Beginning
Paulo Aitetea Huduma yake
10 Mimi, Paulo, ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo. Wengine wanasema kuwa nina ujasiri ninapowaandikia nikiwa mbali, lakini ni mwoga kusema jambo lo lote ninapokuwa pamoja nanyi. 2 Wanadhani sababu ya kutenda yale tunayoyafanya ni kama zile za kidunia. Ninapanga kuwa jasiri sana kinyume chao watu hao hapo ninapokuja kwenu. Tafadhali ninawaomba, sitahitaji kutumia ujasiri huo kwenu. 3 Tunaishi katika ulimwengu huu, lakini hatupigani vita yetu kama ulimwengu unavyopigana. 4 Silaha tunazozitumia si za kibinadamu. Silaha zetu zina nguvu kutoka kwa Mungu na zinaweza kuharibu ngome za adui. Tunaharibu mabishano ya watu, 5 na tunasambaratisha kila wazo la kiburi linalojiinua kinyume cha elimu ya Mungu. Pia tunateka kila wazo na kulitiisha ili limtii Kristo. 6 Tuko tayari kumwadhibu kila mtu asiyetii, lakini tunataka ninyi muwe watiifu ipasavyo kwanza.
7 Mnatakiwa kuchunguza ukweli halisi wa mambo ulio mbele ya macho yenu. Ikiwa mna uhakika kuwa ninyi ni wa Kristo, mnapaswa kukumbuka kuwa na sisi ni wa Kristo kama ninyi mlivyo wa Kristo. 8 Inaweza kuonekana kana kwamba tunajivuna sana kupita kiasi kidogo kuhusu mamlaka ambayo Bwana ametupa sisi. Lakini alitupa mamlaka hii ili kuwatia nguvu ninyi, na sio kuwaumiza. Hivyo sitaona haya kwa lolote ambalo tumejisifu kwalo. 9 Sitaki mfikiri kuwa najaribu kuwatisha kwa barua zangu. 10 Wengine wanasema, “Barua za Paulo zina shuruti na matakwa mengi, Lakini anapokuwa pamoja nasi, ni mdhaifu na msemaji asiyefaa.” 11 Watu hao wanapaswa kulielewa jambo hili: tutakapokuwa pamoja nanyi, tutatenda mambo kwa ujasiri ule ule tunaouonyesha sasa katika barua zetu.
12 Hatujaribu kujiweka katika daraja moja na wale wanaojisifu wenyewe. Hatujilinganishi na watu hao. Wao wanatumika wenyewe kwa kujipima wenyewe, na wanajilinganisha miongoni mwao wenyewe. Hili linadhihirisha kuwa hawajui lolote.
13 Lakini hatutajisifia lolote nje ya kazi tuliyopewa kuifanya. Tutaweka ukomo wa kujisifia kwetu katika kazi aliyotupa Mungu kuifanya, lakini kazi hii inajumuisha kazi yetu kwenu. 14 Tungekuwa tunajivuna zaidi na zaidi ikiwa tungekuwa hatujafika kabisa kwenu. Lakini tulikuwa wa kwanza kufika kwenu na Habari Njema ya Kristo. 15 Tumeweka ukomo wa kujivuna kwetu katika kazi ambayo ni yetu. Hatujivunii kazi ambayo wameifanya watu wengine. Tunatumaini kuwa imani yenu itaendelea kukua. Tunatumaini kuwa mtaisadia kazi yetu kukua zaidi na zaidi. 16 Tunataka kuieneza habari njema katika maeneo ya mbali zaidi kupita mji wenu. Hatutaki kujisifia juu ya kazi ambayo imefanywa na mtu mwingine katika eneo lake. 17 “Yeyote anayejisifu na ajisifu juu ya Bwana tu.”(A) 18 Kile watu wanachosema kuhusu wao wenyewe hakina maana yeyote. Cha muhimu ni ikiwa Bwana anasema kuwa wamefanya vizuri.
