Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Waefeso 1

Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu Mungu mwenyewe alitaka.

Kwa watakatifu wa Mungu walioko katika mji wa Efeso,[b] waamini walio wa Kristo Yesu.

Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.

Baraka za Rohoni katika Kristo

Sifa kwake Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Kristo, Mungu ametupa baraka zote za rohoni zilizoko mbinguni. Kwa kuwa anatupenda alituchagua katika Kristo kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu ili tuwe watakatifu wake, tusio na hatia tunaoweza kusimama mbele zake. Aliamua tangu mwanzo kutufanya kuwa watoto wake kupitia Yesu Kristo. Hivi ndivyo Mungu alivyotaka na ilimpendeza yeye kufanya hivyo. Sifa kwake Mungu kwa sababu ya neema yake ya ajabu aliyotupa bure kupitia Kristo anayempenda.

Tumewekwa huru katika Kristo kupitia sadaka ya damu yake. Tumesamehewa dhambi kwa sababu ya wingi na ukuu wa neema ya Mungu. Mungu alitupa bure neema hiyo yote, pamoja na hekima na uelewa wote, na ametuwezesha kuujua mpango wake wa siri. Hivi ndivyo Mungu alitaka, na alipanga kuutekeleza kupitia Kristo. 10 Lengo la Mungu lilikuwa kuukamilisha mpango wake muda sahihi utakapofika. Alipanga kuwa vitu vyote vilivyoko mbinguni na duniani viunganishwe pamoja na Kristo kama kichwa.

11 Tulichaguliwa katika Kristo ili tuwe milki ya Mungu. Mungu alikwisha panga ili tuwe watu wake, kwa sababu ndivyo alivyotaka. Na ndiye ambaye hufanya kila kitu kifanyike kulingana na utashi na maamuzi yake. 12 Sisi Wayahudi ndiyo tuliokuwa wa kwanza kutumaini katika Kristo. Na tulichaguliwa ili tuweze kumletea sifa Mungu katika utukufu wake wote. 13 Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Mliusikia ujumbe wa kweli, yaani Habari Njema kuhusu namna ambavyo Mungu anavyowaokoa. Mlipoisikia Habari Njema hiyo, mkamwamini Kristo. Na katika Kristo, Mungu aliwatia alama maalum kwa kuwapa Roho Mtakatifu aliyeahidi. 14 Roho ni malipo ya kwanza yanayothibitisha kuwa Mungu atawapa watu wake kila kitu alichonacho kwa ajili yao. Sisi sote tutaufurahia uhuru kamili uliowekwa tayari kwa ajili ya walio wake. Na hili litamletea Mungu sifa katika utukufu wake wote.

Sala ya Paulo

15-16 Ndiyo sababu daima ninawakumbuka katika maombi yangu na ninamshukuru Mungu kwa ajili yenu. Nimekuwa nikifanya hivi tangu niliposikia kuhusu imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watu wote wa Mungu. 17 Daima ninamwomba Baba aliye mkuu na mwenye utukufu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ninaomba awape Roho anakayewawezesha kuijua kweli kuhusu Mungu na awasaidie kuzielewa kweli hizo ili mweze kumjua vyema.

18 Ninaomba Mungu afungue mioyo yenu ili mwone kweli yake. Kisha mtalijua tumaini alilochagua kwa ajili yetu. Mtajua kuwa baraka ambazo Mungu amewaahidi watu wake ni nyingi na zimejaa utukufu. 19 Na mtajua kuwa uweza wa Mungu ni mkuu sana kwetu sisi tunaoamini. Ni sawa na nguvu zake kuu 20 alizotumia kumfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumweka akae upande wa kulia wa kiti chake cha enzi huko mbinguni. 21 Amemweka Kristo juu ya watawala wote, mamlaka zote, nguvu zote na wafalme wote. Amempa mamlaka juu ya kila kitu chenye nguvu katika ulimwengu huu na ujao. 22 Mungu alikiweka kila kitu chini ya nguvu za Kristo na kumfanya kuwa kichwa cha kila kitu kwa manufaa ya kanisa. 23 Kanisa ndiyo mwili wa Kristo, yeye ndiye amejaa ndani ya kanisa. Anakikamilisha kila kitu katika kila namna.

