Beginning
Msiwaruhusu Watu Wenu Waishi Katika Dhambi
5 Sitaki kuyaamini yale ninayosikia, ya kwamba kuna uzinzi katikati yenu. Na ni aina mbaya ya uzinzi ambayo hata wasiomwamini Mungu wetu hawauruhusu. Watu wanasema kuwa huko kwenu kuna mtu anayetenda dhambi ya zinaa na mke wa baba yake. 2 Na mna kiburi! Mngepaswa kuwa na huzuni badala yake. Na mtu aliyetenda dhambi hiyo ilipaswa kuwa amefukuzwa kutoka katika kundi lenu. 3 Siwezi kuwa hapo pamoja nanyi ana kwa ana, lakini niko pamoja nanyi katika roho. Na nimekwisha mhukumu mtu aliyetenda hii kama ambavyo ningemhukumu ikiwa ningekuwa hapo. 4 Nanyi pia mnapaswa kufanya vivyo hivyo. Kusanyikeni pamoja katika jina la Bwana wetu Yesu. Nitakuwa pamoja nanyi katika roho, na nguvu ya Bwana Yesu itakuwa pamoja nanyi. 5 Mtoeni mtu huyu kwa Shetani ili tabia yake ya kujisifu[a] iangamizwe lakini mtu mwenyewe na kanisa, lilojazwa Roho, liweze kuokolewa siku Bwana atakaporudi.
6 Kujisifu kwenu si kuzuri. Mnajua msemo unaosema, “Chachu kidogo huchahua donge zima.” 7 Ondoeni chachu ya zamani ili muwe donge jipya. Ninyi kwa hakika ni mkate usio na chachu, mkate wa Pasaka,[b] Ndiyo, Kristo aliye Mwanakondoo wetu wa Pasaka[c] amekwisha usawa. 8 Hivyo na tuule mlo wetu wa Pasaka, lakini si pamoja na mkate wenye chachu ya zamani, yaani dhambi na matendo mabaya. Lakini tule mkate usio na chachu. Huu ni mkate wenye ukweli na chachu njema.
9 Katika barua yangu niliwaandikia kuwa msishirikiane na wazinzi. 10 Lakini sikuwa na maana ya watu wa ulimwengu huu. La sivyo ingewalazimu kuhama katika ulimwengu huu ili mweze kujitenga na wazinzi au walio walafi na waongo, au wale wanaoabudu sanamu. 11 Nilikuwa na maana kuwa msishirikiane na mtu yeyote yule anayedai kuwa anaamini lakini anaendelea kuishi katika dhambi. Usimkaribishe nyumbani kwa chakula kaka ama dada aliye mzinzi, mlafi, anayeabudu sanamu, mtukanaji, mlevi au mwongo.[d]
12-13 Si kazi yangu kuwahukumu wasio sehemu ya kundi la waamini. Mungu atawahukumu, lakini ni lazima mwahukumu wale walio katika kundi lenu. Maandiko yanasema, “Mwondoe mwovu katika kundi lako.”(A)
Kutatua Migogoro Miongoni Mwa Waamini
6 Kwa nini mnakwenda kwenye mahakama za kisheria mmoja wenu anapokuwa na shauri dhidi ya mwingine aliye miongoni mwenu? Mnajua ya kwamba mahakimu wa aina hiyo hawawezi kutegemewa kuamua kwa haki iliyo ya kweli. Sasa kwa nini mnawaruhusu wawaamulie aliye na haki? Kwa nini msiwaruhusu watakatifu wa Mungu waamue ni nani aliye na haki? 2 Hamjui kuwa watakatifu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Hivyo, ikiwa mtauhukumu ulimwengu, hakika mnaweza kutatua mashauri kama hayo miongoni mwenu. 3 Hakika mnajua kuwa tutawahukumu malaika. Kwa kuwa hiyo ni kweli basi hakika tunaweza kuhukumu masuala ya kawaida ya maisha. 4 Sasa, ikiwa mna masuala kama haya ya kawaida ya maisha yanayotakiwa kuamuliwa, kwa nini mnayapeleka kwa wasio waamini? Hao ambao hawana umuhimu wo wote kwenu? 5 Ninasema hivi ili kuwatahayarisha. Nina uhakika yupo mwenye hekima miongoni mwa waamini katika kanisa lenu anayeweza kutatua mgogoro kati ya waamini wawili. 6 Lakini sasa mwamini mmoja anamshtaki mwamini mwenzake na mnaruhusu watu wasio waamini wawaamulie!
