Beginning
5 Tunafahamu kuwa miili yetu, ambayo ni hema tunaloishi ndani yake hapa duniani itaharibiwa. Hilo litakapotokea, Mungu atakuwa na nyumba tayari kwa ajili yetu kuishi ndani yake. Haitakuwa nyumba kama ambayo watu hujenga hapa duniani. Itakuwa nyumba ya mbinguni itakayodumu milele. 2 Lakini wakati bado tunaishi katika miili hii, tunaugua kwa sababu tuna shauku kubwa mbele za Mungu ya kutupa mwili wetu mpya wa mbinguni ili tuweze kujivika. 3 Tutauvaa mwili wa mbinguni kama vazi jipya na hatutakuwa uchi. 4 Tunapoishi katika “hema” hili la kidunia, tunaugua na kuelemewa na mizigo. Lakini, hiyo si kwa sababu tunataka kuivua miili hii ya zamani. Hapana, ni kwa sababu tunataka kuivaa miili yetu mipya. Kisha mwili huu unao kufa utafunikwa na uzima. 5 Hii ndiyo sababu Mungu mwenyewe ndiye aliyetuandaa kwa kusudi hili hasa. Na ametupata Roho kama malipo ya awali kutuhakikishia maisha yajayo.
6 Hivyo tuna ujasiri daima. Tunafahamu kuwa tunapoendelea kuishi katika mwili huu, tunakuwa mbali na makao yetu pamoja na Bwana. 7 Tunaishi kwa msingi wa yale tunayoamini kuwa yatatokea na siyo kwa msingi wa yale tunayoyaona. 8 Hivyo ninasema tuna ujasiri. Na tungependa kuondoka na kutokuwa katika mwili huu na kuwa nyumbani pamoja na Bwana. 9 Lengo letu pekee ni kumpendeza Bwana, kwamba tupo nyumbani au mbali. 10 Tutasimama sote mbele za Kristo ili tuhukumiwe. Kila mtu atalipwa anachostahili. Kila mtu atalipwa kutokana na matendo yake, mazuri au mabaya, alipoishi katika mwili huu wa kidunia.
Kuwasaidia Watu Ili Wawe Rafiki wa Mungu
11 Tunafahamu maana ya kuwa na hofu na Bwana, hivyo tunajitahidi kuwashawishi watu waipokee. Mungu anafahamu tulivyo, na ni matarajio yangu kuwa nanyi mioyoni mwenu mnatufahamu sisi pia. 12 Hatujaribu tena kujithibitisha kwenu sasa. Lakini tunawapa sababu za ninyi kujivuna kwa ajili yetu. Kisha mtaweza kuwa na majibu kwa ajili wanaojivuna kwa ajili ya yale yanayoonekana. Hawajali kuhusu kilicho katika moyo wa mtu. 13 Ikiwa tuna wazimu, ni kwa ajili ya Mungu na ikiwa tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu. 14 Upendo wa Kristo unatutawala, kwa sababu tunafahamu kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote. Hivyo wote wamekufa. 15 Alikufa kwa ajili ya wote ili wanaoishi wasiendelee kuishi kwa ajili yao wenyewe. Alikufa kwa ajili yao na alifufuka toka kwa wafu ili waishi kwa ajili yake.
16 Kuanzia sasa hatumfikirii mtu yeyote kama ulimwengu unavyowafikiria watu. Ni kweli kuwa zamani kale tulimfikiria Kristo kwa mtazamo wa kidunia. Lakini hatufikirii hivyo sasa. 17 Mtu anapokuwa ndani ya Kristo, anakuwa kiumbe[a] kipya kabisa. Mambo ya zamani yanakoma; na ghafla kila kitu kinakuwa kipya! 18 Yote haya yatoka kwa Mungu. Kupitia Kristo, Mungu alifanya amani katika yake na sisi. Na Mungu alitupa kazi ya kuleta amani kati ya watu na Mungu. 19 Tunachosema ni kuwa kupitia Kristo, Mungu alikuwa anaweka amani kati yake na ulimwengu. Alikuwa anatoa ujumbe wa msamaha kwa kila mtu kwa matendo mabaya waliyotenda kinyume naye. Na alitupa ujumbe huu wa amani ili kuwaeleza watu. 20 Hivyo tumetumwa kwa ajili ya Kristo. Ni kama Mungu anawaita watu kupitia sisi. Tunazungumza kwa niaba ya Kristo tunapowasihi ninyi kuwa na amani na Mungu. 21 Kristo hakuwa na dhambi,[b] ila Mungu alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu ili ndani ya Kristo tuweze kufanyika kielelezo cha wema wa uaminifu wa Mungu.
