Beginning
Yesu Aiosha Miguu ya Wafuasi wake
13 Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Yesu alijua kwamba wakati wake wa kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ulikuwa umefika. Daima Yesu aliwapenda watu wa ulimwengu huu waliokuwa wake. Huu ulikuwa wakati alipowaonesha upendo wake mkuu.
2 Yesu na wafuasi wake walikuwa wakila chakula cha jioni. Ibilisi alikuwa tayari amekwisha kumshawishi Yuda Iskariote kumsaliti Yesu kwa maadui zake. (Yuda alikuwa Mwana wa Simoni.) 3 Baba alikuwa amempa Yesu uwezo juu ya kila kitu. Naye Yesu alilifahamu hili. Alijua pia kuwa yeye alitoka kwa Mungu. Tena alijua kuwa alikuwa anarudi kwa Mungu. 4 Kwa hiyo walipokuwa wakila,[a] Yesu alisimama na kulivua vazi lake. Akachukua taulo na kuifunga kiunoni mwake. 5 Kisha akamimina maji katika bakuli na kuanza kuwaosha miguu[b] wafuasi wake. Kisha akaifuta miguu yao kwa taulo aliolifunga kiunoni mwake.
6 Akamfikia Simoni Petro, naye Simoni Petro akamwambia, “Bwana, huwezi kuiosha miguu yangu.”
7 Yesu akamjibu, “Huyaelewi ninayofanya hivi sasa. Lakini utayaelewa baadaye.”
8 Petro akasema, “Hapana! Huwezi kamwe kuniosha miguu yangu kamwe.”
Yesu akamjibu, “Kama sitakuosha miguu yako, basi hutakuwa miongoni mwa watu wangu.”
9 Simoni Petro akasema, “Bwana, utakapomaliza miguu, unioshe mikono na kichwa pia!”
10 Yesu akamwambia, “Baada ya mtu kuoga, mwili wake wote huwa safi. Anahitaji tu kunawa miguu. Nanyi mko safi, lakini sio nyote.” 11 Yesu alimjua yule atakayemsaliti mbele ya adui zake. Ndiyo maana alisema, “Sio wote mlio safi.”
12 Yesu alipomaliza kuwaosha miguu wafuasi, alivaa nguo zake na kurudi pale mezani. Akawauliza, “Je, mmelielewa nililowafanyia? 13 Mnaniita mimi ‘Mwalimu’. Tena mnaniita mimi ‘Bwana’. Hayo ni sahihi, kwa sababu hivyo ndivyo nilivyo. 14 Mimi ni Bwana na Mwalimu wenu. Lakini niliwaosha miguu yenu kama mtumishi. Hivyo nanyi mnapaswa kuoshana miguu yenu. 15 Nilifanya hivyo kama mfano. Hivyo nanyi mnapaswa kuhudumiana ninyi kwa ninyi kama nilivyowahudumia. 16 Mniamini mimi, watumishi huwa sio wakubwa kuzidi bwana zao. Wale waliotumwa kufanya jambo fulani sio wakubwa kumzidi yule aliyewatuma. 17 Sasa, mkielewa maana ya yale niliyotenda, Mungu atawabariki mkiyatendea kazi.
18 Nami sizungumzii habari zenu nyote. Nawafahamu watu wale niliowachagua. Lakini Maandiko yanapaswa kutimia kama yanavyosema: ‘Mtu aliyekula chakula pamoja nami amenigeuka.’[c] 19 Ninawaambia hili sasa kabla halijatokea. Hivyo litakapotokea, mtaweza kuamini kuwa MIMI NDIYE.[d] 20 Hakika nawaambieni, yeyote anayempokea mtu yule niliyemtuma ananipokea mimi pia. Na yeyote anayenipokea mimi humpokea pia yeye aliyenituma.”
Yesu Amtaja Atakayemgeuka
(Mt 26:20-25; Mk 14:17-21; Lk 22:21-23)
21 Baada ya Yesu kuyasema mambo haya, alisumbuka sana moyoni. Akasema kwa uwazi, “Mniamini ninaposema kwamba mmoja wenu atanisaliti kwa maadui zangu.”
22 Wafuasi wake wote wakatazamana wao kwa wao. Hawakuelewa kuwa Yesu alikuwa anamzungumzia nani. 23 Mmoja wa wafuasi wake alikaa karibu na Yesu na alikuwa amemwegemea. Huyu alikuwa yule aliyependwa sana na Yesu. 24 Simoni Petro akaonyesha ishara kwa mfuasi huyo amwulize Yesu alikuwa anamzungumzia nani.
