Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Waefeso 4-6

Umoja wa Mwili wa Kristo

Hivyo, mimi niliye mfungwa kwa ajili ya Bwana nawasihi mwishi kwa jinsi inavyowapasa watu wa Mungu, kwa sababu aliwachagua muwe wake. Iweni wanyenyekevu na wapole siku zote. Mvumiliane na kuchukuliana ninyi kwa ninyi katika upendo. Mmeunganishwa pamoja kwa amani na Roho. Jitahidini mwezavyo kudumu kuutunza umoja huo, mkiunganishwa pamoja kwa amani. Kuna mwili mmoja na Roho moja, na Mungu aliwachagua ili muwe na tumaini moja. Kuna Bwana mmoja, imani moja, na ubatizo mmoja. Mungu ni mmoja na ni Baba wetu sote, anayetawala juu ya kila mtu. Hutenda kazi kupitia kwetu sote na ndani yetu sote.

Kristo alimpa kila mmoja wetu karama. Kila mmoja alipokea kwa jinsi alivyopenda yeye kuwapa. Ndiyo maana Maandiko yanasema,

“Alipaa kwenda mahali pa juu sana;
    aliwachukua wafungwa pamoja naye,
    na akawapa watu vipawa.”(A)

Inaposema, “Alipaa juu,” inamaanisha nini? Inamaanisha kuwa kwanza alikuja chini duniani. 10 Hivyo Kristo alishuka chini, na ndiye aliyekwenda juu. Alikwenda juu ya mbingu za juu zaidi ili avijaze vitu vyote pamoja naye. 11 Na Kristo huyo huyo aliwapa watu hawa vipawa: aliwafanya wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kwenda na kuhubiri Habari Njema, na wengine kuwa wachungaji[a] ili wawafundishe watu wa Mungu. 12 Mungu aliwapa hao ili kuwaandaa watakatifu wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma, kuufanya imara mwili wa Kristo. 13 Kazi hii inabidi iendelee hadi wote tutakapounganishwa pamoja katika lile tunaloliamini na tunalolijua kuhusu Mwana wa Mungu. Lengo letu ni kufanana na mtu mzima aliyekomaa na kuwa kama Kristo tukiufikia ukamilifu wake wote.

14 Ndipo tutakapokuwa si kama watoto wachanga. Hatutakuwa watu ambao nyakati zote hubadilika kama meli inayochukuliwa na mawimbi huku na kule. Hatutaweza kuathiriwa na fundisho lolote jipya tutakalosikia kutoka kwa watu wanaojaribu kutudanganya. Hao ni wale wanaoweka mipango ya ujanja na kutumia kila aina ya mbinu kuwadanganya wengine waifuate njia iliyopotoka. 15 Hapana, tunapaswa kusema ukweli kwa upendo. Tutakua na kuwa kama Kristo katika kila njia. Yeye ni kichwa, 16 na mwili wote unamtegemea yeye. Viungo vyote vya mwili vimeunganishwa na kushikanishwa pamoja, huku kila kiungo kikitenda kazi yake. Hili huufanya mwili wote ukue na kujengeka katika upendo.

Mnavyopaswa Kuishi

17 Nina kitu cha kuwaambia kutoka kwa Bwana. Ninawaonya: Msiendelee kuishi kama wale wasiomwamini Mungu wetu. Mawazo yao hayafai kitu. 18 Hawana ufahamu, na hawajui lolote kwa sababu wamekataa kusikiliza. Hivyo hawawezi kupata maisha mapya Mungu anayowapa watu. 19 Wamepoteza hisia zao za aibu na wanayatumia maisha yao kutenda yale yaliyo mabaya kimaadili. Zaidi ya hapo wanataka kutenda kila aina ya uovu. 20 Lakini aina hiyo ya maisha haiko kama ile mliyojifunza mlipomjua Kristo. 21 Najua kwamba mlisikia juu yake, na ndani yake mlifundishwa ukweli. Ndiyo, ukweli umo ndani ya Yesu. 22 Mlifundishwa kuacha utu wenu wa kale. Hii inamaanisha kwamba mnapaswa kuacha kuishi katika njia za uovu mlivyoishi zamani. Utu wenu wa kale huharibika zaidi na zaidi, kwa sababu watu hudanganywa na uovu wanaotaka kuutenda. 23 Mnapaswa kufanywa upya katika mioyo yenu na katika fikra zenu. 24 Kila mmoja wenu auvae utu ule mpya ulioumbwa kwa kufananishwa na Mungu, ambao kwa hakika una wema na ni wenye kumpendeza Mungu.

25 Hivyo mnapaswa kuacha kusema uongo, “Nyakati zote mseme ukweli tu,”(B) kwa sababu wote sisi tunahusiana na ni wa mwili mmoja. 26 “Unapokasirika, usiruhusu hasira hiyo ikusababishe wewe kutenda dhambi,”(C) na usiendelee na hasira kwa siku nzima. 27 Usimwachie Ibilisi nafasi ya kukushinda. 28 Yeyote ambaye amekuwa akiiba anapaswa kuacha kuiba na afanye kazi. Unapaswa kutumia mikono yako kufanya kitu chenye kufaa. Hapo utakuwa na kitu cha kuwashirikisha walio maskini.

