Beginning
Luka Aandika Kitabu Kingine
1 Mpendwa Theofilo:
Katika kitabu cha kwanza niliandika kuhusu kila kitu ambacho Yesu alitenda na kufundisha tangu mwanzo 2 mpaka siku alipochukuliwa juu mbinguni. Kabla hajaondoka, alizungumza na mitume aliowachagua kwa msaada wa Roho Mtakatifu kuhusu mambo waliyotakiwa kufanya. 3 Hii ilikuwa baada ya kifo chake, ambapo aliwathibitishia kwa namna nyingi kuwa alikuwa hai. Mitume walimwona Yesu mara nyingi kwa muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kutoka kwa wafu. Naye Yesu alizungumza nao kuhusu ufalme wa Mungu. 4 Wakati mmoja Yesu alipokuwa akila pamoja nao, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu. Aliwaambia, “Kaeni hapa mpaka mtakapopokea kile ambacho Baba aliahidi kutuma. Kumbukeni, niliwaambia juu yake. 5 Yohana aliwabatiza watu kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
Yesu Achukuliwa Juu Mbinguni
6 Mitume walipokuwa pamoja, walimwuliza Yesu, “Bwana, huu ni wakati wako wa kuwarudishia Waisraeli ufalme wao tena?”
7 Yesu akawaambia, “Baba peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na nyakati. Si juu yenu kujua. 8 Lakini Roho Mtakatifu atawajia na kuwapa nguvu. Nanyi mtakuwa mashahidi wangu. Mtawahubiri watu kuhusu mimi kila mahali, kuanzia humu Yerusalemu, Uyahudi yote, katika Samaria na hatimaye kila mahali ulimwenguni.”
9 Baada ya kusema haya, alichukuliwa juu mbinguni. Walipokuwa wanaangalia juu angani, wingu lilimficha na hawakuweza kumwona. 10 Walikuwa bado wanatazama angani alipokuwa anakwenda. Ghafla malaika wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama pembeni mwao. 11 Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, kwa nini mmesimama hapa na mnatazama angani? Mlimwona Yesu akichukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni. Atarudi katika namna hii hii kama mlivyomwona akienda.”
Mtume Mpya Achaguliwa
12 Ndipo mitume walirudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, ulio umbali wa kama kilomita moja[a] kutoka Yerusalemu. 13 Walipoingia mjini, walikwenda kwenye chumba cha ghorofani walikokuwa wanakaa. Hawa ndiyo wale waliokuwepo: Petro, Yohana, Yakobo, na Andrea, Filipo, Thomasi, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo (mwana wa Alfayo), na Simoni Mzelote, na Yuda (mwana wa Yakobo).
14 Mitume hawa wote walikuwa pamoja na waliomba kwa nia moja. Baadhi ya wanawake, Mariamu mama wa Yesu na wadogo zake Bwana Yesu walikuwepo pale pamoja na mitume.
15 Baada ya siku chache waamini waliokuwa kama mia moja na ishirini walikutana pamoja. Petro alisimama na kusema, 16-17 “Kaka na dada zangu, katika Maandiko Roho Mtakatifu alisema kupitia Daudi kwamba jambo fulani lazima litatokea. Alizungumza kuhusu Yuda, yule aliyekuwa katika kundi letu wenyewe. Yuda alihudumu pamoja nasi. Roho alisema Yuda atawaongoza watu kumkamata Yesu.”
18 (Kwa kufanya hili Yuda alilipwa pesa. Alinunulia shamba pesa hizo. Lakini aliangukia kichwa chake, mwili wake ukapasuka, na matumbo yake yote yakamwagika nje. 19 Na watu wote wa Yerusalemu wanalijua hili. Ndiyo maana waliliita shamba hilo Akeldama, ambalo maana yake kwa Kiaramu ni “Shamba la Damu”.)
