Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 24-25

Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao

(Mk 13:1-31; Lk 21:5-33)

24 Yesu alipokuwa anaondoka eneo la Hekalu, wanafunzi wake walimwendea na kumwonyesha majengo ya Hekalu. Akawauliza, “Mnayaona majengo haya? Ukweli ni kuwa, yataharibiwa. Kila jiwe litadondoshwa chini, hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe jingine.”

Baadaye, Yesu alipokuwa ameketi mahali fulani katika Mlima wa Mizeituni, Wafuasi wake walimwendea faraghani. Wakasema, “Twambie mambo haya yatatokea lini. Na nini kitatokea ili kutuandaa kwa ajili ya ujio wako na mwisho wa nyakati?”

Yesu akajibu, “Mjihadhari! Msimruhusu mtu yeyote awadanganye. Watu wengi watakuja na watatumia jina langu. Watasema, ‘Mimi ndiye Masihi.’ Na watawadanganya watu wengi. Mtasikia kuhusu vita vinanavyopiganwa na pia matetesi ya kuwapo vita vingine. Lakini msiogope. Mambo haya lazima yatokee na mwisho wenyewe hautafuata palepale. Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. Utakuwepo wakati wa njaa ambapo watu watakosa chakula. Na kutakuwa matetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. Mambo haya ni mwanzo wa matatizo, kama uchungu wa kwanza mwanamke anapozaa.

Kisha mtakamatwa na kupelekwa kwa wenye mamlaka ili mhukumiwe na kuuawa. Watu wote katika ulimwengu watawachukia kwa sababu mnaniamini mimi. 10 Nyakati hizo watu wengi wataacha kuwa wafuasi wangu. Watasalitiana na kuchukiana. 11 Manabii wengi watatokea na kusababisha watu wengi kuamini mambo yasiyo ya kweli. 12 Kutakuwepo na uovu mwingi sana duniani kiasi kwamba upendo wa waaminio wengi utapoa. 13 Lakini yeyote yule atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 14 Na Habari Njema niliyoihubiri kuhusu Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote. Itatawanywa katika kila taifa. Kisha mwisho utakuja.

15 Nabii Danieli alizungumza kuhusu ‘jambo la kutisha litakalosababisha uharibifu.’[a] Mtakapoliona jambo hili la kutisha limesimama patakatifu.” (Asomaye hili anapaswa kuelewa jambo hili linamaanisha nini.) 16 “Watu walio Uyahudi wakimbilie milimani. 17 Wakimbie pasipo kupoteza muda ili kuchukua kitu chochote. Wakiwa darini wasiteremke ili kuchukua kitu na kukitoa nje ya nyumba. 18 Wakiwa shambani wasirudi nyumbani kuchukua koti.

19 Itakuwa hali ngumu kwa wanawake wenye mimba na wenye watoto wachanga! 20 Ombeni isiwe majira ya baridi au isiwe siku ya Sabato mambo haya yatakapotokea na mkalazimika kukimbia, 21 kwa sababu utakuwa wakati wa dhiki kuu. Kutakuwepo na usumbufu mwingi sana kuliko ule uliowahi kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu. Na hakuna jambo baya kama hilo litakalotokea tena.

22 Lakini Mungu amekwisha amua kuufupisha wakati huo. Ikiwa usingefupishwa, hakuna ambaye angeendelea kuishi. Lakini Mungu ataufupisha ili kuwasaidia watu aliowachagua.

23 Wakati huo watu wataweza kuwaambia, ‘Tazama, Masihi yuko kule!’ Au wakasema, ‘Ni yule!’ Msiwaamini. 24 Manabii wa uongo na masihi wa uongo watatokea na kufanya miujiza na maajabu[b] makuu, ili ikiwezekana wawadanganye wateule. 25 Na sasa nimewatahadharisha kuhusu hili kabla halijatokea.

Yesu Atakaporudi Tena

(Mk 13:24-31; Lk 17:23-24,37; 21:25-32)

26 Inawezekana mtaambiwa, ‘Masihi yuko jangwani!’ Msiende jangwani kumtafuta. Mtu mwingine anaweza akasema, ‘Masihi yuko katika chumba kile!’ Msiamini. 27 Mwana wa Adamu atakapokuja, kila mtu atamwona. Itakuwa kama radi inavyowaka angani na kuonekana kila mahali. 28 Ni kama kutafuta mzoga: Mzoga hupatikana mahali ambapo tai wengi wamekusanyika.

29 Mara baada ya mateso ya siku hizo, mambo haya yatatokea:

‘Jua litakuwa jeusi,
    na mwezi hautatoa mwanga.
Nyota zitaanguka kutoka angani,
    na kila kitu kilicho angani
    kitatikiswa kutoka mahali pake.’[c]

30 Kisha kutatokea ishara angani kuwa Mwana wa Adamu anakuja. Watu wote wa ulimwengu watajipiga kifuani wakiomboleza. Kila mtu atamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani akiwa na nguvu na utukufu mkuu. 31 Naye atatumia parapanda kuu kuwatuma malaika zake kila mahali duniani. Nao watawakusanya wateule wake kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.

