Beginning
Mitume Mbele ya Baraza Kuu la Wayahudi
4 Petro na Yohana walipokuwa wanazungumza na watu, ghafla baadhi ya viongozi wa Kiyahudi waliwaendea. Walikuwepo baadhi ya makuhani, mkuu wa askari wanaolinda Hekalu na baadhi ya Masadukayo. 2 Walikasirika kwa sababu ya mafundisho ambayo Petro na Yohana walikuwa wanawafundisha na kuwaambia watu kuhusu Yesu. Mitume walikuwa wanafundisha pia kwamba watu watafufuka kutoka kwa wafu. 3 Waliwakamata Petro na Yohana. Kwa kuwa ilikuwa jioni tayari, waliwaweka gerezani usiku ule mpaka siku iliyofuata. 4 Lakini watu wengi waliowasikia mitume waliamini walichosema. Na siku hiyo idadi ya watu katika kundi la waamini ikafikia watu 5,000.
5 Siku iliyofuata, watawala wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria walikutana Yerusalemu. 6 Kuhani mkuu Anasi alikuwepo. Kayafa, Yohana, Iskanda na jamaa wengine wa kuhani mkuu walikuwepo pia. 7 Waliwasimamisha Petro na Yohana mbele ya watu wote. Wakawauliza maswali mengi, “Mliwezaje kumponya mlemavu wa miguu huyu? Mlitumia nguvu gani? Mmefanya hili kwa mamlaka ya nani?”
8 Ndipo Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akawaambia, “Enyi watawala nanyi wazee wa watu, 9 mnatuuliza leo ni nini tulifanya kumsaidia huyu mlemavu wa miguu? Mnatuuliza nini kilimponya? 10 Tunataka ninyi nyote na watu wote wa Israeli mtambue kuwa mtu huyu aliponywa na nguvu ya Yesu Kristo kutoka Nazareti. Mlimpigilia Yesu msalabani, lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Mtu huyu alikuwa mlemavu wa miguu, lakini sasa ni mzima. Anaweza kusimama hapa mbele zenu kwa sababu ya nguvu ya Yesu! 11 Yesu ndiye
12 Yesu peke yake ndiye anayeweza kuokoa watu. Jina lake ndiyo nguvu pekee iliyotolewa kumwokoa mtu yeyote ulimwenguni. Ni lazima tuokoke kupitia yeye!”
13 Viongozi wa Kiyahudi walijua kuwa Petro na Yohana walikuwa watu wa kawaida wasio na elimu yo yote. Lakini walikuwa wanazungumza kwa ujasiri bila woga; viongozi walishangaa. Walitambua pia kuwa Petro na Yohana walikuwa pamoja na Yesu. 14 Walimwona aliyeponywa akiwa amesimama kwa miguu yake mwenyewe pembeni mwa mitume. Na hivyo walishindwa kuzungumza chochote kilicho kinyume na mitume.
15 Viongozi wa Kiyahudi wakawaambia mitume watoke nje ya chumba cha mkutano wa baraza. Kisha viongozi wakajadiliana wao wenyewe juu ya nini wanachopaswa kufanya. 16 Wakaulizana, “Tuwafanye nini watu hawa? Kila mtu katika Yerusalemu anajua kuhusu muujiza walioufanya kama ishara kutoka kwa Mungu. Ni dhahiri, hatuwezi kusema muujiza huo haukufanyika. 17 Lakini ni lazima tuwatishe ili wasiendelee kuwaambia watu kutumia jina lile.[b] Ili tatizo hili lisisambae miongoni mwa watu.”
18 Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaita Petro na Yohana ndani tena. Wakawaambia wasiseme wala kufundisha kitu chochote kwa kutumia jina la Yesu. 19 Lakini Petro na Yohana wakawajibu, “Mnadhani kipi ni sahihi? Mungu angetaka nini? Je, tunapaswa kuwatii ninyi au tumtii Mungu? 20 Hatuwezi kukaa kimya. Ni lazima tuwaambie watu kuhusu yale tuliyoona na kusikia.”
21-22 Viongozi wa Kiyahudi hawakupata sababu za kuwaadhibu mitume, kwa sababu watu wote walikuwa wanamsifu Mungu kwa kile kilichotendeka. Muujiza huu ulikuwa ishara kutoka kwa Mungu. Mtu aliyeponywa alikuwa na miaka zaidi ya arobaini. Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaonya mitume tena na kuwaacha waende wakiwa huru.
