Beginning
1 Salamu kutoka kwa mtume Paulo. Sikutumwa na kundi lolote la watu au mtu yeyote hapa duniani niwe mtume. Sikupewa mamlaka yangu na mwanadamu yeyote. Nilipewa mamlaka haya moja kwa moja kutoka kwa Kristo Yesu[a] na Mungu Baba, aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu. 2 Salamu pia kutoka kwa wote walio familia ya Mungu, walio pamoja nami.
Kwa makanisa yaliyoko Galatia:[b]
3 Namwomba Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo awe mwema kwenu na awape neema na amani. 4 Yesu alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu ili atuweke huru kutoka katika uovu wa ulimwengu huu tunamoishi. Hili ndilo Mungu Baba yetu alitaka. 5 Mungu Baba yetu anastahili utukufu milele na milele! Amina.
Kuna Ujumbe Mmoja tu wa Habari Njema
6 Wakati mfupi tu uliopita Mungu aliwaita mkamfuata. Aliwaita katika neema yake kwa njia ya Kristo. Lakini sasa nashangazwa kwamba kwa haraka hivi mmegeuka mbali na kuamini kitu kingine tofauti kabisa na Habari Njema tuliyowahubiri. 7 Hakuna ujumbe mwingine wa Habari Njema, lakini baadhi ya watu wanawasumbua. Wanataka kuibadili Habari Njema ya Kristo. 8 Tuliwahubiri ninyi ujumbe wa Habari Njema tu. Hivyo laana ya Mungu impate mtu yeyote yule anayewahubiri ninyi ujumbe ulio tofauti, hata ikiwa ni mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni! 9 Nitalisema tena lile nililolisema hapo mwanzo. Ninyi mmekwishaipokea Habari Njema. Yeyote atakayewahubiri kitu kingine tofauti na ile Habari Njema mliyoipokea, basi mjue kwamba Mungu atamlaani mtu huyo!
10 Sasa mnafikiri ninajaribu kuwapendeza wanadamu? Hapana, ninataka kumpendeza Mungu siyo wanadamu. Kama ningekuwa najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumwa wa Kristo.
Mamlaka ya Paulo ni Kutoka kwa Mungu
11 Ndugu zangu, ninawataka mjue kuwa ujumbe wa Habari Njema niliowaambia haukuandaliwa na mtu yeyote. 12 Sikuupata ujumbe wangu kutoka kwa mwanadamu yeyote. Habari Njema siyo kitu nilichojifunza kutoka kwa watu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia Habari Njema ninayowahubiri watu.
13 Mmesikia juu ya mwenendo wangu hapo zamani nilipokuwa mfuasi hodari wa dini ya Kiyahudi. Nililitesa kwa nguvu kanisa la Mungu, nikiwa na shabaha ya kuliangamiza kabisa. 14 Nilipata maendeleo makubwa katika dini ya Kiyahudi kwa kufanya kazi na kusoma kwa bidii kwa sababu nilikuwa mwaminifu kwa desturi za baba zetu.
15 Lakini Mungu alikuwa na mpango maalumu kwa ajili yangu hata kabla sijazaliwa.[c] Hivyo aliniita kwa neema yake. Na ilimpendeza 16 kumfunua Mwanaye ili niweze kuwahubiri Habari Njema watu wasio Wayahudi. Hicho ndicho nilichofanya baada ya hapo. Sikuomba ushauri ama msaada wowote kutoka kwa mtu yeyote. 17 Sikwenda Yerusalemu kuwaona wale waliokuwa mitume kabla mimi sijawa mtume. Badala yake, kwanza nilienda moja kwa moja Arabia. Kisha baadaye, nikarudi katika mji wa Dameski.
18 Miaka mitatu baadaye nilikwenda Yerusalemu kumwona Petro.[d] Nilikaa naye kwa siku 15. 19 Sikuonana na mtume mwingine yeyote, isipokuwa Yakobo mdogo wake Bwana peke yake. 20 Mungu anajua kuwa hakuna ninachowaandikia kisicho cha kweli. 21 Baadaye, nilielekea katika majimbo ya Shamu na Kilikia.
22 Lakini kwa wakati ule, makanisa ya Kristo yaliyokuwa Uyahudi yalikuwa bado hayajanifahamu mimi binafsi. 23 Walikuwa wamesikia tu juu yangu: “Mtu huyu alikuwa anatutesa. Lakini sasa anawaambia watu juu ya imani ile ile aliyojaribu kuiangamiza huko nyuma.” 24 Waamini hawa walimsifu Mungu kwa sababu yangu.
