Book of Common Prayer
Paulo Ajaribu Kumshawishi Agripa
24 Paulo alipokuwa bado anajitetea, Festo alipaza sauti akasema, “Paulo, umerukwa na akili! Kusoma kwingi kumekufanya kichaa.” 25 Paulo akasema, “Mheshimiwa Festo, mimi si kichaa. Ninachokisema ni kweli na kinaingia akilini. 26 Mfalme Agripa analifahamu hili, na ninaweza kuzungumza naye kwa uhuru. Ninafahamu kwamba amekwisha kusikia kuhusu mambo haya, yalitokea mahali ambako kila mtu aliyaona. 27 Mfalme Agripa, unaamini yale ambayo manabii waliandika? Ninajua unaamini!”
28 Mfalme Agripa akamwambia Paulo, “Unadhani unaweza kunishawishi kirahisi kiasi hicho ili niwe Mkristo?”
29 Paulo akasema, “Haijalishi kwangu, ikiwa ni vigumu au rahisi. Ninaomba tu kwa Mungu kwamba si wewe peke yako lakini kila mtu anayenisikiliza leo angeokolewa ili awe kama mimi, isipokuwa kwa minyororo hii!”
30 Mfalme Agripa, Gavana Festo, Bernike, na watu wote waliokaa pamoja nao wakasimama 31 na kuondoka chumbani. Walikuwa wanaongea wenyewe. Walisema, “Mtu huyu hajafanya chochote kinachostahili kuuawa au kuwekwa gerezani.” 32 Kisha Agripa akamwambia Festo, “Tungemwachia huru, lakini ameomba kumwona Kaisari.”
Paulo Aenda Rumi
27 Iliamriwa kwamba tutakwenda Italia. Ofisa wa Jeshi aliyeitwa Yulio, aliyetumika katika jeshi maalumu la mfalme mkuu, aliwekwa kuwa kiongozi wa kumlinda Paulo na baadhi ya wafungwa wengine safarini. 2 Tuliingia kwenye meli katika mji wa Adramatio. Meli hiyo ilikuwa inasafiri kupitia sehemu mbalimbali za Asia. Aristarko, mtu Thesalonike katika makedonia alisafiri pamoja nasi.
3 Siku iliyofuata tulifika kwenye mji wa Sidoni. Yulio alikuwa mwema sana kwa Paulo na akampa uhuru wa kwenda kuwatembelea rafiki zake pale, walimpa chochote alichohitaji. 4 Tuliondoka katika mji ule na tukatweka tanga tukasafiri karibu na kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa unavuma kinyume nasi. 5 Tulikwenda kwa kukatisha bahari upande wa Kilikia na Pamfilia. Kisha tukafika katika mji wa Mira katika jimbo la Likia. 6 Tulipofika hapo ofisa wa jeshi akapata meli iliyotoka katika mji wa Iskanderia iliyokuwa inakwenda Italia. Akatupandisha humo.
7 Tulitweka tanga na kusafiri taratibu kwa siku nyingi. Ilikuwa vigumu kwetu kufika katika mji wa Nido kwa sababu upepo ulikuwa unavuma kinyume chetu. Hatukuweza kuendelea zaidi kwa kupitia njia hiyo, hivyo tulitweka tanga tukasafiri kupitia upande wa kusini mwa kisiwa cha Krete karibu na Salmone. 8 Tulisafiri sambamba na pwani, lakini kwa shida. Ndipo tukafika mahali palipoitwa Bandari Salama, karibu na mji wa Lasea.
Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa
(Mt 9:18-26; Mk 5:21-43)
40 Yesu aliporudi Galilaya, watu walimkaribisha. Kila mtu alikuwa anamsubiri. 41-42 Mtu mmoja jina lake Yairo, aliyekuwa mkuu wa sinagogi alimwendea. Alikuwa na binti mmoja tu mwenye umri wa miaka kumi na mbili na alikuwa mgonjwa sana katika hali ya kufa. Hivyo Yairo alisujudu miguuni pa Yesu na akamsihi aende nyumbani kwake.
Yesu alipokuwa akienda nyumbani kwa Yairo, watu walimzonga kila upande. 43 Mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili alikuwepo katika umati huo. Alikuwa ametumia mali zake zote kwa madaktari,[a] lakini hakuna daktari aliyeweza kumponya. 44 Alikwenda nyuma ya Yesu na kugusa pembe ya vazi lake. Wakati huo huo damu ikaacha kumtoka. 45 Ndipo Yesu akasema, “Nani amenigusa?”
Kila mtu alikataa kuwa hajamgusa, Petro akasema, “Mkuu, watu wamekuzunguka na wanakuzongazonga kila upande.”
46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu amenigusa. Nimesikia nguvu ikinitoka.” 47 Yule mwanamke alipoona ya kwamba hataweza kujificha akajitokeza akitetemeka. Akasujudu mbele ya Yesu. Huku kila mmoja akisikia, akaeleza sababu iliyomfanya amguse, na kwamba alipona wakati ule ule alipomgusa. 48 Yesu alimwambia, “Binti yangu umeponywa kwa sababu uliamini. Nenda kwa amani.”
49 Yesu alipokuwa bado anaongea, mtu mmoja kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi alikuja na akasema, “Binti yako amekwisha kufa! Hakuna haja ya kuendelea kumsumbua Mwalimu.”
50 Yesu aliposikia maneno hayo, alimwambia Yairo, “Usiogope! Amini tu na binti yako ataponywa.”
51 Yesu akaenda nyumbani, alipofika akaruhusu Petro, Yohana, Yakobo pamoja na baba na mama wa yule mtoto tu kuingia ndani pamoja naye. 52 Kila mtu alikuwa akilia na kusikia huzuni kwa sababu msichana alikuwa amekufa. Lakini Yesu akasema, “Msilie. Hajafa. Amelala usingizi tu.”
53 Watu wakamcheka, kwa sababu walijua kuwa amekwisha kufa. 54 Lakini Yesu akamshika mkono na kumwambia, “Mtoto inuka!” 55 Roho yake ikamrudia, akasimama hapo hapo. Yesu akasema, “Mpeni chakula.” 56 Wazazi wa yule binti wakashangaa. Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote lililotokea.
© 2017 Bible League International