Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
2 Wakorintho 1-4

Salamu kutoka kwa Paulo, Mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alitaka. Na Timotheo ndugu yetu katika Kristo.

Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho na kwa watakatifu wote wa Mungu walio jimbo lote la Akaya.

Neema na Amani iwe kwenu kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Paulo Anamshukuru Mungu

Sifa na zimwendee Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni baba aliyejaa rehema, Mungu aliye mwingi wa faraja. Hutufariji kila wakati tunapokuwa katika hali ya matatizo ili wengine wawapo katika matatizo, tuweze kuwafariji kwa namna ile ile ambayo Mungu ametufariji sisi. Twashiriki katika mateso mengi ya Kristo. Na kwa namna hiyo hiyo, faraja nyingi hutujia kwa njia ya Kristo. Ikiwa tuko katika mateso, tuko kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu. Na ikiwa tunafarijika, ni kwa sababu tuweze kuwafariji ninyi. Hili huwasaidia katika kuyakubali mateso yale yale tunayopata kwa uvumilivu. Tumaini letu kwenu liko imara. Tunafahamu kuwa mnashiriki katika mateso yetu. Hivyo tunafahamu pia kuwa mnashiriki katika faraja yetu pia.

Ndugu zangu, tunapenda mfahamu juu ya mateso tuliyoyapata hapa Asia. Tulikuwa na mzigo sana huko, ulikuwa mzito kuliko hata nguvu zetu. Hata tulipoteza tumaini la kuishi. Ukweli ni kuwa, ilionekana kana kwamba Mungu alikuwa anatuambia kuwa tunakwenda kufa. Lakini haya yalitokea ili tusizitumainie nguvu zetu bali tumtumainie Mungu, ambaye huwainua watu toka mautini. 10 Yeye alituokoa toka katika hatari hizi kubwa za mauti, na ataendelea kutuokoa. Twajisikia kuwa na hakika kuwa ataendelea kutuokoa. 11 Nanyi mnaweza kutusaidia kwa njia ya maombi. Ndipo watu wengi wataweza kumshukuru Mungu kwa ajili yetu; kwamba Mungu alitubariki kutokana na maombi yao mengi.

Mabadiliko katika Mipango ya Paulo

12 Hili ndilo tunalojivunia, na naweza kusema kwa dhamiri safi kwamba ni kweli: Katika kila kitu tulichofanya duniani, Mungu ametuwezesha kukifanya kwa moyo safi. Na hili ni kweli zaidi katika yale tuliyowatendea ninyi. Tulifanya hivyo kwa neema ya Mungu, si kwa hekima ambayo ulimwengu unayo. 13 Tunawaandikia mambo mnayoweza kusoma na kuyaelewa. Na nina matumaini kuwa mtayaelewa inavyopasa 14 kama ambavyo tayari mmekwisha kuyafahamu mambo mengi kuhusu sisi. Natumaini mtaelewa kuwa mnaweza kuona fahari juu yetu, kama nasi tutakavyoona fahari juu yenu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja.

15 Nilikuwa na uhakika sana juu ya haya yote. Ndiyo maana niliweka mpango wa kuwatembelea kwanza. Kisha mngebarakikwa mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nilipokuwa nikienda Makedonia na nilipokuwa ninarudi. Na nilipanga kuwaomba mniletee kutoka huko hadi Yudea chochote ambacho nilihitaji kwa ajili ya safari yangu. 17 Je! Mnadhani nilipanga mipango hii bila kufikiri? Au mnadhani ninafanya mipango kama vile dunia inavyofanya, lugha yetu kwenu si ndiyo na hapana kwa wakati mmoja.

