Beginning
1 Salamu kutoka kwa Paulo. Mimi ni mtume kwa sababu Kristo Yesu[a] alinichagua. Alinichagua kwa sababu hivyo ndivyo Mungu alitaka. Naandika barua hii kwa msaada wa Sosthenesi[b] aliye kaka yetu katika Kristo.
2 Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, ninyi ambao mmefanywa watakatifu kwa sababu mmeunganishwa kwa Kristo Yesu. Mlichaguliwa kuwa watakatifu wa Mungu pamoja na watu wote kila mahali wanaomwamini Bwana[c] Yesu Kristo, Bwana wao na Bwana wetu.
3 Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.
Paulo Amshukuru Mungu
4 Ninamshukuru Mungu daima kwa sababu ya neema aliyowapa katika Kristo Yesu. 5 Ambaye kwa njia yake Mungu amewabariki sana kwa namna mbalimbali hata miongoni mwenu wapo watu wenye vipawa vya kuzungumza na wengine wana vipawa vya maarifa! 6 Hii ni kwa sababu yale tuliyowaambia kuhusu Kristo yamedhihirika kuwa kweli katikati yenu. 7 Na sasa mna karama zote mnapomsubiri Mungu audhihirishie ulimwengu jinsi Bwana wetu Yesu Kristo alivyo wa ajabu. 8 Ataendelea kuwatia nguvu na hakuna atakayeweza kuwashtaki mpaka siku ya mwisho Bwana wetu Yesu atakaporudi. 9 Mungu ni mwaminifu. Na ndiye aliyewachagua ninyi ili mshiriki uzima pamoja na Mwanaye, Yesu Kristo Bwana wetu.
Acheni Mabishano Miongoni Mwenu
10 Ndugu zangu, kwa mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, ninawasihi mpatane ninyi kwa ninyi. Msigawanyike katika makundi. Lakini iweni pamoja tena katika kuwaza kwenu na katika nia zenu.
11 Kaka na dada zangu, baadhi ya jamaa wa Kloe wamenitaarifu kuwa kuna mabishano miongoni mwenu. 12 Baadhi yenu husema, “Mimi ninamfuata Paulo,”[d] na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Apolo.” Mwingine husema, “Mimi ninamfuata Petro,”[e] na mwingine husema, “Mimi ninamfuata Kristo.” 13 Kristo hawezi kugawanywa katika makundi. Je, Paulo ndiye alikufa msalabani kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa katika jina la Paulo? 14 Ninashukuru kwa kuwa sikumbatiza mtu yeyote kwenu isipokuwa Krispo na Gayo. 15 Ninashukuru kwa sababu hakuna anayeweza kusema kuwa mlibatizwa katika jina langu. 16 (Niliwabatiza pia watu wote wa nyumbani mwa Stefana, lakini sikumbuki kuwa niliwabatiza watu wengine) 17 Kristo hakunipa kazi ya kubatiza watu. Alinipa kazi ya kuhubiri Habari Njema pasipo kutumia hekima ya maneno, inayoweza kubatilisha nguvu iliyo katika msalaba[f] wa Kristo.
Nguvu ya Mungu na Hekima Katika Kristo Yesu
18 Mafundisho kuhusu msalaba yanaonekana ni ya kipuuzi kwao wao wanaoelekea kwenye uharibifu. Lakini ni nguvu ya Mungu kwetu sisi tunaookolewa. 19 Kama Maandiko yanavyosema,
“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima.
Nitaukanganya uelewa wa wenye akili.”(A)
20 Je, hii inasema nini kuhusu mwenye hekima, mtaalamu wa sheria au yeyote katika ulimwengu huu mwenye ujuzi wa kutengeneza hoja zenye nguvu? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upuuzi. 21 Hii inadhihirisha wazi kuwa, Mungu katika hekima yake aliamua kuwa hawezi kupatikana kwa kutumia hekima ya ulimwengu. Hivyo Mungu aliutumia ujumbe unaoonekana kuwa upuuzi kuwaokoa wale wanaouamini.
22 Na hii ndiyo sababu Wayahudi wanataka ishara za miujiza na Wayunani wanataka hekima. 23 Lakini ujumbe tunaomwambia kila mtu unahusu Masihi aliyekufa msalabani. Ujumbe huu ni kikwazo kwa Wayahudi na kwa Wayunani ni upuuzi. 24 Lakini kwa Wayahudi na Wayunani walioteuliwa na Mungu, Masihi huyu aliyesulibiwa ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. 25 Maana upumbavu wa Mungu ni hekima zaidi ya hekima ya kibinadamu, na udhaifu wa Mungu ni nguvu zaidi ya nguvu ya kibinadamu.