Petro na Yohana Warudi kwa Waamini
23 Petro na Yohana waliondoka kwenye mkutano wa viongozi wa Kiyahudi na kurudi kwa waamini wenzao. Wakalieleza kundi la waamini kila kitu walichoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 24 Waamini waliposikia hili, wote kwa pamoja wakamwomba Mungu wakiwa na nia moja. Wakasema, “Bwana wa wote, wewe ndiye uliyeumba mbingu, dunia, bahari na kila kitu ulimwenguni. 25 Baba yetu Daudi alikuwa mtumishi wako. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliandika maneno haya:
‘Kwa nini mataifa yanatenda kwa kiburi?
Kwa nini watu wanapanga mipango isiyofaa kama hii?
26 Wafalme wa dunia hujiandaa kwa mapigano,
na watawala hukusanyika pamoja kinyume na Bwana
na kinyume na Masihi wake.’(B)
27 Ndicho hasa kilichotokea wakati Herode, Pontio Pilato, mataifa mengine na watu wa Israeli walipokusanyika pamoja hapa Yerusalemu wakawa kinyume na Yesu; Masihi, Mtumishi wako mtakatifu. 28 Watu hawa waliokusanyika pamoja kinyume na Yesu waliwezesha mpango wako kukamilika. Ilifanyika kwa sababu ya nguvu zako na matakwa yako. 29 Na sasa, Bwana, sikiliza wanayosema. Wanajaribu kututisha. Sisi ni watumishi wako. Tusaidie ili tuseme yale unayotaka tuseme bila kuogopa. 30 Tusaidie, ili tuwe jasiri kwa kutuonesha nguvu zako. Ponya Wagonjwa. Fanya ishara na maajabu kutokea kwa mamlaka[c] ya Yesu mtumishi wako mtakatifu.”
31 Baada ya waamini kuomba, mahali walipokuwa palitikisika. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, na wakaendelea kuhubiri Habari Njema bila woga.
Ushirika wa Waamini
32 Kundi lote la waamini waliungana katika kuwaza na katika mahitaji yao. Hakuna aliyesema vitu alivyokuwa navyo ni vyake peke yake. Badala yake walishirikiana kila kitu. 33 Kwa nguvu kuu mitume walifanya ijulikane kwa kila mmoja kwamba Bwana Yesu alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na Mungu aliwabariki sana waamini wote. 34 Hakuna aliyepungukiwa kitu. Kila aliyemiliki shamba au nyumba aliuza na kuleta pesa alizopata, 35 na kuzikabidhi kwa mitume. Kisha kila mtu akapewa kiasi alichohitaji.
36 Mmoja wa waamini aliitwa Yusufu. Mitume walimwita Barnaba, jina linalomaanisha “Mtu anayewatia moyo wengine.” Alikuwa Mlawi mzaliwa wa Kipro. 37 Yusufu aliuza shamba alilomiliki. Akaleta pesa na kuwapa mitume.
Anania na Safira
5 Alikuwepo mtu aliyeitwa Anania na mke wake aliyeitwa Safira. Anania aliuza shamba lake, 2 lakini aliwapa mitume sehemu tu ya pesa alizopata baada ya kuuza shamba lake. Kwa siri alibakiza kiasi cha pesa kwa ajili yake mwenyewe. Mke wake alilijua hili na akalikubali.
3 Petro akasema, “Anania, kwa nini umemruhusu Shetani aitawale akili yako kwa wazo la namna hii? Umebakiza sehemu ya pesa kwa ajili yako mwenyewe na kumdanganya Roho Mtakatifu! 4 Je, kabla ya kuuza shamba, halikuwa lako? Na hata baada ya kuliuza, ungeweza kutumia pesa kwa namna yoyote unayotaka. Imekuwaje hata ufikirie kufanya jambo hili? Hukutudanganya sisi bali Mungu!”
5-6 Anania aliposikia hili, alianguka chini na kufa. Baadhi ya vijana wakaja na kuufunga mwili wake. Wakautoa nje na kuuzika. Kila mtu aliyelisikia hili aliingiwa hofu.
7 Baada ya kama saa tatu baadaye, mkewe naye alifika. Safira hakujua kilichompata mumewe. 8 Petro akamwambia, “Niambie mlipata pesa kiasi gani baada ya kuuza shamba lenu. Kilikuwa kiasi hiki?”
Safira akajibu, “Ndiyo, hicho ndicho tulichopata baada ya kuuza shamba.”
9 Petro akamwambia, “Kwa nini wewe na mume wako mlikubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Unasikia vishindo hivyo vya miguu? Watu waliomzika mume wako, wako mlangoni. Watakuchukua nje kwa njia hiyo hiyo.” 10 Safira akaanguka miguuni kwa Petro na kufa papo hapo. Vijana wakaingia, walipomwona amekwisha kufa, walimchukua na kumzika kando ya mume wake. 11 Kanisa lote na watu wote waliosikia kuhusu hili waliingiwa hofu.