Mitume Wengine Wamkubali Paulo
2 Baada ya miaka 14 nilirudi tena Yerusalemu nikiwa na Barnaba na nilimchukua Tito pia. 2 Nilikwenda kule maana Mungu alinionyesha kuwa ninapaswa kwenda. Niliwafafanulia Habari Njema kama nilivyoihubiri kwa watu wasio Wayahudi. Pia nilikutana faragha na wale waliokuwa wanatazamiwa kuwa viongozi. Nilitaka niwe na uhakika kuwa tulikuwa tunapatana ili kazi yangu ya nyuma na ile niliyokuwa naifanya sasa zisipotee bure.
3 Tito, aliyekuwa pamoja nami ni Myunani. Hata hivyo viongozi hawa hawakulazimisha kumtahiri. 4 Tulihitaji kuyazungumzia matatizo haya, kwa sababu wale waliojifanya kuwa ni ndugu zetu walikuja kwenye kundi letu kwa siri. Waliingia kama wapelelezi kutafiti kuhusu uhuru tuliokuwa nao ndani ya Kristo Yesu. Walitaka watufanye sisi watumwa, 5 lakini hatukujiweka chini ya chochote ambacho hawa ndugu wa uongo walikitaka. Tulitaka ukweli wa Habari Njema ubaki ule ule na hatimaye uwafikie na ninyi.
6 Na watu wale ambao walihesabiwa kuwa viongozi muhimu hawakuongeza lolote katika ujumbe wa Habari Njema niliyowahubiria watu. (Haijalishi kwangu kuwa walikuwa wa “muhimu” au la. Kwa Mungu binadamu wote ni sawa.) 7 Lakini viongozi hawa waliona kuwa Mungu alinipa kazi maalumu ya kuhubiri Habari Njema kwa wasio Wayahudi, kama vile alivyomwagiza Petro[e] kufanya kazi hiyo hiyo ya kuhubiri Habari Njema miongoni mwa Wayahudi. 8 Mungu alimpa Petro uwezo wa kufanya kazi kama mtume lakini kwa walio Wayahudi. Mungu akanipa mimi pia uwezo wa kufanya kazi kama mtume, lakini kwa wasiokuwa Wayahudi. 9 Yakobo, Petro na Yohana walikuwa viongozi muhimu kanisani. Hawa wakaona kuwa Mungu alinipa kipaji hiki maalumu cha huduma, hivyo wakatupa mkono wa shirika mimi pamoja na Barnaba. Wakakubali kuwa sisi tutaendelea kufanya kazi miongoni mwao wasio Wayahudi, na wao wataendelea kufanya kazi miongoni mwao walio Wayahudi. 10 Wakatuomba jambo moja tu, ya kwamba tukumbuke kuwahudumia waaminio walio maskini.[f] Na kwa hakika hili lilikuwa jambo nililojitahidi kufanya.
Paulo Aonesha Kuwa Petro Alikosea Kule Antiokia
11 Petro alipokuja Antiokia, alifanya kitu ambacho hakikuwa sahihi. Nami nikampinga, kwa sababu hakika alikuwa na hatia mbele za Mungu. 12 Hivi ndivyo ilivyotokea: Petro alipokuja Antiokia, hapo awali kabla ya Wayahudi kufika, alikula na kujumuika na wasio Wayahudi. Lakini baada ya Wayahudi kufika kutoka kwa Yakobo, Petro akajitenga na wasio Wayahudi. Akaacha kula pamoja nao kwa sababu aliwaogopa Wayahudi. 13 Hivyo Petro akafanya kama mnafiki, na waamini wengine pale Antiokia wakaungana naye katika unafiki huo. Wakamfanya hata Barnaba naye kuwa mnafiki kama wao. 14 Hawakuwa wakiifuata kweli ya Habari Njema. Nilipoona hili, nilimweleza Petro mbele ya kila mtu. Nilisema, “Petro, wewe ni Myahudi, lakini huenendi kama Myahudi. Unaenenda kama mtu asiye Myahudi. Hivyo kwa nini unajaribu kuwalazimisha wale wasio Wayahudi kuenenda kama Wayahudi?
15 Sisi ni Wayahudi kwa kuzaliwa. Hatukuzaliwa tukiwa ‘watenda dhambi’, kama vile Wayahudi wanavyowaita wale wasio Wayahudi. 16 Lakini tunajua kuwa hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Ni kwa kuamini katika[g] Yesu Kristo ndiko kunamfanya mtu ahesabiwe haki mbele za Mungu. Hivyo hata nasi Wayahudi tumeiweka imani yetu katika Kristo Yesu, kwa sababu tulitaka kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Na tumehesabiwa haki kwa imani[h] ya Yesu Kristo, siyo kwa sababu tuliifuata sheria. Naweza kusema hili kwa sababu hakuna anayeweza kuhesabiwa haki kwa kuifuata Sheria ya Musa.
