Book of Common Prayer
4 Ninalolisema ni hili: Wakati mrithi wa vyote alivyomiliki baba yake bado ni mdogo, hana tofauti yo yote na mtumwa. Haijalishi kuwa anamiliki vitu vyote. 2 Wakati wa utoto bado anapaswa kuwatii wale waliochaguliwa kumtunza. Lakini anapoufikia umri ambao baba yake ameuweka, anakuwa huru. 3 Ndivyo ilivyo hata kwetu sisi. Mwanzoni tulikuwa kama watoto, tukiwa watumwa wa mamlaka za uovu[a] zinazoutawala ulimwengu huu wa sasa. 4 Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu akamtuma Mwanaye, aliyezaliwa na mwanamke na akaishi chini ya sheria. 5 Mungu alifanya hivi ili aweze kuwaweka huru wale waliokuwa chini ya sheria. Kusudi la Mungu lilikuwa kutuasili[b] sisi kama watoto wake.
6 Ninyi sasa ni watoto wa Mungu. Na ndiyo sababu Mungu amemtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu. Huyo Roho aliye ndani yetu hulia “Aba,[c] yaani Baba.” 7 Sasa ninyi si watumwa kama mwanzo. Ni watoto wa Mungu, na mtapokea kila kitu ambacho Mungu aliwaahidi watoto wake. Hii yote ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu amewatendea ninyi.
Upendo wa Paulo kwa Waamini wa Galatia
8 Zamani hamkumjua Mungu. Mlikuwa watumwa wa miungu isiyokuwa halisi. 9 Lakini sasa mnamjua Mungu wa kweli. Hakika, Mungu ndiye anayewajua ninyi. Hivyo kwa nini sasa mnavigeukia vikosi dhaifu na visivyo na manufuaa yoyote mlivyovifuata hapo mwanzo? Mnataka kuwa watumwa wa mambo haya tena? 10-11 Inanipa wasiwasi kwa kuwa mnaadhimisha siku, miezi, misimu na miaka. Nina hofu ya kuwa nimefanya kwa bidii kazi bure kwa ajili yenu.
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mt 15:21-28)
24 Yesu akaondoka mahali pale na kuenda katika eneo lililozunguka Tiro. Aliingia katika nyumba na hakutaka mu yeyote ajue hilo, lakini hakuweza kufanya siri kuwepo kwake. 25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo mchafu mara moja akasikia juu ya Yesu hivyo alimwijia na kuanguka chini yake. 26 Mwanamke huyo alikuwa ni Mgiriki na siyo Myahudi, na alikuwa amezaliwa Foeniki ya Shamu. Yeye alimsihi amfukuze pepo yule kutoka kwa binti yake.
27 Yesu akamwambia, “Kwanza waache watoto watosheke, kwani sio haki kuwanyanganya watoto mkate wao na kuwapa mbwa.”
28 Lakini yeye akajibu, “Bwana hata mbwa walio chini ya meza wanakula mabaki ya chakula cha watoto.”
29 Kisha Yesu akamwambia, “kwa majibu haya unaweza kwenda nyumbani kwa amani: pepo mbaya amekwisha mtoka binti yako.”
30 Kwa hiyo akaenda nyumbani na akamkuta amelala akipumzika kitandani, na yule pepo tayari amekwisha mtoka.
Yesu Amponya Asiyesikia
31 Yesu akarudi kutoka katika eneo kuzunguka jiji la Tiro na akapita katika jiji la Sidoni hadi Ziwa Galilaya akipita katika jimbo la Dekapoli. 32 Pale watu wengine wakamletea mtu asiyeweza kusikia na tena aliyesema kwa shida. Nao wakamwomba Yesu amwekee mikono yake na kumponya.
33 Yesu akamchukua pembeni, kutoka katika kundi, na akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake. Kisha Yesu akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 Akaangalia juu mbinguni, akapumua na kumwambia “Efatha” yaani, “Funguka!” 35 Mara masikio ya mtu yule yakafunguka, na ulimi wake ukawa huru, na akaanza kuzungumza, vizuri.
36 Lakini kadiri jinsi alivyowaamuru wasimwambie mtu ndivyo walivyozidi kueneza habari hiyo. 37 Na watu wakashangazwa kabisa na kusema, “Yesu amefanya kila kitu vyema. Kwani amewafanya wale wasiosikia kusikia na wasiosema kusema.”
© 2017 Bible League International