Book of Common Prayer
3 Kama tukitii mambo ambayo Mungu ametuamuru kuyafanya, tunapata uhakika ya kuwa tunamjua. 4 Kama tukisema kuwa tunamjua Mungu lakini hatuzitii amri zake, tunasema uongo. Kweli haimo ndani mwetu. 5 Lakini tunapotii mafundisho ya Mungu, kwa hakika upendo wake unakamilika ndani yetu. Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa tunaishi ndani yake. 6 Kama tukisema kuwa tunaishi ndani ya Mungu, ni lazima tuishi kwa namna ambvyo Yesu aliishi.
Yesu Alituagiza Kuwapenda Wengine
7 Wapendwa rafiki zangu, siwaandiki ninyi amri mpya. Ni amri ile ile ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ni fundisho lile lile ambalo mmekwishalisikia. 8 Lakini kile ninachokiandika pia ni amri mpya. Ni kweli; Mnaweza kuiona kweli ndani ya Yesu na ndani yenu ninyi wenyewe. Giza linatoweka, na nuru ya kweli tayari inang'aa.
9 Mtu anaweza kusema, “Niko nuruni,” lakini ikiwa anamchukia ndugu yeyote katika familia ya Mungu, basi angali bado katika giza. 10 Wao wanaowapenda ndugu wanaishi katika nuru, na hakuna kitu ndani yao cha kuwafanya watende mabaya. 11 Lakini yeyote anayemchukia nduguye wa kike au wa kiume yuko gizani. Anaishi katika giza. Hajui anakoenda, kwa sababu giza limemfanya asiweze kuona.
Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
12 Baadaye Yesu akazungumza tena na watu. Akasema, “Mimi ndiye nuru ya ulimwengu. Yeyote atakayenifuata mimi hataishi gizani kamwe. Atakuwa na nuru inayoleta uzima.”
13 Lakini Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Unapojishuhudia mwenyewe, unakuwa ni wewe peke yako unayethibitisha kuwa mambo haya ni kweli. Hivyo hatuwezi kuyaamini unayosema.”
14 Yesu akajibu, “Ndiyo, nasema mambo haya juu yangu mwenyewe. Lakini watu wanaweza kuamini ninayosema, kwa sababu mimi najua nilikotoka. Pia najua ninakoenda. Lakini ninyi hamjui mimi ninakotoka wala ninakoenda. 15 Mnanihukumu kama watu wanavyowahukumu wengine. Mimi simhukumu mtu yeyote. 16 Lakini ikiwa ninahukumu, basi hukumu yangu ni ya kweli, kwa sababu ninapohukumu sifanyi hivyo peke yangu. Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17 Sheria yenu inasema kwamba mashahidi wawili wakilisema jambo hilo hilo, basi mnapaswa kukubali wanayosema. 18 Mimi shahidi ninayeshuhudia mambo yangu mwenyewe. Na Baba yangu aliyenituma ndiye shahidi wangu mwingine.”
19 Watu wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?”
Yesu akajibu, “Hamnijui mimi wala Baba yangu hamumjui. Lakini mngenijua mimi, mngemjua Baba pia.”
© 2017 Bible League International