20 Petro akasema, “Katika kitabu cha Zaburi, jambo hili limeandikwa kuhusu Yuda:
‘Watu wasipakaribie mahali pake;
Yeyote asiishi hapo.’(A)
Pia imeandikwa kuwa:
‘Mtu mwingine achukue kazi yake.’(B)
21-22 Hivyo ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi ili awe shahidi wa ufufuo wa Bwana Yesu. Ni lazima awe mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana Yesu alipokuwa pamoja nasi. Ni lazima awe yule ambaye amekuwa pamoja nasi tangu Yohana alipokuwa anabatiza watu mpaka siku ambayo Bwana Yesu alichukuliwa kutoka kwetu na kwenda mbinguni.”
23 Kisha waliwasimamisha watu wawili mbele ya kundi. Mmoja aliitwa Yusufu Barsaba, ambaye pia aliitwa Yusto. Mwingine aliitwa Mathiasi. 24-25 Wakaomba wakisema, “Bwana unajua mioyo ya watu wote. Tuonyeshe kati ya watu hawa wawili uliyemchagua kufanya kazi hii. Yuda aliiacha na kuifuata njia yake. Bwana tuonyeshe ni nani achukue sehemu yake kama mtume!” 26 Kisha wakapiga kura kumchagua mmoja kati ya watu hao wawili. Kura ikaonesha Mathiasi ndiye Bwana anamtaka. Hivyo akawa mtume pamoja na wale wengine kumi na moja.
Kuja kwa Roho Mtakatifu
2 Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. 2 Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. 3 Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. 4 Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi.
5 Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. 6 Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.
7 Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya.[b] 8 Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: 9 Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, 11 Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.”
12 Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” 13 Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa.
Petro Azungumza na Watu
14 Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15 Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16 Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:
17 ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
Vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 Katika siku hizo nitaimimina Roho
yangu kwa watumishi wangu,
wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19 Nitafanya maajabu juu angani.
Nitasababisha ishara chini duniani.
Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20 Jua litakuwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21 Na kila amwombaye Bwana’[c] ataokolewa.(C)
22 Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. 23 Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. 24 Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia. 25 Daudi alilisema hili kuhusu Yesu:
‘Sijasahau kuwa Bwana yu pamoja nami.
Yupo hapa pembeni yangu,
hivyo hakuna kinachoweza kunidhuru.
26 Ndiyo sababu ninafurahi sana,
na ninaimba kwa furaha!
Lipo tumaini hata kwa ajili ya mwili wangu huu dhaifu,
27 kwa sababu wewe Bwana hutaniacha kaburini.[d]
Hautauacha mwili wa mtumishi wako mwaminifu[e] kuozea huko.
28 Umenionyesha njia iendayo uzimani.
Kuwa pamoja nawe kutanijaza furaha.’(D)
29 Ndugu zangu, ninaweza kuwaambia kwa ujasiri kuhusu Daudi, baba yetu mkuu. Alikufa, akazikwa, na kaburi lake liko hapa pamoja nasi hata leo. 30 Alikuwa nabii na alijua kitu ambacho Mungu alisema. Mungu alimwahidi Daudi kwa kuweka Agano kuwa mzaliwa katika familia yake mwenyewe ataketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi kama mfalme.[f] 31 Daudi aliliona hili kabla halijatokea. Ndiyo maana alisema hivi kuhusu mfalme ajaye:
‘Hakuachwa kaburini.
Mwili wake haukuozea humo.’[g]
Daudi alizungumza kuhusu Masihi kufufuka kutoka kwa wafu. 32 Yesu ndiye ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi sote ni mashahidi wa jambo hili. Tulimwona. 33 Yesu alichukuliwa juu mbinguni. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu. Baba amempa Roho Mtakatifu, kama alivyoahidi. Hivyo Yesu amemimina huyo Roho Mtakatifu na hiki ndicho mnachoona na kusikia 34 Daudi hakuchukuliwa mpaka mbinguni. Daudi mwenyewe alisema,
‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kuume
35 hadi nitakapowaweka maadui zako chini ya udhibiti wako.’[h](E)
36 Hivyo, watu wote wa Israeli wanapaswa kulijua hili bila kuwa na mashaka: Mungu amemfanya Yesu kuwa Bwana na Masihi. Ndiye yule mliyempigilia msalabani!”
