Beginning
Timotheo Afuatana na Paulo na Sila
16 Paulo alikwenda Derbe kisha Listra, ambako mfuasi wa Yesu aliyeitwa Timotheo aliishi. Mamaye Timotheo alikuwa mwamini wa Kiyahudi, lakini baba yake alikuwa Myunani. 2 Waamini katika miji ya Listra na Ikonia walimsifu Timotheo kwa mambo mema. 3 Paulo alitaka kusafiri pamoja na Timotheo, lakini Wayahudi wote walioishi katika eneo lile walijua kuwa baba yake alikuwa Myunani. Hivyo ikamlazimu Paulo amtahiri Timotheo ili kuwaridhisha Wayahudi.
4 Kisha Paulo na wale waliokuwa pamoja naye wakasafiri kupitia miji mingine. Wakawapa waamini kanuni na maamuzi yaliyofikiwa na mitume na wazee wa Yerusalemu. Wakawaambia wazitii kanuni hizo. 5 Hivyo makanisa yakawa yanaongezeka katika imani, na idadi ya waamini iliongezeka kila siku.
Paulo Aitwa Makedonia
6 Paulo na wale waliokuwa pamoja naye walisafiri kwa kupita katika maeneo ya Frigia na Galatia kwa sababu Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuzihubiri Habari Njema katika jimbo la Asia. 7 Walipofika kwenye mpaka wa Misia, walijaribu kwenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu kwenda huko. 8 Hivyo wakapita Misia na kwenda katika mji wa Troa.
9 Usiku ule Paulo aliona maono kwamba mtu kutoka Makedonia alimjia Paulo. Mtu huyo alisimama mbele yake na kumsihi akisema, “Vuka njoo Makedonia utusaidie.” 10 Baada ya Paulo kuona maono yale, tulijiandaa[a] haraka na tukaondoka kwenda Makedonia. Tulielewa kuwa Mungu ametuita ili tukahubiri Habari Njema huko Makedonia.
Kuongoka kwa Lydia
11 Tulisafiri kwa merikebu kutoka Troa na tukaabili kwenda katika kisiwa cha Samothrake. Siku iliyofuata tukasafiri kwenda katika mji wa Neapoli. 12 Kisha tulisafiri kwa nchi kavu mpaka Filipi, koloni la Rumi na mji maarufu katika la Makedonia. Tulikaa pale kwa siku chache.
13 Siku ya Sabato tulikwenda mtoni, nje ya lango la mji. Tulidhani tungepata mahali ambapo Wayahudi hukutana mara kwa mara kwa ajili ya kuomba. Baadhi ya wanawake walikuwa wamekusanyika huko, na hivyo tulikaa chini na kuzungumza nao. 14 Miongoni mwao alikuwepo mwanamke aliyeitwa Lydia kutoka katika mji wa Thiatira. Alikuwa mwuza rangi ya zambarau. Alikuwa mwabudu Mungu wa kweli. Lydia alimsikiliza Paulo, na Bwana akaufungua moyo wake kuyakubali yale Paulo alikuwa anasema. 15 Yeye na watu wote waliokuwa wakiishi katika nyumba yake walibatizwa. Kisha akatualika nyumbani mwake. Alisema, “Ikiwa mnaona mimi ni mwamini wa kweli wa Bwana Yesu, njooni mkae nyumbani mwangu.” Alitushawishi tukae nyumbani mwake.
Paulo na Sila Wakiwa Gerezani
16 Siku moja tulipokuwa tunakwenda pale mahali pa kufanyia kuomba, mtumishi mmoja msichana alikutana nasi. Msichana huyu alikuwa na roho ya ubashiri[b] ndani yake iliyompa uwezo wa kutabiri mambo yatakayotokea baadaye. Kwa kufanya hivi alipata fedha nyingi kwa ajili ya waliokuwa wanammiliki. 17 Akaanza kumfuata Paulo na sisi sote kila mahali akipaza sauti na kusema, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu! Wanawaambia mnavyoweza kuokolewa!” 18 Aliendelea kufanya hivi kwa siku kadhaa na ikamuudhi Paulo, akageuka na kumkemea yule roho akisema, “Kwa uwezo wa Yesu Kristo, ninakuamuru utoke ndani yake!” Mara ile roho chafu ikamtoka.
