Book of Common Prayer
1 Salamu kutoka kwa Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo.
Kwenu ninyi nyote mliopokea imani inayowapa baraka sawa nasi. Mlipewa imani kwa sababu Mungu wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo hufanya yaliyo mema na haki.
2 Mpewe neema na amani zaidi na zaidi, kwa sababu sasa mnamjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
Mungu Ametupa Kila Kitu Tunachohitaji
3 Yesu ana nguvu ya Mungu. Na nguvu yake imetupa heshima ili tuishi maisha yanayomtukuza na kumpendeza Mungu. Tuna vitu hivi kwa sababu tunamjua. Yesu alitualika kwa utukufu na nguvu ya uungu wake. 4 Na kupitia haya, alitupa ahadi kuu mno. Ili kwamba kwa hizo mnaweza kushiriki katika kuwa kama Mungu na ukaepuka maangamizo ya kiroho yanayokuja kwa watu ulimwenguni kwa sababu ya mambo maovu wanayotaka.
5 Kwa sababu mna baraka hizi, jitahidini kadri mnavyoweza kuongeza mambo haya: katika imani yenu ongezeni wema, katika wema wenu ongezeni maarifa; 6 katika maarifa yenu ongezeni kiasi; katika kiasi chenu ongezeni uvumilivu; katika uvumilivu wenu ongezeni kumwabudu Mungu; 7 katika kumwabudu Mungu kwenu ongezeni huruma kwa ndugu katika Kristo na kwa wema huu ongezeni upendo. 8 Ikiwa mambo haya yote yatakaa ndani yenu na kukua, mtazaa matunda mazuri yakiwa ni matokeo ya ninyi kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. 9 Lakini wale wasiokua na sifa hizi ndani yao ni wasiyeona. Hawataweza kuona kwa uwazi yale waliyonayo. Wamesahau kuwa dhambi zao ziliondolewa kutoka kwao na wakawa safi.
10 Ndugu zangu, Mungu aliwaita na akawachagua ili muwe wake. Jitahidini mhakikishe kuwa mnapata yale aliyonayo Mungu kwa ajili yenu. Mkifanya hivi hamtajikwa na kuanguka. 11 Na mtakaribishwa kwa baraka kuu katika ufalme usio na mwisho, ufalme wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Yesu Aomba Akiwa Peke Yake
(Mt 26:36-46; Mk 14:32-42)
39-40 Yesu akaondoka mjini akaenda Mlima wa Mizeituni. Wafuasi wake wakaenda pamoja naye. (Alikuwa akienda huko mara kwa mara.) Akawaambia wafuasi wake, “Ombeni ili mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”
41 Kisha Yesu akaenda kama hatua hamsini mbali nao. Akapiga magoti na akaomba akisema, 42 “Baba, ukiwa radhi, tafadhali usinifanye ninywe katika kikombe[a] hiki. Lakini fanya unalotaka wewe, siyo ninalotaka mimi.” 43 Kisha malaika kutoka mbinguni akaja akamtia nguvu. 44 Yesu aliomba kwa nguvu zaidi na kustahimili zaidi kama mpiganaji wa mieleka akiwa katika mapambano makali. Jasho kama matone ya damu likadondoka kutoka kwenye uso wake.[b] 45 Alipomaliza kuomba, alikwenda kwa wafuasi wake. Akawakuta wamelala, wamechoka kwa sababu ya huzuni. 46 Yesu akawaambia, “Kwa nini mnalala? Amkeni, ombeni mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”
Yesu Akamatwa
(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Yh 18:3-11)
47 Yesu alipokuwa anaongea, kundi likaja. Lilikuwa linaongozwa na Yuda, mmoja wa mitume kumi na wawili. Akamwendea Yesu ili ambusu.
48 Lakini Yesu akamwambia, “Yuda unatumia busu la urafiki kumsaliti Mwana wa Adamu kwa adui zake?” 49 Wafuasi wa Yesu walikuwa wamesimama pale pia. Walipoona kilichokuwa kinatokea, wakamwambia Yesu, “Bwana, tutumie panga zetu?” 50 Na mmoja wao akautumia upanga wake. Akakata sikio la kulia la mtumishi wa kuhani mkuu.
51 Yesu akasema, “Acha!” Kisha akaligusa sikio la mtumishi na akamponya.
52 Yesu akaliambia lile kundi lililokuja kumkamata. Walikuwa viongozi wa makuhani, viongozi wa wazee wa Kiyahudi na askari walinzi wa Hekalu. Akawaambia, “Kwa nini mmekuja hapa mkiwa na mapanga na marungu? Mnadhani mimi ni mhalifu? 53 Nilikuwa pamoja nanyi kila siku katika eneo la Hekalu. Kwa nini hamkujaribu kunikamata pale? Lakini sasa ni wakati wenu, wakati ambao giza linatawala.”
© 2017 Bible League International