6 Sisi ni watenda kazi pamoja na Mungu. Hivyo tunawasihi: Neema mliyoipokea kutoka kwa Mungu iwe na manufaa kwenu. 2 Mungu anasema,
“Nilikusikia kwa wakati sahihi,
na nikakusaidia siku ya wokovu.”(A)
Ninawaambia kwamba “wakati uliokubalika” ni huu sasa. Na “Siku ya wokovu” ni leo.
3 Hatutaki watu waone makosa katika kazi yetu. Hivyo hatutendi jambo lolote litakalokuwa kikwazo kwa wengine. 4 Lakini kwa kila njia tunaonesha kuwa sisi ni watumishi wa Mungu. Hatukati tamaa, ingawa tunakutana na matatizo, mambo magumu na matatizo ya kila namna. 5 Tumepigwa na kutupwa gerezani. Watu wameanzisha fujo dhidi yetu. Tumefanya kazi kwa bidii, mara nyingi pasipo kula ama kulala. 6 Tunadhihirisha kuwa sisi tu watumishi wa Mungu kutokana na maisha yetu safi, kwa ufahamu wetu, kwa subira yetu na kwa upole wetu. Tunadhihirisha hilo kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo wetu wa kweli, 7 kwa kusema iliyo kweli, na kwa kuzitegemea nguvu za Mungu. Njia hii iliyo sahihi ya kuishi imetuandaa kujitetea wenyewe kinyume na kila aina ya shambulizi.
8 Baadhi ya watu wanatuheshimu, lakini wengine wanatudhihaki. Wengine wanasema mema juu yetu, lakini wengine wasema mabaya juu yetu. Wengine wanatusema kuwa tu waongo, lakini tunasema kweli. 9 Kwa wengine hatufahamiki, lakini twajulikana sana. Tunaonekana kama watu wanaostahili kufa, lakini angalia! Twadumu kuishi. Tunaadhibiwa, lakini hatuuawi. 10 Tuna huzuni nyingi, lakini tunafuraha kila siku. Tu maskini, lakini tunawafanya watu wengi kuwa matajiri katika imani. Hatuna kitu, lakini tunakila kitu.
11 Tumesema kwa uhuru kwenu ninyi watu wa Korintho. Tumefungua mioyo yetu kwenu. 12 Upendo wetu kwenu haujakoma. Ninyi ndiyo mliouzuia upendo wenu kwetu. 13 Ninawaambia kama watoto wangu. Fanyeni vivyo hivyo kama sisi tulivyotenda kwenu; fungueni mioyo yenu pia.
Sisi ni Hekalu la Mungu
14 Ninyi hamko sawa na wale wasioamini. Hivyo msifungwe nira pamoja nao. Wema na ubaya havikai pamoja. Nuru na giza haviwezi kukaa pamoja katika chumba kimoja. 15 Itawezekanaje kuwe na mapatano kati ya Kristo na beliali?[c] Je, mwamini anashirika gani na asiye amini? 16 Hekalu la Mungu halina mapatano yoyote na sanamu, na sisi tu hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu anavyosema,
“Nitakaa kati yao
na kutembea nao;
Nitakuwa Mungu wao,
na watakuwa watu wangu.”(B)
17 “Hivyo tokeni nje kati yao
na jitengeni nao, asema Bwana.
Msishike chochote kilicho kichafu,
nami nitawakaribisha.”(C)
18 “Nitakuwa baba yenu,
nanyi mtakuwa wana wangu na binti zangu,
asema Bwana Mwenyezi.”(D)
7 Rafiki wapendwa, tuna ahadi hizi toka kwa Mungu. Hivyo tujitakase maisha yetu na kuwa huru kutoka kwa kila kinachofanya miili yetu ama roho zetu kuwa najisi. Heshima yetu kwa Mungu itufanye tujaribu kuwa watakatifu kabisa kwa namna tunavyoishi.
