Beginning
Je, ni Sahihi Kuponya Siku ya Sabato?
14 Siku moja ya Sabato Yesu alikwenda nyumbani kwa miongoni mwa viongozi wa Mafarisayo kula chakula pamoja naye. Watu wote mahali pale walikuwa wanamwangalia kwa makini kuona atafanya nini. 2 Mbele yake kulikuwa na mtu aliyekuwa na ugonjwa mbaya.[a] 3 Yesu akawauliza wanasheria na Mafarisayo, “Je, ni halali au kosa kuponya siku ya Sabato?” 4 Lakini walishindwa kujibu swali lake. Hivyo akamshika yule mgonjwa, na kumponya, akamruhusu aende zake. 5 Kisha akawaambia Mafarisayo na wanasheria, “Ikiwa mwanao au mnyama wako atatumbukia kisimani siku ya Sabato, mnatambua kuwa mtamtoa haraka.” 6 Mafarisayo na wanasheria hawakuweza kujibu kinyume na alivyosema.
Usijifanye Mtu wa Muhimu
7 Ndipo Yesu akagundua kuwa baadhi ya wageni walikuwa wanachagua sehemu za heshima za kukaa mezani. Ndipo akawaambia, 8 “Ukialikwa na mtu katika sherehe ya harusi, usikae katika sehemu za heshima. Wanaweza kuwa wamemwalika mtu muhimu kuliko wewe. 9 Na kama umekaa katika kiti muhimu zaidi, watakuja kwako na kukuambia ‘toka ulipokaa umpishe huyu!’ Ndipo itakulazimu kuhamia sehemu zisizo za heshima na utaaibika.
10 Hivyo ukialikwa, nenda ukae mahali pasipo pa heshima, ili yule aliyekualika akija, akuambie, ‘Rafiki, njoo huku mbele zaidi mahali pazuri.’ Ndipo utaheshimiwa mbele ya wageni wote walio mezani pamoja nawe. 11 Kila ajikwezaye atashushwa. Lakini ajishushaye atakwezwa.”
Utazawadiwa
12 Kisha Yesu akamwambia Farisayo aliyemwalika, “Unapoandaa chakula, usiwaalike rafiki zako tu, au ndugu zako, au jamaa zako, wala jirani zako matajiri. Kwa sababu wao pia watakualika, na kwa kufanya hivyo watakuwa wanakulipa. 13 Lakini ufanyapo sherehe waalike maskini, waliolemaa, walemavu wa miguu, na wasiyeona. 14 Utabarikiwa, kwa sababu watu hawa hawana kitu cha kukulipa. Lakini Mungu atakupa thawabu wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
Mfano Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Chakula
(Mt 22:1-10)
15 Basi mmoja wa watu waliokuwa mezani pamoja naye aliposikia hayo akamwambia Yesu, “Wamebarikiwa watakaokula karamu katika ufalme wa Mungu.”
16 Yesu akamwambia, “Mtu mmoja aliandaa sherehe kubwa, na kuwaalika watu wengi. 17 Wakati wa kuanza sherehe ulipofika, alimtuma mtumishi wake awaambie wale walioalikwa, ‘Tafadhalini njooni sasa. Kila kitu kiko tayari.’ 18 Lakini wageni waalikwa wote walisema kuwa hawawezi kuja. Kila mmoja alitoa udhuru. Wa kwanza alisema, ‘Nimenunua shamba, hivyo ni lazima niende nikalitazame. Tafadhali unisamehe.’ 19 Mwingine alisema, ‘Nimenunua ng'ombe wa kulimia jozi tano; ni lazima niende kuwajaribu. Tafadhali unisamehe.’ 20 Na mtu wa tatu alisema, ‘Nimeoa mke, kwa sababu hiyo siwezi kuja.’
21 Hivyo mtumishi alirudi na kumjulisha bwana kilichotokea. Bwana wake akakasirika, akamwambia mtumishi wake, ‘Fanya haraka! Nenda mitaani na katika vichochoro vya mji. Niletee maskini, vilema, wasiyeona na walemavu wa miguu!’
22 Baadaye mtumishi akamwambia, ‘Mkuu nimefanya kama ulivyoniagiza, lakini bado tuna nafasi kwa ajili ya watu wengine zaidi.’ 23 Hivyo bwana wake akamwambia mtumishi, ‘Toka nje uende kwenye barabara zinazoelekea vijijini na kando kando ya mashamba. Waambie watu huko waje, ninataka nyumba yangu ijae! 24 Ninakwambia, sitaki mtu hata mmoja kati ya wale niliowaalika kwanza atakayekula chakula hiki nilichoandaa.’”