26 Kaka na dada zangu, fikirini kuhusu hili kwamba Mungu aliwachagua ili muwe milki yake. Wachache wenu mlikuwa na hekima kwa namna dunia inavyoichukulia hekima. Wachache wenu mlikuwa mashuhuri na wachache wenu mnatoka katika familia maarufu. 27 Lakini Mungu aliyachagua mambo ambayo wanadamu huyachukulia kuwa ya kipumbavu ili ayaaibishe yenye hekima. Aliyachagua mambo yanayoonekana kuwa manyonge ili ayaaibishe yenye nguvu. 28 Aliwachagua wasio kitu ili ayaangamize yale ambayo ulimwengu unadhani ni muhimu. 29 Mungu alifanya hivi ili mtu yeyote asisimame mbele zake na akajisifu kuwa yeye ni bora kuliko mwingine. 30 Lakini Mungu ameyafungamanisha maisha yenu na Kristo Yesu. Yeye alifanywa kuwa hekima yetu kutoka kwa Mungu. Na kupitia kwake tumehesabiwa haki na Mungu na tumefanywa kuwa watakatifu. Kristo ndiye aliyetuokoa, akatufanya watakatifu na akatuweka huru mbali na dhambi. 31 Hivyo, kama Maandiko yanavyosema, “Kila anayejisifu, ajisifu juu ya Bwana tu.”(B)
Ujumbe Wangu: Yesu Kristo Msalabani
2 Wapendwa kaka na dada zangu katika Kristo, nilipokuja kwenu, niliwaambia siri ya kweli iliyofunuliwa na Mungu. Lakini sikuja kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuongea au mwenye hekima ya juu. 2 Nilipokuwa pamoja nanyi, niliamua kusahau kila kitu isipokuwa Yesu Kristo na kifo chake msalabani. 3 Nilipokuja kwenu nilikuwa mdhaifu na mwenye hofu. 4 Mafundisho na kuzungumza kwangu hakukuwa kwa maneno yenye hila. Lakini uthibitisho wa mafundisho yangu ilikuwa nguvu inayotolewa na Roho. 5 Nilifanya hivi ili imani yenu iwe katika nguvu ya Mungu siyo katika hekima ya kibinadamu.
Hekima ya Mungu
6 Tunafundisha hekima kwa watu ambao macho yao yamefunguliwa ili waione hekima ya siri ya Mungu. Si hekima ya watawala wa ulimwengu huu wanaobatilika. 7 Tunaisema hekima ya Mungu katika namna ambayo baadhi wanaweza kuiona na wengine hawawezi. Ni hekima iliyofichwa mpaka wakati huu na Mungu aliipanga hekima hii kabla ya kuumba ulimwengu, kwa ajili ya utukufu wetu. 8 Hakuna mtawala yeyote wa ulimwengu huu aliyeielewa hekima hii. Ikiwa wangeielewa, wasingemwua Bwana wetu mkuu na mwenye utukufu mwingi msalabani. 9 Lakini kama Maandiko yanavyosema,
“Hakuna aliyewahi kuona,
hakuna aliyewahi kusikia,
hakuna aliyewahi kufikiri
kuhusu kile ambacho Mungu amewaandalia wanaompenda.”(C)
10 Lakini Mungu ametuonesha mambo haya kupitia Roho.
Roho anaweza kuchunguza mambo yote. Anajua hata siri za ndani kabisa za Mungu. 11 Hakuna mtu anayejua mawazo ya mtu mwingine. Ni roho inayoishi ndani ya mtu huyo ndiyo inajua mawazo ya mtu huyo. Ndivyo ilivyo hata kwa Mungu, ni Roho wa Mungu peke yake ndiye anayeyajua mawazo ya Mungu. 12 Tulipokea Roho wa Mungu, si roho wa ulimwengu. Tulimpokea Roho wa Mungu ili tuweze kujua yote aliyotupa Mungu.
13 Tunapozungumza, hatutumii hoja tulizofundishwa na wenye hekima. Bali hoja tulizofundishwa na Roho. Tunatumia hoja za Roho kuelezea kweli za Roho. 14 Watu wasio na Roho wa Mungu, hawakubali vitu vinavyotoka kwa Roho. Hudhani kuwa ni vitu vya kipuuzi. Hawavielewi, kwa sababu havieleweki pasipo msaada wa Roho. 15 Aliye na Roho anaweza kujua mambo yote anayofundisha Roho. Na hatutahukumiwa kuwa na hatia na mtu yeyote.[g] 16 Kama Maandiko yanavyosema,
“Nani anaweza kujua anachokiwaza Bwana?