19 Wamiliki wa mtumishi yule msichana walipoona hili, wakatambua kuwa hawataweza kumtumia tena ili kupata pesa. Hivyo wakawakamata Paulo na Sila na kuwaburuta mpaka kwa watawala. 20 Wakawaleta Paulo na Sila mbele ya maofisa wa Kirumi na kusema, “Watu hawa ni Wayahudi, wanafanya vurugu katika mji wetu. 21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Rumi haturuhusiwi kuzifuata wala kutenda.”
22 Umati wote wa watu ukawa kinyume na Paulo na Sila. Maofisa wakawachania nguo Paulo na Sila na wakaamuru wapigwe bakora. 23 Walichapwa sana kisha wakawekwa gerezani. Maofisa wakamwambia mkuu wa gereza, “Walinde watu hawa kwa umakini!” 24 Mkuu wa gereza aliposikia amri hii maalumu, aliwaweka Paulo na Sila ndani zaidi gerezani na kuwafunga miguu yao kwenye nguzo kubwa za miti.
25 Usiku wa manane Paulo na Sila walipokuwa wakiomba na kumwimbia Mungu nyimbo za sifa, wafungwa wengine wakiwa wanawasikiliza. 26 Ghafla kulitokea tetemeko kubwa lililotikisa msingi wa gereza. Milango yote ya gereza ilifunguka, na minyororo waliyofungwa wafungwa wote ikadondoka. 27 Mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza imefunguliwa. Alidhani wafungwa wametoroka, hivyo alichukua upanga wake ili ajiue.[c] 28 Lakini Paulo alipaza sauti akamwambia, “Usijidhuru! Sote tuko hapa!”
29 Mkuu wa gereza akaagiza aletewe taa. Kisha akakimbia kuingia ndani, akitetemeka kwa woga, akaanguka mbele ya Paulo na Sila. 30 Kisha akawatoa nje na kusema, “Nifanye nini ili niokoke?”
31 Wakamwambia, “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokolewa pamoja na watu wote waishio katika nyumba yako.” 32 Hivyo Paulo na Sila wakamhubiri ujumbe wa Bwana mkuu wa gereza na watu wote walioishi katika nyumba yake. 33 Ilikuwa usiku sana, lakini mkuu wa gereza aliwachukua Paulo na Sila na akawaosha majeraha yao. Kisha mkuu wa gereza na watu wote katika nyumba yake wakabatizwa. 34 Baada ya hili mkuu wa gereza akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake akawapa chakula. Watu wote walifurahi kwa sababu sasa walikuwa wanamwamini Mungu.
35 Asubuhi iliyofuata maofisa wa Kirumi waliwatuma baadhi ya askari kwenda gerezani na wakamwambia mkuu wa gereza, “Waachie watu hawa huru.”
36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo, “Maofisa wamewatuma askari hawa ili kuwaachia huru. Mnaweza kuondoka sasa. Nendeni kwa amani.”
37 Lakini Paulo akawaambia askari, “Wale maofisa hawakuthibitisha kuwa tulifanya chochote kibaya, lakini walitupiga kwa bakora hadharani na kutuweka gerezani. Nasi ni raia wa Rumi.[d] Na sasa wanataka tuondoke kimya kimya. Haiwezekani, ni lazima waje hapa wao wenyewe kisha watutoe nje!”
38 Askari wakawaambia maofisa alichosema Paulo. Waliposikia kwamba Paulo na Sila ni raia wa Rumi, waliogopa. 39 Hivyo walikwenda gerezani kuwaomba msamaha. Waliwatoa nje ya gereza na kuwaomba waondoke mjini. 40 Lakini Paulo na Sila walipotoka gerezani, walikwenda nyumbani kwa Lydia. Wakawaona baadhi ya waamini pale, wakawatia moyo. Kisha wakaondoka.