18 Kama ambavyo kwa hakika mnaweza kumwamini Mungu, basi mnaweza kuamini kuwa lile tunalowaambia kamwe haliwezi kuwa ndiyo na hapana kwa pamoja. 19 Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, Yeye ambaye Sila, Timotheo, na mimi tuliwaeleza habari zake, hakutokea kuwa ni ndiyo na hapana kwa ahadi za Mungu. Kinyume chake ndiyo ya Mungu imethibitika daima katika Kristo kuwa ni ndiyo. 20 Ndiyo kwa ahadi zote za Mungu katika Kristo. Na hii ndiyo maana twasema “Amina” Katika Kristo kwa utukufu wa Mungu. 21 Na Mungu ndiye anayewafanya ninyi na sisi kuwa imara katika Kristo. Mungu pia ndiye aliyetuchagua kwa ajili ya kazi yake.[b] 22 Aliweka alama yake juu yetu ili kuonesha kuwa tu mali yake. Ndiyo, amemweka roho wake ndani ya mioyo yetu kama malipo ya awali yanayotuhakikishia mambo yote atakayotupa.

23 Ninawaambia hili, na ninamwomba Mungu awe shahidi wangu kuwa ni la kweli: Sababu iliyonifanya nisirudi tena Korintho ni kuwa nilitaka niepuke kuwapa karipio lenye nguvu. 24 Sina maana ya kuwa tunataka kuitawala imani yenu. Ninyi mpo imara katika imani. Lakini tunatenda kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu wenyewe.

Hivyo niliamua moyoni mwangu mwenyewe kuwa sitafanya safari nyingine ya huzuni kuja kwenu. Ikiwa nitawafanya muwe na huzuni nani atanifanya niwe na furaha? Ni ninyi tu ndiyo mnaweza kunifanya niwe na furaha. Ni ninyi ambao niliwahuzunisha. Naliwaandikia barua ili kwamba nijapo kwenu nisihuzunishwe na wale ambao wanapaswa kunifanya niwe na furaha. Nilijisikia kuwa na hakika ya kuwa ninyi nyote mtashiriki furaha yangu. Nilipowaandikia barua ya kwanza, niliiandika macho yangu yakibubujika machozi mengi. Sikuandika ili kuwafanya muwe na huzuni, bali kuwafanya mjue kwa jinsi gani ninavyowapenda.

Msamehe Mtu Aliye Fanya Kosa

Mtu mmoja katika kusanyiko lenu amesababisha maumivu, ila si kwangu, bali amesababisha maumivu kwenu nyote kwa kiwango fulani. Nina maanisha amewakwaza nyote kwa namna fulani. (Sitaki ionekane kuwa mbaya sana kuliko ilivyo) Adhabu ambayo walio wengi miongoni mwa kusanyiko lenu walimpa inatosha. Lakini msameheni na kumtia moyo sasa. Hili litamsaidia asiwe na huzuni sana na asikate tamaa kabisa. Hivyo ninawasihi mwonesheni kuwa mnampenda. Hii ndiyo sababu niliandika ile barua. Nilitaka kuwapima na kuona ikiwa mna utii katika kila kitu. 10 Mkimsamehe mtu, ndipo nami husamehe pia. Na kile nilichosamehe, kama nilikuwa na jambo la kusamehe, nilisamehe kwa ajili yenu. Na Kristo akithibitisha. 11 Nilifanya hivi ili Shetani asipate ushindi wowote kutoka kwetu. Tunafahamu sote mipango yake ilivyo.

Mungu Anatupa Ushindi Dhidi ya Masumbufu

12 Nilikwenda Troa kuwaambia watu Habari Njema juu ya Kristo. Bwana alinipa fursa ya pekee kule. 13 Lakini sikuwa na amani kwa sababu sikumwona Tito pale. Hivyo niliaga na kwenda Makedonia.