7 Ule ukweli kuwa mnayo mashitaka baina yenu ninyi kwa ninyi tayari ni uthibitisho wa kushindwa kwenu kabisa. Ingekuwa bora kwenu kustahimili yasiyo haki ama kulaghaiwa. 8 Lakini ninyi ndiyo mnaotenda mabaya kwa kudanganya. Na mnawafanyia hivi ndugu zenu katika Kristo!
9 Msijidanganye. Hamjui ya kuwa wanaowatendea mabaya hawana nafasi katika ufalme wa Mungu. Ninasema kuhusu wazinzi, wanaoamini miungu wa uongo, wasio waaminifu katika ndoa, nao wanaolawitiana.[e] 10 Pia wezi, walafi, walevi, watukanaji, au waongo wanaowadanganya wengine ili wawaibie hawatakuwa na sehemu katika ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa hivyo huko nyuma. Lakini mlisafishwa mkawa safi, mkafanywa kuwa watakatifu na mkahesabiwa haki na Mungu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.
Miili Yenu Itumike kwa Ajili ya Utukufu wa Mungu
12 Mtu mmoja anaweza kusema, “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote.” Nami ninawaambia ya kuwa si vitu vyote vilivyo na manufaa. Hata kama ni kweli kuwa “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote,” Sitaruhusu kitu chochote kinitawale kama vile ni mtumwa. 13 Mmoja wenu anasema, “Chakula ni kwa ajili ya tumbo na tumbo ni kwa ajili ya chakula, na Mungu ataviteketeza vyote.” Hiyo ni dhahiri, lakini mwili si kwa ajili ya zinaa, bali kwa ajili ya Bwana, na Bwana ni kwa ajili ya mwili. 14 Na Mungu ataifufua pia miili yetu kutoka kwa wafu kwa nguvu yake, kama alivyomfufua Bwana Yesu. 15 Hakika mnajua kuwa miili yenu ni sehemu ya Kristo mwenyewe. Hivyo sitakiwi kamwe kuchukua sehemu ya Kristo na kuiunganisha na kahaba! 16 Maandiko yanasema, “Watu wawili watakuwa mmoja.”(B) Hivyo mnapaswa kujua kuwa kila aliyeungana na kahaba, amekuwa mwili mmoja na kahaba. 17 Lakini aliyeungana na Bwana, yu mmoja naye katika roho.
18 Hivyo ikimbieni dhambi ya uzinzi. Mnasema kuwa, “Kila dhambi ni kitu kilichomo katika akili tu haihusiki na mwili.” Lakini ninawaambia, anayetenda dhambi ya uzinzi anautendea dhambi mwili wake mwenyewe. 19 Nina uhakika mnajua kuwa mwili wenu ni hekalu[f] kwa ajili ya Roho Mtakatifu mliyepewa na Mungu na Roho Mtakatifu anaishi ndani yenu. Hamjimiliki ninyi wenyewe. 20 Mungu alilipa gharama kubwa ili awamiliki. Hivyo mtukuzeni Yeye kwa kutumia miili yenu.
Kuhusu Ndoa
7 Sasa nitazungumza kuhusu mambo yale mliyoniandikia. Mliuliza ikiwa ni bora mwanaume asimguse mwanamke kabisa. 2 Lakini dhambi ya uzinzi ni ya hatari, hivyo kila mwanaume anapaswa kumfurahia mke wake, na kila mwanamke anapaswa kumfurahia mume wake. 3 Mume anapaswa kumtosheleza mkewe, vivyo hivyo mke amtosheleze mume wake. 4 Mke hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mume ana mamlaka juu ya mwili wa mkewe. Mume hana mamlaka kabisa juu ya mwili wake, bali mke ana mamlaka juu ya mwili wa mumewe. 5 Msinyimane miili yenu. Lakini mnaweza kukubaliana kutojamiiana kwa muda ili mtumie muda huo katika maombi. Kisha mkutane tena ili Shetani asiwajaribu kutokana na kushindwa kujizuia tamaa zenu. 6 Ninasema hivi ili kuwaruhusu mtengane kwa muda tu. Lakini hii siyo amri. 7 Mimi ningependa kila mtu angekuwa kama mimi nilivyo. Lakini Mungu amempa kila mtu uwezo tofauti. Huwafanya wengine kuwa hivi na wengine kuwa vile.
8 Sasa kwa ajili ya wale ambao hawajaoa ama hawajaolewa na kwa ajili ya wajane ninawaambia ya kwamba ni vizuri mkae bila kuoa au kuolewa kama mimi. 9 Lakini ikiwa mtashindwa kudhibiti tamaa zenu, basi mwoe au muolewe. Ni vyema kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa.