Kutoka Mauti hadi Uzima

Zamani mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi na mambo mliyotenda kinyume na Mungu. Ndiyo, zamani maisha yenu yalijaa dhambi hizo. Mliishi kwa namna ya ulimwengu; mkimfuata mkuu wa nguvu za uovu[c] zilizo katika anga, roho hiyo hiyo inatenda kazi sasa ndani ya watu wasiomtii Mungu. Tuliishi hivyo zamani, tukijaribu kuzifurahisha tamaa zetu za mwili. Tulitenda mambo ambayo miili na akili zetu zilitaka. Kama ilivyo kwa kila mtu ulimwenguni, tulistahili kuteseka kutokana na hasira ya Mungu kwa sababu ya jinsi tulivyokuwa.

Lakini Mungu ni mwingi wa rehema na anatupenda sana. Tulikuwa wafu kiroho kwa sababu ya matendo maovu tuliyotenda kinyume naye. Lakini yeye alitupa maisha mapya pamoja na Kristo. (Mmeokolewa na neema ya Mungu.) Ndiyo, ni kwa sababu sisi ni sehemu ya Kristo Yesu, ndiyo maana Mungu alitufufua pamoja naye kutoka kwa wafu na akatuketisha pamoja naye mbinguni. Mungu alifanya hivi ili wema wake kwetu sisi tulio wa Kristo Yesu uweze kuonesha nyakati zote zijazo utajiri wa ajabu wa neema yake.

Nina maana ya kuwa mmeokolewa kwa neema kwa sababu mliweka imani yenu kwake.[d] Hamkujiokoa ninyi wenyewe; bali ni zawadi kutoka kwa Mungu. Msijisifu kwa kuwa hamkuokolewa kutokana na matendo yenu. 10 Mungu ndiye aliyetufanya hivi tulivyo. Ametuumba wapya katika Kristo Yesu ili tutende mambo mema katika maisha yetu. Mambo aliyokwisha kutupangia.

Wamoja Katika Kristo

11 Hamkuzaliwa mkiwa Wayahudi. Ninyi ni watu ambao Wayahudi huwaita “Wasiotahiriwa”,[e] na wao wakijiita “Waliotahiriwa” (Tohara yao ni ile inayofanyika kwenye miili yao kwa mikono ya binadamu.) 12 Kumbukeni ya kwamba zamani hamkuwa na Kristo. Hamkuwa raia wa Israeli na hamkujua kuhusu mapatano ya maagano[f] ambayo Mungu aliyaweka kwa watu wake. Hamkuwa na tumaini na hamkumjua Mungu. 13 Lakini sasa mmeungana na Kristo Yesu. Ndiyo, wakati fulani hapo zamani mlikuwa mbali na Mungu, lakini sasa mmeletwa karibu naye kupitia sadaka ya damu ya Kristo.

14 Kristo ndiye sababu ya amani yetu. Yeye ndiye aliyetufanya sisi Wayahudi nanyi msio Wayahudi kuwa wamoja. Tulitenganishwa na ukuta wa chuki uliokuwa kati yetu, lakini Kristo aliubomoa. Kwa kuutoa mwili wake mwenyewe, 15 Kristo aliisitisha sheria pamoja na kanuni na amri zake nyingi. Kusudi lake lilikuwa ni kuyafanya makundi mawili yawe wanadamu wamoja waliounganishwa naye. Kwa kufanya hivi alikuwa analeta amani. 16 Kupitia msalaba Kristo alisitisha uhasama kati ya makundi mawili. Na baada ya makundi haya kuwa mwili mmoja, alitaka kuwapatanisha wote tena kwa Mungu. Alifanya hivi kwa kifo chake msalabani. 17 Kristo alikuja na kuwaletea ujumbe wa amani ninyi msio Wayahudi mliokuwa mbali na Mungu. Na aliwaletea pia ujumbe huo wa amani watu waliokaribu na Mungu. 18 Ndiyo, kupitia Kristo sisi sote tuna haki ya kumjia Baba katika Roho mmoja.