17 Kwa hiyo tunaamini uhusiano wetu kwa Kristo utatufanya tuhesabiwe haki mbele za Mungu. Ikiwa hiyo inatufanya tuonekane kama ‘watenda dhambi’ wasio Wayahudi, je itakuwa na maana kuwa Kristo anasababisha dhambi kuongezeka. Kwa hakika sivyo? 18 Sheria ilijenga ukuta baina yetu Wayahudi na watu wengine wote, ukuta ambao nilijitahidi kuuvunja. Kweli nitakosea sana kuujenga tena ukuta huo. 19 Sheria yenyewe iliyafikisha mwisho maisha yangu chini ya sheria. Nikafa katika sheria hiyo na kuwa huru ili niweze kuishi kwa ajili ya Mungu. Nimepigiliwa misumari msalabani pamoja na Kristo. 20 Hivyo siyo mimi ninayeishi sasa; ni Kristo ndiye anayeishi ndani yangu. Bado naishi katika mwili wangu, lakini naishi kwa imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda na kujitoa mwenyewe kuniokoa mimi. 21 Si mimi ninayeikataa neema ya Mungu kama vile haina manufaa yoyote. Kwa sababu ikiwa kwa kuifuata sheria ndivyo watu wanahesabiwa haki mbele za Mungu, basi Kristo alikufa pasipo faida!”
Baraka za Mungu Huja Kwa Imani
3 Ninyi watu wa Galatia, je mmepoteza fahamu zenu? Nilidhani mmeelewa kwa nini Yesu Kristo alisulubiwa msalabani! Niliwaeleza wazi kabisa jambo hilo, kama vile kuchora na kupaka rangi picha mbele ya macho yenu. Je, kuna mtu yeyote aliyewaloga mkasahau? 2 Niambieni jambo hili moja: Ni jinsi gani mlimpokea Roho? Je, mlimpokea Roho kwa kufuata sheria? Hapana, mlimpokea Roho kwa sababu ya ujumbe kuhusu Yesu unaoleta imani. 3 Mliyaanza maisha yenu mapya pamoja na Roho. Inakuwaje sasa mdhani kuwa mnaweza kukamilishwa na kitu kinyonge kama tohara kilichofanyika katika miili yenu?[i] Basi mmepoteza fahamu zenu! 4 Je, mlipata uzoefu huo mwingi pasipo manufaa yoyote? Sidhani kama hivyo ndivyo! 5 Je, Mungu anawapa ninyi Roho na kutenda miujiza miongoni mwenu kwa kuwa mnaifuata sheria? Hapana sivyo! Mungu anawapa ninyi baraka hizi kwa njia ya ujumbe unaoleta imani katika kumwamini Yesu.
6 Maandiko yanasema kitu hicho hicho kuhusu Ibrahimu. “Ibrahimu alimwamini Mungu, na Mungu akaikubali imani yake na akamhesabia haki.”(A) 7 Hivyo mnapaswa kuelewa kuwa watoto sahihi wa Ibrahimu ni wale walio na imani. 8 Maandiko yalieleza ambacho kingetokea katika siku zijazo. Maandiko haya yalisema kwamba Mungu angewafanya wasio Wayahudi kuwa wenye haki kwa njia ya imani. Mungu alizisema Habari Njema hizi kwa Ibrahimu kabla haijatokea. Mungu alimwambia Ibrahimu, “Kwa kukubariki wewe, nitawabariki watu wote duniani.”(B) 9 Kwa hiyo, wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu ndiyo wanaobarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwaminifu.
10 Lakini watu wale wanaodhani kuwa kutii sheria ndicho kitu muhimu sana daima hukaa chini ya tishio la laana. Kama vile Maandiko yanavyosema, “Amelaaniwa mtu yeyote atakayeacha kuzishika na kuzitii sheria hizi zote.”(C) 11 Hivyo ni dhahiri kuwa hakuna anayeweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Maandiko yanasema, “Mwenye haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.”(D)
12 Sheria haitegemei imani. Hapana, inasema kuwa njia pekee ambayo mtu anaweza kupata uzima kwa njia ya sheria ni kwa kutii amri zake.[j] 13 Sheria inasema kuwa sisi Wayahudi tuko chini ya laana kwa kutokuitii daima. Lakini Kristo alituweka huru kutoka katika laana hiyo. Alikubali kulaaniwa na sheria ili atuokoe. Maandiko yanasema, “Yeyote anayening'inizwa mtini[k] yuko chini ya laana.”(E) 14 Kwa sababu ya yale aliyoyafanya Kristo Yesu, baraka ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu zilitolewa pia kwa wasio Wayahudi. Kristo alikufa ili kwamba kwa kumwamini sisi sote, Wayahudi na wasio Wayahudi, tuweze kumpokea Roho ambaye Mungu aliahidi.