10 Na sasa ninawaamuru wale walio katika ndoa. Si amri kutoka kwangu, lakini ndivyo Bwana aliamuru. Mke hapaswi kuondoka kwa mume wake. 11 Lakini ikiwa mke anaondoka, anapaswa kukaa bila kuolewa au arudi kwa mume wake. Na mume hapaswi kumtaliki mke wake.
12 Ushauri nilionao kwa wengine unatoka kwangu. Bwana hajatupa mafundisho mengine kuhusu hili. Ukiwa na mke asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. 13 Na kama una mume asiyeamini, usimtaliki ikiwa yuko radhi kuendelea kuishi pamoja nawe. 14 Mume asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mke wake anayeamini. Na mke asiyeamini ametengwa kwa ajili ya Bwana kupitia mume wake anayeamini. Ikiwa hii si sahihi basi watoto wenu wasingefaa kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Lakini sasa wametengwa kwa ajili yake.
15 Lakini mume au mke asiyemwamini akiamua kuondoka katika ndoa. Hili linapotokea, ndugu aliye katika Kristo anakuwa huru. Mungu aliwachagua ili muwe na maisha ya amani. 16 Inawezekana ninyi wake mtawaokoa waume zenu; nanyi waume mtawaokoa wake zenu kwani bado hamjui kitakachotokea baadaye.
Ishini Kama Mlivyokuwa Mungu Alivyowaita
17 Kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuishi katika namna ambayo Bwana Mungu amewapa, kuishi kama mlivyoishi Mungu alipowaita. Ninawaambia watu katika makanisa yote kufuata kanuni hii. 18 Mwanaume asibadili tohara yake ikiwa alikuwa ametahiriwa alipoitwa. Ikiwa hakuwa ametahiriwa alipoitwa, asitahiriwe. 19 Kutahiriwa au kutotahiriwa si muhimu. Kilicho muhimu ni kutii amri za Mungu. 20 Kila mmoja wenu awe katika hali aliyokuwa nayo Mungu alipomwita. 21 Usijisikie vibaya ikiwa ulipochaguliwa na Mungu ulikuwa mtumwa. Lakini ikiwa unaweza kujikomboa, basi fanya hivyo. 22 Kama ulikuwa mtumwa Bwana alipokuita, uko huru sasa katika Bwana. Wewe ni wa Bwana. Vivyo hivyo, kama ulikuwa huru ulipoitwa, wewe ni mtumwa wa Kristo sasa. 23 Mungu alilipa gharama kubwa kwa ajili yako, hivyo usiwe mtumwa kwa mtu yeyote tena. 24 Ndugu zangu, katika maisha yenu mapya pamoja na Mungu, kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuwa katika hali ya tohara kama alivyokuwa Mungu alipowaita.
Maswali Kuhusu Kuoa au Kuolewa
25 Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu watu ambao hawajaoa au kuolewa.[g] Sina amri kutoka kwa Bwana kuhusu hili, lakini haya ni maoni yangu. Na ninaweza kuaminiwa kwa sababu Bwana amenipa rehema. 26 Huu ni wakati mgumu. Hivyo nadhani ni vyema mtu akikaa kama alivyo. 27 Ikiwa umefungwa kwa mke, usijaribu kufunguliwa. Ikiwa hujaoa, usijaribu kuoa. 28 Lakini si dhambi ukiamua kuoa. Lakini waliooa watapata dhiki katika maisha haya, nami ninataka msiipitie dhiki hiyo.
29 Kaka zangu nina maana ya kuwa muda uliosalia ni mchache, wale waliooa waishi kama vile hawajaoa.[h] 30 Wale wanaolia wawe kama wasiolia, wenye furaha wawe kama hawana furaha na wale wanaonunua vitu wawe kama hawavimiliki vitu hivyo. 31 Vitumieni vitu vya ulimwengu pasipo kuviruhusu viwe vya muhimu kwenu. Hivi ndivyo mnapaswa kuishi, kwa sababu ulimwengu huu kwa namna ulivyo sasa, unapita.
32 Nataka msisumbuke. Mwanaume ambaye hajaoa hujishughulisha na kazi ya Bwana naye hujitahidi kumpendeza Bwana. 33 Lakini mwanaume aliyeoa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu, ili ampendeze mke wake. 34 Ni lazima afikirie mambo mawili; kumpendeza mke wake na kumpendeza Bwana. Mwanamke ambaye hajaolewa au msichana ambaye hajawahi kuolewa hujishughulisha na kazi ya Bwana. Hutaka kuutoa mwili na roho yake kikamilifu kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu ili ampendeze mume wake. 35 Ninasema hili ili niwasaidie. Si kuwawekea vikwazo, lakini ninataka mwishi katika njia sahihi. Na ninataka mjitoe kikamilifu kwa Bwana pasipo kuchukuliwa katika mambo mengine.
