Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Warumi 11-13

Mungu Hajawakataa Watu wake

11 Hivyo ninauliza, “Je, Mungu aliwakataa watu wake?” Hapana! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, wa ukoo wa Ibrahimu, katika kabila la Benjamini. Mungu aliwachagua Waisraeli wawe watu wake kabla hawajazaliwa. Na hajawakataa. Hakika mnajua Maandiko yanavyosema kuhusu Eliya anapomwomba Mungu dhidi ya watu wa Israeli. Anasema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuharibu madhabahu zako. Mimi ndiye nabii pekee niliyebaki hai, na sasa wanajaribu kuniua mimi pia.”(A) Lakini ni jibu gani Mungu alilompa Eliya? Mungu alisema, “Nimejihifadhia watu elfu saba wasiomwabudu Baali.”(B)

Ndivyo ilivyo sasa. Mungu amewachagua watu wachache kwa neema yake. Na kama aliwachagua kwa neema yake, hivyo si kwa sababu ya matendo yao yaliyowafanya wawe watu wake. Kama wangefanywa kuwa watu wake kutokana na matendo yao, zawadi yake ya neema isingekuwa zawadi halisi.

Hivyo hivi ndivyo ilivyotokea: Watu wa Israeli wanazitaka sana baraka za Mungu, lakini si wote waliozipata. Watu aliowachagua walipata baraka zake, lakini wengine wakawa wagumu na wakakataa kumsikiliza. Kama Maandiko yanavyosema,

“Mungu aliwafanya watu walale usingizi.”(C)
“Mungu aliyafumba macho yao ili wasione,
    na aliyaziba masikio yao ili wasisikie.
Hili linaendelea hata sasa.”(D)

Na Daudi anasema,

“Watu hawa na wakamatwe na kunaswa
    katika tafrija wanazofurahia.
Nyakati hizo nzuri ziwasababishe waanguke
    ili wapate adhabu wanayoistahili.
10 Yapofushe macho yao ili wasiweze kuona.
    Ipindishe migongo yao kwa mzigo wa matatizo.”(E)

11 Hivyo nauliza: Pale watu wa Mungu walipojikwaa na kuanguka, Je, hawakuweza kuinuka tena? Hakika hapana! Lakini kujikwaa kwao katika mwendo kulileta wokovu kwa wale wasio Wayahudi. Kusudi la hili lilikuwa kuwafanya Wayahudi wapate wivu. 12 Kosa lao na hasara yao vilileta baraka za utajiri kwa ulimwengu kwa wasio Wayahudi. Hivyo fikirini ni kwa kiasi gani baraka hizi zitakuwa kubwa kwa ulimwengu pale idadi ya kutosha ya Wayahudi watakapokuwa watu wa aina ile anayoitaka Mungu.

13 Nasema na ninyi watu msio Wayahudi. Kwa vile mimi ndiye ambaye Mungu ameniteua niwe mtume kwa wale wasio Wayahudi, nitafanya kwa bidii yote kuiheshimu huduma hii. 14 Natarajia kuwafanya watu wangu wawe na wivu. Kwa njia hiyo, labda naweza kuwasaidia baadhi yao waweze kuokolewa. 15 Mungu aliwaacha kwa muda. Hilo lilipotokea, akawa rafiki wa watu wengine ulimwenguni. Hivyo anapowakubali Wayahudi, ni sawa na kuwafufua watu baada ya kifo. 16 Kama sehemu ya kwanza ya mkate inatolewa kwa Mungu, basi mkate mzima unakuwa umetakaswa. Kama mizizi ya mti ni mitakatifu, matawi ya mti huo pia ni matakatifu.