Amua Ikiwa Unaweza Kunifuata
(Mt 10:37-38)
25 Watu wengi walikuwa wanasafiri pamoja na Yesu. Akawaambia, 26 “Ikiwa unakuja kwangu na hauko tayari kuiacha familia yako, huwezi kuwa mfuasi wangu. Ukimpenda zaidi baba yako, mama yako, mke wako, watoto wako, kaka na dada zako na hata maisha yako zaidi yangu huwezi kuwa mwanafunzi wangu. 27 Yeyote ambaye hatauchukua msalaba atakaopewa na akanifuata, hawezi kuwa mfuasi wangu.
28 Ikiwa unataka kujenga nyumba, kwanza utakaa na kuamua ili kujua itakugharimu kiasi gani. Ni lazima uone ikiwa una pesa za kutosha kumaliza kazi ya ujenzi. 29 Usipofanya hivyo, unaweza ukaanza kazi, lakini ukashindwa kumaliza kujenga nyumba. Na usipoweza kuimaliza, kila mtu atakucheka, 30 Watasema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini alishindwa kumalizia.’
31 Ikiwa mfalme anakwenda kupigana vita na mfalme mwingine, atakaa chini kwanza na kupanga. Ikiwa ana askari elfu kumi, ataamua ikiwa ana uwezo wa kumshinda mfalme mwenye askari elfu ishirini. 32 Akiona hawezi kumshinda mfalme mwingine, atatuma baadhi ya watu kwa mfalme mwingine ili wapatane akiwa bado yuko mbali.
33 Ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wenu. Lazima uache kila kitu ulichonacho. La sivyo, huwezi kuwa mfuasi wangu.
Msipoteze Umuhimu Wenu
(Mt 5:13; Mk 9:50)
34 Chumvi ni kitu kizuri; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, huwezi kuitengenezea ladha tena. 35 Haifai. Huwezi hata kuitumia kama uchafu au mbolea. Watu huitupa tu.
Mnaonisikiliza, sikilizeni!”
Furaha Mbinguni
(Mt 18:12-14)
15 Watoza ushuru na wenye dhambi wengi waliendelea kuja kumsikiliza Yesu. 2 Hivyo Mafarisayo na walimu wa sheria wakaanza kulalamika wakisema, “Mtazameni mtu huyu[b] huwakaribisha wenye dhambi na hata kula pamoja nao!”
3 Hivyo Yesu akawaambia mfano huu, 4 “Chukulia mmoja wenu ana kondoo mia, lakini mmoja akapotea. Utafanya nini? Utawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta yule mmoja aliyepotea mpaka umpate. 5 Na ukishampata, utafurahi sana. Utambeba mabegani mwako 6 mpaka nyumbani. Kisha utakwenda kwa majirani na rafiki zako na utawaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyepotea!’ 7 Katika namna hiyo hiyo ninawaambia, kunakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mtu anayeacha dhambi zake. Kuna furaha zaidi kwa ajili ya mtu mmoja anayeacha dhambi kuliko watu wema tisini na tisa ambao hudhani hawahitaji kubadilika.
8 Fikiria kuhusu mwanamke mwenye sarafu kumi za fedha,[c] lakini akapoteza sarafu moja kati ya hizo. Atawasha taa na kuifagia nyumba. Ataitafuta sarafu kwa bidii mpaka aione. 9 Na akiiona, atawaita rafiki na jirani zake na kuwaaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu niliyoipoteza!’ 10 Katika namna hiyo hiyo, ni furaha kwa malaika wa Mungu, mwenye dhambi mmoja anapotubu.”
Simulizi Kuhusu Mwana Mpotevu
11 Kisha Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. 12 Mwana mdogo alimwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya mali ninayotarajia kurithi baadaye.’ Hivyo baba yake akagawa utajiri wake kwa wanawe wawili.
13 Baada ya siku chache yule mdogo akauza mali zake, akachukua pesa zake na akaondoka. Akasafiri mbali katika nchi nyingine. Huko alipoteza pesa zake zote katika starehe na anasa. 14 Baada ya kutumia vyote alivyokuwa navyo, kukatokea njaa kali katika nchi ile yote. Akawa na njaa na mhitaji wa pesa. 15 Hivyo alikwenda kutafuta kazi kwa mwenyeji mmoja wa nchi ile, naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16 Alikuwa anasikia njaa kiasi kwamba alikuwa anatamani kula chakula walichokula nguruwe. Lakini hakuna mtu aliyempa chakula.
