Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Luka 17-18

Dhambi na Msamaha

(Mt 18:6-7,21-22; Mk 9:42)

17 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi yatatokea hakika. Lakini ole wake mtu anayesababisha hili litokee. Ingekuwa vizuri kwa mtu huyo kama jiwe la kusagia lingefungwa shingoni mwake, na akatupwa baharini, kuliko kusababisha mmojawapo wa wanyenyekevu hawa kutenda dhambi. Hivyo iweni waangalifu!

Ikiwa ndugu au dada yako katika familia ya Mungu akikukosea, umwonye. Akitubu, msamehe. Hata kama akikukosea mara saba katika siku moja, lakini akakuomba msamaha kila anapokukosea, msamehe.”

Imani Yako Ni Kubwa Kiasi Gani?

Kisha mitume wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”

Bwana akasema, “Imani yenu ingekuwa kubwa kama mbegu ya haradali, mngeuambia mforosadi huu, ‘Ng'oka, ukajipandikize baharini,’ nao ungewatii.

Iweni Watumishi Wema

Chukulia mmoja wenu ana mtumishi ambaye amekuwa shambani akilima au akichunga kondoo shambani. Akirudi kutoka shambani au machungani, utamwambia nini? Je, utamwambia, ‘Njoo ndani, keti, ule chakula’? Hapana! Utamwambia mtumishi wako, ‘Nitayarishie chakula nile. Jitayarishe na unihudumie. Nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo utakula.’ Mtumishi asipewe shukrani maalumu kwa kufanya kazi yake. Anafanya kile alichoagizwa na mkuu wake. 10 Vivyo hivyo nanyi. Mkimaliza kufanya yote mliyoamriwa kufanya, mseme, ‘Sisi ni watumwa, hatustahili shukrani yoyote maalumu. Tumefanya kazi tunayotakiwa kufanya.’”

Yesu Awaponya Baadhi ya Wayahudi na Msamaria

11 Yesu alikuwa anasafiri kwenda Yerusalemu. Alipotoka Galilaya alisafiri akipita kando ya mpaka wa Samaria. 12 Aliingia katika mji mdogo, na wanaume kumi walimwendea. Hawakumkaribia, kwa sababu wote walikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. 13 Lakini watu wale wakaita kwa kupaza sauti wakisema, “Yesu! Mkuu! Tafadhali utusaidie!”

14 Yesu alipowaona, akasema, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.”[a]

Wale watu kumi walipokuwa wanakwenda kujionesha kwa makuhani, waliponywa. 15 Mmoja wao alipoona kuwa amepona, alirudi kwa Yesu huku akimsifu Mungu kwa kupaza sauti. 16 Akaanguka kifudifudi miguuni pa Yesu, akamshukuru. (Alikuwa Msamaria.) 17 Yesu akasema, “Watu kumi wameponywa, wengine tisa wako wapi? 18 Mtu huyu wala si mmoja wa watu wetu. Ni yeye peke yake aliyerudi kumsifu Mungu?” 19 Ndipo Yesu akamwambia, “Inuka! Unaweza kwenda. Umeponywa kwa sababu uliamini.”

Kuja Kwa Ufalme Wa Mungu

(Mt 24:23-28,37-41)

20 Baadhi ya Mafarisayo walimuuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Yesu akajibu, “Kuja kwa ufalme wa Mungu si kitu unachoweza kuona. 21 Watu hawatasema, ‘Tazama ufalme wa Mungu uko hapa’ au ‘Ule pale!’ Hapana, Ufalme wa Mungu upo hapa pamoja nanyi.”[b]

22 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Wakati utakuja, ambapo mtatamani angalau kuwa na Mwana wa Adamu hata kwa siku moja, lakini hamtaweza. 23 Watu watawaambia, ‘Tazameni, yuko kule!’ au ‘Tazameni, yuko hapa!’ Kaeni pale mlipo; msitoke kwenda kumtafuta. 24 Iweni na subira kwa sababu Mwana wa Adamu atakaporudi, mtatambua. Siku hiyo atang'aa kama mwanga wa radi umulikavyo angani kutoka upande mmoja hadi mwingine. 25 Lakini kwanza, ni lazima Mwana wa Adamu ateseke kwa mambo mengi na watu wa leo watamkataa.

26 Mwana wa Adamu atakaporudi, itakuwa kama ilivyokuwa Nuhu alipoishi. 27 Watu walikuwa wakila, wakinywa, wakioa na kuolewa hata siku Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo gharika ilikuja na kuwaangamiza wote.

