Book of Common Prayer
12 Hivyo, kaka na dada zangu, ni lazima tusitawaliwe na udhaifu wa kibinadamu kwa kufuata tamaa zake. 13 Ikiwa mtayatumia maisha yenu kufanya yale ambayo udhaifu wenu wa kibinadamu unataka, mtakufa kiroho. Lakini ikiwa mtaupokea msaada wa Roho na mkaacha kutenda mambo mabaya mnayotenda na miili yenu, mtakuwa na uzima wa kweli.
14 Watoto wa kweli wa Mungu ni wale wanaokubali kuongozwa na Roho wa Mungu. 15 Roho tuliyempokea si roho anayetufanya kuwa watumwa tena na kutusababisha tuwe na hofu. Roho tuliye naye hutufanya tuwe watoto waliochaguliwa na Mungu. Na kwa Roho huyo twalia “Aba,[a] yaani Baba.” 16 Na Roho mwenyewe huzungumza na roho zetu na kutuhakikishia kuwa sisi ni watoto wa Mungu. 17 Nasi kwa kuwa ni watoto wa Mungu, basi sisi ni warithi, warithi wa Mungu na warithi pamoja na Kristo. Mungu atatupa yale yote aliyompa Kristo. Sisi tunaoteseka sasa kama Kristo alivyoteseka tutashiriki katika utukufu wake.
Wakati Wetu wa Utukufu Unakuja
18 Nanayachukulia mateso ya sasa kuwa si kitu ukilinganisha na utukufu mkuu tunaoutarajia. 19 Hata uumbaji una shauku kuu, ukisubiri kwa hamu wakati ambapo atawadhihirisha “watoto halisi wa Mungu”[b] kuwa ni na. 20 Kila alichokiumba Mungu kiliruhusiwa kuwa na mapungufu kana kwamba hakitafikia utimilifu wake. Hilo halikuwa kwa matakwa ya viumbe, lakini Mungu aliruhusu hayo yatokee kwa mtazamo wa tumaini hili: 21 kwamba uumbaji ungewekwa huru mbali na uharibifu, na kwamba kila alichokiumba Mungu kiwe na uhuru na utukufu ule ule ulio wa watoto wa Mungu.
22 Tunajua kuwa kila kitu alichoumba Mungu kimekuwa kikingoja hadi sasa katika kuugua na uchungu kama wa mwanamke aliye tayari kuzaa mtoto. 23 Siyo uumbaji tu, bali sisi pia tumekuwa tukingoja kwa kuugua na uchungu ndani yetu. Tunaye Roho kama sehemu ya kwanza ya ahadi ya Mungu. Kwa hiyo tunamngoja Mungu amalize kutufanya sisi watoto wake yeye mwenyewe. Nina maana kuwa tunasubiri kuwekwa huru kwa miili yetu. 24 Tuliokolewa ili tuwe na tumaini hili. Ikiwa tunaweza kuona kile tunachokisubiri, basi hilo siyo tumaini la kweli. Watu hawatumaini kitu ambacho tayari wanacho. 25 Lakini tunatumaini kitu tusichokuwa nacho, na hivyo tunakisubiri kwa uvumilivu.
26 Roho hutusaidia pia. Sisi ni dhaifu sana, lakini Roho hutusaidia katika udhaifu wetu. Hatujui jinsi ya kuomba kama Mungu anavyotaka, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa Mungu kwa kuungua kusikotamkika. 27 Tayari Mungu anayajua mawazo yetu ya ndani sana. Na anaelewa Roho anataka kusema nini, kwa sababu Roho huomba kwa ajili ya watu wa Mungu katika namna inayokubaliana na mapenzi ya Mungu.
41 Baadhi ya Wayahudi walianza kumlalamikia Yesu kwa vile alisema, “Mimi ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu ni Yesu. Tunawajua baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa Yusufu. Anawezaje kusema, ‘Nilishuka kutoka mbinguni’?”
43 Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika miongoni mwenu. 44 Baba ndiye aliyenituma, na ndiye anayewaleta watu kwangu. Nami nitawafufua siku ya mwisho. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipoletwa na Baba yangu. 45 Hii iliandikwa katika vitabu vya manabii: ‘Mungu atawafundisha wote.’(A) Watu humsikiliza Baba na hujifunza kutoka kwake. Hao ndiyo wanaokuja kwangu. 46 Sina maana kwamba yupo yeyote aliyemwona Baba. Yule pekee aliyekwisha kumwona Baba ni yule aliyetoka kwa Mungu. Huyo amemwona Baba.
47 Hakika nawaambieni kila anayeamini anao uzima wa milele. 48 Maana mimi ni mkate unaoleta uzima. 49 Baba zenu walikula mana waliyopewa na Mungu kule jangwani, lakini haikuwazuia kufa. 50 Hapa upo mkate unaotoka mbinguni. Yeyote anayekula mkate huu hatakufa kamwe. 51 Mimi ni mkate ulio hai ulioshuka kutoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu. Nitautoa mwili wangu ili watu wa ulimwengu huu waweze kupata uzima.”
© 2017 Bible League International