29 Unapozungumza, usiseme chochote kilicho kibaya. Bali useme mambo mazuri ambayo watu wanayahitaji ili waimarike. Ndipo kile unachosema kitakuwa ni baraka kwa wale wanaokusikia. 30 Tena usimhuzunishe Roho Mtakatifu. Mungu alikupa Roho Mtakatifu kama uthibitisho kwamba wewe ni wake na kwamba atakulinda hadi siku atakapokufanya uwe huru kabisa. 31 Usiwe na uchungu, wala kukasirika. Kamwe usiongee kwa hasira au kusema chochote ili uwaumize wengine. Usifanye chochote kilicho kiovu. 32 Mwe mwema na mpendane ninyi kwa ninyi. Msameheane ninyi kwa ninyi kama Mungu alivyowasamehe ninyi kwa njia ya Kristo.

Ninyi ni watoto wa Mungu wapendwao, hivyo jitahidini kuwa kama yeye. Ishini maisha ya upendo. Wapendeni wengine kama Kristo alivyotupenda sisi. Alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu na kuwa sadaka ya harufu ya manukato mazuri na dhabihu kwa Mungu.

Lakini hakupaswi kuwepo dhambi ya zinaa kati yenu. Hakupaswi kuwepo aina yoyote ya uasherati au matamanio ya zinaa, kwa sababu mambo kama hayo hayastahili kwa watakatifu wa Mungu. Vivyo hivyo, pasiwepo na mazungumzo maovu miongoni mwenu. Msizungumze mambo ya kipuuzi au ya uchafu. Hayo siyo kwa ajili yenu. Bali mnatakiwa kutoa shukrani kwa Mungu. Mnaweza kuwa na uhakika wa hili: Hakuna atakayepata sehemu katika ufalme wa Kristo na wa Mungu kama mtu huyo atakuwa anafanya dhambi ya uzinzi, au akitenda mambo maovu, au kama atakuwa mtu wa kutamani vitu zaidi na zaidi. Mtu mwenye choyo kama huyo atakuwa anamtumikia mungu wa uongo.

Msimruhusu mtu yeyote awadanganye kwa maneno yasiyo ya kweli. Mungu huwakasirikia sana watu wasipomtii kama hivyo. Hivyo msiwe na jambo lolote pamoja nao. Hapo zamani mlijaa giza, lakini sasa mmejaa nuru katika Bwana. Hivyo ishini kama watoto wa nuru. Nuru hii huleta kila aina ya wema, maisha ya haki, na kweli. 10 Jaribuni kutafuta yale yanayompendeza Bwana. 11 Msishiriki katika mambo yanayotendwa na watu wa giza, yasiyosababisha jambo lolote zuri. Badala yake, mwambieni kila mtu jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. 12 Hakika, ni aibu hata kuyazungumzia mambo haya wanayoyatenda sirini. 13 Lakini nuru inaonesha wazi jinsi mambo hayo yasivyokuwa sahihi. 14 Ndiyo, kila kitu kinawekwa wazi na nuru. Ndiyo maana tunasema,

“Amka, wewe unayelala!
    Fufuka kutoka kwa wafu,
    na Kristo atakuangazia nuru yake.”

15 Hivyo, muwe makini sana jinsi mnavyoishi. Ishini kwa busara, si kama wajinga. 16 Nasema kwamba jitahidini kutumia kila fursa mliyo nayo katika kutenda mema, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17 Hivyo msiwe kama wajinga katika maisha yenu, bali mfahamu yale ambayo Bwana anapenda ninyi mfanye. 18 Msilewe kwa mvinyo, ambao utaharibu maisha yenu, bali mjazwe Roho. 19 Mhimizane ninyi kwa ninyi katika zaburi, nyimbo za sifa, na nyimbo zinazoongozwa na Roho. Imbeni na msifuni Bwana katika mioyo yenu. 20 Siku zote mshukuruni Mungu Baba kwa mambo yote katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Ushauiri Kwa Mke na Mume

21 Mwe radhi kuhudumiana ninyi kwa ninyi kwa kuwa mnamheshimu Kristo.

22 Wake, muwe radhi kuwahudumia waume zenu kama mlivyo radhi kumtumikia Bwana. 23 Mume ni kichwa cha mke wake, kama Kristo alivyo kichwa cha kanisa. Kristo ni Mwokozi wa kanisa, ambalo ni mwili wake. 24 Kanisa hutumika chini ya Kristo, hivyo ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi wake. Mnapaswa kuwa radhi kuwahudumia waume zenu katika kila jambo.

25 Waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa na kuyatoa maisha yake kwa ajili yake. 26 Alikufa ili alitakase kanisa lake. Alitumia ujumbe wa Habari Njema kulisafisha kanisa kwa kuliosha katika maji. 27 Kristo alikufa ili aweze kujiletea mwenyewe kanisa lililo kama bibi harusi katika uzuri wake wote. Alikufa ili kanisa liweze kuwa takatifu na lisilo na dosari, lisilokuwa na uovu au dhambi au chochote kilicho kibaya ndani yake.