25 Yule mfuasi alisogea karibu sana na Yesu na kumwuliza, “Bwana, ni nani huyo?”
26 Yesu akamjibu, “Nitachovya mkate huu kwenye bakuli. Mtu yule nitakayempa mkate huo ndiye mwenyewe.” Kwa hiyo Yesu akachukua kipande cha mkate, akakichovya, na akampa Yuda Iskariote, Mwana wa Simoni. 27 Yuda alipoupokea mkate ule, Shetani akamwingia. Yesu akamwambia Yuda, “Yale unayotaka kuyafanya, yafanye haraka!” 28 Hakuna hata mmoja pale mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia Yuda hayo. 29 Kwa vile Yuda ndiye aliyekuwa msimamizi wa fedha[e] zao,[f] baadhi yao walidhani kuwa Yesu alikuwa na maana kuwa Yuda aende kununua vitu ambavyo wangehitaji kwa ajili ya sherehe. Au walidhani kuwa Yesu alitaka Yuda aende na kuwapa maskini cho chote.
30 Yuda akaula mkate aliopewa na Yesu. Kisha akatoka nje mara hiyo hiyo. Wakati huo ulikuwa ni usiku.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
31 Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa ni wakati wa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu. Na Mungu ataupokea utukufu kupitia kwake. 32 Kama Mungu hupokea utukufu kupitia kwake, atampa Mwana Utukufu kupitia kwake yeye mwenyewe. Na hilo litatimia haraka sana.”
33 Yesu akasema, “Watoto wangu, nitakuwa nanyi kwa kipindi kifupi tu kijacho. Nanyi mtanitafuta, lakini nawaambia sasa yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: Kule niendako ninyi hamwezi kuja.”
34 “Nawapa amri mpya: Pendaneni ninyi kwa ninyi. Mnapaswa kupendana kama mimi nilivyowapenda ninyi. 35 Endapo mtapendana ninyi kwa ninyi watu wote watatambua kuwa ninyi ni wafuasi wangu.”
Yesu Asema Petro Atamkana
(Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Lk 22:31-34)
36 Simoni Petro akamwuliza Yesu, “Bwana, unaenda wapi?”
Yesu akajibu, “Kule niendako hamwezi kunifuata sasa. Lakini mtanifuata baadaye.”
37 Petro akauliza, “Bwana, kwa nini nisikufuate sasa? Mimi niko radhi kufa kwa ajili yako!”
38 Yesu akajibu, “Je, ni kweli utayatoa maisha yako kwa ajili yangu? Hakika nakwambia, kabla jogoo hajawika, utasema mara tatu kwamba hunijui mimi.”
Yesu Awafariji Wafuasi Wake
14 Yesu akasema, “Msisumbuke. Mwaminini Mungu, na mniamini na mimi. 2 Kuna vyumba vya kutosha katika nyumba ya Baba yangu. Nisingewaambia hivi ikiwa isingelikuwa kweli. Ninaenda huko kuandaa mahali kwa ajili yenu. 3 Nitakapomaliza kuandaa, nitarudi. Kisha nitawachukua ili muwe pamoja nami mahali niliko. 4 Mnaijua njia iendayo kule ninakokwenda.”
5 Thomaso akasema, “Bwana, hatujui unakokwenda, sasa tutaijuaje njia?”
6 Yesu akajibu, “Mimi ndiye njia, kweli, na uzima. Njia pekee ya kwenda kwa Baba ni kupitia kwangu. 7 Kwa kuwa sasa ninyi nyote mmenijua, mtamjua Baba yangu pia. Kwa kweli, sasa mnamjua Baba na mmekwisha kumwona.”
8 Filipo akamwambia, “Bwana, utuonyeshe Baba. Hilo tu ndilo tunalohitaji.”
9 Yesu akajibu, “Nimekuwa pamoja nanyi kwa kipindi kirefu. Hivyo wewe, Filipo unapaswa kunijua. Yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba pia. Hivyo kwa nini unasema, ‘Utuonyeshe Baba’? 10 Hamwamini kuwa mimi nimo ndani ya Baba na Baba naye yumo ndani yangu? Mambo niliyowaambia hayatoki kwangu. Baba anakaa ndani yangu, naye anafanya kazi yake mwenyewe. 11 Mniamini ninaposema kwamba nimo ndani ya Baba na Baba yumo ndani yangu. Vinginevyo muamini kwa sababu ya miujiza niliyoifanya.