Nani anaweza kumshauri?”(D)
Lakini sisi tumepewa tunawaza kama Kristo.
Walimu ni Watumishi tu wa Mungu
3 Ndugu zangu, nilipokuwa kwenu, sikuzungumza nanyi kama ninavyozungumza na watu wanaoongozwa na Roho. Nilizungumza nanyi kama watu wa kawaida wa duniani. Mlikuwa kama watoto katika Kristo. 2 Mafundisho niliyowafundisha yalikuwa kama maziwa, siyo chakula kigumu. Nilifanya hivi kwa kuwa hamkuwa tayari kwa chakula kigumu. Na hata sasa hamjawa tayari. 3 Bado hamwenendi katika Roho, mnaoneana wivu na mnabishana ninyi kwa ninyi kila wakati. Hii inaonesha kuwa bado mnazifuata tamaa zenu wenyewe. Mnaenenda kama watu wa kawaida wa ulimwengu huu. 4 Mmoja wenu anasema, “Mimi ninamfuata Paulo,” na mwingine anasema, “Ninamfuata Apolo.” Mnaposema mambo kama haya, mnaenenda kama watu wa ulimwengu.
5 Je, Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Apolo na mimi si watumishi tu ambao Mungu alitutumia ili mmwamini Yesu Kristo. Kila mmoja wetu alifanya kazi aliyopewa na Bwana. 6 Nilipanda mbegu na Apolo akamwagilia maji. Lakini Mungu ndiye aliyeiotesha na kuikuza. 7 Hivyo aliyepanda na kuimwagilia si wa muhimu. Mungu ndiye wa muhimu, kwa sababu ndiye anayevifanya vitu viote vikue. 8 Anayepanda na anayemwagilia maji wote wana nia moja. Na kila mmoja atalipwa kutokana na kazi yake yeye mwenyewe. 9 Ninyi ni shamba la Mungu, ambamo tulifanya kazi pamoja kwa ajili yake.
Nanyi pia ni jengo la Mungu. 10 Nami kama mjenzi stadi nilijenga msingi wa nyumba hiyo kwa kutumia karama alizonipa Mungu. Wengine wanajenga pia katika msingi huo. Lakini kila mtu lazima awe mwangalifu kwa namna anavyojenga. 11 Yesu Kristo ndiye msingi uliokwishajengwa, na hakuna yeyote anayeweza kujenga msingi mwingine. 12 Watu wanaweza kujenga juu ya msingi huo kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, mbao, nyasi au majani. 13 Kila kazi atakayoifanya kila mtu itaonekana siku ya hukumu itakapofika, na itaonekana ilivyo mbaya au nzuri. Siku hiyo kila kazi ya mtu itajaribiwa kwa moto. 14 Mungu atampa thawabu mtu anayejenga juu ya msingi huu ikiwa kazi yake haitateketea kwa moto. 15 Lakini ikiwa itateketea atapata hasara. Lakini yeye mwenyewe ataokolewa, lakini itakuwa kama mtu anayeokolewa kutoka kwenye moto.
16 Hakika mnajua kuwa ninyi ni hekalu la Mungu na Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. 17 Ndiyo, ninyi nyote kwa pamoja ni Hekalu la Mungu. Na yeyote atakayeliharibu Hekalu la Mungu ataadhibiwa na Mungu, kwa sababu Hekalu la Mungu ni mali yake yeye mwenyewe.
18 Msijidanganye. Yeyote anayejiona kuwa ana hekima kwa viwango vya ulimwengu huu, basi na awe mpumbavu. Hiyo ndiyo njia pekee itakayomfanya kuwa na hekima. 19 Ninasema hivi kwa sababu hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu huwanasa katika mitego yao wenyewe wale wanaojidhania kuwa na hekima.”(E) 20 Pia Maandiko yanasema, “Bwana anajua mawazo ya wenye hekima. Anajua kuwa mawazo yao hayana maana.”(F) 21 Hivyo hakuna mtu yeyote duniani ambaye ninyi mnapaswa kujivunia. Kila kitu ni chenu: 22 Paulo, Apolo, Petro, ulimwengu, uzima, mauti, wakati uliopo na ujao, vyote hivi ni vyenu. 23 Ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.