17 Alipotambua namna alivyokuwa mjinga, akafikiri moyoni mwake na kusema, ‘Wafanyakazi wote wa baba yangu wana chakula kingi. Lakini niko hapa kama niliyekufa kwa sababu sina chakula. 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu. Nitamwambia hivi: Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe. 19 Sistahili kuitwa mwanao tena. Lakini niruhusu niwe kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ 20 Hivyo akaondoka na kurudi kwa baba yake.
Alipokuwa mbali na nyumbani kwao, baba yake alimwona, akamwonea huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia na kumbusu sana. 21 Mwanaye akasema, ‘Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe; sistahili kuitwa mwanao tena.’
22 Lakini baba akawaambia watumishi wake, ‘Fanyeni haraka, leteni vazi maalumu, mvikeni. Pia, mvisheni viatu vizuri na pete kwenye kidole chake. 23 Na leteni ndama aliyenona, mchinjeni ili tule na kusherehekea. 24 Kwa sababu mwanangu alikuwa amekufa, lakini sasa yuko hai tena! Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kusherehekea.
25 Mwanaye mkubwa alikuwa shambani. Alipoikaribia nyumba, alisikia sauti za muziki na kucheza. 26 Akaita mmoja wa watumishi na akamwuliza, ‘Kuna nini?’ 27 Mtumishi akasema, ‘Mdogo wako amerudi, na baba yako amechinja ndama aliyenona. Anafurahi kwa sababu amempata mwanaye akiwa salama na mzima.’
28 Mwana mkubwa alikasirika na hakutaka kwenda kwenye sherehe. Hivyo baba yake akatoka nje kumsihi. 29 Lakini alimwambia baba yake, ‘Tazama, miaka yote hii nimekutumikia kama mtumishi, kamwe sijaacha kukutii! Lakini hujawahi kunipa hata mbuzi mdogo ili nisherehekee pamoja na rafiki zangu. 30 Lakini alipokuja huyu mwanao aliyepoteza mali zako kwa makahaba, umemchinjia ndama aliyenona!’
31 Baba yake akamwambia, ‘Mwanangu, daima umekuwa pamoja nami, na vyote nilivyo navyo ni vyako. 32 Lakini tulipaswa kusherehekea. Mdogo wako alikuwa amekufa, lakini sasa ni hai tena. Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”
Utajiri Halisi
16 Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Alikuwepo mtu mmoja tajiri, aliyekuwa na msimamizi wa kuangalia biashara zake. Baadaye akagundua kuwa msimamizi wake alikuwa anapoteza pesa zake. 2 Hivyo, akamwita, akamwambia, ‘Nimesikia mambo mabaya juu yako. Nipe taarifa namna ulivyosimamia pesa zangu. Huwezi kuendelea kuwa msimamizi wangu.’
3 Hivyo msimamizi akawaza moyoni mwaka, ‘Nitafanya nini? Bwana wangu ananiachisha kazi yangu ya usimamizi. Sina nguvu za kulima, kuomba omba naona aibu. 4 Najua nitakalofanya! Nitafanya kitu nipate marafiki. Ili nitakapopoteza kazi yangu, watanikaribisha katika nyumba zao.’
5 Hivyo msimamizi akawaita mmoja mmoja wale waliokuwa wanadaiwa pesa na bwana wake. Akamwuliza wa kwanza, ‘Mkuu wangu anakudai kiasi gani?’ 6 Akamjibu, ‘Ananidai mitungi[d] 100 ya mafuta ya zeituni.’ Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, kaa chini, fanya haraka, badilisha iwe mitungi hamsini.’
7 Kisha akamwambia mwingine, ‘Na wewe kiasi gani unadaiwa?’ Akajibu, ‘Vipimo[e] mia moja vya ngano.’ Akamwambia, ‘Chukua hati yako ya deni, ibadilishe iwe vipimo themanini.’
8 Baadaye bwana wake akamsifu msimamizi asiye mwaminifu kwa sababu ya kutenda kwa busara. Ndiyo, watu wa ulimwengu huu wana busara katika kufanya biashara kati yao kuliko wana wa Mungu.