12 Hakika nawaambia, yeyote anayeniamini atafanya mambo kama yale niliyoyafanya. Naye atafanya mambo makubwa zaidi ya yale niliyofanya, kwa sababu mimi naenda kwa Baba. 13 Na kama mtaomba jambo lo lote kwa jina langu, nitawafanyia. Kisha utukufu wa Baba utadhihirishwa kupitia kwa Mwana wake. 14 Ikiwa mtaniomba chochote kwa jina langu, mimi nitakifanya.
Ahadi ya Roho Mtakatifu
15 Ikiwa mnanipenda, mtafanya ninayowaagiza. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi[g] mwingine atakayekuwa nanyi siku zote. 17 Huyo Msaidizi ni Roho wa Kweli ambaye watu wa ulimwengu hawawezi kumpokea, kwa sababu hawamwoni wala hawamjui. Lakini ninyi mnamjua kwa kuwa anakaa pamoja nanyi, na atakuwa ndani yenu.
18 Mimi sitawaacha peke yenu kama watu wasiokuwa na wazazi. Bali nitakuja tena kwenu. 19 Katika kipindi kifupi watu wa ulimwengu hawataniona tena. Lakini ninyi mtaniona. Mtaishi kwa sababu mimi ninaishi. 20 Katika siku hiyo mtaelewa kuwa mimi nimo ndani ya Baba. Kadhalika mtajua pia kuwa ninyi mmo ndani yangu nami nimo ndani yenu. 21 Wale wanaonipenda kweli ni wale ambao si tu kwamba wanazijua amri zangu bali pia wanazitii. Baba yangu atawapenda watu wa jinsi hiyo, nami pia nitawapenda. Nami nitajitambulisha kwao.”
22 Kisha Yuda (siyo Yuda Iskariote) akasema, “Bwana, utawezaje kujitambulisha kwetu, lakini si kwa ulimwengu?”
23 Yesu akajibu, “Wale wote wanipendao watayafuata mafundisho yangu. Naye Baba yangu atawapenda. Kisha Baba yangu na mimi tutakuja kwao na kukaa pamoja nao. 24 Lakini yeyote asiyenipenda hafuati mafundisho yangu. Mafundisho haya mnayosikia kwa hakika siyo yangu. Ni kutoka kwa Baba yangu aliyenituma.
25 Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini yule Msaidizi atawafundisha kila kitu na kuwafanya mkumbuke kila nilichowaambia. Huyu Msaidizi ni Roho Mtakatifu[h] ambaye Baba atamtuma kwa jina langu.
27 Nawaachia amani. Ninawapa amani yangu mwenyewe. Ninawapa amani kwa namna tofauti kabisa na jinsi ulimwengu unavyofanya. Hivyo msihangaike. Msiogope. 28 Mlinisikia nikiwaambia, ‘Naondoka, lakini nitakuja tena kwenu.’ Mngenipenda, mngefurahi kuwa naenda kwa Baba, kwa sababu Baba ni mkuu kuliko mimi. 29 Nawaambia haya hivi sasa, kabla hayajatokea. Kisha yatakapotokea, mtaamini.
30 Sitaendelea kuongea nanyi kwa muda mrefu zaidi. Mtawala wa ulimwengu[i] huu anakuja. Hata hivyo hana nguvu juu yangu. 31 Lakini ni lazima ulimwengu utambue kuwa ninampenda Baba. Hivyo ninafanya yale Baba aliyoniambia.
Njooni sasa, twendeni.”
Yesu ni Kama Mzabibu
15 Yesu akasema, “Mimi ndiye mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Yeye hulikata kutoka kwangu kila tawi lisilozaa matunda.[j] Pia hupunguza majani katika kila tawi linalozaa matunda ili kuliandaa liweze kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmewekwa tayari[k] kwa ajili ya kuzaa matunda[l] kutokana na mafundisho yale niliyowapa. 4 Hivyo mkae mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nitakaa nikiwa nimeunganishwa kwenu. Hakuna tawi linaloweza kuzaa matunda likiwa liko peke yake. Ni lazima liwe limeunganishwa katika mzabibu. Ndivyo ilivyo hata kwenu. Hamwezi kutoa matunda mkiwa peke yenu. Ni lazima muwe mmeunganishwa kwangu.