28 Ilikuwa vivyo hivyo katika wakati wa Lutu, Mungu alipoteketeza Sodoma. Watu wa Sodoma walikuwa wakila, wakinywa, wakinunua, wakiuza, wakipanda na kujijengea nyumba. 29 Lakini siku ambayo Lutu alitoka Sodoma, moto na baruti vilinyesha kutoka mbinguni na kuwaua wote. 30 Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ambayo Mwana wa Adamu atarudi.

31 Siku hiyo, ikiwa mtu atakuwa juu ya paa ya nyumba yake, hatakuwa na muda wa kushuka kwenda ndani ya nyumba kuchukua vitu vyake. Ikiwa atakuwa shambani, hataweza kurudi nyumbani. 32 Kumbukeni yaliyompata mke wa Lutu![c]

33 Kila atakayejaribu kutunza maisha aliyonayo atayaangamiza. Lakini yeyote atakayeyasalimisha maisha yake atayaokoa. 34 Usiku ule watu wawili wataweza kuwa wamelala katika chumba kimoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 35 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.” 36 [d]

37 Wafuasi wake wakamuuliza, “Hii itakuwa wapi Bwana?”

Yesu akajibu, “Ni kama kuutafuta mzoga, utaupata pale ambapo tai wamekusanyika.”

Mungu Atawajibu Watu Wake

18 Kisha Yesu akawafundisha wafuasi wake kwamba wanapaswa kuomba daima bila kupoteza tumaini. Akatumia simulizi hii kuwafundisha. Akasema, “Kulikuwa na mwamuzi katika mji fulani. Hakumcha Mungu wala hakujali watu walikuwa wanamfikiriaje. Na katika mji huo huo alikuwepo mwanamke mjane. Huyu alimjia mwamuzi huyu mara nyingi akimwambia, ‘Kuna mtu anayenitendea mambo mabaya. Nipe haki yangu!’ Mwanzoni mwamuzi hakutaka kumsaidia yule mwanamke. Lakini baada ya muda kupita, akawaza moyoni mwake yeye mwenyewe, ‘Simchi Mungu. Na sijali watu wananifikiriaje. Lakini mwanamke huyu ananisumbua. Nikimpa haki yake ataacha kunisumbua. Nisipomsaidia, ataendelea kunijia na anaweza kunishambulia.’”

Bwana akasema, “Sikilizeni, maneno aliyosema mwamuzi mbaya yana mafundisho kwa ajili yenu. Daima Mungu atawapa mahitaji yao wateule wanaomwomba usiku na mchana. Hatachelewa kuwajibu. Ninawaambia, Mungu atawapa haki yao watu wake haraka. Lakini Mwana wa Adamu atakaporudi, atawakuta duniani watu ambao bado wanamwamini?”

Farisayo na Mtoza Ushuru

Walikuwepo baadhi ya watu waliojiona kuwa wenye haki na waliwadharau wengine. Yesu alitumia simulizi hii kuwafundisha: 10 “Siku moja Farisayo na mtoza ushuru walikwenda Hekaluni kuomba. 11 Farisayo alisimama peke yake mbali na mtoza ushuru. Farisayo aliomba akisema, ‘Ee Mungu, ninakushukuru kwa kuwa mimi si mwovu kama watu wengine. Mimi siyo kama wezi, waongo au wazinzi. Ninakushukuru kwa kuwa mimi ni bora kuliko huyu mtoza ushuru. 12 Ninafunga mara mbili kwa wiki na kutoa sehemu ya kumi ya vyote ninavyopata!’

13 Mtoza ushuru alisimama peke yake pia. Lakini alipoanza kuomba, hakuthubutu hata kutazama juu mbinguni. Alijipigapiga kifua chake akijinyenyekeza mbele za Mungu. Akasema, ‘Ee Mungu, unihurumie, mimi ni mwenye dhambi.’ 14 Ninawaambia, mtu huyu alipomaliza kuomba na kwenda nyumbani, alikuwa amepatana na Mungu. Lakini Farisayo, aliyejisikia kuwa bora kuliko wengine, hakuwa amepatana na Mungu. Watu wanaojikweza watashushwa. Lakini wale wanaojishusha watakwezwa.”