17 Ni kama vile baadhi ya matawi ya mzeituni yamevunjwa, na tawi la mzeituni mwitu limeunganishwa katika ule mti wa kwanza. Ikiwa wewe si Myahudi, uko sawa na tawi la mzeituni mwitu, na sasa unashiriki nguvu na uhai wa mti wa kwanza. 18 Lakini msienende kama mlio bora kuliko matawi yale yaliyovunjwa. Hamna sababu ya kujivuna, kwa sababu hamleti uhai katika mzizi. Mzizi ndiyo huleta uhai kwenu. 19 Mnaweza kusema, “Matawi yalivunjwa ili niweze kuunganishwa katika mti wake.” 20 Hiyo ni kweli. Lakini matawi hayo yalivunjwa kwa sababu hayakuamini. Na mnaendelea kuwa sehemu ya mti kwa sababu tu mnaamini. Msijivune, bali muwe na hofu. 21 Ikiwa Mungu hakuyaacha matawi ya asili ya mti huo yawepo, hataweza kuwaacha ninyi muwepo mtakapoacha kuamini.

22 Hivyo mnaona kwamba Mungu yu mwema, lakini anaweza pia kuwa mkali. Huwaadhibu wale wanaoacha kumfuata. Lakini ni mwema kwenu ikiwa mtaendelea kumwamini katika wema wake. Kama hamtaendelea kumtegemea yeye, mtakatwa kutoka katika mti. 23 Na kama Wayahudi watamwamini Mungu tena, yeye atawapokea tena. Ana uwezo wa kuwarudisha pale walipokuwa. 24 Kwa asili, tawi la mzabibu mwitu haliwezi kuwa sehemu ya mti mzuri. Lakini ninyi msio Wayahudi ni kama tawi lililovunjwa kutoka katika mzeituni pori. Na mliunganishwa na mti wa mzeituni ulio mzuri. Lakini Wayahudi ni kama matawi yaliyostawi kutokana na mti mzuri. Hivyo kwa hakika yanaweza kuunganishwa pamoja katika mti wao tena.

25 Ndugu zangu, ieleweni siri hii ya ukweli. Kweli hii itawasaidia ninyi mjue kuwa hamfahamu kila kitu. Kweli ni hii: Sehemu ya Israeli wamefanywa kuwa wakaidi, lakini hiyo itabadilika wasio Wayahudi, wengi, watakapokuja kwa Mungu. 26 Na hivyo ndivyo Israeli wote watakavyookolewa. Kama Maandiko yanavyosema,

“Mwokozi atakuja kutoka Sayuni;
    atauondoa uovu kutoka kwa wazaliwa wa Yakobo.
27 Nami nitalifanya patano hili na watu wale
    nitakapoziondoa dhambi zao.”(F)

28 Kwa sasa, Wayahudi wanaokataa kuzipokea Habari Njema wamekuwa adui wa Habari Njema. Hili limetokea kwa manufaa yenu ninyi msio Wayahudi. Lakini bado Wayahudi ni wateule wa Mungu, na anawapenda kwa sababu ya ahadi alizozifanya kwa baba zao. 29 Mungu habadili mawazo yake kuhusu watu anaowaita. Kamwe haamui kuzirudisha baraka alizokwisha kuwapa. 30 Wakati mmoja ninyi pia mlikataa kumtii Mungu. Lakini sasa mmeipokea rehema, kwa sababu Wayahudi walikataa kutii. 31 Na sasa wao ndiyo wanaokataa kutii, kwa sababu Mungu aliwaonesha ninyi rehema zake. Lakini hili limetokea ili nao pia waweze kupokea rehema kutoka kwake. 32 Mungu amemfungia kila mmoja katika gereza la kutokutii. Lakini amefanya hivi ili aweze kuonesha rehema yake kwa wote.

Sifa kwa Mungu

33 Ndiyo, utajiri wa Mungu ni mkuu sana! Hekima yake na ufahamu wake havina mwisho! Hakuna awezaye kuelezea yale Mungu anayoyaamua. Hayupo awezaye kuzielewa njia zake. 34 Kama Maandiko yanavyosema,

“Nani anaweza kuyajua yaliyo katika mawazo ya Bwana?
    Nani anaweza kumshauri?”(G)
35 “Nani amewahi kumpa Mungu kitu chochote?
    Mungu hadaiwi kitu chochote na mtu yeyote.”(H)

36 Ndiyo, Mungu ameviumba vitu vyote. Na kila kitu kinaendelea kuwepo kwa njia na kwa ajili yake. Utukufu uwe kwa Mungu milele yote! Amina.