28 Na waume wawapende hivyo wake zao. Wawapende wake zao kama vile ni miili yao wenyewe. Mtu anayempenda mkewe anajipenda mwenyewe, 29 kwa sababu kamwe hakuna anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza. Na hivyo ndivyo Kristo anavyolifanyia kanisa 30 kwa sababu sisi sote ni viungo vya mwili wake. 31 Maandiko yanasema, “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake na kuungana na mkewe, nao hao wawili watafanyika mwili mmoja.”(D) 32 Siri hiyo ya kweli ni ya muhimu sana, ninazungumza juu ya Kristo na kanisa. 33 Lakini kila mmoja wenu anapaswa kumpenda mkewe kama anavyojipenda mwenyewe. Na mke anapaswa kumheshimu mume wake.

Watoto na Wazazi Wao

Watoto, watiini wazazi wenu katika namna ambayo Bwana anataka, kwa sababu hili ni jambo sahihi kutenda. Amri husema, “Waheshimu baba yako na mama yako.”(E) Hii ndiyo amri ya kwanza iliyo na ahadi pamoja nayo. Na hii ndiyo ahadi: “Ndipo utakapofanikiwa, na utakuwa na maisha marefu duniani.”(F)

Wababa, msiwakasirishe watoto wenu, lakini waleeni kwa mafunzo na mausia mliyopokea kutoka kwa Bwana.

Watumwa na Bwana

Watumwa, watiini bwana zenu hapa duniani kwa hofu na heshima. Na fanyeni hivi kwa moyo ulio wa kweli, kama mnavyomtii Kristo. Mfanye hivi siyo tu kwa kuwafurahisha bwana zenu wakati wanapowaona, bali wakati wote. Kwa vile ninyi hakika ni watumwa wa Kristo, mfanye kwa mioyo yenu yale Mungu anayotaka. Fanyeni kazi zenu, na mfurahie kuzifanya. Fanyeni kana kwamba mnamtumikia Bwana, siyo tu bwana wa duniani. Kumbukeni kwamba Bwana atampa kila mmoja zawadi kwa kufanya vema. Kila mmoja, mtumwa au aliye huru, atapata zawadi kwa mambo mema aliyotenda.

Mabwana, kwa jinsi hiyo hiyo, muwe wema kwa watumwa wenu. Msiseme mambo ya kuwatisha. Mnajua kuwa yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, na humchukulia kila mmoja sawa.

Vaeni Silaha Zote za Mungu

10 Hapa lipo neno moja la mwisho la ushauri: Mtegemeeni Bwana kwa ajili ya nguvu zenu. Wekeni matumaini yenu katika nguvu zake kuu. 11 Vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kupigana dhidi ya hila za Shetani. 12 Mapigano yetu si juu ya watu duniani. Tunapigana dhidi ya watawala, mamlaka na nguvu za giza za ulimwengu huu. Tunapigana dhidi ya nguvu za uovu katika ulimwengu wa roho. 13 Ndiyo sababu mnahitaji silaha zote za Mungu. Ili siku ya uovu, mweze kusimama imara. Na mtakapomaliza mapigano yote, mtaendelea kusimama.

14 Hivyo simameni imara mkiwa mmefungwa mkanda wa kweli viunoni mwenu, na katika vifua vyenu mkiwa mmevaa kinga ya maisha ya haki. 15 Miguuni mwenu vaeni Habari Njema za amani ili ziwasaidie msimame imara. 16 Pia itumieni ngao ya imani ambayo itatumika kuizuia mishale inayowaka moto inayotoka kwa yule Mwovu. 17 Upokeeni wokovu wa Mungu kama chapeo yenu. Na chukueni upanga wa Roho, yaani mafundisho ya Mungu. 18 Ombeni katika Roho kila wakati. Ombeni maombi ya aina zote, na ombeni kila mnachohitaji. Ili mfanye hivi ni lazima muwe tayari. Msikate tamaa. Waombeeni watu wa Mungu daima.

19 Pia ombeni kwa ajili yangu ili ninapoongea, Mungu anipe maneno ili niweze kusema siri ya kweli juu ya Habari Njema bila woga. 20 Ninayo kazi ya kuhubiri Habari Njema, na hicho ndicho ninachofanya sasa humu gerezani. Niombeeni ili ninapowahubiri watu Habari Njema, nihubiri kwa ujasiri kama inavyonipasa kuhubiri.

Salamu za Mwisho

21 Namtuma kwenu Tikiko, ndugu yetu mpendwa na msaidizi mwaminifu katika kazi ya Bwana. Atawaeleza kila kitu kinachonipata. Kisha mtaelewa jinsi nilivyo na ninachofanya. 22 Ndiyo sababu namtuma yeye ili awajulishe hali zetu na tuwatie moyo.

23 Namwomba Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo awape amani, upendo na imani ndugu zangu wote mlio huko. 24 Naomba neema ya Mungu iwe pamoja nanyi nyote mnaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa pendo lisilo na mwisho.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International