Yesu Awakaribisha Watoto

(Mt 19:13-15; Mk 10:13-16)

15 Baadhi ya watu waliwaleta hata watoto wao wadogo kwa Yesu ili awawekee mikono kuwabariki. Lakini wafuasi walipoona hili, waliwakataza. 16 Lakini Yesu aliwaalika watoto kwake na kuwaambia wafuasi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu. Msiwazuie, kwa kuwa ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama watoto wadogo hawa. 17 Ukweli ni kwamba, ni lazima uupokee ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo anavyopokea vitu, la si hivyo hautauingia.”

Mtu Tajiri Akataa Kumfuata Yesu

(Mt 19:16-30; Mk 10:17-31)

18 Kiongozi wa dini akamuuliza Yesu, “Mwalimu Mwema, ni lazima nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?”

19 Yesu akamwambia, “Kwa nini unaniita mwema? Mungu peke yake ndiye mwema. 20 Na unazijua amri zake: ‘Usizini, usiue, usiibe, usiseme uongo, na ni lazima uwaheshimu baba na mama yako.’”(A)

21 Lakini yule kiongozi akasema, “Nimezitii amri zote hizi tangu nilipokuwa mdogo.”

22 Yesu aliposikia hili, akamwambia, “Lakini kuna jambo moja unatakiwa kufanya. Uza kila kitu ulichonacho na uwape maskini pesa. Utakuwa na utajiri mbinguni. Kisha, njoo unifuate.” 23 Lakini yule mtu aliposikia Yesu anamwambia kutoa pesa zake, alihuzunika. Hakutaka kufanya hivi kwa sababu alikuwa tajiri sana.

24 Yesu alipoona kuwa amehuzunika, akasema, “Itakuwa vigumu sana kwa matajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 25 Ni rahisi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

26 Watu waliposikia hili, wakasema, “Sasa ni nani anayeweza kuokolewa?”

27 Yesu akajibu, “Lisilowezekana kwa wanadamu, linawezekana kwa Mungu.”

28 Petro akasema, “Tazama! Tumeacha vyote tulivyokuwa navyo na kukufuata.”

29 Yesu akasema, “Ninaahidi kuwa kila aliyeacha nyumba, mke, ndugu, wazazi, au watoto kwa ajili ya ufalme wa Mungu, 30 atapokea zaidi ya kile alichoacha. Atapokea mara nyingi zaidi katika maisha haya. Na katika ulimwengu ujao atapata mara nyingi zaidi.”

Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake

(Mt 20:17-19; Mk 10:32-34)

31 Kisha Yesu alizungumza na mitume wake kumi na mbili wakiwa peke yao. Akawaaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu. Kila kitu ambacho Mungu aliwaambia manabii waandike kuhusu Mwana wa Adamu kitatokea. 32 Atakabidhiwa kwa wasio Wayahudi, ambao watamcheka, watamtukana na kumtemea mate. 33 Watamchapa kwa mijeledi kisha watamuua. Lakini katika siku ya tatu baada ya kifo chake, atafufuka kutoka kwa wafu.” 34 Mitume walijaribu kulielewa hili, lakini hawakuweza; maana yake ilifichwa wasiielewe.

Yesu Amponya Asiyeona

(Mt 20:29-34; Mk 10:46-52)

35 Yesu alipofika karibu na mji wa Yeriko, mwanaume mmoja asiyeona alikuwa amekaa kando ya barabara, akiomba pesa. 36 Aliposikia kundi la watu linapita barabarani, akauliza, “Nini kimetokea?”

37 Walimwambia, “Yesu kutoka Nazareti anapitia hapa.”

38 Kipofu akapasa sauti yake, akaita, “Yesu, Mwana wa Daudi, tafadhali nisaidie!”

39 Watu waliotangulia, wakiongoza kundi, wakamkanya asiyeona, wakamwambia anyamaze. Lakini alizidi sana kupaza sauti zaidi na zaidi, “Mwana wa Daudi, tafadhali unisaidie!”

40 Yesu alisimama pale na akasema, “Mleteni yule asiyeona kwangu!” Yule asiyeona alipofika kwa Yesu, Yesu akamwuliza, 41 “Unataka nikufanyie nini?”

Asiyeona akasema, “Bwana, nataka kuona.”

42 Yesu akamwambia, “Unaweza kuona sasa. Umeponywa kwa sababu uliamini.”

43 Yule mtu akaanza kuona saa ile ile. Akamfuata Yesu, akimshukuru Mungu. Kila mtu aliyeliona hili alimsifu Mungu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International