Book of Common Prayer
19 Ndipo baadhi ya Wayahudi wakaja kutoka Antiokia na Ikonia na kuwashawishi watu ili wampinge Paulo. Hivyo wakamtupia mawe na kumburuza kumtoa nje ya mji. Wakidhani kuwa wamemwua. 20 Lakini wafuasi wa Yesu walipokusanyika kumzunguka, aliamka na kuingia mjini. Siku iliyofuata yeye na Barnaba waliondoka na kwenda katika mji wa Derbe.
Kurudi Antiokia ya Shamu
21 Walihubiri pia Habari Njema katika mji wa Derbe, na watu wengi wakawa wafuasi wa Yesu. Kisha Paulo na Barnaba walirudi katika miji ya Listra, Ikonia na Antiokia. 22 Katika miji hiyo waliwasaidia wafuasi kukua na kuwa na nguvu katika imani yao na waliwatia moyo kuendelea kumwamini Mungu. Waliwaambia, “Ni lazima tuteseke kwa mambo mengi katika safari yetu ya kwenda katika ufalme wa Mungu.” 23 Waliwachagua pia wazee katika kila kanisa na kuacha kula kwa muda ili kuwaombea. Wazee hawa walikuwa wanaume wanaomtumaini Bwana Yesu, hivyo Paulo na Barnaba wakamwomba Bwana awalinde.
24 Paulo na Barnaba walipita katikati ya eneo la Pisidia. Kisha walifika katika jimbo la Pamfilia. 25 Waliwahubiri watu ujumbe wa Mungu katika mji wa Perge, kisha wakateremka kwenda katika mji wa Attalia. 26 Na kutoka huko wakatweka tanga kwenda katika mji wa Antiokia ya Shamu. Huu ni mji ambako waamini waliwaweka katika uangalizi wa Mungu na kuwatuma kufanya kazi hii. Na sasa walikuwa wameimaliza.
27 Paulo na Barnaba walipofika, walilikusanya kanisa pamoja. Waliwaambia waamini yote ambayo Mungu aliwatumia kutenda. Walisema, “Mungu amefungua mlango kwa watu wasio Wayahudi kuamini!” 28 Na walikaa pale pamoja na wafuasi wa Bwana kwa muda mrefu.
Kifo cha Lazaro
11 Alikuwepo mtu aliyekuwa mgonjwa aliyeitwa Lazaro. Huyo aliishi katika mji wa Bethania, mahali ambapo Mariamu na dada yake Martha waliishi. 2 (Mariamu ni mwanamke yule aliyempaka Bwana manukato na kumpangusa miguu kwa nywele zake.) Ndugu wa Mariamu alikuwa Lazaro, ambaye sasa alikuwa mgonjwa. 3 Kwa hiyo Mariamu na Martha walimtuma mtu kwa Yesu kumwambia, “Bwana, rafiki yako mpendwa Lazaro ni mgonjwa.”
4 Yesu aliposikia hayo alisema, “ugonjwa huu sio wa kifo. Isipokuwa, ugonjwa huu ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hili limetokea ili kuleta utukufu kwa Mwana wa Mungu.” 5 Yesu aliwapenda Martha, na dada yake na Lazaro. 6 Hivyo aliposikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, akabaki alipokuwa kwa siku mbili zaidi, 7 kisha akawaambia wafuasi wake, “Inatupasa kurudi tena Uyahudi.”
8 Wakamjibu, “Lakini Mwalimu, ni muda mfupi tu uliopita viongozi wa Wayahudi pale walijitahidi kukuua kwa mawe. Sasa unataka kwenda huko tena?”
9 Yesu akajibu, “Yako masaa kumi na mawili ya mchana katika siku. Yeyote anayetembea mchana hatajikwaa na kuanguka kwani anamulikiwa na nuru ya ulimwengu huu. 10 Lakini yeyote anayetembea usiku atajikwaa kwa sababu hana nuru[a] inayomwongoza.”
11 Kisha Yesu akasema, “Rafiki yetu Lazaro sasa amelala, lakini nitakwenda ili nimwamshe.”
12 Wafuasi wake wakajibu, “Lakini, Bwana, kama amelala ataweza kupona.” 13 Walifikiri kwamba Yesu alikuwa na maana kwamba Lazaro alikuwa amelala usingizi, lakini Yeye alikuwa na maana kuwa amefariki.
14 Kisha hapo Yesu akasema wazi wazi, “Lazaro amekufa. 15 Na ninafurahi sikuwepo hapo. Ninafurahi kwa ajili yenu kwa sababu sasa mtaniamini mimi. Twendeni kwake sasa.”
16 Ndipo Tomaso, pia aliyeitwa “Pacha”, akawaambia wafuasi wengine, “Nasi pia tutaenda kule kufa pamoja na Yesu.”
© 2017 Bible League International