Paulo na Mitume wa Uongo
11 Natamani mngekuwa na subira nami hata pale ninapokuwa mjinga kidogo. Tafadhali muwe na subira nami. 2 Nina wivu unaotoka kwa Mungu kwa ajili yenu. Niliahidi kuwatoa ninyi kama bibi harusi kwa mume mmoja. Niliahidi kuwatoa ninyi kwa Kristo muwe bibi harusi[a] wake aliye safi. 3 Ila nina hofu kuwa nia zenu zitapotoshwa muache kujitoa kwa dhati na kumfuata Yesu Kristo kwa moyo safi. Hili laweza kutokea kama vile Hawa alivyodanganywa na nyoka kwa akili zake za ujanja wenye udanganyifu. 4 Mnaonekana kuwa na subira na mtu yeyote anayekuja kwenu na kuwaeleza habari za Yesu aliye tofauti na Yesu yule ambaye sisi tuliwaambia habari zake. Mnaonekana kuwa radhi kuipokea roho au ujumbe ulio tofauti na roho na ujumbe ambao mlioupokea kutoka kwetu.
5 Sidhani kuwa hao “mitume wakuu” ni bora kuliko mimi nilivyo. 6 Ni kweli kuwa mimi siye mtu nilyefunzwa kwa mzungumzaji, lakini nina ufahamu wa mambo. Tumeliweka hili wazi kwenu kwa njia zote na kwa mazingira yote.
7 Nilifanya kazi ya kutangaza Habari Njema za Mungu kwenu bila malipo. Nilijinyenyekeza ili kuwafanya ninyi kuwa wa muhimu. Je! Mwadhani nilikosea katika hilo? 8 Nilipokea malipo toka makanisa mengine. Ilikuwa kana kwamba nimechukua fedha toka kwao ili niweze kuwatumikia ninyi. 9 Kama nilihitaji chochote nilipokuwa nanyi, sikumsumbua yeyote kati yenu. Kina kaka waliofika kutoka Makedonia walinipa yote niliyohitaji. Sikutaka kuwa mzigo kwenu kwa namna yeyote ile. Na kamwe sitakuwa mzigo kwenu. 10 Hakuna mtu yeyote katika jimbo lote la Akaya anayeweza kunizuia kujivuna juu ya hilo. Nasema hili katika kweli ya Kristo iliyo ndani yangu. 11 Kwa nini siwalemei? Je! Mnadhani ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kwamba ninawapenda.
12 Na nitaendelea kufanya kile ninachokifanya sasa, kwa sababu nataka kuwazuia watu hao wasiwe na sababu ya kujivunia. Wangependa kusema kuwa kazi ile wanayojivunia ni sawa na kazi yetu. 13 Wao ni mitume wa uongo, watenda kazi walio wadanganyifu. Wao hujifanya kuwa ni mitume wa Kristo. 14 Hilo halitushangazi sisi, kwa sababu hata Shetani mwenyewe hujigeuza na kujifanya kuwa malaika wa nuru.[b] 15 Hivyo, hiyo haitufanyi sisi kustaajabu ikiwa watumishi wa shetani watajigeuza na kujifanya kuwa watumishi wanaofanya yaliyo ya haki. Lakini mwishowe watapokea hukumu wanayostahili.
Paulo aelezea juu ya Mateso yake
16 Ninawaambia tena: Asiwepo yeyote wa kudhani kuwa mimi ni mjinga. Lakini kama mnadhani kuwa mimi ni mjinga, basi nipokeeni kama vile ambavyo mngempokea mjinga. Kisha nami naweza kujivuna angalau kidogo zaidi pia. 17 Lakini mimi sizungumzi kwa namna ambavyo Bwana angelizungumza. Mimi ninajivuna kama vile mjinga. 18 Wengi wengine wanajivuna jinsi ambavyo watu wa dunia hii wanafanya. Hivyo, nami nitajivuna kwa namna hiyo. 19 Mna busara, hivyo mtamvumilia kwa furaha mjinga! 20 Nasema haya kwa sababu mnamvumilia hata mtu yule anayewatumia vibaya. Mnawavumilia wale wanaowarubuni akili na kudhani kuwa wao ni bora kuliko ninyi, au wanaowapiga usoni! 21 Ninaona aibu kusema haya, lakini tulikuwa “dhaifu sana” kuyafanya mambo kama hayo kwenu.