37 Watu waliposikia hili wakahuzunika sana. Wakawauliza Petro na mitume wengine, “Ndugu zetu, tufanye nini?”
38 Petro akawaambia, “Geuzeni mioyo na maisha yenu na kila mmoja wenu abatizwe katika jina la Yesu Kristo. Ndipo Mungu atawasamehe dhambi zenu, na mtapokea zawadi ya Roho Mtakatifu. 39 Ahadi hii ni kwa ajili yenu ninyi, watoto wenu na vizazi vijavyo. Ni kwa kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu anamwita kwake mwenyewe.”
40 Petro aliwaonya kwa maneno mengine mengi; aliwasihi, akawaambia, “Jiokoeni na uovu unaofanywa na watu wanaoishi sasa!” 41 Ndipo wale walioyakubali yale aliyosema Petro wakabatizwa. Yapata watu elfu tatu waliongezwa kwenye kundi la waamini siku ile.
Ushirika wa Waamini
42 Waamini walitumia muda wao kusikiliza mafundisho ya mitume. Walishirikiana kila kitu kwa pamoja. Walikula[i] na kuomba pamoja. 43 Maajabu mengi na ishara nyingi zilikuwa zinatokea kupitia mitume, na hivyo kila mtu aliingiwa na hofu na akamtukuza Mungu. 44 Waamini wote walikaa pamoja, na kushirikiana kila kitu. 45 Waliuza mashamba yao na vitu walivyomiliki, kisha wakatoa fedha na kuwapa wenye kuhitaji. 46 Waamini waliendelea kukutana pamoja katika eneo la Hekalu. Pia walikula pamoja katika nyumba zao. Walikuwa na furaha kushirikiana chakula chao na walikula kwa mioyo mikunjufu. 47 Waamini walimsifu Mungu na waliheshimiwa na watu wote. Watu wengi zaidi waliokolewa kila siku, na Bwana alikuwa akiwaongeza kwenye kundi lao.
Petro Amponya Kiwete
3 Siku moja Petro na Yohana walikwenda eneo la Hekalu saa tisa mchana, muda wa kusali na kuomba Hekaluni kama ilivyokuwa desturi. 2 Walipokuwa wanaingia katika eneo la Hekalu, mtu aliyekuwa mlemavu wa miguu maisha yake yote alikuwa amebebwa na baadhi ya rafiki zake waliokuwa wanamleta Hekaluni kila siku. Walimweka pembezoni mwa mojawapo ya Malango nje ya Hekalu. Lango hilo liliitwa Lango Zuri. Na mtu huyo alikuwa akiwaomba pesa watu waliokuwa wanaingia Hekaluni. 3 Siku hiyo alipowaona Petro na Yohana wakiingia eneo la Hekalu, aliwaomba pesa.
4 Petro na Yohana, walimtazama mtu huyo, wakamwambia, “Tutazame!” 5 Akawatazama akitumaini kuwa wangempa pesa. 6 Lakini Petro akasema, “Sina fedha wala dhahabu yoyote, lakini nina kitu kingine ninachoweza kukupa. Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama na utembee!”
7 Kisha Petro akamshika mkono wake wa kulia, akamnyenyua na kumsimamisha. Ndipo nyayo na vifundo vyake vikatiwa nguvu papo hapo. 8 Akaruka juu, akasimama kwa miguu yake na akaanza kutembea. Akaingia ndani ya eneo la Hekalu pamoja nao huku akitembea na kurukaruka akimsifu Mungu. 9-10 Watu wote walimtambua. Walimjua kuwa ni mlemavu wa miguu ambaye mara nyingi huketi kwenye Lango Zuri la Hekalu akiomba pesa. Lakini sasa walimwona anatembea na kumsifu Mungu. Walishangaa na hawakuelewa hili limewezekanaje.