Yatoeni Maisha Yenu kwa Mungu

12 Hivyo, dada na kaka zangu, upokeeni wema mkuu ambao Mungu alituonyesha. Itoeni miili yenu[a] kama sadaka hai kwake. Ishini kwa ajili ya Mungu tu na mweze kumpendeza yeye. Mkizingatia kwa makini yale aliyoyatenda, ni sahihi na inapasa kumwabudu Mungu kwa njia hii. Msifikiri au kuenenda kama watu wa ulimwengu huu, bali mruhusuni Mungu aibadilishe namna yenu ya kufikiri ndani yenu. Ndipo mtaweza kuelewa na kuyathibitisha yale Mungu anayotaka kutoka kwenu; yote yaliyo mema, yanayompendeza yeye na yaliyo makamilifu.

Mungu amenipa mimi zawadi maalumu, na ndiyo sababu nina kitu cha kusema na kila mmoja wenu. Msifikiri kuwa ninyi ni bora kuliko jinsi mlivyo kwa asili. Mnapaswa kujiona kadri mlivyo. Mjipime wenyewe jinsi mlivyo kwa imani ambayo Mungu alimpa kila mmoja wetu. Kila mmoja wetu anao mwili mmoja, na mwili huo una viungo vingi. Viungo hivi vyote havifanyi mambo yanayofanana. Kwa jinsi hiyo hiyo, sisi ni watu wengi, lakini kwa sababu ni wa Kristo, sote ni mwili mmoja. Sisi sote ni viungo vya mwili huo, na kila kiungo ni sehemu ya viungo vingine vyote.

Sote tunazo karama tofauti tofauti. Kila karama ilikuja kwa sababu ya neema aliyotupa Mungu. Yule aliye na karama ya unabii anapaswa kuitumia karama hiyo kwa namna inayokubalika kiimani. Aliye na karama ya kuhudumia anapaswa kuhudumia. Aliye na karama ya kufundisha anapaswa kufundisha. Aliye na karama ya kufariji wengine anapaswa kufanya hivyo. Aliye na karama ya kuhudumia mahitaji ya wengine anapaswa kutoa kwa moyo mweupe. Aliye na karama ya kuongoza anapaswa kufanya kwa juhudi katika hiyo. Aliye na karama ya kuonesha wema kwa wengine anapaswa kufanya hivyo kwa furaha.

Upendo wenu unapaswa kuwa halisi. Uchukieni uovu. Fanyeni yaliyo mema tu. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kama wa familia moja. Na jitahidini kuwa wa kwanza katika kumpa heshima kila mmoja baina yenu. 11 Mnapoendelea kumtumikia Bwana, fanyeni kwa juhudi wala msiwe wavivu. Mchangamke juu ya utumishi wenu kwa Mungu.[b] 12 Mfurahi kwa sababu ya tumaini mlilonalo. Mvumilieni mnapokutana na mateso. Ombeni nyakati zote. 13 Washirikishe ulichonacho watu wa Mungu wanaohitaji msaada. Wakaribisheni katika nyumba zenu wale wanaosafiri au wanaohitaji msaada.

14 Watakieni mema wale wanaowafanyia mabaya. Mwombeni Mungu awabariki, na sio kuwalaani. 15 Furahini pamoja na wanaofurahi. Huzunikeni na wanaohuzunika. 16 Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, lakini iweni radhi kuwa rafiki wa wasio na umuhimu kwa wengine. Msijihesabu kuwa wenye akili kuliko wengine wote.