Uthibitisho kutoka kwa Mungu
12 Mitume walipewa nguvu ya kufanya ishara nyingi za miujiza na maajabu katikati ya watu. Walikuwa wanakutanika pamoja mara kwa mara katika eneo la Hekalu lililoitwa Ukumbi wa Sulemani. 13 Hakuna mtu yeyote ambaye hakuwa mwamini alikaa na kushirikiana nao, lakini kila mtu alisema mambo mazuri juu yao. 14 Watu wengi zaidi na zaidi walimwamini Bwana; na watu wengi, wanaume kwa wanawake waliongezwa katika kundi la waamini. 15 Hivyo watu waliwatoa wagonjwa majumbani na kuwaweka mitaani katika vitanda vidogo na mikeka. Walitumaini kuwa ikiwa Petro atapita karibu yao na kivuli chake kikawaangukia watapona. 16 Watu walikuja kutoka katika miji kuzunguka Yerusalemu. Waliwaleta wagonjwa au waliosumbuliwa na pepo wachafu. Wote waliponywa.
Mitume Wakamatwa
17 Kuhani mkuu na wafuasi wake wote wa karibu, kundi liitwalo Masadukayo wakaingiwa wivu sana. 18 Waliwakamata mitume na kuwafunga katika gereza la mji. 19 Lakini wakati wa usiku, malaika wa Bwana alifungua milango ya gereza. Malaika akawaongoza mitume nje ya gereza na kusema, 20 “Nendeni mkasimame katika eneo la Hekalu. Waelezeni watu kila kitu kuhusu maisha haya mapya.” 21 Mitume waliposikia hili, walifanya kama walivyoambiwa. Walikwenda katika eneo la Hekalu asubuhi na mapema jua lilipokuwa linachomoza na kuanza kuwafundisha watu.
Kuhani mkuu na wafuasi wake wakakusanyika na kuitisha mkutano wa Baraza kuu na wazee wa Kiyahudi. Wakawatuma baadhi ya watu gerezani ili wawalete mitume kwao. 22 Watu wale walipokwenda gerezani, hawakuwaona mitume. Hivyo walirudi na kuwaambia viongozi wa Kiyahudi kuhusu hili. 23 Walisema, “Gereza lilikuwa limefungwa na milango ilikuwa imefungwa. Walinzi walikuwa wamesimama milangoni. Lakini tulipofungua milango, gereza lilikuwa tupu!” 24 Mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani walipolisikia hili, walichanganyikiwa na kujiuliza maana yake ni nini.
25 Ndipo mtu mwingine akaja na kuwaambia, “Sikilizeni! Watu mliowafunga gerezani wamesimama katika eneo la Hekalu wanawafundisha watu!” 26 Mkuu wa walinzi na askari walinzi wa Hekalu walikwenda na kuwarudisha mitume. Lakini askari hawakutumia nguvu, kwa sababu waliwaogopa watu. Waliogopa watu wangewapiga kwa mawe mpaka wafe.
27 Askari waliwaleta mitume na kuwasimamisha mbele ya baraza. Kuhani mkuu akawauliza. 28 Akisema, “Tuliwaambia msifundishe tena kwa kutumia jina lile. Lakini tazameni mlichofanya! Mmeujaza mji wa Yerusalemu kwa mafundisho yenu. Na mnajaribu kutulaumu sisi kwa sababu ya kifo chake.”
29 Petro na mitume wengine wakajibu, “Ni lazima tumtii Mungu, siyo wanadamu! 30 Mlimwua Yesu kwa kumpigilia msalabani. Lakini Mungu, Mungu yule yule wa Baba zetu, alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. 31 Yesu ndiye ambaye Mungu amemtukuza kwa kumpa nafasi upande wake wa kuume. Amemfanya kuwa Kiongozi na Mwokozi wetu. Mungu alifanya hivi ili kuwapa watu wote wa Israeli fursa ya kubadilika na kumgeukia Mungu ili dhambi zao zisamehewe. 32 Tuliona mambo haya yote yakitokea, na tunathibitisha kuwa ni ya kweli. Pia, Roho Mtakatifu anaonesha kuwa mambo haya ni ya kweli. Mungu amemtoa Roho huyu kwa ajili ya wote wanaomtii Yeye.”
