Beginning
Haki Ambazo Paulo Hajazitumia
9 Mnajua kuwa mimi ni mtu niliye huru. Mnajua kuwa mimi ni mtume na kwamba nilimwona Yesu Bwana wetu. Na ninyi ni kielelezo cha kazi yangu katika Bwana. 2 Wengine wanaweza wasikubali kuwa mimi ni mtume, lakini hakika ninyi mnakubali. Ninyi ni uthibitisho kuwa mimi ni mtume wa Bwana.
3 Ninataka kuwajibu baadhi ya watu wanaotaka kunichunguza. 4 Je, hatuna haki ya kula na kunywa? 5 Je, hatuna haki ya kusafiri pamoja na mke aliye mwamini? Mitume wengine wote, wadogo zake Bwana na Petro hufanya hivi. 6 Na je, ni mimi na Barnaba tu ndiyo ambao ni lazima tufanya kazi ili tupate kipato cha kutuwezesha kuishi? 7 Ni askari gani aendaye vitani kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi la kondoo na hanywi maziwa?
8 Lakini nina mifano mingi kutoka katika maisha ya kila siku inayosisitiza hoja yangu. Sheria ya Mungu inasema vivyo hivyo pia. 9 Ndiyo, imeandikwa katika Sheria ya Musa kuwa; “Mnyama wa kazi anapotumika kupura nafaka, usimzuie kula nafaka.”(A) Je, Mungu aliposema hivi, alikuwa anawawazia wanyama pekee? Hapana. 10 Hakika Mungu alizungumza kuhusu sisi. Ndiyo, iliandikwa kwa ajili yetu. Wote wawili, anayelima na anayepura nafaka, wana haki ya kupata nafaka kutokana na kazi yao. 11 Ikiwa tulipanda mbegu ya kiroho mioyoni mwenu, je, hatustahili kupata vitu kwa ajili ya maisha haya kutoka kwenu? 12 Ikiwa wengine wana haki ya kupata vitu kutoka kwenu, hakika hata sisi tuna haki pia. Lakini hatuitumii haki hii. Tunavumilia katika hali zote ili tusimfanye mtu yeyote akaacha kuitii Habari Njema ya Kristo. 13 Hakika mnajua ya kuwa wanaotumika Hekaluni hula chakula kutoka Hekaluni. Na wale wanaotumika madhabahuni hupata sehemu ya yale yanayotolewa madhabahuni. 14 Vivyo hivyo kwa wale wenye kazi ya kuhubiri Injili. Bwana ameamuru kuwa nao wataishi kutokana na kazi hiyo.
15 Lakini sijatumia haki hizi, na si kwamba ninataka kitu chochote kutoka kwenu. Ijapokuwa ninaandika hivi hilo si lengo langu. Ni bora nife kuliko mtu yeyote kuchukua kutoka kwangu kitu ninachojivunia. 16 Sijivuni kwa sababu ya kazi yangu ya kuhubiri Habari Njema kwa sababu ni wajibu wangu ambao ni lazima nifanye; ole wangu nisipowahubiri watu Habari Njema. 17 Ikiwa ningehubiri kwa sababu ya utashi kwangu, ningestahili kulipwa. Lakini sikuchagua kufanya kazi hii. Ni lazima nihubiri Habari Njema. Hivyo ninafanya kazi niliyokabidhiwa. 18 Sasa, kwa kufanya kazi hii ninapata nini? Thawabu yangu, ni kuwa ninapowahubiri watu Habari Njema, ninawapa bure na sizitumii haki zinazoambatana na kufanya kazi hii.
19 Niko huru. Similikiwi na mtu yeyote, lakini ninakuwa mtumwa ili watu wengi waokoke. 20 Kwa Wayahudi nilienenda kama Myahudi ili nisaidie Wayahudi wengi waokolewe. Sitawaliwi na sheria, lakini kwa wanaotawaliwa na sheria nilikuwa kama ninayetawaliwa na sheria. Nilifanya hivi kuwasaidia wanaotawaliwa na sheria, ili waokoke. 21 Kwa wasio na sheria nilikuwa kama nisiye na sheria, ili niwasaidie wasio na sheria kuokoka. Mimi si kama mtu asiye na Sheria ya Mungu, ninatawaliwa na sheria ya Kristo. 22 Kwa waliodhaifu, nilikuwa dhaifu ili niwasaidie kuokoka. Nilifanyika kila kitu kwa watu wote ili nifanye kila kinachowezekana niweze kuwasaidia watu waokolewe. 23 Ninafanya kila ninachoweza ili Habari Njema ijulikane na niweze kushiriki katika Habari zake.