19 Hivyo ninyi msio Wayahudi si wageni wala wahamiaji, lakini ninyi ni raia pamoja na watakatifu wa Mungu. Ninyi ni wa familia ya Mungu. 20 Ninyi mnaoamini ni kama jengo linalomilikiwa na Mungu. Jengo hilo limejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii. Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la muhimu sana[g] katika jengo hilo. 21 Jengo lote limeunganishwa katika Kristo, naye hulikuza na kuwa hekalu[h] takatifu katika Bwana. 22 Na katika Kristo mnajengwa pamoja na watu wake wengine. Mnafanywa kuwa makazi ambapo Mungu anaishi katika Roho.

Huduma ya Paulo kwa Wasio Wayahudi

Hivyo, mimi Paulo ni mfungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi msio Wayahudi. Mnajua hakika ya kuwa Mungu alinipa kazi hii kupitia neema yake ili niwasaidie. Mungu alinionyesha na nikaweza kuujua mpango wake wa siri. Nimekwisha kuandika kiasi fulani juu ya hili. Na ikiwa mtasoma nilichowaandikia, mtajua kuwa ninaielewa siri ya kweli kuhusu Kristo. Watu walioishi zamani hawakuambiwa siri hiyo. Lakini sasa, kupitia Roho, Mungu amewawezesha mitume na manabii wake watakatifu kuijua siri hiyo. Na siri hiyo ni hii: Kwa kuikubali Habari Njema, wale wasio Wayahudi watashiriki pamoja na Wayahudi katika baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake. Wao ni sehemu ya mwili mmoja, na wanashiriki manufaa ya ahadi ambayo Mungu aliitimiza kupitia Kristo Yesu.

Kwa kipawa cha neema ya Mungu, nilifanywa mtumishi wa kuihubiri Habari Njema. Alinipa neema hiyo kwa nguvu zake. Mimi nisiye na umuhimu zaidi miongoni mwa watu wa Mungu. Lakini alinipa kipawa hiki cha kuwahubiri wasio Wayahudi Habari Njema kuhusu utajiri alionao Kristo. Utajiri huu ni mkuu na si rahisi kuuelewa kikamilifu. Pia Mungu alinipa kazi ya kuwaambia watu kuhusu mpango wa siri yake ya kweli. Aliificha siri hii ya kweli ndani yake tangu mwanzo wa nyakati. Ndiye aliyeumba kila kitu. 10 Lengo lake lilikuwa kwamba watawala wote na mamlaka zote zilizo mbinguni zijue njia nyingi anazotumia kuionesha hekima yake. Watalijua hili kwa sababu ya kanisa. 11 Hii inaendana na mpango aliokuwa nao Mungu tangu mwanzo wa nyakati. Alitekeleza mpango wake kupitia Kristo Yesu Bwana wetu. 12 Kwa kuwa tu wake Kristo tunakuja mbele za Mungu tukiwa huru bila woga. Tunaweza kufanya hivi kwa sababu ya uaminifu wake Kristo.[i] 13 Hivyo ninawaomba msikate tamaa kutokana na yale yanayonipata. Mateso yangu ni faida kwenu, na pia ni kwa ajili ya heshima na utukufu wenu.

Upendo wa Kristo

14 Hivyo ninapiga magoti nikimwomba Baba. 15 Ambaye katika yeye kila familia iliyoko mbinguni na duniani inapewa jina. 16 Ninamwomba Baba kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake awajaze nguvu za ndani kwa nguvu za Roho wake. 17 Ninaomba kwamba Kristo aishi katika mioyo yenu kwa sababu ya imani yenu. Ninaomba maisha yenu yawe na mizizi mirefu na misingi imara katika upendo. 18 Na ninaomba ili ninyi na watakatifu wote wa Mungu muwe na uwezo wa kuuelewa upana, urefu, kimo na kina cha ukuu wa upendo wa Kristo. 19 Upendo wa Kristo ni mkuu kuliko namna ambavyo mtu yeyote anaweza kujua, lakini ninawaombea ili mweze kuujua. Ndipo mtajazwa kwa kila kitu alichonacho Mungu kwa ajili yenu.

20 Tukiwa na nguvu za Mungu zinazotenda kazi ndani yetu, anaweza kufanya zaidi, zaidi ya kila kitu tunachoweza kuomba au kufikiri. 21 Atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kila wakati, milele na milele. Amina.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International