5 Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Mtatoa matunda mengi sana mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nimeunganishwa kwenu. Lakini mkitenganishwa mbali nami hamtaweza kufanya jambo lo lote. 6 Kama hamtaunganishwa nami, basi mtakuwa sawa na tawi lililotupwa pembeni nanyi mtakauka. Matawi yote yaliyokufa jinsi hiyo hukusanywa, hutupwa katika moto na kuchomwa. 7 Hivyo ninyi mbaki mmeunganishwa nami, na mfuate mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, mnaweza kuomba kitu chochote mnachohitaji, nanyi mtapewa. 8 Ninyi mdhihirishe kuwa mmekuwa wafuasi wangu kwa kutoa matunda mengi. Kwani hiyo itamletea Baba utukufu.[m]
9 Mimi nimewapenda kama vile Baba alivyonipenda. Sasa mdumu katika upendo wangu. 10 Nimezitii amri za Baba yangu, naye anaendelea kunipenda. Kwa jinsi hiyo, nami nitaendelea kuwapenda mkizitii amri zangu. 11 Nimewaambia haya ili mpate furaha ya kweli kama ile niliyonayo mimi. Nami ninatamani muwe na furaha iliyo kamilifu. 12 Hii ndiyo amri yangu kwenu: Mpendane ninyi kwa ninyi kama mimi nilivyowapenda. 13 Hakuna anayeweza kuonesha pendo lolote kuu zaidi ya kuwa tayari kufa kwa ajili ya rafiki zake. Upendo wa hali ya juu unaoweza kuoneshwa na watu ni kufa badala ya rafiki zao. 14 Nanyi ni rafiki zangu mnapoyafanya yale ninayowaambia myafanye. 15 Siwaiti tena watumwa, kwa sababu watumwa hawajui yale yanayofanywa na bwana zao. Lakini sasa nawaita marafiki, kwa sababu nimewaambia yote aliyoniambia Baba yangu.
16 Ninyi hamkunichagua mimi. Bali ni mimi niliyewachagua ninyi. Nami niliwapa kazi hii: Kwenda na kutoa matunda; matunda ambayo yatadumu. Ndipo Baba atakapowapa chochote mtakachomwomba katika jina langu. 17 Hii ndiyo amri yangu: Mpendane ninyi kwa ninyi.
Yesu Awatahadharisha wafuasi Wake
18 Endapo ulimwengu utawachukia, mkumbuke kwamba umenichukia mimi kwanza. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu huu, ulimwengu ungewapenda kama watu wake. Lakini ulimwengu unawachukia kwa sababu ninyi siyo wa ulimwengu huu. Badala yake, mimi niliwachagua ninyi ili muwe tofauti na ulimwengu.
20 Kumbukeni somo nililowafundisha: Watumwa sio wakubwa kuliko mabwana wao. Kama watu walinitendea mimi vibaya, watawatendea vibaya hata nanyi pia. Na kama waliyatii mafundisho yangu, watayatii hata ya kwenu pia. 21 Watawatendea yale waliyonitendea mimi, kwa sababu ninyi ni wangu. Wao hawamjui yeye aliyenituma. 22 Kama nisingekuwa nimekuja na kusema na watu wa ulimwengu, basi wasingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa nimekwisha sema nao. Hivyo hawana cha kisingizio cha dhambi zao.
23 Yeyote anayenichukia mimi anamchukia na Baba pia. 24 Mimi nilifanya mambo miongoni mwa watu wa ulimwengu ambayo hayajawahi kufanywa na mtu yeyote mwingine. Kama nisingefanya mambo hayo, wao nao wasingekuwa na hatia ya dhambi. Ijapokuwa waliyaona niliyofanya, bado wananichukia mimi na Baba yangu. 25 Lakini haya yalitokea ili kuweka wazi yaliyoandikwa katika sheria zao: ‘Walinichukia bila sababu yoyote.’”[n]
26 Mimi, “Nitamtuma Msaidizi kutoka kwa Baba. Huyo Msaidizi ni Roho wa kweli anayekuja kutoka kwa Baba. Yeye atakapokuja, atasema juu yangu. 27 Nanyi pia mtawajulisha watu juu yangu, kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.
© 2017 Bible League International