33 Wajumbe wa Baraza waliposikia haya, walikasirika sana. Walianza kupanga namna ya kuwaua mitume. 34 Lakini mjumbe mmoja wa Baraza, Farisayo aliyeitwa Gamalieli, akasimama, alikuwa mwalimu wa sheria na watu wote walimheshimu. Aliwaambia wajumbe wawatoe nje mitume kwa dakika chache. 35 Kisha akawaambia, “Wanaume wa Israeli, iweni waangalifu kwa kile mnachopanga kuwatendea watu hawa. 36 Mnakumbuka Theuda alipotokea? Alijidai kuwa alikuwa mtu mkuu, na wanaume kama mia nne waliungana naye. Lakini aliuawa na wote waliomfuata walitawanyika. 37 Baadaye, wakati wa sensa, mtu mmoja aitwaye Yuda alikuja kutoka Galilaya. Watu wengi walijiunga kwenye kundi lake, lakini yeye pia aliuawa na wafuasi wake wote walitawanyika. 38 Na sasa ninawaambia, kaeni mbali na watu hawa. Waacheni. Ikiwa mpango wao ni kitu walichopanga wao wenyewe, utashindwa. 39 Lakini ikiwa ni mpango wa Mungu, hamtaweza kuwazuia. Mnaweza kuwa mnapigana kinyume na Mungu mwenyewe!”
Viongozi wa Kiyahudi wakakubaliana na kile alichosema Gamalieli. 40 Wakawaita mitume ndani tena. Wakawachapa viboko na kuwakanya waache kusema na watu kwa kutumia jina la Yesu. Kisha wakawaachia huru. 41 Mitume waliondoka kwenye mkutano wa Baraza, wakifurahi kwamba wamepewa heshima ya kudharauliwa kwa ajili ya Yesu. 42 Mitume hawakuacha kuwafundisha watu. Waliendelea kuzisema Habari Njema, kwamba Yesu ni Masihi. Walifanya hivi kila siku katika eneo la Hekalu na katika nyumba za watu.
Watu Saba Wachaguliwa kwa Kazi Maalumu
6 Watu wengi zaidi walipokuwa wafuasi wa Yesu. Wafuasi waliokuwa wakizungumza Kiyunani walianza kuwalalamikia wafuasi wenzao waliokuwa wanazungumza Kiebrania au Kiaramu. Walisema kuwa wajane wao walikuwa hawapewi mgao wao kutokana na kile wafuasi walikuwa wanapewa kila siku. 2 Mitume kumi na mbili wakaita kundi lote la wafuasi pamoja.
Mitume wakawaambia, “Haitakuwa sahihi sisi kuacha kazi yetu ya kuwafundisha watu neno la Mungu ili tuwe wasimamizi wa ugawaji wa chakula kwa watu. 3 Hivyo, kaka zetu na dada zetu, chagueni wanaume saba miongoni mwenu wenye ushuhuda mzuri, watu waliojaa hekima na Roho. Nasi tutawaweka kuwa wasimamizi wa kazi hii muhimu. 4 Na hivyo itatuwezesha sisi kutumia muda wetu wote katika kuomba na kufundisha neno la Mungu.”
5 Kundi lote la waamini likakubaliana na wazo hili. Hivyo wakawachagua wanaume saba: Stefano (aliyejaa imani na Roho Mtakatifu), Filipo,[d] Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena, na Nikolasi (mtu wa Antiokia aliyeongoka na kufuata dini ya Kiyahudi). 6 Kisha, wakawaweka watu hawa mbele ya mitume, nao mitume waliwaombea na kuweka mikono juu yao.
7 Neno la Mungu lilikuwa linawafikia watu wengi zaidi. Kundi la wafuasi katika Yerusalemu likawa kubwa sana. Hata idadi kubwa ya makuhani wa Kiyahudi waliamini na kutii.
Baadhi ya Wayahudi Wampinga Stefano
8 Mungu alimpa Stefano nguvu ya kutenda maajabu makuu na miujiza katikati ya watu. 9 Lakini baadhi ya Wayahudi pale waliotoka katika sinagogi la Watu Huru,[e] kama lilivyoitwa. Kundi hili lilijumuisha Wayahudi kutoka Kirene, Iskanderia, Kilikia na Asia. Walianza kubishana na Stefano. 10 Lakini Roho Mtakatifu alimwezesha kuzungumza kwa hekima. Maneno yake yalikuwa na nguvu hata Wayahudi hawa hawakuweza kubishana naye.
11 Hivyo wakawaambia baadhi ya watu waseme, “Tumemsikia Stefano akimtukana Musa na Mungu!” 12 Jambo hili liliwakasirisha sana watu, wazee wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Wakamkamata Stefano na kumpeleka mbele ya Baraza Kuu.
13 Wayahudi wakawaleta baadhi ya watu kwenye mkutano ili kusema uongo kuhusu Stefano. Watu hawa walisema, “Daima mtu huyu husema maneno kinyume na mahali hapa patakatifu na kinyume na Sheria ya Musa. 14 Tulimsikia akisema kwamba Yesu kutoka Nazareti atapaharibu mahali hapa na kubadilisha yale ambayo Musa aliyotuambia kufanya.” 15 Kila mtu aliyekuwa kwenye mkutano wa baraza alikuwa akimshangaa Stefano kwani uso wake ulionekana kama uso wa malaika.
© 2017 Bible League International