24 Mnajua kuwa katika riadha, wanariadha wengi hukimbia, lakini mmoja tu hupata zawadi. Hivyo kimbieni hivyo. Kimbieni ili mshinde! 25 Wote wanaoshiriki katika mchezo hufanya mazoezi kwa bidii ili waweze kushinda na kupata zawadi. Lakini zawadi wanazopata hazidumu milele. Lakini zawadi yetu ni ile inayodumu milele. 26 Hivyo ninakimbia kama mtu mwenye malengo. Ninapigana ngumi kama mpiganaji anayepiga kitu, si kama anayepiga hewa. 27 Ninaudhibiti mwili wangu kikamilifu na kuufanya unitiii kwa kila jambo ninalotaka kutenda. Ninafanya hivi ili mimi binafsi nisiikose thawabu baada ya kuwahubiri wengine Habari Njema.
Tahadhari Kutokana na Yaliyotokea Zamani
10 Ndugu zangu, sitaki mshindwe kutambua umuhimu wa kile kilichowatokea baba zetu waliokuwa na Musa. Walifunikwa na wingu,[a] na walipita katika bahari. 2 Walibatizwa[b] wote katika Musa katika wingu na katika bahari. 3 Wote walikula chakula kilichotolewa na Roho wa Mungu, 4 na wote walikunywa kinywaji kinachotolewa na Roho wa Mungu. Kinywaji walichokunywa kilitoka katika mwamba wa roho uliokuwa pamoja nao, na mwamba huo ni Kristo. 5 Lakini Mungu hakupendezwa na wengi wao, na hivyo waliangamizwa jangwani.
6 Mambo haya yaliyotokea ni tahadhali kwa ajili yetu. Mifano hii itufanye tuache kutamani maovu kama baadhi yao walivyofanya. 7 Msiabudu sanamu kama ambavyo baadhi yao walifanya. Na kama Maandiko yanavyosema, “Waliketi chini kula na kunywa kisha wakasimama kucheza.”(B) 8 Tusifanye dhambi ya uzinzi kama baadhi yao walivyofanya na watu ishirini na tatu elfu miongoni mwao wakafa. 9 Tusimjaribu Kristo[c] kama vile baadhi yao walivyofanya. Kwa sababu hiyo, waliuawa na nyoka. 10 Na msinung'unike kama baadhi yao walivyofanya na wakauawa na malaika anayeangamiza.
11 Mambo yaliyowapata wale watu ni mifano na yaliandikwa ili kututahadharisha sisi tunaoishi nyakati hizi za mwisho. 12 Hivyo kila anayedhani kuwa yuko imara katika imani yake, basi awe mwangalifu asianguke. 13 Majaribu mliyonayo ni yale yale waliyonayo watu wote. Lakini Mungu ni mwaminifu maana hataacha mjaribiwe kwa kiwango msichoweza kustahimili. Mnapojaribiwa, Mungu atawapa mlango wa kutoka katika jaribu hilo. Ndipo mtaweza kustahimili.
14 Hivyo rafiki zangu wapenzi, zikimbieni ibada za sanamu. 15 Ninyi ni watu wenye akili. Upimeni ukweli wa haya ninayosema sasa. 16 Kikombe cha baraka[d] tunachokitolea shukrani ni ushirika wa sadaka ya damu ya Kristo, sawa? Na mkate ule tunaomega, ni ushirika wa mwili wa Kristo, sawa? 17 Kuna mkate mmoja, nasi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa kuwa tunashiriki katika mkate huo mmoja.
18 Na fikirini kuhusu Waisraeli wanavyofanya. Wanapokula sadaka, wanaunganishwa pamoja kwa kugawana kile kilichotolewa kwenye madhabahu. 19 Je, ninataka kuthibitisha kitu gani? Je, ninasema kwamba nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu ni hakika najisi kwa kiasi fulani? Je, ninasema kwamba sanamu ni mungu wa kweli? Hapana. 20 Lakini ninasema kuwa chakula kinapotolewa sadaka kwa sanamu, ni sadaka kwa mashetani, siyo kwa Mungu. Nami sitaki ninyi muungane na hao wengine katika kuyaabudu mashetani. 21 Hamwezi kukinywea kikombe cha Bwana na kisha mkakinywea kiombe kinachotukuza mashetani. Hamwezi kushiriki kula chakula na kunywa pamoja kwenye meza ya Bwana kisha mkaenda kushiriki kula chakula na kunywa pamoja kwenye meza inayotukuza mashetani. 22 Kufanya hivyo kunamtia wivu Bwana.[e] Je, mnafikiri tunaweza kujaribu kumfanya Bwana apate wivu? Mnadhani tuna nguvu kuliko yeye?