Paulo na Sila Wakiwa Thesalonike
17 Paulo na Sila walisafiri kupitia miji ya Amfipoli na Apolonia. Wakafika katika mji wa Thesalonike, ambako kulikuwa sinagogi la Kiyahudi. 2 Paulo aliingia katika sinagogi kuwaona Wayahudi kama alivyokuwa akifanya. Wiki tatu zilizofuatia, kila siku ya Sabato alijadiliana nao kuhusu Maandiko. 3 Alifafanua Maandiko kuwaonesha kuwa Masihi ilikuwa afe na kufufuka kutoka kwa wafu. Aliwaambia, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake ndiye Masihi.” 4 Baadhi ya Wayahudi pale waliwaamini Paulo na Sila na waliamua kujiunga nao. Idadi kubwa ya Wayunani waliokuwa wanamwabudu Mungu wa kweli na wanawake wengi maarufu walijiunga nao pia.
5 Lakini Wayahudi ambao hawakuamini wakaingiwa na wivu, hivyo wakawakusanya baadhi ya watu wabaya katikati ya mji ili kufanya vurugu. Wakaunda kundi na wakanzisha vurugu mjini. Walikwenda nyumbani kwa Yasoni kuwatafuta Paulo na Sila. Walitaka kuwaleta mbele ya watu. 6 Walipowakosa wakamkamata na kumburuta Yasoni na baadhi ya waamini wengine na kuwapeleka kwa viongozi wa mji. Watu wakapasa sauti na kusema, “Watu hawa Wamesababisha matatizo mengi kila mahali ulimwenguni, na sasa wamekuja hapa pia! 7 Yasoni amewaweka nyumbani mwake. Wanavunja sheria za Kaisari. Wanasema kuna mfalme mwingine anayeitwa Yesu.”
8 Viongozi wa mji na watu wengine waliposikia hili waliudhika sana. 9 Wakawalazimisha Yasoni na waamini wengine kuweka dhamana ya fedha kuthibitisha kuwa hakutakuwa vurugu tena. Kisha wakawaruhusu kuondoka.
Paulo na Sila Waenda Berea
10 Usiku ule ule waamini wakawapeleka Paulo na Sila katika mji mwingine ulioitwa Berea. Walipofika pale, walikwenda katika sinagogi la Kiyahudi. 11 Watu wa Berea walikuwa radhi kujifunza kuliko watu wa Thesalonike. Walifurahi waliposikia ujumbe aliowaambia Paulo. Waliyachunguza Maandiko kila siku ili kuhakikisha kuwa waliyoyasikia ni ya kweli. 12 Matokeo yake ni kuwa watu wengi miongoni mwao waliamini, wakiwemo wanawake maarufu Wayunani na wanaume.
13 Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipojua kuwa Paulo alikuwa anawahubiri Ujumbe wa Mungu katika mji wa Berea, walikwenda huko pia. Waliwakasirisha watu na kufanya vurugu. 14 Hivyo waamini walimpeleka Paulo sehemu za pwani, lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. 15 Wale waliokwenda na Paulo walimpeleka katika mji wa Athene. Waliporudi Berea, waliwapa ujumbe kutoka kwa Paulo Timotheo na Sila kuwa waende kuungana naye haraka kadiri watakavyoweza.
Paulo Akiwa Athene
16 Paulo alipokuwa akiwasubiri Sila na Timotheo katika mji wa Athene, aliudhika kwa sababu aliona mji ulikuwa umejaa sanamu. 17 Alipokuwa katika sinagogi alizungumza na Wayahudi na Wayunani waliokuwa wakimwabudu Mungu wa kweli. Alikwenda pia katika sehemu za wazi za umma za mikutano na kuzungumza na kila aliyekutana naye. 18 Baadhi ya wanafalsafa Waepikureo[e] na baadhi ya wanafalsafa Wastoiko[f] walibishana naye.