Furaha ya Paulo
2 Fungueni mioyo yenu kwetu. Hatujamtendea vibaya wala kumwumiza mtu yeyote. Na hatujamdanganya mtu yeyote. 3 Sisemi haya kuwalaumu. Nimekwishawaeleza kuwa tunawapenda sana kiasi kwamba hakuna chochote katika maisha ama katika kifo kitakachotutenganisha na ninyi. 4 Ninajisikia kwamba ninaweza kuwaambia lolote. Ninajivunia sana ninyi. Licha ya matatizo yote tuliyoyapata, nimetiwa moyo sana na ninajisikia kuwa mwenye furaha sana.
5 Tulipokuja Makedonia, hatukupumzika. Tulisumbuliwa kwa kila namna. Tulikuwa na vita kwa nje na hofu ndani yetu. 6 Lakini Mungu huwapa moyo wale wanaosumbuliwa, na kwa hakika na sisi alitupa moyo kwa kumleta Tito kwetu. 7 Ilikuwa furaha kumwona, lakini tulitiwa moyo zaidi tuliposikia jinsi nanyi mlivyomtia moyo yeye pia. Naye alitueleza kuwa mlikuwa na shauku ya kuniona mimi na kwamba mnayajutia yale mlivyofanya. Na akatueleza jinsi mlivyokuwa na shauku ya kusimama upande wangu. Niliposikia hili, nilifurahishwa sana.
8 Hata kama barua nilyowaandikieni iliwahuzunisha, sijutii kuiandika. Nafahamu kuwa barua ile iliwatia huzuni, ninasikitika kwa hilo. Lakini iliwapa huzuni kwa muda mfupi. 9 Sasa ninafurahi, si kwa sababu mlipata huzuni, bali kwa sababu huzuni yenu iliwasababisha mkaamua kubadilika. Hilo ndilo ambalo Mungu alilitaka, hivyo hatukuwaumiza kwa namna yo yote. 10 Aina ya huzuni ambayo Mungu anaitaka inawafanya watu waamue kubadili maisha yao. Hili linawaelekeza kwenye wokovu, nasi hatuwezi kulijutia hilo. Lakini huzuni dunia huleta mauti. 11 Mlikuwa na huzuni ambayo Mungu alitaka muwe nayo. Sasa mmetambua kile ambacho huzuni hiyo imewaletea: Imewafanya muwe makini sana. Imewafanya mtafute kuthibitisha kuwa hamkufanya makosa. Iliwafanya mkasirike na mwogope. Imewafanya muwe na shauku ya kuniona. Imewafanya muwe na azma ya kufanya kile nilichowaagiza. Imewafanya muwe na shauku ya kuona kuwa haki inatendeka. Mlithibitisha kuwa hamkuwa na hatia katika sehemu yoyote ya tatizo hilo. 12 Sababu kubwa ya kuandika barua ile haikuwa kwa sababu ya yule aliyefanya kosa au aliyeumia. Niliandika ili mtambue, mbele za Mungu, jinsi mnavyotujali sana sisi. 13 Na hili ndilo lililokuwa faraja kwetu sisi.
Tulitiwa moyo sana, lakini hasa tulifurahishwa kuona jinsi Tito alivyokuwa mwenye furaha. Ninyi nyote mlimfanya apate utulivu moyoni. 14 Nilijisifu juu yenu kwake Tito, na ninyi hamkuniaibisha. Siku zote tumewaambia ninyi kweli, na sasa yale tuliyomwambia Tito kwa habari zenu yamedhihirika kuwa ni kweli. 15 Na upendo wake kwenu una nguvu anapokumbuka kuwa mlikuwa tayari kutii. Mlimpokea kwa heshima na hofu. 16 Ninafuraha sana kwa kuwa ninaweza kuwaamini kikamilifu.