Lakini kama kuna mtu aliye jasiri vya kutosha kujivuna, nami nitajivuna pia. (Ninaongea hivi kama mjinga.) 22 Je, watu hao ni Wayahudi? Mimi pia. Je, ni Waebrania? Mimi pia. Je, wanatoka katika familia ya Ibrahimu? Mimi pia. 23 Je, wanamtumikia Kristo? Mimi ninamtumikia zaidi sana. (Je, mimi ni mwendawazimu kuongea kwa jinsi hii?) Nimefanya kazi kwa juhudi kuliko wao. Nimekuwa gerezani mara nyingi. Nimepigwa vibaya sana. Nimekuwa katika hali za hatari ya kufa mara nyingi.
24 Mara tano Wayahudi wamenipa adhabu ya viboko 39. 25 Mara tatu katika nyakati tofauti nimepigwa kwa fimbo. Mara moja nilikuwa karibu kuuawa kwa kupigwa kwa mawe. Mara tatu nimevunjikiwa na merikebu, na mara moja katika hizo nilikesha usiku na kushinda kutwa nzima tukielea baharini. 26 Katika safari zangu za mara kwa mara nimekuwa katika hatari za kwenye mito, majambazi, watu wangu wenyewe, na toka kwa watu wasio Wayahudi. Nimekuwa katika hatari mijini, katika maeneo wasioishi watu, na katika bahari. Na nimekuwa katika hatari za watu wanaojifanya kuwa waamini lakini siyo waamini.
27 Nimefanya kazi ngumu na za kuchosha, na mara nyingi sikuweza kulala usingizi. Nimekuwa mwenye njaa na kiu. Mara nyingi nimekosa kula chakula. Nimekuwa katika hali ya baridi na kutokuwa na nguo za kujifunika. 28 Na kuna matatizo mengine mengi zaidi. Mojawapo ya hayo ni mzigo nilio nao kila siku wa majukumu yangu: Ninawaza juu ya makanisa yote. 29 Ninajisikia kuwa mdhaifu kila mara mtu mwingine anapokuwa dhaifu. Ninapata hasira sana pale mtu yeyote anapoingizwa dhambini.
30 Ikiwa ni lazima nisifu, nitajisifu katika vitu vinavyonidhihirisha kuwa mimi ni dhaifu. 31 Mungu ajua kuwa sisemi uongo. Yeye ni Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na anapaswa kutukuzwa milele. 32 Nilipo kuwa Dameski, gavana wa mfalme Areta alitaka kunikamata, hivyo aliweka walinzi nje ya malango ya jiji. 33 Lakini baadhi ya marafiki wakaniweka ndani ya kikapu. Kisha wakaniteremsha chini kupitia dirisha lililokuwa kwenye katika ukuta wa mji. Hivyo nikamtoroka gavana.
Nguvu ya Paulo Inatoka Katika Udhaifu
12 Inanipasa kuendelea kujivuna juu yangu mwenyewe. Hiyo haitasaidia, lakini nitazungumza juu ya maono na mafunuo kutoka kwa Bwana. 2 Ninamjua mtu mmoja[c] katika Kristo aliyechukuliwa juu katika mbingu ya tatu. Hili lilitokea miaka 14 iliyopita. Sifahamu ikiwa mtu huyu alikuwa ndani ya mwili wake au nje ya mwili wake, lakini Mungu anajua. 3-4 Na ninajua kuwa mtu huyu alichukuliwa juu paradiso. Sijui kama alikuwa katika mwili wake au nje ya mwili wake. Mungu pekee ndiye anajua. Lakini mtu huyu aliyasikia mambo ambayo hana uwezo wa kuyasimulia. Alisikia mambo ambayo mtu yeyote anaruhusiwa kuyasema. 5 Nitajivunia mtu wa namna hiyo, lakini sitajivuna juu yangu mwenyewe. Nitajivuna tu katika madhaifu yangu.