Sheria na Ahadi
15 Ndugu zangu, hebu niwape mfano kutoka maisha ya kila siku: Fikiri kuhusu makubaliano ambayo mtu hukubaliana na mwingine. Baada ya makubaliano hayo kufanywa rasmi, hakuna anayeweza kuongeza chochote kwenye makubaliano hayo na hakuna anayeweza kulipuuza. 16 Mungu aliweka agano kwa Ibrahimu na uzao wake. Maandiko hayasemi, “na kwa ajili ya uzao wenu”. Hilo lingekuwa na maana ya watu wengi. Lakini linasema, “na kwa uzao wako”. Hiyo ina maana ya uzao mmoja tu, na uzao huo ni Kristo. 17 Hii ndiyo maana yangu: Agano ambalo Mungu aliliweka na Ibrahimu lilifanywa rasmi na Mungu muda mrefu kabla ya kuja kwa sheria. Sheria ilikuja miaka 430 baadaye. Hivyo sheria haingeweza kulifuta agano hilo na kuibadili ahadi ya Mungu.
18 Baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake hazipatikani kwa njia ya sheria. Ikiwa ingekuwa hivyo, basi isingekuwa ahadi ya Mungu inayotuletea sisi baraka hiyo. Lakini Mungu aliitoa bure baraka yake kwa Ibrahamu kama agano.
19 Hivyo kwa nini sheria ilitolewa? Sheria ililetwa baadaye kwa sababu ya makosa wanayotenda[l] watu. Lakini sheria ingeendelea kutumika hadi kuja kwa Uzao wa Ibrahimu. Huyu ni Uzao unaotajwa katika agano lililotolewa na Mungu. Lakini sheria ilitolewa kupitia malaika na malaika walimtumia Musa kama mpatanishi wa kuwapa watu sheria. 20 Hivyo mpatanishi anahitajika pale ambapo upande mmoja unapaswa kufikia mapatano. Lakini Mungu ambaye ni mmoja, hakumtumia mpatanishi alipompa ahadi Ibrahimu.[m]
Lengo la Sheria ya Musa
21 Je, hili lamaanisha kwamba sheria hutenda kazi kinyume na ahadi za Mungu? La hasha. Sheria iliyotolewa kamwe haikuwa na uwezo wa kuwaletea watu maisha mapya. Ingekuwa hivyo, basi tungehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. 22 Lakini hilo halikuwa kusudi la sheria. Maandiko yanauweka ulimwengu wote chini ya udhibiti wa dhambi kama aina ya kifungo gerezani. Ili kile ambacho Mungu aliahidi kipokelewe kwa njia ya imani katika[n] Yesu Kristo. Hii hutolewa kwa wale wanaomwamini.
23 Kabla ya aliye mwaminifu kuja, sheria ilituweka sisi kama wafungwa. Hatukuwa huru hadi imani hii inayokuja[o] ilipofunuliwa kwetu. 24 Nina maana kuwa sheria ilikuwa ni mlezi aliyetusimamia[p] tu hadi Kristo alipokuja. Baada ya kuja kwake, tungefanyika kuwa wenye haki mbele za Mungu kwa njia ya imani. 25 Sasa kwa sababu imani hii imekuja, hatuhitaji tena kusimamiwa na kulelewa na sheria.
26 Hii ni kwa sababu ninyi nyote ni mali ya Kristo Yesu na ni watoto wa Mungu kwa njia ya imani. 27 Ndiyo, nyote mlibatizwa ili muunganike na Kristo. Hivyo sasa Kristo anawafunika kabisa kama kubadilisha nguo mpya kabisa. 28 Sasa, ndani ya Kristo haijalishi kama wewe u Myahudi au Myunani, mtumwa au huru, mwanaume au mwanamke. Wote mko sawa katika Kristo Yesu. 29 Na kwa vile ninyi ni wa Kristo, hivyo ninyi wazaliwa wa Ibrahamu. Ninyi ndiyo mtakaopokea baraka zote ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu.
© 2017 Bible League International