Msaada kwa Watu wa Mungu Katika Uyahudi
8 Na sasa, kaka na Dada zetu, tunataka kuwaambia kile ambacho neema ya Mungu imefanya katika makanisa ya makedonia. 2 Waamini hawa wamepitia katika masumbufu makubwa, na ni maskini sana. Lakini furaha yao kubwa iliwafanya kuwa wakarimu zaidi katika kutoa kwao. 3 Ninaweza kuwaambia kwamba walitoa kulingana na uwezo wao na hata zaidi ya uwezo wao. Hakuna mtu yeyote aliyewaambia kufanya hivyo. Hilo lilikuwa wazo lao. 4 Walituuliza tena na tena na walitusihi tuwaruhusu kushiriki katika huduma hii kwa ajili ya watu wa Mungu. 5 Na walitoa kwa namna ambayo sisi wenyewe hatukutegemea: kwanza walijitoa wenyewe kwa Mungu na kwetu kabla ya kutoa fedha zao. Hili ndilo Mungu anataka. 6 Kwa hiyo tulimwomba Tito awasaidie ninyi kuikamilisha kazi hii maalum ya kutoa. Tito ndiye aliyeianzisha kazi hii kwanza miongoni mwenu. 7 Ninyi ni matajiri kwa kila kitu; katika imani, katika uwezo wa kuzungumza, katika maarifa, katika utayari wa kusaidia kwa njia yo yote, na katika upendo mliojifunza kutoka kwetu. Hivyo sasa tunawataka muwe matajiri katika kazi hii ya kutoa pia.
8 Siwashurutishi ninyi kutoa, ila nataka niujaribu upendo wenu kuona ni wa kiasi gani kuwalinganisha na wengine ambao wamekuwa tayari na wana hiari ya kusaidia. 9 Mnaifahamu neema ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mnafahamu kuwa aliacha utajiri wake mbinguni na kufanyika maskini kwa ajili yenu. Aliacha kila kitu ili ninyi mbarikiwe kwa wingi zaidi.
10 Hili ndilo ninafikiri mnapaswa kufanya: mwaka jana mlikuwa wa kwanza kutaka kutoa, na mkawa wa kwanza kutoa. 11 Hivyo sasa ikamilisheni kazi mliyoianzisha. Kisha kutenda kwenu kutakuwa sawa na “kutaka” kwenu “kutenda”. Toeni kutokana na kile mlicho nacho. 12 Ikiwa mnataka kutoa, sadaka yenu itapokelewa. Sadaka yenu itahukumiwa kutokana na kile mlicho nacho, si kwa kile msichonacho. 13 Hatupendi muwe na mizigo wakati wengine wanastarehe. Tunataka kila kitu kiwe katika hali ya usawa. 14 Wakati huu mnavyo vingi na kuzidi na mnaweza kuwapa kila wanachohitaji. Kisha baadaye, watakapokuwa navyo vingi, wataweza kuwapa mnavyohitaji. Kisha kila mmoja atakuwa na mgao ulio sawa. 15 Kama Maandiko yanavyosema,
“Wale waliokusanya vingi hawakuwa na vingi zaidi,
na wale waliokusanya kidogo hawakuwa na vichache zaidi.”(E)
Tito na Wale Watakaosafiri Pamoja Naye
16 Namshukuru Mungu kwa sababu alimpa Tito upendo ule ule nilionao mimi kwenu. 17 Tito alikubali kufanya vile tulivyomwomba. Yeye mwenyewe alitamani sana kuja kwenu. 18 Tunamtuma Tito pamoja ndugu anayekubalika katika makanisa yote. Anasifiwa kwa sababu ya huduma yake ya Habari Njema. 19 Pia, alichaguliwa na makanisa kuambatana nasi tunapoleta sadaka hii. Tunafanya huduma hii kumpa Bwana heshima[d] na kuonesha kuwa tunapenda kusaidia.
20 Tunajitahidi kuwa waangalifu ili asiwepo mtu wa kutukosoa kwa namna ambavyo tunashugulika na sadaka hii kubwa. 21 Tunajaribu kutenda lililo jema. Tunataka kufanya kile ambacho Bwana anakubali kuwa sahihi na kile ambacho watu wanafikiri kuwa ni sahihi.
22 Pia, tunawatuma pamoja nao kaka yetu ambaye yuko tayari siku zote kutoa msaada. Amethibitisha hili kwetu mara nyingi na kwa njia nyingi. Na anataka kusaidia zaidi sasa kwa sababu ana imani zaidi nanyi.