14 Lakini ashukuriwe Mungu ambaye siku zote hutuongoza katika gwaride la ushindi la Kristo. Mungu anatutumia sisi kueneza ufahamu juu ya Kristo kila mahali kama vile marashi yanayonukia vizuri. 15 Maisha yetu ni sadaka ya harufu nzuri ya manukato ya Kristo inayotolewa kwa Mungu. Harufu nzuri ya sadaka hii huwaendea wale wanaokolewa na kwa wale wanaopotea. 16 Kwao wanaopotea, marashi haya yananukia kama mauti, na huwaletea kifo. Ila kwao wanaookolewa, ina harufu nzuri ya uzima, na inawaletea afya ya uzima. Kwa hiyo ni nani aliye bora kuifanya kazi hii? 17 Kwa hakika sio wale wanaozunguka wakiuuza ujumbe wa Mungu ili kupata faida! Lakini sisi hatufanyi hivyo. Kwa msaada wa Kristo tunaisema kweli ya Mungu kwa uaminifu, tukifahamu kuwa tunazungumza kwa ajili yake na mbele zake.

Watumishi wa Agano Jipya la Mungu

Je, mnadhani tunaanza kujitafutia sifa? Je, tunahitaji barua za utambulisho kuja kwenu au kutoka kwenu kama wengine? Hapana, ninyi wenyewe ni barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu. Inafahamika na kusomwa na watu wote. Mnaonyesha kuwa ninyi ni barua toka kwa Kristo aliyoituma kupitia sisi. Barua ambayo haikuandikwa kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai. Haikuandikwa katika mbao za mawe[c] lakini katika mioyo ya wanadamu.

Tunaweza kusema hili, kwa sababu Kristo ndiye anayetupa uhakika huu mbele za Mungu. Simaanishi kuwa tuna uwezo wa kufanya jambo lolote jema kwa uwezo wetu wenyewe. Mungu ndiye anatuwezesha kufanya yote tunayoyafanya. Ametuwezesha pia kuwa watumishi wa agano jipya lililotoka kwake kwenda kwa watu wake. Si agano la sheria zilizoandikwa, ni la Roho. Sheria zilizoandikwa huleta mauti, bali Roho huleta uzima.

Namna Nzuri ya Kumtumikia Mungu

Agano la kale lililoleta mauti, lililoandikwa kwenye mawe, lilikuja na utukufu wa Mungu. Kwa kweli, uso wa Musa ulikuwa unang'aa utukufu (Utukufu uliokuwa na ukomo) hata watu wa Israel hawakuweza kuendelea kumtazama usoni. Hivyo kwa hakika zaidi huduma ya agano jipya linalokuja kutoka kwa Roho anayeleta uzima lina utukufu zaidi. Maana yangu ni kuwa: utaratibu wa zamani wa kumtumikia Mungu uliwaweka watu katika hatia ya dhambi na kuwapa hukumu, lakini lilikuwa na utukufu. Hivyo kwa hakika utaratibu mpya wa kumtumikia Mungu unaowaweka huru watu kutoka hukumu una utukufu mkubwa zaidi. 10 Utaratibu wa zamani wa utumishi kwa Mungu ulikuwa na utukufu. Lakini kwa hakika unapoteza utukufu wake unapolinganishwa na utukufu mkubwa zaidi wa utaratibu mpya wa utumishi kwa Mungu. 11 Ikiwa utumishi ule wa muda ulikuja na utukufu, basi utumishi wa kudumu umekuja na utukufu mkubwa zaidi.

12 Kwa sababu tuna tumaini hili tunatenda kwa ujasiri mkubwa. 13 Hatuko kama Musa, ambaye alifunika uso wake ili watu wa Israel wasiendelee kuona kuwa utaratibu wa zamani wa kumtumikia Mungu ulikuwa unaelekea mwisho. 14 Lakini mioyo yao ilikuwa imefungwa. Na hata leo, watu wale wanapolisoma agano la kale, fahamu zao zinakuwa zimefunikwa. Ni kwa kupitia Yesu Kristo tu agano la kale linaondolewa. 15 Ndiyo, hata leo, wanaposoma sheria ya Musa, fahamu zao zimefunikwa. 16 Lakini, kama maandiko yanavyosema juu ya Musa, “Kila anapomgeukia Bwana, ufahamu wake unafunuliwa.” 17 Katika maandiko hayo Bwana ni Roho, na palipo na Roho wa Bwana, pana uhuru. 18 Na sura zetu hazikufunikwa. Sote tunaendelea kuutazama utukufu wa Bwana, na tunabadilishwa na kufanana na mfano huo huo tunaouona. Badiliko hili linatuletea utukufu zaidi na zaidi, na linatoka kwa Bwana, ambaye ni Roho.