Petro Azungumza na Watu
11 Huku wakishangaa, watu wale waliwakimbilia Petro na Yohana pale walikokuwa katika Ukumbi wa Sulemani. Mtu yule aliyeponywa alikuwa akingali amewang'anga'nia Petro na Yohana.
12 Petro alipoona hili, aliwaambia watu: “Ndugu zangu Wayahudi, kwa nini mnashangaa hili? Mnatutazama kama vile ni kwa nguvu zetu tumemfanya mtu huyu atembee. Mnadhani hili limetendeka kwa sababu sisi ni wema? 13 Hapana, Mungu ndiye aliyetenda hili! Ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Ni Mungu aliyeabudiwa na baba zetu wote. Kwa kufanya hili, alimtukuza Yesu mtumishi wake, yule ambaye ninyi mlimtoa ili auawe. Pilato alipotaka kumwachia huru, mlimwambia Pilato kuwa hamumtaki Yesu. 14 Yesu alikuwa Mtakatifu na mwema, lakini mlimkataa na badala yake mlimwambia Pilato amwache huru mwuaji[j] na awape ninyi. 15 Na hivyo mlimwua yule awapaye uzima! Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi ni mashahidi wa jambo hili kwani tuliliona kwa macho yetu wenyewe.
16 Huyu mlemavu wa miguu ameponywa kwa sababu tunalo tumaini katika Yesu. Nguvu ya Yesu ndiyo iliyomponya. Mnamwona na mnamfahamu mtu huyu. Ameponywa kabisa kwa sababu ya imani inayotokana na Yesu. Ninyi nyote mmeona hili likitokea!
17 Kaka zangu, ninajua kwamba hamkujua mlilomtendea Yesu wakati ule. Hata viongozi wenu hawakujua walilokuwa wanatenda. 18 Lakini Mungu alikwishasema kupitia manabii kuwa mambo haya yangetokea. Masihi wake angeteseka na kufa. Nimewaambia jinsi ambavyo Mungu alifanya jambo hili likatokea. 19 Hivyo lazima mbadili mioyo na maisha yenu. Mrudieni Mungu, naye atawasamehe dhambi zenu. 20 Kisha Bwana atawapa muda wa faraja kutokana na masumbufu yenu. Atamtuma Yesu kwenu, aliyemchagua kuwa Masihi wenu.
21 Lakini Yesu lazima akae mbinguni mpaka wakati ambapo kila kitu kitafanywa upya tena. Mungu alikwisha sema kuhusu wakati huu tangu zamani kupitia manabii wake watakatifu. 22 Musa alisema, ‘Bwana Mungu wako atakupa nabii. Nabii huyo atatoka miongoni mwa watu wako. Atakuwa kama mimi. Ni lazima mtii kila kitu atakachowaambia. 23 Na yeyote atakayekataa kumtii nabii huyo atakufa na kutengwa na watu wa Mungu.’(F)
24 Samweli, na manabii wengine wote walisema kwa niaba ya Mungu. Baada ya Samweli, walisema kuwa wakati huu ungekuja. 25 Na kile ambacho manabii walikisema ni kwa ajili yenu ninyi wazaliwa wao. Mmepokea Agano ambalo Mungu alilifanya na baba zenu. Mungu alimwambia baba yenu Ibrahimu kuwa, ‘Kila taifa duniani litabarikiwa kupitia wazaliwa wako.’(G) 26 Mungu amemtuma Yesu, mtumishi wake maalumu. Alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kuwageuza kila mmoja wenu aache njia zake za uovu.”
© 2017 Bible League International