6 Lakini ikiwa nilitaka kujivuna, sitakuwa nikizungumza kama mjinga, kwa sababu ningekuwa nasema iliyo kweli. Lakini sitajivuna tena zaidi, kwa sababu sitaki watu wanifikirie kwa ubora zaidi kuliko wanavyoniona nikitenda ama kusikia ninayosema.
7 Lakini imenipasa kutojivuna zaidi juu ya mambo ya ajabu yaliyoonyeshwa kwangu. Kwa sababu hiyo nilipewa tatizo lenye maumivu;[d] malaika toka kwa Shetani; aliyetumwa kwangu kunitesa, ili nisiweze kufikiri kwamba mimi ni bora zaidi kuliko watu wengine. 8 Nilimwomba Bwana mara tatu kuliondoa tatizo hili kwangu. 9 Lakini Bwana alisema, “Neema yangu ndiyo unayoihitaji. Ni pale tu unapokuwa dhaifu ndipo kila kitu kinapoweza kufanyika katika uwezo wangu.” Hivyo nitajivunia udhaifu wangu kwa furaha. Hapo ndipo uweza wa Kristo unaweza kukaa ndani yangu. 10 Ndiyo, nina furaha kuwa na madhaifu ikiwa ni kwa ajili ya Kristo. Nina furaha kuaibishwa na kupitia magumu. Nina furaha ninapoteswa na kupata matatizo, kwa sababu ni pale nilipodhaifu ndipo ninapokuwa na nguvu.
Upendo wa Paulo kwa Waamini wa Korintho
11 Nimekuwa nikizungumza kama mjinga, lakini ninyi ndiyo mliosababisha nikafanya hivyo. Ninyi ndiyo mnaopaswa kuzungumza mema juu yangu. Mimi si kitu, lakini mimi si myonge kwa njia yeyote ile kwa hao “mitume wakuu”. 12 Nilipokuwa pamoja nanyi, nilifanya kwa uvumilivu wote vitu vilivyo nilidhihirisha kuwa mimi ni mtume kwa ishara, maajabu na miujiza. 13 Kwa hiyo mlipokea kila kitu ambacho makanisa yote yalipata. Kitu kimoja tu ndicho kilikuwa cha tofauti na cha kipekee: Sikuwa mzigo au msumbufu kwenu. Mnisamehe kwa hilo.
14 Niko tayari sasa kuwatembelea kwa mara ya tatu, na sitakuwa mzigo kwenu. Mimi sitafuti kitu chochote kilicho chenu. Ninawataka ninyi tu. Watoto wasiweke akiba vitu vya kuwapa wazazi wao. Wazazi wanapaswa kuweka akiba vitu vya kuwapa watoto wao. 15 Kwa hiyo ninayo furaha kutumia kile nilichonacho kwa ajili yenu. Na mimi mwenyewe nitajitoa kikamilifu kwa ajili yenu. Je, kama upendo wangu kwenu utakuwa mkubwa, upendo wenu kwangu utapungua?
16 Ni wazi kuwa sikuwa mzigo kwenu, lakini baadhi yenu wanadhani kuwa nilikuwa mjanja, na kutumia hila kuwaweka mtegoni. 17 Je, niliwadanganya kwa kuwatumia mtu yeyote kati ya wale niliyowatuma kwenu? Mnafahamu kuwa sikufanya hivyo. 18 Nilimwomba Tito aje kwenu, na nilimtuma kaka yetu afuatane naye. Tito hakuwadanganya, je alifanya hivyo? Hapana! Na kwa hiyo mjue kuwa matendo yangu na tabia yangu ilikuwa ya dhati kama ilivyokuwa kwake.