23 Na sasa kuhusu Tito, yeye ni mshirika mwenzangu. Anafanya kazi pamoja nami kuwasaidia ninyi. Na kuhusu hawa kaka wawili wengine: wao wametumwa kutoka katika makanisa mengine, na wanaleta heshima kwa Kristo. 24 Hivyo waonesheni watu hawa kuwa mna upendo. Waonesheni kwa nini tunajisifia ninyi. Ndipo makanisa yote yatakapo tambua hili.
Msaada Kwa Ajili ya Watu wa Mungu
9 Kwa hakika sina haja ya kuwaandikia ninyi juu ya msaada huu kwa watu wa Mungu. 2 Ninajua kuwa mnataka kusaidia. Nimekuwa ninajisifu sana juu yenu kwa watu wa Makedonia. Niliwaeleza kwamba ninyi watu wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana. Na shauku yenu ya kutoa zaidi imewafanya watu walio wengi zaidi hapa wawe tayari kutoa pia. 3 Lakini ninawatuma kaka hawa kwenu. Sipendi kujisifia kwetu juu yenu kuthibitishwe kuwa ni batili. Nataka muwe tayari kama ambavyo nimesema kuwa mtakuwa tayari. 4 Ikiwa baadhi ya Wamakedonia walio wengi wangefuatana nami na kuwakuta hamko tayari, tutaaibika. Tutaibika kwa kuwa tulikuwa na uhakika sana juu yenu. Na ninyi mtaaibika pia! 5 Hivyo nikafikiri kuwa niwaombe ndugu hawa waje kwenu kabla ya mimi kuja. Wao watasaidia kufanya maandalizi mapema kwa ajili ya sadaka yenu yenye ukarimu mliyoahidi. Kisha sadaka hii itakuwa tayari tutakapokuja, na itaonekana kuwa baraka, na si kitu kidogo ambacho hamkutaka kutoa.
6 Kumbukeni hili: Yeye apandaye mbegu chache atapata mavuno kidogo. Lakini apandaye kwa wingi atapata mavuno mengi. 7 Kila mmoja wenu atoe kama alivyo kusudia kutoa katika moyo wake. Hampaswi kutoa ikiwa mnajisia huzuni kufanya hivyo au ikiwa mnasikia kulazimishwa kutoa. Mungu anawapenda wale wanaotoa kwa furaha. 8 Na Mungu anaweza kuwapeni baraka zaidi kuliko mlivyo katika kuhitaji kwenu, na daima mtakuwa na kila kitu mnachokihitaji. Mtakuwa na vingi vya ziada vya kutoa kwa kila kazi njema. 9 Kama Maandiko yanavyosema,
“Hawakuwa na choyo waliwapa maskini.
Mambo mema waliyoyafanya yatadumu millele.”(F)
10 Mungu ndiye huwapa mbegu wale wanaopanda, na anatoa mkate kuwa chakula. Na Mungu atawapeni “mbegu” na kuifanya ile mbegu ikue. Atazalisha mazao makubwa kutokana na wema wenu. 11 Mungu atawatajirisha katika namna zote ili mweze kutoa kwa uhuru kila mara. Na kutoa kwenu kulikosimamiwa na sisi kutawafanya watu wamshukuru Mungu.
12 Huduma mnayoitoa inawasaidia watu wa Mungu katika mahitaji yao, lakini si hayo tu itendayo. Inaleta pia shukrani nyingi zaidi na zaidi kwa Mungu. 13 Huduma hii ni uthibitisho wa imani yenu, na watu watamsifu Mungu kwa sababu kwa uhuru mlitoa mkawapa sehemu pamoja na watu wengine pia. Watamsifu Mungu kwa sababu wanaona jinsi mnavyoifuata injili ya Yesu Kristo ambayo mliipokea kwa wazi kabisa. 14 Na wanapoomba kwa ajili yenu, watatamani wangekuwa pamoja nanyi. Watajisikia hivi kwa sababu ya neema ya ajabu aliyowapa Mungu. 15 Mungu apewe shukrani kwa kipawa chake ambacho ni ajabu sana kukielezea.
© 2017 Bible League International