Baadhi yao walisema, “Mtu huyu hakika hajui anachokisema. Anajaribu kusema nini?” Paulo alikuwa anawaambia Habari Njema kuhusu Yesu na ufufuo. Hivyo walisema, “Anaonekana anatueleza kuhusu baadhi ya miungu wa kigeni.”
19 Walimchukua Paulo kwenye mkutano wa baraza la Areopago. Wakasema, “Tafadhali tufafanunile hili wazo jipya ambalo umekuwa ukifundisha. 20 Mambo unayosema ni mapya kwetu. Hatujawahi kusikia mafundisho haya, na tunataka kufahamu yana maana gani.” 21 (Watu wa Athene na wageni walioishi pale walitumia muda wao bila kufanya kazi yoyote isipokuwa kusikiliza na kuzungumza kuhusu mawazo mapya.)
22 Ndipo Paulo alisimama mbele ya mkutano wa baraza la Areopago na kusema, “Watu wa Athene, kila kitu ninachokiona hapa kinanionyesha kuwa ninyi ni watu wa dini sana. 23 Nilikuwa natembea katika mji wenu na nimeona mambo mnayoyaabudu. Niliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya juu yake: ‘Kwa Mungu Asiyejulikana.’ Mnamwabudu mungu msiyemjua. Huyu ni Mungu ninayetaka kuwaambia habari zake.
24 Ni Mungu aliyeumba ulimwengu na kila kitu ndani yake. Ni Bwana wa mbingu na nchi. Haishi katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya kibinadamu. 25 Ndiye anayewapa watu uzima, pumzi na kila kitu wanachohitaji. Hahitaji msaada wowote kutoka kwao. Ana kila kitu anachohitaji. 26 Mungu alianza kwa kumwumba mtu mmoja, na kutoka kwake aliumba mataifa yote mbalimbali, na akawaweka kila mahali ulimwenguni. Na aliamua ni wakati gani na wapi ambapo angewaweka ili waishi.
27 Mungu alitaka watu wamtafute yeye, na pengine kwa kumtafuta kila mahali, wangempata. Lakini hayuko mbali na kila mmoja wetu. 28 Ni kupitia Yeye tunaweza kuishi, kufanya yale tunayofanya na kuwa kama tulivyo. Kama baadhi ya methali zenu zilivyokwisha sema, ‘Sote tunatokana naye.’
29 Huo ndio ukweli. Sote tunatokana na Mungu. Hivyo ni lazima msifikiri kuwa Yeye ni kama kitu ambacho watu hukidhania au kukitengeneza. Hivyo ni lazima tusifikiri kuwa ametengenezwa kwa dhahabu, fedha au jiwe. 30 Hapo zamani watu hawakumwelewa Mungu, naye Mungu hakulijali hili. Lakini sasa anawaagiza wanadamu kila mahali kubadilika na kumgeukia Yeye. 31 Amekwisha chagua siku ambayo atawahukumu watu wote ulimwenguni katika namna isiyo na upendeleo. Atafanya hili kwa kumtumia mtu aliyemchagua zamani zilizopita. Na alithibitisha kwa kila mtu kwamba huyu ndiye mtu atakayefanya. Alilithibitisha kwa kumfufua kutoka kwa wafu!”
32 Watu waliposikia kuhusu mtu kufufuliwa kutoka kwa kifo, baadhi yao walicheka. Lakini wengine walisema, “Tutasikiliza mengi kuhusu hili kutoka kwako baadaye.” 33 Hivyo Paulo akaondoka kwenye mkutano wa baraza. 34 Lakini baadhi ya watu waliungana na Paulo na kuwa waamini. Miongoni mwao walikuwa Dionisi, ambaye alikuwa mjumbe wa baraza la Areopago, na mwanamke aliyeitwa Damari na baadhi ya wengine.
© 2017 Bible League International