Mitume wa Kristo Yesu
4 Tuchukulieni sisi kuwa ni watumishi wa Kristo, ambao Mungu ametuamini tufanye kazi ya kuwaambia wengine siri zake za kweli. 2 Wale walioaminiwa kwa kazi muhimu kama hii imewapasa kuonesha ya kuwa wao ni waaminifu. 3 Lakini siichukulii hukumu yenu kuhusu hili kuwa kitu. Hata hukumu yo yote katika mahakama ya kibinadamu isingekuwa na maana yoyote. Sijihukumu hata mimi mwenyewe. 4 Sikumbuki kosa lolote nililofanya, lakini hiyo hainifanyi mimi kujihesabia haki. Bwana pekee ndiye anayepaswa kunihukumu ikiwa nimefanya vyema au la. 5 Hivyo, msimhukumu mtu yeyote sasa. Hukumu itakuwa wakati Bwana atakaporudi. Ataangaza mwanga kwa kila kitu kilichofichwa gizani. Ataziweka wazi nia za siri za mioyo yetu. Ndipo sifa ambayo kila mtu anapaswa kuipata itatoka kwa Mungu.
6 Ndugu zangu, nimemtumia Apolo na mimi mwenyewe kama mfano kwa ajili yenu. Nimefanya hivi ili mjifunze kutoka kwetu maana ya maneno yanayosema, “Uwe mwangalifu kufuata kilichoandikwa.”[h] 7 Kwa nini mnajisifu? Mlipewa kila kitu mlicho nacho. Sasa, ikiwa mlipewa kila kitu mlicho nacho, kwa nini mnajisifu kana kwamba mlipata vitu vyote kwa nguvu zenu wenyewe?
8 Mnadhani kwamba tayari mna kila kitu mnachohitaji. Mnadhani kwamba mmekwisha tajirika. Laiti mngekwisha fanywa wafalme, kwa sababu tungekuwa wafalme pamoja nanyi. 9 Lakini inaonekana kana kwamba Mungu amenipa mimi na mitume wengine mahali pa mwisho. Sisi ni kama wafungwa waliohukumiwa kufa, waliosimamishwa katika gwaride ili ulimwengu wote uwaone, si watu tu bali hata malaika pia. 10 Tu wapumbavu kwa kuwa sisi ni wa Kristo, lakini mnadhani kuwa ninyi ni wenye hekima katika Kristo. Sisi ni dhaifu, lakini mnadhani kuwa mna nguvu. Watu wanawaheshimu ninyi, na hawatuheshimu sisi. 11 Hata sasa hatuna vyakula vya kutosha kula au kunywa, na hatuna nguo za kutosha. Mara kwa mara tunapigwa na hatuna makazi. 12 Tunafanya kazi sana kwa mikono yetu ili tupate chakula. Watu wanapotutukana, tunamwomba Mungu awabariki. Watu wanapotutendea vibaya, tunavumilia. 13 Watu wanaposema mabaya juu yetu, tunawajibu kwa upole. Lakini watu wanaendelea kutuona kama takataka.
14 Siwaambii haya ili kuwatahayarisha, lakini ninaandika haya ili kuwaonya kama watoto wangu mwenyewe ninaowapenda. 15 Mnaweza kuwa na walimu elfu kumi katika Kristo, lakini hamna baba wengi. Kupitia Habari Njema mimi nilifanyika baba kwenu katika Kristo Yesu. 16 Ndiyo sababu ninawahimiza mfuate mfano wangu. 17 Ndiyo sababu ninamtuma Timotheo kwenu. Ni mwanangu katika Bwana. Ninampenda na ni mwaminifu. Atawasaidia ili mkumbuke namna ninavyoishi kama mfuasi wa Kristo Yesu, kama ninavyofundisha katika kila kanisa kila mahali ninakokuwa.
18 Baadhi yenu mnajivuna, mkidhani kuwa sitakuja kuwatembelea tena. 19 Lakini nitakuja kwenu hivi karibuni ikiwa Bwana atanijalia. Ndipo nitajua ikiwa hawa wanaojivuna wana nguvu za kutenda jambo lolote zaidi ya kuzungumza. 20 Mungu huonesha kuwa anatawala katika maisha kwa yale wanayoweza kufanya na si kwa maneno yao. 21 Je, nitakapokuja kwenu, nije nikiwa na adhabu au nije kwa upendo na upole?
© 2017 Bible League International