Utumieni Uhuru Wenu Kumtukuza Mungu
23 Mnasema “Vitu vyote vimeruhusiwa.” Lakini si vitu vyote vinafaa. “Vitu vyote vimeruhusiwa.” Lakini vitu vingine havisaidii katika kuliimarisha kanisa. 24 Jitahidi kuwafanyia mema wengine badala ya kufanya mema kwa ajili yako wewe wenyewe.
25 Kuleni chakula chochote kinachouzwa sokoni. Msiulize maswali ili kutafuta kujua kama ni sahihi ama la kwako kukila. 26 Mnaweza kula chakula hicho, “Kwa sababu dunia na kila kitu kilichomo ndani yake ni vya Bwana.”(C)
27 Asiye mwamini anaweza kuwaalika kula chakula. Ikiwa mtakwenda, basi mle chochote kitakachowekwa mbele yenu. Msiulize ulize maswali. 28 Lakini mtu akiwaambia, “Chakula hicho kilitolewa sadaka katika hekalu la miungu,” basi msile. Kwa sababu kinaweza kumwathiri mtu na uhusiano wake na Mungu. 29 Na hapa sizungumzii kuhusu uhusiano wenu na Mungu, bali uhusiano wa mtu yule aliyewaambia na Mungu. Kwa nini uhuru wangu mwenyewe uhukumiwe na mawazo ya mtu mwingine? 30 Ikiwa mimi nitakula chakula nikiwa na shukrani, kwa nini basi nisikosolewa kwa sababu ya kitu ambacho kwa hicho ninamshukuru Mungu?
31 Ninachosema ni kwamba: ukila, au ukinywa, au ukifanya jambo lolote, lifanye kwa ajili ya utukufu wa Mungu. 32 Kamwe usifanye jambo lolote litakalowafanya watu wengine kutenda mabaya, iwe ni Wayahudi, wasio Wayahudi au mtu yeyote katika kanisa la Mungu. 33 Ninafanya vivyo hivyo. Ninajitahidi kwa njia yeyote ile kumpendeza kila mtu. Mimi sijaribu kutenda yaliyo mema kwangu. Ninajaribu kutenda yale yaliyo na manufaa kwa watu wengine ili waweze kuokoka.
11 Fuateni mfano wangu, kama ninavyoufuata mfano wa Kristo.
Kanuni kwa Ajili ya Mikutano Yenu
2 Nawasifu kwa sababu daima mnanikumbuka mimi na kuyafuata mafundisho niliyowapa. 3 Lakini ninataka mwelewe kuwa kichwa cha kila mwanaume ni Kristo. Na Kichwa cha mwanamke ni mwanaume.[f] Na Kichwa cha Kristo ni Mungu.
4 Kila mwanaume anayeomba au kutabiri akiwa amefunika kichwa chake, anakiaibisha kichwa chake. 5 Lakini kila mwanamke anayeomba au kutabiri pasipo kufunika kichwa chake anakiaibisha kichwa chake. Kwa jinsi hiyo anakuwa sawa na mwanamke yule aliyenyoa nywele zake. 6 Ikiwa mwanamke hatafunika kichwa chake, basi na azinyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukata nywele zake au kuzinyoa kichwani mwake. Hivyo anapaswa kufunika kichwa chake.
7 Lakini mwanaume hapaswi kufunika kichwa chake, kwa sababu ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanaume. 8 Mwanaume hakutoka kwa mwanamke bali mwanamke ndiye aliyetoka kwa mwanaume. 9 Na mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke lakini mwanamke ndiye aliumbwa kwa ajili ya mwanaume. 10 Hivyo, kutokana na nilivyosema, mwanamke anapaswa kukitawala kichwa chake kwa kukifunika anapoomba au anapotabiri. Pia, anapaswa kufanya hivi kwa sababu ya malaika.[g]
11 Lakini katika Bwana mwanamke anamhitaji mwanaume, na mwanaume anamhitaji mwanamke. 12 Hii ni kweli kwa sababu mwanamke alitoka kwa mwanaume, lakini pia mwanaume anazaliwa na mwanamke. Hakika, kila kitu kinatoka kwa Mungu.