32 Jifunze kwa mtini: Matawi yake yanapokuwa ya kijani na laini na kuanza kutoa majani mapya, ndipo mnatambua kuwa majira ya joto yamekaribia. 33 Katika namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yakitokea, mtajua kuwa wakati[d] umekaribia wa kile kitakachotokea. 34 Ninawahakikishia kuwa mambo haya yote yatatokea wakati ambao baadhi ya watu wa nyakati hizi wakiwa bado hai. 35 Ulimwengu wote, dunia na anga vitaangamizwa, lakini maneno yangu yatadumu milele.

Mungu Peke Yake Ndiye Ajuaye Siku ya Kurudi kwa Mwana wa Adamu

(Mk 13:32,35; Lk 17:26-30,34-36)

36 Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua.

37 Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. 38 Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. 39 Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote.

Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. 40 Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

42 Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. 43 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. 44 Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia.

Watumishi Wema na Wabaya

(Mk 13:33-37; Lk 12:41-48)

45 Fikiria mtumishi aliyewekwa na bwana wake kuwapa chakula watumishi wake wengine katika muda uliopangwa. Ni kwa namna gani mtumishi huyo atajionyesha kuwa ni mwangalifu na mwaminifu? 46 Bwana wake atakaporudi na kumkuta anafanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha kwa mtumishi huyo. 47 Ninawaambia bila mashaka yoyote kuwa, bwana wake atamchagua mtumishi huyo awe msimamizi wa kila kitu anachomiliki yule Bwana.

48 Lakini nini kitatokea ikiwa mtumishi huyo ni mbaya na akadhani kuwa bwana wake hatarudi karibuni? 49 Ataanza kuwapiga watumishi wengine na kuanza kunywa na kula na walevi. 50 Ndipo bwana wake atakuja wakati asioutarajia, ambapo mtumishi hakujiandaa. 51 Bwana atamwadhibu mtumishi huyo na kumpeleka anakostahili kuwapo pamoja na watumishi wengine waliojifanya kuwa wema. Huko watalia na kusaga meno kwa maumivu.

Wanawali Kumi

25 Nyakati hizo, ufalme wa Mungu utafanana na wanawali kumi waliokwenda kusubiri kuwasili kwa bwana arusi wakiwa na taa zao. Watano kati yao walikuwa na hekima, na watano walikuwa wajinga. Wanawali wajinga walichukua taa zao bila ya kubeba mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao. Wanawali wenye hekima walichukua taa zao pamoja na mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao katika chupa. Bwana arusi alipochelewa sana, walichoka na wote wakasinzia.

Usiku wa manane ulipofika, ikatangazwa, ‘Bwana arusi anakuja! Njooni mumlaki!’

Wasichana wote waliamka. Wakatayarisha taa zao. Lakini wanawali wajinga wakawaambia wanawali wenye hekima, ‘Tupeni mafuta kiasi kwa sababu mafuta katika taa zetu yamekwisha.’

Wanawali wenye hekima wakajibu, ‘Hapana! Mafuta tuliyonayo hayatatutosha sisi sote. Lakini nendeni kwa wauza mafuta mkanunue.’

10 Hivyo wanawali wajinga wakaenda kununua mafuta. Walipoondoka, bwana arusi akafika. Wanawali waliokuwa tayari wakaingia kwenye sherehe ya arusi pamoja na bwana arusi. Kisha mlango ukafungwa.

11 Baadaye wanawali waliokwenda kununua mafuta wakarudi. Wakasema, ‘bwana, bwana! Fungua mlango tuingie.’

12 Lakini bwana arusi akajibu, ‘Kwa hakika hapana! Wala siwajui ninyi.’

13 Hivyo iweni tayari kila wakati. Hamjui siku wala muda ambao Mwana wa Adamu atakuja.

Simulizi Kuhusu Watumishi Watatu

(Lk 19:11-27)

14 Pia, ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyekuwa akiondoka nyumbani kwake kusafiri safari ndefu. Aliwaita watumishi wake na kuwaweka kuwa wasimamizi wa mali zake. 15 Alimgawia kila mtumishi kiasi cha mali atakachosimamia. Alimpa mmoja talanta[e] tano. Alimpa mtumishi mwingine talanta mbili na akampa mtumishi wa tatu talanta moja. Kisha akaondoka. 16 Mtumishi aliyepewa talanta tano alikwenda akazifanyia biashara na talanta zile tano zikazaa talanta tano zingine. 17 Mtumishi aliyepewa talanta mbili alifanya vivyo hivyo. Mtumishi huyo alizifanyia biashara talanta mbili alizopewa na zikazaa talanta mbili zingine. 18 Lakini mtumishi aliyekabidhiwa talanta moja, alikwenda akachimba shimo kisha akaifukia talanta moja aliyopewa na bwana wake.

19 Baada ya muda mrefu kupita bwana wao alirudi. Aliwauliza watumishi wake walizifanyia nini talanta alizowaachia. 20 Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano alimletea bwana wake talanta tano alizomwachia na talanta zingine tano zaidi. Mtumishi akamwambia bwana wake, ‘Bwana, uliniamini ukaniachia talanta tano kuzitunza, hivyo nilizifanyia biashara na kupata talanta tano zaidi.’

