Book of Common Prayer
17 Mungu alitaka kuthibitisha kuwa ahadi yake ilikuwa kweli. Alitaka kuthibitisha hili kwa wale ambao wataipokea ahadi. Aliwataka waelewe kwa uwazi kwamba makusudi yake kamwe hayabadiliki. Hivyo Mungu akisema kitu fulani kingetokea, na akathibitisha aliyosema kwa kuongezea kiapo. 18 Mambo haya mawili hayawezi kubadilika: Mungu hawezi kusema uongo anaposema kitu, na hawezi kudanganya anapoweka kiapo.
Hivyo mambo yote hayo ni ya msaada mkubwa kutusaidia sisi tuliomjia Mungu kwa ajili ya usalama. Yanatuhimiza kuling'ang'ania tumaini lililo letu. 19 Tumaini hili tulilonalo ni kama nanga kwetu. Ni imara na la uhakika na hutulinda salama. Huenda hadi nyuma ya pazia[a] katika mahali patakatifu zaidi kwenye hekalu la kimbingu la Mungu. 20 Tayari Yesu amekwisha kuingia hapo na kuifungua njia kwa ajili yetu. Amefanyika kuhani mkuu milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.
Kuhani Melkizedeki
7 Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu. Alikutana na Ibrahimu wakati Ibrahimu alipokuwa akirudi baada ya kuwashinda wafalme. Siku hiyo Melkizedeki alimbariki Ibrahimu. 2 Kisha Ibrahimu akampa sehemu ya kumi ya kila kitu alichokuwa nacho.
Jina Melkizedeki, mfalme wa Salemu, lilikuwa na maana mbili. Kwanza, Melkizedeki inamaanisha “mfalme wa haki.” Na “mfalme wa Salemu” inamaanisha “mfalme wa amani.” 3 Hakuna ajuaye baba na mama yake walikuwa ni kina nani au walitokea wapi.[b] Na hakuna ajuaye alizaliwa lini au alikufa lini. Melkizedeki ni kama Mwana wa Mungu kwa vile siku zote atakuwa kuhani.
4 Unaweza kuona kuwa Melkizedeki alikuwa mkuu sana. Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa yeye sehemu ya kumi ya kila alichoshinda kule vitani. 5 Sasa sheria inasema kwamba wale wa ukoo wa Lawi waliokuja kuwa makuhani wanastahili kupata sehemu ya kumi kutoka kwa watu wao, hata kama wao na watu wao ni wa familia ya Ibrahimu. 6 Melkizedeki wala hakutoka katika kabila la Lawi, lakini Ibrahimu akampa sehemu ya kumi ya alivyokuwa navyo. Na Melkizedeki akambariki Ibrahimu yule aliyekuwa na ahadi za Mungu. 7 Na kila mtu anajua kwamba mtu aliye wa muhimu zaidi humbariki mtu yule ambaye ana umuhimu mdogo.
8 Makuhani hawa hupata sehemu ya kumi, lakini wao ni binadamu tu wanaoishi kisha hufa. Lakini Melkizedeki, aliyepata sehemu ya kumi kutoka kwa Ibrahimu, anaendelea kuishi, kama Maandiko yanavyosema. 9 Sasa wale wa kutoka ukoo wa Lawi ndiyo wanaopata sehemu ya kumi kutoka kwa watu. Lakini tunaweza kusema kuwa Ibrahimu alipompa Melkizedeki sehemu ya kumi, kisha Lawi naye akatoa. 10 Lawi alikuwa bado hajazaliwa, lakini alikuwepo katika baba yake Ibrahimu wakati Melkizedeki alipokutana naye.
27 Wakati huo huo wafuasi wa Yesu wakarudi toka mjini. Nao walishangaa kwa sababu walimwona Yesu akiongea na mwanamke. Lakini hakuna aliyemwuliza yule mwanamke, “Unataka nini?” Wala Yesu, “Kwa nini unaongea naye?”
28 Yule mwanamke akauacha mtungi wake wa maji na kurudi mjini. Akawaambia watu kule, 29 “Mwanaume mmoja amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya. Njooni mkamwone. Inawezekana yeye ndiye Masihi.” 30 Hivyo wale watu wakatoka mjini wakaenda kumwona Yesu!
31 Wakati huyo mwanamke akiwa mjini, wafuasi wa Yesu wakamsihi Bwana wao wakamwambia, “Mwalimu, ule chakula chochote.”
32 Lakini Yesu akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkijui.”
33 Hapo wafuasi wake wakaulizana, “Kwani kuna mtu yeyote hapa aliyemletea chakula mapema?”
34 Yesu akasema, “Chakula changu ni kuimaliza kazi ile ambayo aliyenituma amenipa niifanye. 35 Mnapopanda mimea, huwa mnasema, ‘Bado miezi minne ya kusubiri kabla ya kuvuna mazao.’ Lakini mimi ninawaambia, yafumbueni macho yenu na kuyaangalia mashamba. Sasa yako tayari kuvunwa. 36 Hata sasa, watu wanaovuna mazao wanalipwa. Wanawaleta ndani wale watakaoupata uzima wa milele. Ili kwamba watu wanaopanda waweze kufurahi wakati huu pamoja na wale wanaovuna. 37 Ni kweli tunaposema, ‘Mtu mmoja hupanda, lakini mwingine huvuna mazao.’ 38 Mimi niliwatuma kukusanya mazao ambayo ninyi hamkuyahangaikia. Wengine waliyahangaikia, nanyi mnapata faida kutokana na juhudi na kazi yao.”
39 Wasamaria wengi katika mji huo wakamwamini Yesu. Wakaamini kutokana na yale ambayo walisikia yule mwanamke akiwaambia juu ya Yesu. Aliwaambia, “Yeye amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya.” 40 Wasamaria wakaenda kwa Yesu. Wakamsihi akae pamoja nao. Naye akakaa nao kwa siku mbili. 41 Watu wengi zaidi wakamwamini Yesu kutokana na mambo aliyoyasema.
42 Watu hao wakamwambia mwanamke, “Mwanzoni tulimwamini Yesu kutokana na jinsi ulivyotueleza. Lakini sasa tunaamini kwa sababu tumemsikia sisi wenyewe. Sasa tunajua kwamba hakika Yeye ndiye atakayeuokoa ulimwengu.”
© 2017 Bible League International