19 Je! Mnadhani tumekuwa tukijitetea? Hapana, tunasema haya katika Kristo na mbele za Mungu. Ninyi ni rafiki zetu wapendwa, na kila tunachofanya tunakifanya ili muwe imara. 20 Ninafanya hivi kwa sababu ninaogopa kuwa nitakapokuja, hamtakuwa kama vile ninavyotaka muwe. Na pia nina wasiwasi kuwa sitakuwa kwa namna ile mnayotaka mimi niwe. Nina hofu kuwa nitawakuta mkibishana, wenye wivu, wenye hasira, mkipigana kwa ubinafsi wenu, wenye misemo mibaya, watetaji, wenye kiburi, na machafuko huko. 21 Nina wasiwasi kuwa nitakapokuja kwenu, Mungu wangu ataninyenyekeza tena mbele yenu. Nitalazimika kuomboleza kwa ajili ya wale ambao wametenda dhambi. Wengi wao hawajarejea na kutubia maisha yao ya uovu, dhambi za zinaa, na mambo ya aibu waliyotenda.
Maonyo ya Mwisho na Salamu
13 Hii itakuwa ni safari yangu ya tatu kuwatembelea. Na mkumbuke, “Kila shitaka ni lazima lithibitishwe na mashahidi wawili au watatu wanaosema kuwa jambo hilo ni la kweli.”(B) 2 Nilipokuwa pamoja nanyi mara ya pili, nilitoa maonyo kwa wale waliotenda dhambi. Sipo hapo sasa, ila natoa onyo lingine kwao na kwa yeyote aliyetenda dhambi: Nitakapo kuja tena kwenu, nitawaadhibu walio miongoni mwenu ambao bado wanatenda dhambi. 3 Mnatafuta uthibitisho kuwa Kristo anasema kupitia mimi. Uthibitisho wangu ni kuwa yeye si dhaifu kuwashughulikia bali yeye anaonesha uweza wake miongoni mwenu. 4 Ni kweli kuwa Kristo alikuwa dhaifu alipouawa msalabani, lakini yu hai kwa nguvu za Mungu. Ni kweli pia kwamba twashiriki unyonge wake, lakini kwa kushughulika nanyi, tutakuwa hai pamoja nae katika uweza wa Mungu.
5 Jiangalieni ninyi wenyewe. Mjipime ninyi wenyewe mkaone kama mngali mnaishi katika imani. Hamtambui kuwa Kristo Yesu yu ndani yenu? La mkishindwa jaribio hilo; ikiwa hamtakuwa mkiishi katika imani; basi Kristo hayumo ndani yenu. 6 Lakini ni matumaini yangu kuwa mtagundua ya kwamba hatujashindwa jaribio hilo. 7 Tunawaombea kwa Mungu msifanye lolote lililo baya. Tunachojali hapa si kwamba watu waone kuwa tumeshinda jaribio katika ile kazi tuliyofanya pamoja nanyi. Tunachokitaka zaidi ni ninyi kufanya lililo jema, hata ikiwa itaonekana kuwa tumeshindwa jaribio. 8 Hatuwezi kufanya lolote lililo kinyume na kweli bali lile linalodumisha kweli. 9 Tunafuraha kuonekana tu wadhaifu ikiwa ninyi mko imara. Na hili ndilo tunaloomba, kwamba maisha yenu yatakamilishwa katika haki tena. 10 Ninaandika haya kabla sijaja kwa kuwa niko mbali nanyi ili nijapo nisilazimike kutumia mamlaka kuwaadhibu. Bwana alinipa mamlaka hayo kuwaimarisha, na sio kuwaharibu.
11 Sasa, wapendwa dada zangu na kaka zangu mjazwe furaha. Jitahidini kutengeneza njia zenu, fanyeni nilichowaomba kufanya. Mpatane kila mmoja na mwenziwe, na ishini katika amani. Ndipo Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.
12 Msalimiane kwa salamu maalum ya watu wa Mungu.[e] Watakatifu wote wa Mungu hapa nao wanawasalimu.
13 Ninawaombea ili ninyi nyote mfurahie neema ya Bwana Yesu Kristo, upendo wa Mungu, na Ushirika[f] wa Roho Mtakatifu.
© 2017 Bible League International