21 Bwana wake akajibu, ‘Ulifanya vyema. Wewe ni mtumishi mwema unayeweza kuaminiwa. Ulifanya vizuri kwa kiasi kidogo hicho cha pesa. Hivyo nitakufanya kuwa msimamizi wa mambo makuu. Njoo usherehekee pamoja nami.’

22 Kisha mtumishi aliyepewa talanta mbili akaja kwa bwana wake. Akasema, ‘Bwana ulinipa talanta mbili ili nizitunze. Nilizifanyia biashara talanta hizi mbili na nimepata zingine mbili zaidi.’

23 Bwana wake akajibu, ‘Ulifanya vyema. Wewe ni mtumishi mwema unayeweza kuaminiwa. Ulifanya vizuri kwa kiasi kidogo hicho cha pesa. Hivyo nitakufanya kuwa msimamizi wa mambo makuu. Njoo usherehekee pamoja nami.’

24 Ndipo mtumishi aliyeachiwa talanta moja akaja kwa bwana wake. Akasema, ‘Bwana, nilijua wewe ni mkorofi sana. Unavuna usichopanda. Unakusanya mazao mahali ambapo hukupanda mbegu yoyote. 25 Hivyo niliogopa. Nilienda nikaificha talanta yako ardhini. Hii hapa ni ile talanta moja ya fedha uliyonipa.’

26 Bwana wao akamjibu, ‘Wewe ni mtumishi mbaya na mvivu! Unasema kwamba ulijua ninavuna nisichopanda na ninakusanya mazao ambayo sikupanda mbegu yo yote. 27 Hivyo ungeweka pesa yangu benki. Kisha, wakati nitakaporudi ningepata talanta yangu pamoja na faida ambayo ingezalishwa na talanta yangu.’

28 Hivyo bwana wao akawaambia watumishi wake wengine, ‘Mnyang'anyeni talanta moja mtumishi huyo na kumpa mtumishi mwenye talanta kumi. 29 Kila aliyezalisha faida atapata zaidi. Atakuwa na vingi kuzidi mahitaji yake. Lakini wale wasiotumia walivyonavyo kuleta faida watanyang'anywa kila kitu.’ 30 Kisha bwana wao akasema, ‘Mtupeni nje, gizani mtumishi huyo asiyefaa, ambako watu watalia na kusaga meno kwa maumivu.’

Yesu, Mwana wa Adamu Atawahukumu Watu Wote

31 Mwana wa Adamu atakuja akiwa katika utukufu wake, pamoja na malaika wote. Ataketi kwenye kiti chake cha enzi akiwa mfalme. 32 Watu wote wa ulimwenguni watakusanywa mbele zake, kisha atawagawa katika makundi mawili. Itakuwa kama mchungaji anavyowatenga kondoo kutoka katika kundi la mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wa kushoto.

34 Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kuume, ‘Njooni, baba yangu ana baraka kuu kwa ajili yenu. Ufalme alioahidi ni wenu sasa. Uliandaliwa kwa ajili yenu tangu dunia ilipoumbwa. 35 Ni wenu kwa sababu nilipokuwa na njaa, mlinipa chakula. Nilipokuwa na kiu, mlinipa maji ya kunywa. Nilipokosa mahali pa kukaa, mlinikaribisha katika nyumba zenu. 36 Nilipokosa nguo, mlinipa mavazi ya kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa, mlinijali. Nilipofungwa gerezani, mlikuja kunitembelea.’

37 Kisha wenye haki watajibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakupa chakula? Lini tulikuona una kiu tukakupa maji ya kunywa? 38 Lini tulikuona huna mahali pa kukaa tukakukaribisha katika nyumba zetu? Lini tulikuona huna nguo za kuvaa na tukakuvisha? 39 Lini tulikuona unaumwa au uko gerezani tukaja kukuona?’

40 Kisha mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, kila mlichowafanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si watu wa thamani, mlinifanyia mimi pia.’

41 Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu. Mungu amekwisha amua kuwa mtaadhibiwa. Nendeni katika moto uwakao milele, moto ulioandaliwa kwa ajili ya yule Mwovu na malaika zake. 42 Ondokeni kwa sababu nilipokuwa na njaa, hamkunipa chakula nile. Nilipokuwa na kiu, hamkunipa maji ya kunywa. 43 Nilipokosa mahali pa kukaa, hamkunikaribisha katika nyumba zenu. Nilipokosa nguo za kuvaa, hamkunipa nguo za kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa au mfungwa gerezani hamkunijali.’

44 Ndipo watu hao watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu? Lini tulikuona huna mahali pa kukaa? Au ni lini tulikuona huna nguo au mgonjwa au ukiwa gerezani? Tuliona haya yote lini na hatukukusaidia?’

45 Mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, chochote mlichokataa kumfanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si wa muhimu, mlikataa kunifanyia mimi.’

46 Ndipo watu hawa watakapondolewa ili kuadhibiwa milele. Lakini wenye haki watakwenda kuyafurahia maisha ya milele.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International