17 Mtu akikukosea, usimlipize ubaya. Mjaribu kufanya lile ambalo kila mtu anaona kuwa ni sahihi. 18 Mjitahidi kadri mwezavyo kuishi kwa amani na kila mtu. 19 Rafiki zangu, msijaribu kumwadhibu yeyote anayewakosea. Msubiri Mungu katika hasira yake awaadhibu. Katika Maandiko Bwana anasema, “Nitawaadhibu wao kwa ajili ya yale waliyofanya.”(I) 20 Badala yake,

“ikiwa una adui wenye njaa,
    wapeni chakula wale.
Ikiwa wana kiu,
    wapeni kinywaji wanywe.
Kwa kufanya hivyo mtawafanya wajisikie aibu.”[c](J)

21 Msiruhusu uovu uwashinde, bali ushindeni uovu kwa kutenda mema.

Kutii Watawala

13 Watiini watawala wa serikali. Hakuna anayeweza kutawala bila mamlaka ya Mungu. Mamlaka ya kutawala hutoka kwa Mungu. Hivyo yeyote anayekuwa kinyume na serikali hakika anakuwa kinyume na kitu ambacho Mungu amekiweka. Wale walio kinyume na serikali wanajiletea adhabu wao wenyewe. Watu wanaotenda mema hawawaogopi watawala. Bali wale wanaotenda mabaya ni lazima wawaogope watawala. Je, mnataka kuwa huru mbali na kuwaogopa hao? Basi mfanye yaliyo sahihi tu, nao watawasifu ninyi.

Watawala ni watumishi wa Mungu kwa ajili ya kuwasaidia ninyi. Lakini mkifanya yasiyo sahihi, mnayo sababu ya kuwa na woga. Hao wanayo mamlaka ya kuwaadhibu, na watayatumia mamlaka hayo. Wao ni watumishi wa Mungu ili wawaadhibu wale wanaofanya yale yasiyo sahihi. Kwa hiyo mnapaswa kuitii serikali, siyo tu kwa sababu mtaadhibiwa, bali kwa sababu mnajua kuwa ni jambo lililo sahihi kufanya hivyo.

Na hii ndiyo sababu mnalipa kodi. Watawala hawa wanapaswa kulipwa kwa ajili ya kutimiza wajibu wao wote walionao wa kutawala. Hakika wanatumika kwa ajili ya Mungu. Wapeni watu wote vile wanavyowadai. Kama wanawadai aina yoyote ya kodi, basi lipeni. Onesheni heshima kwa wale mnaopaswa kuwaheshimu. Na onesheni uadilifu kwa wale mnaopaswa kuwafanyia hivyo.

Kuwapenda Wengine Ndiyo Sheria Pekee

Msidaiwe chochote na mtu, isipokuwa mdaiwe upendo baina yenu. Mtu anayewapenda wengine anakuwa amefanya yote yanayoamriwa na sheria. Sheria inasema, “Usizini, usiue, usiibe, usitamani kitu cha mtu mwingine.”(K) Amri hizo zote na zingine hakika zinajumlishwa na kuwa kanuni moja tu, “Mpende jirani yako[d] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.”(L) 10 Upendo hauwaumizi wengine. Hivyo kupenda ni sawa na kuitii sheria yote.

11 Nalisema hili kwa sababu mnajua kwamba tunaishi katika wakati ulio muhimu. Ndiyo, ni wakati wenu sasa kuamka kutoka usingizini. Wokovu wetu sasa uko karibu zaidi kuliko ilivyokuwa tulipoamini kwa mara ya kwanza. 12 Usiku karibu umekwisha. Na mchana karibu unaingia. Hivyo tunapaswa kuacha kufanya chochote kinachohusiana na giza. Tunapaswa kujiandaa kuupiga uovu kwa silaha za nuru. 13 Tunapaswa kuishi katika njia sahihi, kama watu walio wa mchana. Hatupaswi kuwa na tafrija za ovyo ama kulewa. Hatupaswi kujihusisha katika dhambi ya uzinzi au ya aina yoyote ya mwenendo usiofaa. Hatupaswi kusababisha mabishano au kuwa na wivu. 14 Bali, muwe kama Kristo Yesu katika kila jambo mnalolitenda,[e] ili watu watakapowaangalia, waweze kumwona yeye. Msifikirie namna ya kuridhisha matakwa ya udhaifu wa mwanadamu na tamaa zake.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International