36 Mwanaume anaweza kudhani kuwa hamtendei haki mchumba wake. Mchumba wake huyo anaweza kuwa ameshapita umri mzuri wa kuolewa.[i] Hivyo mwanaume anaweza kujisikia kuwa anapaswa kumwoa mchumba wake huyo. Basi na afanye anachotaka. Si dhambi kwao wakioana. 37 Lakini mwanaume mwingine anaweza kuwa na uhakika akilini mwake ya kuwa hakuna haja ya ndoa, hivyo yuko huru kufanya anachotaka. Ikiwa ameamua moyoni mwake kutomwoa mchumba wake, anafanya jambo sahihi. 38 Hivyo mwanaume anayemwoa mchumba wake anafanya jambo jema, na mwanaume asiyeoa anafanya vyema zaidi.
39 Mwanamke anapaswa kuishi na mume wake kipindi chote mumewe anapokuwa hai. Lakini mume akifa, mwanamke anakuwa huru kuolewa na mwanaume yeyote. Lakini mwanaume huyo lazima awe yule wa Bwana. 40 Ikiwa atabaki kuwa mjane, atakuwa na furaha sana. Haya ni maoni yangu, na ninaamini yanatoka kwa Roho wa Mungu.
Kuhusu Vyakula Vinavyotolewa kwa Sanamu
8 Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu nyama iliyotolewa sadaka[j] kwa sanamu. Ni kweli kuwa “Sote tuna ujuzi”, kama mnavyosema. Lakini ujuzi huu unawajaza watu majivuno. Upendo ndiyo unaolisaidia kanisa kuwa imara. 2 Wale wanaodhani kuwa wanajua jambo fulani bado hawajui chochote kwa namna inavyopaswa. 3 Lakini Mungu anamjua mtu anayempenda.
4 Hivyo sasa vipi kuhusu kula nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu? Tunajua kuwa “sanamu si lolote katika ulimwengu” huu na tunajua kuwa “kuna Mungu mmoja tu”. 5 Baadhi ya watu husema kuwa kuna miungu wanaoishi mbinguni na miungu wengine huishi duniani. Hata kama kuna “miungu” na “mabwana” wanaoaminiwa na watu, hilo si muhimu kwetu. 6 Tuna Mungu mmoja tu, na ambaye ndiye Baba yetu. Vitu vyote vilitoka kwake nasi tunaishi kwa ajili yake. Na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo. Vitu vyote viliumbwa kupitia yeye, nasi tunaishi kwa ajili yake.
7 Lakini si watu wote wanaojua hili. Baadhi ya watu walikuwa na tabia ya kuabudu sanamu huko nyuma. Hivyo wanapokula nyama, bado wanahisi kuhukumiwa kana kwamba wanakula nyama iliyotolewa kwa sanamu. Hawana uhakika ikiwa ni sahihi kula nyama. 8 Lakini chakula hakitatuweka karibu na Mungu. Kukataa kula hakutufanyi tumpendeze kidogo Mungu wala kula hakutuweki karibu na Mungu.
9 Lakini iweni makini na uhuru wenu. Uhuru wa kula kitu unaweza kuwafanya walio na mashaka wakaanguka katika dhambi kwa kula vyakula hivyo. 10 Mnaelewa kuwa inaruhusiwa kula kitu chochote, hivyo unaweza kula hata katika hekalu la sanamu. Lakini hilo linaweza kumfanya mtu mwenye mashaka akaona kuwa kula chakula kama hicho ni kitendo cha kuabudu sanamu. 11 Hivyo ndugu huyu aliye dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, anaweza akaangamizwa kwa sababu ya uelewa wako ulio mzuri zaidi. 12 Unapomtenda dhambi kinyume cha ndugu zako walio katika Kristo kwa namna hii na unawaumiza kwa kuwafanya wafanye mambo wanayoyachukulia kuwa mabaya, nawe pia unamtenda dhambi Kristo. 13 Hivyo ikiwa chakula ninachokula kinamfanya mwamini mwingine kutenda dhambi, siwezi kula chakula hicho tena. Nitaacha kula chakula hicho ili nisimfanye ndugu yangu atende dhambi.
© 2017 Bible League International