Book of Common Prayer
Dunia Yavunwa
14 Nikatazama, na mbele yangu, katika wingu jeupe, alikuwepo mmoja aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa na taji ya dhahabu kwenye kichwa chake na mundu mkali mkononi mwake. 15 Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, akamwambia aliyekaa kwenye wingu, “Chukua mundu wako na ukusanye kutoka duniani. Wakati wa kuvuna umefika, na tunda limeiva duniani.” 16 Hivyo aliyekaa kwenye wingu akaupitisha mundu wake juu ya dunia. Na dunia ikavunwa.
17 Ndipo malaika mwingine akatoka hekaluni mbinguni. Malaika huyu naye alikuwa na mundu mkali. 18 Na malaika mwingine, aliyekuwa msimamizi wa moto wa madhabahu akatoka madhabahuni. Akamwita malaika mwenye mundu mkali na kusema, “Chukua mundu wako wenye makali na ukusanye mafungu ya zabibu kutoka shamba la mizabibu duniani. Zabibu zimeiva duniani.” 19 Malaika akaupitisha mundu juu ya dunia. Akakusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu. 20 Zabibu zikaminywa kwenye shinikizo nje ya mji. Damu ikatiririka kutoka kwenye shinikizo, ikanyanyuka juu kama vichwa vya farasi kwa urefu wa kilomita mia tatu.[a]
Malaika Wenye Mapigo ya Mwisho
15 Ndipo nikaona ajabu nyingine mbinguni, ilikuwa kubwa na ya kushangaza. Walikuwepo malaika saba wenye mapigo saba. Haya ni mapigo ya mwisho kwa sababu baada ya haya, ghadhabu ya Mungu itakuwa imekwisha.
2 Niliona kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Wale wote waliomshinda mnyama na sanamu yake na namba ya jina lake walikuwa wamesimama kando ya bahari. Watu hawa walikuwa na vinubi walivyopewa na Mungu. 3 Waliuimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu na wimbo wa Mwanakondoo:
“Mambo unayotenda ni makuu na ya kushangaza,
Bwana Mungu Mwenye Nguvu.
Njia zako ni sahihi na za kweli,
mtawala wa mataifa.
4 Watu wote watakucha wewe, Ee Bwana.
Watu wote watalisifu jina lako.
Mtakatifu ni wewe peke yako.
Watu wote watakuja na kusujudu mbele yako,
kwa sababu ni dhahiri kuwa wewe hutenda yaliyo haki.”
5 Baada ya hili nikaona hekalu, mahali patakatifu pa Mungu[b] mbinguni. Likiwa wazi; 6 kisha malaika saba wenye mapigo saba wakatoka nje ya hekalu. Walikuwa wamevaa kitani safi inayong'aa. Wamevaa mikanda mipana ya dhahabu vifuani mwao. 7 Kisha mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akawapa malaika bakuli saba za dhahabu. Bakuli zilikuwa zimejaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. 8 Hekalu lilikuwa limejaa moshi uliotoka katika utukufu na nguvu ya Mungu. Hakuna ambaye angeweza kuingia hekaluni mpaka mapigo saba ya malaika saba yamemalizika.
Badilisheni Namna Mnavyoishi
13 Sehemu ya watu waliokuwa pamoja na Yesu pale, walimweleza kilichowapata baadhi ya waabuduo kutoka Galilaya. Pilato alikuwa ameamuru wauawe. Damu zao zilichanganywa na damu za wanyama waliowaleta kwa ajili ya kutoa dhabihu. 2 Yesu alijibu akasema, “Mnadhani hili liliwapata watu hao kwa sababu walikuwa wenye dhambi kuliko watu wengine wote wa Galilaya? 3 Hapana, hawakuwa hivyo. Lakini ikiwa hamtaamua kubadili maisha yenu sasa, ninyi nyote mtaangamizwa kama wao! 4 Na vipi kuhusu wale watu kumi na wanane waliokufa pale mnara wa Siloamu ulipowaangukia? Mnadhani walikuwa na dhambi kuliko watu wengine katika mji wa Yerusalemu? 5 Hawakuwa hivyo. Lakini ninawaambia, ikiwa hamtaamua kubadilika sasa, hata ninyi mtaangamizwa pia!”
Mti Usiozaa Matunda
6 Yesu akawasimulia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa amepanda mtini katika shamba lake. Alipokuja kutafuta matunda kwenye mtini huo hakupata tunda lolote. 7 Alikuwa na mtumishi aliyekuwa akilitunza shamba. Hivyo alimwambia mtumishi wake, ‘Nimekuwa nikitafuta matunda kwenye mti huu kwa miaka mitatu, lakini sijawahi kupata tunda lolote. Ukate mti huu! Kwa maana unaiharibu ardhi.’ 8 Lakini mtumishi alijibu, ‘Mkuu, tuuache mti huu mwaka mmoja zaidi ili tuone ikiwa utazaa matunda. Nitakusanya samadi kuuzunguka ili kuupa mbolea. 9 Unaweza kuzaa matunda mwaka ujao. Ikiwa hautazaa, ndipo utaweza kuukata.’”
© 2017 Bible League International