9 Ninamaanisha hivi: Vitumieni vitu vya kidunia mlivyonavyo sasa ili muwe na ‘marafiki’ kwa ajili ya siku za baadaye. Ili wakati vitu hivyo vitakapotoweka, mtakaribishwa katika nyumba ya milele. 10 Mtu yeyote anayeweza kuaminiwa kwa mambo madogo anaweza kuaminiwa kwa mambo makubwa pia. Mtu asiye mwaminifu katika jambo dogo hawezi kuwa mwaminifu katika jambo kubwa. 11 Ikiwa huwezi kuaminiwa kwa mali za kidunia, huwezi kuaminiwa kwa mali za mbinguni. 12 Na kama hauwezi kuaminiwa kwa vitu vya mtu mwingine, hautapewa vitu kwa ajili yako wewe mwenyewe.
13 Mtumwa hawezi kuwatumikia mabwana wawili wakati mmoja, hata ninyi hamwezi. Utamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au utakuwa mwaminifu kwa mmoja na hautamjali mwingine. Pia, huwezi kumtumikia Mungu na pesa.”[f]
Sheria Ya Mungu Haiwezi Kubadilishwa
(Mt 11:12-13)
14 Mafarisayo walikuwa wakiyasikiliza mambo haya yote. Walimdhihaki Yesu kwa sababu wote walipenda pesa. 15 Yesu aliwaambia, “Mnajifanya kuwa wenye haki mbele za watu, lakini Mungu anajua hakika kilichomo mioyoni mwenu. Jambo ambalo watu hudhani kuwa la muhimu, kwa Mungu ni chukizo.
16 Kabla ya Yohana Mbatizaji kuja, watu walifundishwa Sheria ya Musa na maandishi ya Manabii. Lakini tangu wakati wa Yohana, Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu inahubiriwa. Na kila mtu anajitahidi sana ili kuingia katika ufalme wa Mungu. 17 Ni rahisi sana kwa mbingu na dunia kutoweka, kuliko sehemu ndogo ya herufi katika Sheria ya Musa kutoweka. 18 Mwanaume yeyote anayemtaliki mkewe na kumwoa mke mwingine anazini. Na mwanaume anayeoa mwanamke aliyetalikiwa anazini pia.”
Tajiri na Lazaro
19 Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja, tajiri ambaye daima alivaa nguo za thamani sana, alikuwa tajiri sana kiasi kwamba alifurahia vitu vizuri kila siku. 20 Alikuwepo pia maskini mmoja aliyeitwa Lazaro ambaye mwili wake ulikuwa umejaa vidonda. Mara nyingi aliwekwa kwenye lango la tajiri. 21 Lazaro alitaka tu kula masalia ya vyakula vilivyokuwa sakafuni vilivyodondoka kutoka mezani kwa tajiri. Na mbwa walikuja na kulamba vidonda vyake.
22 Baadaye Lazaro alikufa. Malaika walimchukua na kumweka kifuani pa Ibrahimu. Tajiri naye alikufa na kuzikwa. 23 Alichukuliwa mpaka mahali pa mauti[g] na akawa katika maumivu makuu. Alimwona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro akiwa kifuani pake. 24 Akaita, ‘Baba Ibrahimu, nihurumie! Mtume Lazaro kwangu ili achovye ncha ya kidole chake kwenye maji na kuupoza ulimi wangu, kwa sababu ninateseka katika moto huu!’
25 Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwanangu, unakumbuka ulipokuwa unaishi? Ulikuwa na mambo yote mazuri katika maisha. Lakini Lazaro hakuwa na chochote ila matatizo. Sasa yeye anafarijiwa hapa, na wewe unateseka. 26 Pia kuna korongo pana na lenye kina kati yetu sisi na ninyi. Hakuna anayeweza kuvuka kuja kukusaidia na hakuna anayeweza kuja huku kutoka huko.’
27 Tajiri akasema, ‘Basi, nakuomba baba, mtume Lazaro nyumbani kwa baba yangu duniani, 28 Nina ndugu watano. Mtume ili akawape tahadhari wasije wakafika mahali hapa pa mateso.’
29 Lakini Ibrahimu akasema, ‘Wanayo Sheria ya Musa na maandishi ya manabii kwa ajili ya kuyasoma; wasikilize na kutii.’
30 Tajiri akasema, ‘Hapana Baba Ibrahimu! Lakini ikiwa mtu kutoka kwa wafu akiwaendea ndipo wataamua kutubu na kubadili maisha yao.’
31 Lakini Ibrahimu akamwambia, ‘Ikiwa ndugu zako hawatawasikiliza Musa na manabii, hawataweza kumsikiliza mtu yeyote kutoka kwa wafu.’”
© 2017 Bible League International