Book of Common Prayer
Yesu Aonya Kuhusu Matatizo
(Mk 13:9-13; Lk 21:12-17)
16 Sikilizeni! Ninawatuma, nanyi mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Hivyo muwe na akili kama nyoka. Lakini pia muwe kama njiwa na msimdhuru yeyote. 17 Muwe waangalifu! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka ili kuwashitaki mbele ya mabaraza ya mijini. Watawachapa ndani ya masinagogi yao. 18 Mtasimamishwa mbele ya magavana na wafalme. Watu watawafanyia ninyi hivi kwa sababu mnanifuata. Mtakuwa mashahidi wangu mbele za wafalme na magavana hao na kwa watu wa mataifa mengine. 19 Mtakapokamatwa, msisumbuke kuhusu nini mtakachosema au namna gani mtakavyosema. Katika wakati huo mtapewa maneno ya kusema. 20 Si ninyi mtakaoongea; Roho wa Baba Mungu wenu atakuwa anaongea kupitia ninyi.
21 Ndugu watakuwa kinyume cha ndugu zao wenyewe na kuwapeleka kwenda kuuawa. Baba watawapeleka watoto wao wenyewe kuuawa. Watoto watapigana kinyume na wazazi wao na watawapeleka kuuawa. 22 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. Lakini atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa.
Muwe Makini Jinsi Mnavyoishi
12 Mmekuwa dhaifu, hebu mjitie nguvu tena. 13 Muishi katika njia iliyo sahihi ili muweze kuokolewa na udhaifu wenu hautawasababisha ninyi kupotea.
14 Jitahidini kuishi kwa amani na kila mtu. Na mjitahidi kuyaweka mbali na dhambi maisha yenu. Yeyote ambaye maisha yake siyo matakatifu hawezi kumwona Bwana. 15 Muwe makini ili mtu asije akakosa kuipata neema ya Mungu. Muwe makini ili asiwepo atakayepoteza imani yake na kuwa kama gugu chungu linalomea miongoni mwenu. Mtu wa jinsi hiyo anaweza kuharibu kundi lenu lote. 16 Muwe makini ili asiwepo yeyote atakayefanya dhambi ya uzinzi au kushindwa kumheshimu Mungu moyoni kama alivyofanya Esau. Kama kijana mkubwa katika nyumba ya babaye, Esau angerithi sehemu kubwa ya vitu kutoka kwa baba yake. Lakini akauza kila kitu kwa mlo mmoja tu. 17 Mnakumbuka kwamba baada ya Esau kufanya hivi, akataka kupata baraka za baba yake. Akaitamani sana baraka ile kiasi kwamba akalia. Lakini baba yake akakataa kumpa baraka hiyo, kwa sababu Esau hakupata njia ya kubadili yale aliyotenda.
18 Ninyi ni watu wa Mungu, kama watu wa Israeli walipofika katika Mlima Sinai. Lakini hamjaufikia mlima halisi wa kuweza kushikwa. Mlima huo haupo kama ule waliouona, uliokuwa ukiwaka moto na kufunikwa na giza, utusitusi na dhoruba. 19 Haipo sauti ya tarumbeta au sauti iliyoyasema maneno kama hayo waliyoyasikia. Walipoisikia sauti, wakasihi kamwe wasisikie neno lingine. 20 Hawakutaka kusikia amri: “Kama chochote, hata mnyama, akigusa mlima, lazima kiuawe kwa kupigwa mawe.”(A) 21 Kile walichoona kilikuwa cha kutisha kiasi kwamba Musa akasema, “Natetemeka kwa hofu.”(B)[a]
22 Lakini mmeufikia Mlima Sayuni, kwenye mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni.[b] Mmefika mahali ambapo maelfu wa malaika wamekusanyika kusherehekea. 23 Mmefika katika kusanyiko la watoto wazaliwa wa kwanza wa Mungu. Majina yao yameandikwa mbinguni. Mmemfikia Mungu, hakimu wa watu wote. Na mmefika kwenye roho za watu wema ambao wamekamilishwa. 24 Mmemfikia Yesu; yeye aliyelileta kutoka kwa Mungu agano jipya kwenda kwa watu wake. Mmefika kwenye damu iliyonyunyizwa[c] ambayo inasema habari za mema zaidi kuliko damu ya Habili.
© 2017 Bible League International