natafuta msaada wa kifedha kutoka kwenu. Bali ninataka ninyi mpokee manufaa yanayozidi kukua yanayotokana na kutoa. 18 Nina kila kitu ninachohitaji. Nina zaidi ya hata ninavyohitaji kwa sababu Epafrodito ameniletea kila kitu mlichompa aniletee. Zawadi zenu ni kama sadaka yenye harufu nzuri inayotolewa kwa Mungu. Ni sadaka anayoikubali, na inampendeza. 19 Mungu wangu atatumia utajiri wake wenye utukufu kuwapa ninyi kila kitu mnachohitaji kupitia Kristo Yesu. 20 Utukufu kwa Mungu na Baba yetu milele na milele. Amina.
21 Wasalimuni watakatifu wote wa Mungu walio wake Kristo Yesu. Wale walio katika familia ya Mungu walio pamoja nami wanawasalimu. 22 Na watu wote wa Mungu walio hapa wanawasalimu, hasa wale walio katika utumishi wa Kaisari.
23 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na utu wenu wa ndani.
© 2017 Bible League International