13 Amueni hili ninyi wenyewe: Je, ni sahihi mwanamke kumwomba Mungu akiwa hajafunika kichwa chake? 14 Je, si hata hali ya asili inatufundisha kuwa ni aibu kwa mwanaume kuwa na nywele ndefu? 15 Lakini kuwa na nywele ndefu ni heshima kwa mwanamke. Mwanamke amepewa nywele ndefu ili kufunika kichwa chake. 16 Baadhi ya watu wanaweza kuanzisha mabishano kuhusiana na yale niliyosema. Lakini desturi ambayo sisi na makanisa ya Mungu yanafuata ni hii: ya kwamba wanawake wanaweza kuomba na kutabiri ujumbe kutoka kwa Mungu, vichwa vyao vikiwa vimefunikwa.
Chakula cha Bwana
17 Siwasifu kwa mambo ninayowaambia sasa. Mikutano yenu inawaumiza kuliko inavyowasaidia. 18 Kwanza, nimesikia kuwa mnapokutana kama kanisa mmegawanyika. Hili si gumu kuliamini 19 kwa sababu ya fikra zenu kwamba imewapasa kuwa na makundi tofauti ili kuonesha ni akina nani walio waamini wa kweli!
20 Mnapokusanyika, hakika hamli chakula cha Bwana.[h] 21 Ninasema hivi kwa sababu mnapokula, kila mmoja anakula na kumaliza chakula chake pasipo kula na wengine. Baadhi ya watu hawapati chakula cha kutosha, ama kinywaji cha kutosha na hivyo kubaki na njaa na kiu, ambapo wengine wanakula na kunywa zaidi hata kulewa.[i] 22 Mnaweza kula na kunywa katika nyumba zenu. Inaonekana kuwa mnadhani kanisa la Mungu si muhimu. Mnawatahayarisha wasio na kitu. Niseme nini? Je, niwasifu? Hapana, siwezi kuwasifu katika hili.
23 Mafundisho niliyowafundisha ni yale yale niliyopokea kutoka kwa Bwana, ya kwamba usiku ule ambao Bwana Yesu alikamatwa, aliuchukua mkate 24 na akashukuru. Kisha akaumega na kusema, “Huu ni mwili wangu; ni kwa ajili yenu. Uleni mkate huu kwa ajili ya kunikumbuka mimi.” 25 Kwa namna hiyo hiyo, baada ya wote kula, Yesu alichukua kikombe cha divai na akasema, “Divai hii inawakilisha agano jipya ambalo Mungu anafanya na watu wake, linaloanza kwa sadaka ya damu yangu. Kila mnywapo divai hii, fanyeni hivi kwa ajili ya kunikumbuka mimi.” 26 Hii inamaanisha kuwa kila mnapokula mkate huu na kunywa kikombe hiki, mnawaambia wengine kuhusu kifo cha Bwana mpaka atakaporudi.
27 Hivyo, ukiula mkate na kukinywea kikombe cha Bwana isivyostahili, unautendea dhambi mwili na damu ya Bwana. 28 Unapaswa kujichunguza mwenendo wako kabla ya kula mkate na kunywa kikombe. 29 Ukila na kunywa bila kuwajali wale ambao ndiyo mwili wa Bwana, kula na kunywa kwako kutasababisha uhukumiwe kuwa mwenye hatia. 30 Ndiyo sababu watu wengi katika kanisa lenu ni wagonjwa na dhaifu, na wengi wameshakufa. 31 Lakini ikiwa tungejichunguza kwa usahihi, Mungu asingetuhukumu. 32 Lakini Bwana anapotuhukumu, anatuadhibu ili kutuonesha njia sahihi. Hufanya hivi ili tusishutumiwe kuwa wakosa na tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
33 Hivyo ndugu zangu, mnapokusanyika pamoja ili mle, subirianeni na mkaribishane kwa moyo wa upendo. 34 Ikiwa mtu yeyote anawaza kuhusu njaa yake mwenyewe, basi akae nyumbani kwake na ale huko! Fanyeni hivi ili kukutanika kwenu kusilete hukumu ya Mungu juu yenu. Nitakapokuja nitawaambia nini cha kufanya kuhusu masuala mengine.
© 2017 Bible League International