Hazina ya kiroho katika Vyungu vya Udongo

Mungu, kwa rehema zake, alitupa sisi huduma hii ili tuifanye, hivyo hatukati tamaa. Lakini tumekataa mambo ya aibu ya siri. Hatumdanganyi mtu yeyote, na hatuyabadilii mafundisho ya Mungu. Tunaifundisha kweli wazi wazi. Na hivi ndivyo watu wanaweza kutambua mioyoni mwao sisi ni watu wa namna gani mbele za Mungu. Habari Njema tunazowahubiri watu hazijafichika kwa yeyote isipokuwa kwa waliopotea. Mtawala[d] wa dunia hii amezitia giza akili za wasioamini. Hawawezi kuona nuru ya Habari Njema; ujumbe juu ya uungu wa Kristo, taswira halisi ya Mungu. Hatuwaambii watu habari zetu wenyewe. Lakini tunawaambia habari za Kristo Yesu kuwa ni Bwana, na tunawaambia kuwa sisi ni watumwa wenu kwa ajili ya Yesu. Kuna wakati Mungu alisema, “Na nuru ing'ae gizani”[e] na huyu ni Mungu yule yule anayesababisha nuru ing'ae katika mioyo yetu ili tutambue utukufu wa uungu wake mkuu unaongaa katika sura ya Kristo.

Tuna hazina hii kutoka kwa Mungu, lakini sisi ni kama vyombo vya udongo tu vinavyobeba hazina. Hii ni kuonesha kuwa nguvu ya kustaajabisha tuliyo nayo inatoka kwa Mungu, si kwetu. Tunasumbuliwa kila upande, lakini hatushindwi. Mara kwa mara hatujui tufanye nini, lakini hatukati tamaa. Tunateswa, lakini Mungu hatuachi. Tunaangushwa chini wa nyakati zingine, laki hatuangamizwi. 10 Hivyo tunashiriki kifo cha Yesu katika miili yetu kila wakati, lakini haya yanatokea ili uzima wa Yesu udhihirishwe katika miili yetu. 11 Tuko hai, lakini kwa ajili ya Yesu tupo katika hatari ya kifo kila wakati, ili kwamba uzima wa Yesu udhihirishwe katika miili yetu ya kufa. 12 Kwa hiyo kifo kinafanya kazi ndani yetu, lakini matokeo yake ni kwamba uzima unafanya kazi ndani yenu.

13 Maandiko yanasema, “Niliamini, hivyo nikasema.”(A) Tuna Roho huyo huyo anayetupa imani kama hiyo. Tunaamini, na hivyo tunasema pia. 14 Mungu alimfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu, nasi tunajua kuwa atatufufua pamoja na Yesu. Mungu atatukusanya pamoja nanyi, na tutasimama mbele zake. 15 Mambo yote haya ni kwa ajili yenu. Na hivyo neema ya Mungu inatolewa kwa watu wengi zaidi na zaidi. Hili litaleta shukrani nyingi zaidi na utukufu kwa Mungu.

Kuishi kwa Imani

16 Hii ndiyo sababu hatukati tamaa. Miili yetu inazidi kuzeeka na kuchoka, lakini roho zetu ndani zinafanywa upya kila siku. 17 Tuna masumbufu, lakini ni madogo na ni ya muda mfupi. Na masumbufu haya yanatusaidia kuupata utukufu wa milele ulio mkuu kuliko masumbufu yetu. 18 Hivyo twafikiri juu ya mambo tusiyoweza kuyaona, si tunayoona. Tunayoyaona ni ya kitambo tu, na yale tusiyoyaona yanadumu milele.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International