Book of Common Prayer
16 Kwa mimi hakuna haya[a] katika kuhubiri Habari Njema. Ninayo furaha kwa sababu Habari Njema ni nguvu ya Mungu inayomwokoa kila anayeamini, yaani inawaokoa Wayahudi kwanza, na sasa inawaokoa Mataifa.[b] 17 Ndiyo, wema wa uaminifu wa Mungu umedhihirishwa katika Habari Njema kwa uaminifu wa mmoja, ambao huongoza imani ya wengi. Kama Maandiko yanavyosema, “Aliye na haki mbele za Mungu[c] ataishi kwa imani.”[d]
Mungu ni Mwaminifu Na Atauadhibu Uovu
18 Mungu huonesha hasira yake kutokea mbinguni dhidi ya mambo mabaya ambayo waovu hutenda. Hawamheshimu na wanatendeana mabaya. Maisha yao maovu yanasababisha ukweli kuhusu Mungu usijulikane. 19 Hili humkasirisha Mungu kwa sababu wamekwisha oneshwa Mungu alivyo. Ndiyo, Mungu ameliweka wazi kwao.
20 Yapo mambo yanayoonekana kuhusu Mungu, kama vile nguvu zake za milele na yale yote yanayomfanya awe Mungu. Lakini tangu kuumbwa kwa ulimwengu, mambo haya yamekuwa rahisi kwa watu kuyaona. Maana yake ni kuwa, watu wanaweza kumwelewa Mungu kwa kuangalia yale aliyoumba. Hivyo watu hawana udhuru kwa uovu wanaotenda.
21 Watu walimjua Mungu, lakini hawakumheshimu kama Mungu. Na hawakumpa shukrani. Badala yake waliyageukia mambo ya hovyo yasiyo na manufaa. Akili zao zilichochanganyikiwa zilijaa giza. 22 Walisema kuwa wana hekima, lakini wakawa wajinga. 23 Hawakuuheshimu ukuu wa Mungu, anayeishi milele. Wakaacha kumwabudu Mungu wakaanza kuabudu sanamu, vitu vilivyotengenezwa vikaonekana kama wanadamu, ambao wote mwisho hufa, au kwa mfano wa ndege na wanyama wanaotembea na wanaotambaa.
24 Hivyo Mungu akawaacha wazifuate tamaa zao chafu. Wakawa najisi na wakaivunjia heshima miili yao kwa njia za uovu walizotumia. 25 Waliibadili kweli kuhusu Mungu kwa uongo. Wakasujudu na kuabudu vitu alivyoviumba Mungu badala ya kumwabudu Mungu aliyeviumba vitu hivyo. Yeye ndiye anayepaswa kusifiwa milele yote. Amina.
Yesu Amponya Mwana wa Afisa
(Mt 8:5-13; Lk 7:1-10)
43 Siku mbili baadaye Yesu akaondoka na kwenda Galilaya. 44 (Yesu alikwishasema mwanzoni kwamba nabii huwa haheshimiwi katika nchi yake.) 45 Alipofika Galilaya, watu wa pale walimkaribisha. Hao walikuwepo kwenye sikukuu ya Pasaka kule Yerusalemu na waliona kila kitu alichofanya huko.
46 Naye Yesu akaenda tena kutembelea Kana huko Galilaya. Kana ni mahali alikoyabadili maji kuwa divai. Mmoja wa maafisa muhimu wa mfalme alikuwa anaishi katika mji wa Kapernaumu. Mwanawe afisa huyu alikuwa mgonjwa. 47 Afisa huyo akasikia kwamba Yesu alikuwa amekuja kutoka Uyahudi na sasa yuko Galilaya. Hivyo akamwendea Yesu na kumsihi aende Kapernaumu kumponya mwanawe, aliyekuwa mahututi sana. 48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu ni lazima muone ishara zenye miujiza na maajabu kabla ya kuniamini.”
49 Afisa wa mfalme akasema, “Bwana, uje kabla mwanangu mdogo hajafa.”
50 Yesu akajibu, “Nenda, mwanao ataishi.”
Mtu huyo akayaamini maneno Yesu aliyomwambia na akaenda nyumbani. 51 Akiwa njiani kwenda nyumbani watumishi wake wakaja na kukutana naye. Wakasema, “Mwanao ni mzima.”
52 Mtu huyo akauliza, “Ni wakati gani mwanangu alipoanza kupata nafuu?”
Wakajibu, “Ilikuwa jana saa saba mchana homa ilipomwacha.”
53 Baba yake akatambua kuwa saa saba kamili ulikuwa ndiyo ule wakati aliposema, “Mwanao ataishi.” Hivyo afisa huyo na kila mmoja katika nyumba yake wakamwamini Yesu.
54 Huo ulikuwa muujiza wa pili ambao Yesu aliufanya baada ya kufika kutoka Uyahudi na Galilaya.
© 2017 Bible League International